Historia ya Mombasa na makabila yake

Historia ya Mombasa na makabila yake

Jumbe Kondo

Senior Member
Joined
Oct 18, 2011
Posts
109
Reaction score
68
Mombasa ni mji mkongwe wa Afrika ya mashariki wenye sifa na tarekhe ndefu mno. Mji wenyewe ni kisiwa kilichozungukwa na maji pande zote ambacho kina mikondo miwili ya bahari. Mkondo wa kwanza ni wa kaskazini yaani maeneo ya bandari ya zamani ya Mombasa hadi Mwakirunge, maeneo haya yalikuwa makao ya Waswahili wa miji tisiya (Tisa twaifa) wakiwemo; Wamtwapa, wamvita, Wakatwa, Wabajuni ama Wagunya, Wakilifi,Wafaza,Wajomvu na Washaka. Kati ya makabila haya wengine walihamia Mombasa baada ya kuvundika( kuvunjika) kwa miji yao na wengine walikuja kwa khiari.

Kwenye mkondo wa bahari wa kusini wa kisiwa cha Mombasa waliishi waswahili wa miji mitatu (Thalatha twaifa) nao ni Wakilindini, Wachangamwe na Watangana ambao ndio wenyeji wa asili wa mji Mombasa. Maisha ya watu hao yalitegemeya sana uvuvi,ukulima na biashara. Kulingana na historia hapo kale palikuwa na uhusiano wa kibiashara baina ya miji ya pwani na Uarabuni,Uajemi, bara Hindi na Uchina. Siku hizo za kale biashara ilikuwa ni ya kubadilishana vitu. Kwa mfano Waarabu walileta tende,nguo, chumvi na vyenginevyo kutoka makwao hadi upwa huu wa Afrika mashariki. Baada ya kumaliza kukaa kwao nao walipeleka makwao vitu kama nazi, vyakula na mbao za kuundia majahazi.

Kuhusiana na jina la Mombasa historia yake ni ndefu, na kabla ya jina hilo la "Mombasa" kuna majina mengine sita yaliyolitangulia nayo ni; Faladi,Kongoweya,Gongwa, Mvita, Mji wa Kale, Nyali Kuu na hatimaye kuitwa Mombasa. Na yote haya ni mabadilifu kwa namna mbali mbali.

Kuna hoja tofauti zinazohusiana na usuli wa neno "Mombasa". Hoja ya kwanza ni kuwa jina hili limetokana na maneno mawili ambayo ni "Mambo na Sasa". Hoja ya pili ni kuwa limetokana na neno "Mwambadze?" (ambalo ni la Kimijikenda na maana yake ni kama wasemavyo waswahili wa kimvita- mwambaje?- yaani, kwa "Kiswahili sanifu" husemwa hamujambo?)
Mwandishi: Hamisi Malengo

Mijikenda Ni Kina nani?

2014-04-24

111.jpg


Neno'' Mijikenda'' maana yake ni miji tisa au makabila tisa, pia huitwa ''Makaya Chenda''.
Chimbuko la Wamijikenda latoka nchi ya Congo kama makabila mengine ya kibantu na walikaa Tanzania kisha wakahamia kusini mwa Somalia sehemu iitwayo ''Shungwaya'' ambayo inapatikana baina ya Mto Juba na Webbi Shebeli.Walipokuwa Shungwaya walikuwa wakiitwa ''Ashungwaya au ''Ashuru''.

Mababu wa Wamijikenda walichagua jina hili walipofika Pwani ya Kenya ili kuashiria makabila tisa yanayounda Mijikenda nayo ni: Giriama, Kauma, Chonyi, Kambe, Jibana, Ribe, Rabai, Duruma na Digo.
Mtafiti Thomas Spear anasema kwamba Baba ya Wamijikenda ni ''Muyeye'' na alioa wanawake wawili alipokuwa Shungwaya, wakwanza ni ''Mbodze'' na wapili ni ''Matsezi'' ambao alizaa nao watoto tisa waliopelekea kupatikana kwa makabila ya Mijikenda.

Aliongeza kwamba Shungwaya hakukaa Mijikenda pekee bali kulikuwa na makabila mengine nao ni: Waboni, Wasegeju, Wataita, Wasanye, Wataveta, Wasagalla, Waata na Walangulo.

