JK apingwa
na Happiness Katabazi
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
WATU waliotoa maoni kuhusu hotuba iliyotolewa juzi na Rais Jakaya Kikwete, wamezipinga hatua zilizochukuliwa dhidi ya watu wanaotuhumiwa kuchota mabilioni ya fedha kutoka katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA).
Waliliambia gazeti hili kuwa hatua hizo zilizochukuliwa na rais, zinamfanya aonekane amevunja Ibara ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, kwa kitendo chake cha kuwasamehe watu walioiba na kurejesha fedha za EPA.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Mhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Sengondo Mvungi, alisema Ibara ya 13 ya Katiba ya nchi inatamka usawa mbele ya sheria, hivyo kitendo cha rais kuwasamehe waliorejesha fedha hizo si sahihi na kusema inashangaza kwa nini rais anawakingia kifua watu hao.
"Rais Kikwete amekosea kutoa msamaha kwa hao mafisadi waliorejesha fedha hizo kwa sababu hao waliozirejesha wamekiri kosa na ushaidi wa wizi huo umepatika, kinachotakiwa, mafaili ya waliorejesha na ambao hawajarejesha yapelekwe kwa DPP ili awafungulie kesi mahakamani," alisema Dk. Mvungi ambaye ni mwanasheria kitaaluma.
Dk. Mvungi alimtaka Rais Kikwete asichanganye mtu kukiri kosa na kurudisha alichoiba na madaraka yake ya kusamehe.
Akifafanua, alisema kuwa Ibara ya 145 ya Katiba inampa mamlaka rais kusamehe mtu ambaye ameshahukumiwa na mahakama, baada ya mahakama kumkuta na hatia, na si kumsamehe mtu ambaye hajafikishwa mahakamani na kukutwa na hatia.
"Rais asiwageuze Watanzania mambumbumbu wa sheria… nasisitiza rais amevunja Katiba ya nchi na ninawataka Watanzania tusimame kidete kuitetea Katiba yetu," alisema Dk. Mvungi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, alisema kuwa, juzi rais Kikwete aliwathibitishia wananchi kwamba ana mkakati wa makusudi wa kuwalinda wezi wa EPA.
"Kama Kikwete kwenye hotuba yake aliweza kutaja jina la Rais wa Chama cha Walimu (CWT), alishindwaje kutaja hata jina la fisadi mmoja aliyeiba fedha nyingi BoT? Nasema hivi, rais ana urafiki wa karibu na hawa mafisadi, ndiyo maana anapatwa na kigugumizi cha kutaja majina yao na hata kueleza Kampuni ya Kagoda Agriculture ni ya nani," alisema Mbowe.
Hata hivyo, naye alisisitiza kuwa rais amevunja Katiba ya nchi na kwamba kinachoendelea kujidhiirisha ni ombwe la uongozi katika taifa.
Alisema rais hana mamlaka ya kumsamehe mtu ambaye hajahukumiwa na mahakama kama alivyofanya kuwasamehe waliorejesha fedha bila ya kufikishwa mahakamani.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP) Augustine Mrema, alisema ameshangazwa kwa kitendo cha rais kuutangazia umma kwamba hadi juzi mchana zilikuwa zimerejeshwa sh bilioni 69.3, lakini akashindwa kutaja majina ya watu waliozirudisha fedha hizo.
Aidha, Mrema alisema rais alipaswa kusema fedha hizo zimerejeshwa kwenye benki gani.
Mrema alisema kitendo cha rais kuagiza kamati ya uchunguzi wa wizi huo kuorodhesha majina ya makampuni yaliyoshindwa kurejesha fedha hizo na kuyawasilisha kwa Mkurugenzi wa Mashitaka, ni mbinu nyingine ambayo imelenga kuyashitaki makampuni mahakamani badala ya kuwashitaki watu waliohusika, na kuwaomba wananchi wawe macho na hali hiyo.
"Kama rais anataka wananchi wamuelewe na kuendelea kumheshimu ni vyema ataje majina ya hao waliokwapua fedha hizo na si kuorodhesha makampuni, kwa sababu mwisho wa siku watakaofikishwa mahakamani ni makarani wa makampuni hayo badala ya wahusika wakuu… awataje kwa sababu tutakuwa tumewajua wabaya wetu na hiyo ndiyo itakuwa zawadi ya Krismasi kwa sisi wananchi wake, tutafurahi sana.
"Rais asiwakingie kifua mafisadi hata kama walimsaidia kitu fulani… basi iwe siri yake moyoni na awatose na wananchi tutamlinda. Na ninamtaka aelewe kwamba hotuba yake haina maana, kwa sababu haijataja majina ya mafisadi," alisema Mrema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema amesikitishwa na kupoteza imani ya Rais Kikwete kwa jinsi alivyolishughulikia suala hilo la EPA.
