SEHEMU YA 33...
“Wewe mtoto una uhakika na unachokisema?”
“Ndiyo!”
“Sasa na hao polisi watampataje kama ameondoka na basi kwenda Kilimanjaro?”
“Wanaweza kulifuatilia basi alilopanda!”
Dakika mbili baadaye msichana huyo alikuwa kwenye simu akiongea na polisi juu ya mahali alikokuwa bibi Nyanjige, hata polisi wenyewe walionekana kutoyaamini maneno ya binti huyo.
“Binti una uhakika lakini? Usije kulisumbua jeshi la polisi bure?”
“Ni uhakika!”
“Kwa hiyo yupo wapi?”
“Ameondoka masaa matatu yaliyopita kupelekea maiti huko Marangu Moshi, kama mtaweza kulifuatilia gari lililobeba maiti basi mtakuwa mmempata!”
“Kweli?”
“Ndiyo!”
“Namba za basi walililopanda unaifahamu?”
“Ni TZO 8507!”
“Ok! Ahsante!” Alishukuru askari na kumuaga binti huyo akimpa uhakika kuwa kama bibi Nyanjige angekamatwa huko alikosema basi yeye ndiye angepewa pesa yote iliyoahidiwa kama zawadi, bila kupoteza hata sekunde mbili baada ya kuongea na simu maaskari walinyanyua simu ya upepo na kuanza kuwasiliana na maaskari waliokuwa maeneo ya Chalinze.
“Unanipata afande, ova!”
“Ndiyo ninakusoma, ova!”
“Yule bibi! Yule bibi! Yumo ndani ya basi dogo linalosafirisha maiti kwenda Marangu, ova! Basi dogo lililobeba maiti!”
“Namba zake ni ngapi?”
“TZO 8507,hakikisheni mnamkamata, ova!”
“Mungu wang....!”Alisema askari wa upande wa Chalinze.
“Niniii? Kuna nini kwani?”
Askari aliyekuwa makao makuu hakupata jibu lolote kutoka upande wa pili, askari aliyekuwa akiongea nae alihisi baridi kali ikipita katikati ya uti wake wa mgongo! Mikono yake ilikufa ganzi na simu ya upepo ilianguka chini!
“Vipi?” Mwenzake aliyekuwa jirani alimuuliza hata yeye pia hakumpa jibu zaidi ya kumwambia kuna matatizo yametokea.
Gari lenye namba zilizotajwa ndio lililokuwa limepita kama saa nzima kabla ya simu hiyo ya upepo kupigwa!
Hawakuamini kama bibi Nyanjige alikuwa ndani ya basi hilo kwani waliwakagua karibu watu wote ndani ya basi hilo isipokuwa mtu mmoja tu!
“Nafikiri aliyekuwa amejifunika khanga kwenye kiti cha mwisho kabisa nyuma ya basi, niliyetaka kumwamsha halafu wewe ukasema tuachane alikuwa bibi Nyanjige sasa tutafanya nini?”