Rugemeleza
JF-Expert Member
- Oct 26, 2009
- 668
- 136

Na Saed Kubenea - Imechapwa 10 November 2010

MATOKEO ya uchaguzi mkuu yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), yamejaa utata, MwanaHALISI limegundua.
Taarifa kutoka ndani ya NEC, vyama vya siasa na baadhi ya wagombea, zinasema matokeo yaliyotolewa yanatofautiana na kura halisi zilizopigwa.
Kwa mujibu wa baadhi ya mawakala wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), matokeo mikononi mwao yanatofautiana sana na yale yaliyotangazwa na Tume ya taifa ya uchaguzi (NEC).
Matokeo mikononi mwa mawakala kutoka mikoa 18 ya Tanzania Bara na mitatu ya Zanzibar, hadi juzi Jumatatu, yanathibitisha kuwepo tofauti kati ya idadi ya vituoni na ile iliyotangazwa na NEC.
Uchaguzi mkuu nchini ulifanyika Jumapili iliyopita kwa kuchagua madiwani, wabunge na rais, kwa upande wa Tanzania Bara na masheha, wawakilishi na rais Visiwani.
Katika jimbo la Hai, mkoani Kilimanjaro, matokeo yaliyotangazwa na NEC yanaonyesha kuwa CCM imepata kura za urais 35,910, huku CHADEMA ikionyeshwa kupata kura 18,513.
Lakini matokeo ambayo yamekusanywa na mawakala wa CHADEMA yanaonyesha CCM imepata kura 20,120, huku CHADEMA ikipata kura 26,724.
Katika jimbo la Karatu, mkoani Arusha, hesabu za NEC zinaonyesha CCM imepata kura za urais 24,382, huku CHADEMA ikipata kura 41 tu; angalau kwa mujibu wa matangazo ya televisheni.
Bali kwa mujibu wa matokeo yaliyokusanywa na mawakala na ambayo yamesainiwa na mawakala wa vyama vilivyoshiriki uchaguzi na msimamizi wa uchaguzi katika jimboni hilo, CCM imepata kura 24,364 na CHADEMA imepata kura 43,137.
Jimbo jingine ambalo matokeo yake yamejaa utata ni Geita, mkoani Mwanza. Matokeo yaliyotangazwa na NEC katika jimbo hilo, yanaonyesha kuwa CCM imepata kura 17,792, na CHADEMA imeambulia kura 3,989.
Lakini matokeo mikononi mwa mawakala yanaonyesha kuwa CCM imepata kura 30,960 na CHADEMA kimepata kura 15, 736. NEC ilikiri kuwapo kwa kasoro katika jimbo la Geita na ilikubali kufanyia marekebisho.
Katika jimbo la Ubungo, mkoani Dar es Salaam, matokeo ya NEC yameipa CCM kura 68,727 na CHADEMA kura 65,450.
Hata hivyo, kwa mujibu wa matokeo mikononi mwa mawakala katika jimbo hilo yanaonyesha kuwa CHADEMA imepata kura 72,252 na CCM kura 70,472.
Kuvuja kwa taarifa hizi kumekuja wiki moja baada ya NEC kumtangaza Jakaya Kikwete kuwa mshindi wa kiti cha urais.
Kwa mujibu wa NEC, Kikwete alishinda nafasi hiyo kwa kupata kura 5,276,827 ambazo ni sawa na asilimia 61.17 ya kura zote halali zilizopigwa. Tume imesema kura zizopigwa zilikuwa 8,626,283.
Mshindani mkuu wa Kikwete, ambaye ni mgombea wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa alitangazwa kuwa amepata kura 2,271,941 zilizo sawa na asilimia 26.34 ya kura zote halali zilizopigwa.
Katika mpangilio huo, Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF alipewa kura 695,667 ambazo ni sawa na asilimia 8.06 ya kura zote halali.