"I am totally disappointed' (nimesikitishwa sana)… nilidhani rais angeamuru wale waliorejesha hizo fedha nao wakamatwe na wafikishwe mahakamani, kumbe mwenzetu ameamua kuvunja sheria za nchi kwa makusudi kabisa na kuwaruhusu watuhumiwa hao warejeshe fedha kisha waendelee kutanua mitaani.
"Nasema nimesononeshwa na nimepoteza imani na utawala wa rais, sijui nchi hii anaipeleka wapi," alisema Profesa Lipumba kwa masikitiko.
Alisema mtindo huo wa kiongozi mkuu wa nchi kupindisha sheria kwa sababu walioiba fedha hizo ni maswahiba zake, utakuja kuleta machafuko nchini, kwani anaamini watu ambao ndugu na jamaa zao wapo rumande kwa makosa ya wizi watajisikia vibaya na kuanza kutaka nao ndugu zao wapewe nafasi za kurejesha kile walichoiba ili wafutiwe kesi zinazowakabili.
Naye Mwadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Mwesiga Baregu, alisema ameshindwa kumuelewa Rais Kikwete ana mpango gani na taifa kwa sababu wizi wa fedha za EPA ni makosa ya jinai, lakini anashangaa ni kwa nini amekuwa na kigugumizi kuwachukulia hatua waliorejesha fedha hizo.
"Hivi hao waliorejesha fedha walizikopa kwenye EPA au kwenye Saccos… kwa sababu unapokopa fedha lazima uzirejeshe lakini hawa tumeambiwa waliiba na kama wanazirejesha ni kidhibiti tosha cha kuwaburuza mahakamani… Watanzania tumpinge rais katika hili, kwani amevunja sheria za nchi," alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), John Mnyika, akizungumza kutoka Mwanza, alisema Rais Kikwete ameendelea kuligawanya taifa kwa kuwalinda mafisadi na kugeuza suala lao kuwa la madai badala ya jinai.
Alisema hata mjadala wa OIC umeendelezwa na serikali yake yenyewe (Kikwete).
"Nimeshangaa. Lakini nikashangaa zaidi kwa Rais Kikwete kutofautiana wazi wazi na Waziri wake wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, ambaye Rais Kikwete amemuita kuwa ndiye ana dhamana ya suala hilo. Wakati rais anasema kwamba utafiti wa suala hilo bado haujakamilishwa na Waziri Membe, waziri mwenyewe wakati anahutubia Bunge Agosti 22 mwaka huu alitangaza kwamba wizara yake imeshakamilisha utafiti. Nani mkweli kati yao, Mungu ndiye ajuaye.
"Lakini Mwalimu Nyerere, katika kitabu cha Uongozi wetu na hatma ya Tanzania, alizungumza vizuri kuhusu serikali. Mwalimu aliweka wazi, mkusanyiko wa mawaziri wasiokuwa na dira ya pamoja na uwajibikaji wa pamoja, wanabaki kuwa serikalini kwa mujibu wa sheria tu, lakini kimaadili na kimantiki; hakuna serikali," alisema.
Juzi usiku Rais Kikwete alihutubia taifa pamoja na kuzungumzia mambo mengine, aliiagiza Kamati ya Uchunguzi ya Wizi wa fedha za EPA kuwasilisha majina ya makampuni yaliyoshindwa kurejesha fedha hizo kwa DPP, ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Kikwete alitangaza uamuzi wake huo uliokuwa ukisubiriwa kwa shauku kubwa na Watanzania walio wengi, akitekeleza ahadi aliyoitoa wakati alipohutubia Bunge mjini Dodoma Agosti 21 mwaka huu.
Akizungumzia urejeshwaji wa fedha hizo, Kikwete alisema taarifa alizoletewa juzi mchana zilikuwa zikionyesha kuwa kiasi cha sh bilioni 69.3 kati ya sh bilioni 90.3 zilikuwa zimerejeshwa kutoka katika akaunti ya EPA, kiasi ambacho ni asilimia 76.7 ya fedha zote.
Akizungumzia kuhusu mzozo unaozingira uamuzi wa Tanzania kujiunga katika Jumuiya ya Kiislamu duniani (OIC), alieleza hali hiyo inayogawa watu katika tofauti zao za kiimani kuwa isiyofurahisha na kwamba unaweza kulipeleka taifa pabaya.
Hata hivyo alisema hadi hivi sasa serikali bado haijaamua iwapo Tanzania ijiunge au isijiunge katika jumuiya hiyo, kutokana na ukweli kwamba, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa iliyopewa kazi ya kutafiti inaendelea na kazi ya kulifuatilia suala hilo, hivyo haijawasilisha serikalini matokeo ya utafiti wao pamoja na mapendekezo na kuamuliwa ipasavyo.