SEHEMU YA 20...
Msako wa kumsaka bibi Nyanjige porini uliendelea kwa masaa karibu kumi na mbili bila mafanikio yoyote! Nyumba yake ilisambaratishwa na mashimo mengi yalifukuliwa akitafutwa lakini bado hakuonekana mahali popote wanajeshi walikata tamaa na kuamini alikuwa amekufa.
Miili mingi ya tembo wakiwa wamekufa ilionekana kila mahali msituni, ndege na nzige waliokauka pia walionekana ardhini ilikuwa si rahisi kuiona ardhi sababu ya wingi wa ndege na nzige walioifunika.
Siku hiyohiyo jioni iliamriwa maiti zote zilizokuwa zimekusanywa zisafirishwe kurudi Tanzania wakati kukiwa na mpango kamambe wa kuendelea na operesheni kumsaka bibi Nyanjige siku ya iliyofuata.
Baada ya kauli hiyo ya mkuu wa majeshi maiti zote zilianza kuhamishwa kutolewa kwenye gari na kufungwa katika mifuko maalum ya nailoni tayari kwa kusafirishwa kurudishwa Tanzania, bila kugundulika bibi Nyanjige alifungwa ndani ya mfuko na kupakiwa katika ndege maalum iliyoandaliwa.
Dakika kama mbili hivi baada ya kuwekwa katika mfuko wa nailoni akiwa amepangwa ndani ya ndege bibi Nyanjige alianza kukosa hewa! Alihisi angekufa sababu ya kukosa hewa safi, Kwa kutumia meno yake makali alitoboa tundu katika mfuko wake na kuitega pua yake kwenye tundu hilo akawa anavuta hewa taratibu kutoka nje.
*
*
Ndege ilipoingia Dar es Salaam saa nne ya usiku maiti zote zilipakuliwa na kupakiwa ndani ya gari maalum lililoandaliwa tayari kwa kuzipelekea chumba cha maiti cha hospitali ya jeshi iliyoitwa Military general hospital kuhifadhiwa katika chumba chenye baridi ili zisiharibike zikisubiri operesheni imalizike na wote waliokuwa wazikwe siku moja kwa heshima ya jeshi.
Masaa matatu baada ya kuingizwa katika chumba cha maiti baridi kali iliyokuwemo ndani ya chumba hicho ilimfanya bibi Nyanjige ahisi mwili wake ukiganda aligundua asingeweza kuendelea kuwa ndani ya chumba hicho kwa muda mrefu kabla roho yake haijatoka.