Uchunguzi wa MwanaHALISI umebaini kuwa licha ya tofauti ya matokeo ya vituoni na yale ya NEC, matokeo katika baadhi ya maeneo hayakurekodiwa kwenye karatasi za tume, rasmi kwa shughuli hiyo.
Gazeti hili limeona matokeo yaliyorekodiwa kwenye karatasi za kawaida na magamba magumu ya makasha, ingawa zimegongwa mihuri inayoonekana kuwa ya tume.
Matokeo ya aina hii yanashurutisha kuwepo ujenzi wa shaka juu ya usalama wa kura na uwezekano wa matokeo kugushiwa.
Kwa mfano, katika jimbo la Segerea, mkoani Dar es Salaam, matokeo ya kura za urais yaliandikwa kwenye karatasi ya kawaida ya rangi ya khaki. Karatasi hiyo inaonyesha kuwa imetoka katika kituo Na. B – 2.
Katika kituo B – 4 ambako matokeo yameandikwa kwenye karatasi ya kawaida, CCM imepata kura 90 na CHADEMA kura 55.
Matokeo katika kituo hicho, kwa mujibu wa karatasi hiyo, yanaonyesha kuwa CCM imepata kura 94 na CHADEMA kura 90.
MwanaHALISI limeelezwa kuwa mbali na kasoro hiyo ya kutokuwapo kwa fomu za kurekodia matokeo, katika baadhi ya majimbo yaliyofanya uchaguzi, majumuisho ya kura za urais hayakufanyika.
Gazeti hili lilitaka kujua maoni ya Dk. Slaa juu ya taarifa kuwa kuna maeneo ambako majumuisho ya kura za urais hayakufanyika.
Naye alijibu, "Wewe unazungumzia hilo; matatizo yaliyopo katika uchaguzi huu ni makubwa sana. Kuna uchafu mwingi. Ndiyo maana sisi tunasisitiza kuwa hatuwezi kukubaliana na matokeo yaliyotangazwa."
Amesema, "Tunaendelea kukusanya nyaraka zote za uchaguzi na si muda mrefu ujao, tutaeleza dunia ni kitu gani kilifanyika, wapi na akina nani walihusika. Tutaeleza pia hatua gani itakayofuata baada ya hapa."
Gazeti lina taarifa kuwa baadhi ya majimbo ambako matokeo ya urais hayakutangazwa, ni Kiteto, Segerea, Muheza, Kibakwe, Kinondoni, Ilala na Moshi Vijijini.
"Huku kwetu hatukupewa nafasi ya kushuhudia zoezi la kuhesabu kura. Kazi hiyo ilifanywa na msimamizi wa uchaguzi ambaye alisema kura za rais zitahesabiwa wilayani," anasema John Mrema ambaye aligombea ubunge katika jimbo la Vunjo kupitia CHADEMA.
Anasema, "Lakini tulipofika katika ofisi ya mkurugenzi wa uchaguzi kule wilayani, tulimkuta msimamizi wa uchaguzi akiwa tayari na matokeo yake ya urais. Tulipomuuliza amepataje matokeo hayo wakati kura hazijajumlishwa, alikasirika na kuamua kuchana karatasi zote alizokuwa nazo."
Akiongea kwa kujiamini, Mrema amesema, kwa ufahamu wake, mpaka sasa matokeo ya urais katika jimbo la Moshi Vijijini hayajatangazwa.
Mbali na kuwapo kwa kasoro za majumuisho, taarifa zinasema zaidi ya majimbo 25 yaliyoshiriki uchaguzi hayakuwa na fomu za matokeo Na. 21 (A) na 24 (A).
Aidha, masanduku 36 yaliyosheheni kura za urais, yalikutwa yamehifadhiwa katika shule binafsi ya Biafra iliyopo katika manispaa ya Kinondoni, mkoani Dar es Salaam.
