SEHEMU YA 18...
Jeshi la askari wasiopungua elfu tano liliuvamia msitu huo mkubwa kwa ajili ya kazi hiyo, kila mahali walikopita walishangaa kuona idadi kubwa ya tembo wakiwa wamekufa na kusambazwa kabisa na mabomu lakini hawakumwona bibi Nyanjige mahali popote kila mtu aliamini bibi huyo alikufa katika mashambulizi hayo.
*
*
Hakikuwa kitu rahisi kwa bibi Nyanjige kufa kama walivyotegemea kwani dakika kama ishirini hivi kabla ya jeshi la nchi kavu halijauvamia msitu, bibi alirejewa na fahamu zake na kukuta kila upande wa mwili wake kuna Tembo mkubwa mnene aliyekufa na aliponyanyuka na kukaa kitako macho yake yalipambana na shimo kubwa lililochimbuliwa alijua hiyo ilikuwa ni kazi ya mabomu.
Aliendelea kusikia milipuko sehemu mbalimbali msituni, ndege zilikuwa zikidondosha mabomu, kwa hali hiyo ingawa alikuwa amelewa aliweza kunyanyuka na kujikongoja akipita katikati ya msituni chini ya miti michache iliyokuwa imebaki mbele alisimama alipoiona helkopta iliyoungua huku pembeni mwake kukiwa na maiti za wanajeshi wawili waliokuwa.
Wazo la kujiokoa lilimwijia kichwani mwake kwa sababu alijua wakati wowote angekamatwa, aliivamia moja ya maiti hizo na kuivua magwanda na kuyavaa na akachukua pia kofia na kuivaa kichwani mwake, alipomaliza tu kufanya hivyo alisikia nyasi nyuma yake zikitingishika na aliamini haukuwa upepo.
Walikuwa ni maaskari wa nchi kavu wa Tanzania! Walioibuka kutoka katikati ya nyasi wakiwa na silaha zao mikononi, moyo wa bibi Nyanjige uliingiwa na hofu kubwa na alianza kutetemeka akijua ni lazima angetiwa nguvuni na kuuawa. Pamoja na kuwa bibi kizee lakini alikuwa shupavu kuliko umri wake, alijiangusha karibu kabisa na maiti aliyoivua magwanda.
Kwa jicho la pembeni aliwashuhudia askari wakitembea kuelekea mahali ilipokuwa helkopita iliyoungua, kila mmoja wao alisikika akiongea kwa huzuni hasa walipoziona maiti zikiwa zimelala pembeni, wao waliamini miili yote mitatu iliyolala chini ilikuwa maiti hawakujua kama mtu waliyekuwa wakimsaka alikuwa miongoni mwa miili hiyo.