Masanduku hayo yalikutwa yakiwa na karatasi zake halisi za kupigia kura na yalikuwa bado yamefungwa kwa lakiri. Katika orodha ya masanduku hayo kulikuwa na yale yaliyotolewa kwa Kata za Tandale, Makumbusho, Mwananyamala, Kigogo na Hananasif.
Kwa kata ya Tandale yalikuwa na namba: 162452, 162495, 1624586, 162489 na 162401. Makumbusho Na. 161330, Hananasif Na. 16871, 161051, 160958, 160165 na Kigogo Na. 160665.
Kutoka Morogoro, taarifa zinaeleza utata wa aina yake. Kati ya wapigakura 422 waliotarajiwa kupiga kura katika kituo cha Shule ya Msingi Msufini, kata ya Msufini, manispaa ya Morogoro, hakuna hata mmoja aliyekuwa na shahada ya kupigia kura.
Taarifa hizi ni kwa mujibu wa daftari la wapigakura PDF Na. 00434524.
Katika kituo cha Shule ya Msingi Misufini B – 2, Na. 00006226 kilichopo kata ya Mafinga, kati ya wapigakura 422 ni wapigakura 192 tu ambao walikuwa na sifa ya kupigakura. Hii ni kwa mujibu wa daftari la wapigakura PDF Na. 00434425.
Mbali na kasoro hizo, baadhi ya watu wanaonekana mara mbili katika daftari la wapigakura. Inaonyeshwa pia kuwa wana shahada mbili tofauti za kupigia kura.
Hapa ndipo zinachipuka taarifa zinazodai kuwa kwa kupitia majina hayo, na mengine ya ambao hawakujitokeza kupigakura, ulifanyika uchakachuaji matokeo.
Madai yamezagaa kuwa uchakachuaji kwa njia ya wale ambao hawakujitokeza kupiga kura, ama ulifanyika kupitia mawakala wa vyama vya siasa wasiowaaminifu au wasimamizi wa uchaguzi.
Katika jimbo la Babati Mjini pekee, yamekutwa majina zaidi ya 2,000 ya wapigakura wa aina hiyo. Miongoni mwao ni Ali Khera Sumaye ambaye amekutwa na shahada mbili.
Shahada ya kwanza ya Sumaye ambaye aliwahi kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya chama cha NCCR- Mageuzi kabla ya kurejea CCM, ina Na. 12539414 na nyingine ni Na. 49947458. Taarifa nyingine zote za Sumaye, ikiwamo tarehe ya kuzaliwa zinafanana.
Shahada zote mbili zinamuonyesha Sumaye kuwa amezaliwa 17 Agosti 1952. Taarifa zake zinapatikana katika PDF Na. 00400518 ya daftari la kudumu la wapiga kura.
Naye Amina Abdallah Soono anatumia shahada Na. 1255139 na Na. 12557140; Anna Yakobo Masay, shahada Na. 1255831 na 12558205; Elinake Joseah, shahada Na. 26314248 na 49716656 na Jumapili Ramadhani Moromba mwenye shahada Na. 41226061.
Katika orodha hiyo, wapigakura wengine waliokutwa na shahada mbili ni Mariam Saidi Mohamed ambaye shahada zake ni Na. 12566932 na 49773838 na Ibrahim Richard Shalua Na. 32298659 na 12557313.
Taarifa za wapigakura hawa zinapatikana katika PDF, Na.004000518, Na.004000537 na Na. 00400534.
MwanaHALISI limegundua pia kwamba kuna baadhi ya wapigakura ambao majina yao yamekutwa katika daftari la wapigakura, lakini picha zao zinakosekana.
Haijaweza kufahamika iwapo wapigakura wanaoonyeshwa kuwa na shahada mbili walifanikiwa kupiga kura mara mbili au hata zaidi katika uchaguzi uliomalizika wiki iliyopita.
Lakini katika daftari la wapigakura kunaonyesha pia kuwa katika kituo cha Serikali ya Mt. Mbuyuni – 1 Na. 00006218, kata ya Mafisa, wapigakura 57 kati ya 410 hawakuwa na shahada za kupigia kura.
Miongoni mwa ambao hawakuwa na shahada ni Abas Ali Dunda, Abdallah Ali Matoto na Abas Majemba.
Mbali na kasoro hizo, MwanaHALISI limegundua mkanganyiko katika idadi ya walioandikishwa kupiga kura. Kwa mfano, Mkurugenzi wa NEC, Rajabu Kilavu alinukuliwa akisema tume yake imeandikisha jumla ya watu 21,210,187.
Hata hivyo, idadi hiyo ilipungua hadi kufikia wapigakura 19,686,608. Lakini Mwenyekiti wa Tume, Jaji mstaafu Lewis Makame alisema tume yake iliandikisha wapigakura 20,137,303.
Aidha, imefahamika kuwa timu ya wataalamu wa teknoljia ya habari (IT) ya CHADEMA ilitembelea mtambo wa kupokea matokeo ya uchaguzi siku mbili kabla ya uchaguzi.
Katika ziara hiyo, wataalamu hao waligundua kuwa mtambo huo haukuwa umejaribiwa kwa ajili ya kazi iliyokusudiwa.
"Tulipowaeleza kwamba ni makosa kitaalamu kutojaribu mtambo kama huu, ndipo walipoamua kuujaribu; na mara baada ya kuujaribu, ulikwama palepale," anaeleza Mashinda Mtei, mmoja wa wataalamu wa CHADEMA waliokwenda kukagua mtambo wa NEC.
Anasema wakati wanafanya majaribio waligundua kuwapo kwa kasoro kubwa ya kura za mgombea mmoja kuhamia kwa mgombea mwingine.
Mara baada ya kugundua kasoro hizo, anaeleza Mtei, NEC waliahidi kurejesha Dar es Salaam kompyuta zote zilizokuwa zimesambazwa mikoani na kwamba waliahidi kufanya kazi hiyo na kuikamilisha haraka.
Tume iliahidi kuifahamisha CHADEMA juu ya maendeleo kuhusu kompyuta hizo.
Hata hivyo, katika hali ambayo haijaeleweka, siku hiyohiyo, tarehe 28 Oktoba 2010, Kiravu alimuandikia barua katibu mkuu wa CHADEMA akikiri kuwapo kwa ujumbe wake katika ofisi za NEC.
Barua ya NEC yenye Kumb. Na. EA.75/162/08/99 ya tarehe 28 Oktoba inasema, "Napenda kukujulisha kwamba jana tarehe 27/10/2010, wataalam wa chama chako wa IT walikuja na kuruhusiwa kukagua mfumo wa kujumlisha kura.
Wataalamu hao waliridhika na mfumo huo na ni matumaini yangu kwamba wamekupatia taarifa kamili."
Barua ya Kiravu ilipokelewa CHADEMA terehe 4 Novemba 2010, siku sita baada ya uchaguzi kumalizika.
Gazeti hili ambalo linaendelea kutunga taarifa za uchaguzi kwa makini zaidi, limeshindwa kumpata Kiravu kueleza mapungufu haya na kwa nini barua kutoka NEC kwenda CHADEMA ilichukua zaidi ya siku tano kuwafikia.
Wakati NEC ikisema wataalamu wa IT waliotumwa na CHADEMA wameridhika na mfumo wa kuhesabia kura, taarifa kutoka ndani ya chama hicho na ambazo zimethibitishwa na Dk. Slaa zinasema wataalamu wake waliupinga mfumo huo kwa maelezo kwamba haufahamiki kwa watendaji wa NEC.
Anasema kuthibitisha kwamba watalaamu wa chama walikuwa sahihi, zoezi la kuhesabu kura za rais na hata kumjulisha kura za wabunge ili kupata idadi ya wabunge wa viti maalum, limechukua zaidi ya wiki moja.
Gazeti toleo na. 214