Makabila yote haya yanaishi Pwani ya Kenya lakini idadi yao ni ndogo sana isipokuwa Wataita na Wataveta kwani idadi yao ni kubwa na wanaishi katika Kaunti ya Taita Taveta.
Wamijikenda wanaishi Pwani na Mombasa ndio mji Mkuu wa Pwani na uko mbali na Jiji la Nairobi kwa takriban kilomita 500.

Idadi yao ni inakaribia milioni tatu na sehemu wanazoishi ni:Taita Taveta, Kwale, Mombasa, Kilifi, Malindi, Tana River Tana Delta na Lamu.
Katika upande wa dini Wamijikenda walikuwa wakizitukuza Turathi za Mababu zao ilhali wengine walikuwa wakiabudu Mizimu

. Kila kabila lilikuwa na sehemu ya kufanyia ibada ya kuabudu Mizimu zinazoitwa '‘Kaya'' ambayo ni misitu mikubwa iliofungamana. Kwaajili hiyo imani yao ya kumuabudu Mwenyezi Mungu ilikuwa dhaifu sana.

Hali iligeuka baada ya kuingia ulinganizi wa dini ya Kiislamu na Kikristo katika sehemu zao, watu walianza kuingia katika dini ya Kiislamu kwa wingi, baadhi yao waliingia katika dini ya Kikristo ilhali wengine walibakia katika dini zao za kuabudu Mizimu.

Katika upande wa Siasa Wamijikenda walikuwa wakiongozwa na Wazee ambao walikuwa wakihakikisha kwamba watu wanaishi pamoja na kusaidiana katika mambo mbalimbali na walikuwa wakichaguliwa kulingana na sifa zao njema kama vile Utu, Ushujaa, Ukarimu zikiwemo na sifa zengine.

Wamijikenda walikuwa wanatambulika hata kabla ya Kenya kupata uhuru, waliunda chama chao cha kisiasa mwaka 1945 kilichoitwa ''Muungano wa Wamijikenda'' (MIJIKENDA UNION) na kiliongozwa na marehemu Ronald Ngala ambaye asili yake ni Mgiriama. Chama hiki kiliundwa kwa lengo la kutetea haki za Wamijikenda.


ronald%20ngala.jpg


Katika mwaka 1963, Ronald Ngala alianzisha chama cha kisiasa kilichoitwa ''KADU'' (KENYA AFRICAN DEMOCRATIC UNION) na yeye ndie aliekuwa kiongozi wa chama hicho na Rais mstaafu wa Kenya Daniel Toroitich Arap Moi alikuwa naibu wake.

Mwaka huo huo kulifanyika makubaliano baina ya chama cha KADU na chama cha ''KANU'' (KENYA AFRICAN NATIONAL UNION) ambacho kilikuwa kikiongozwa na aliyekuwa Rais wa kwanza wa Kenya marehemu Mzee Jomo Kenyatta, walikubaliana kukifutilia mbali chama cha KADU ili kuunda chama kimoja cha KANU.

Ronald Ngala alikubali wito huu na alichaguliwa kuwa waziri katika serikali ya Kenya mpaka alipofariki mwaka 1982.
Katika upande wa uchumi Mijikenda wanategemea kilimo na kufuga wanyama.

Wanapanda mimea kama vile: Muhogo, Kunde, Mahindi na Viazi tamu ikiwemo na mimea mengine pia hufuga Ng'ombe, Kondoo na Mbuzi. Walifanya biashara na walikuwa Madalali katika biashara baina ya Waarabu na Wagalla kwani walikuwa wakizichukua ng'ombe kutoka kwa Wagalla na kuwauzia Waarabu ambao walikuwa na mafungamano ya kibiashara na Wabantu kupitia Pwani ya Kenya.

Wamijikenda walianzisha Soko Giriama sehemu iitwayo'' Birya''.
Katika mwaka 1858 Wamaasai walivamia sehemu za Wamijikenda na waliiba idadi kubwa ya ng'ombe kwasababu walikuwa wanaamini kwamba ng'ombe zote Duniani ni zao.

mijikenda2.jpg


Wamijikenda kwa sasa wanategemea kilimo cha Mahindi, Makaa ilhali wengine wanategemea biashara ya kuuza Pombe ya Mnazi.


Katika upande wa mavazi mwanamume huvaa nguo iliyotengenezwa kwa pamba inayoziba sehemu ya chini mpaka magotini iitwayo "Mfulo" na juu yake huvaa kipande cha nguo nyengine iitwayo ''Mkumbuu'' kisha huvaa nguo nyengine juu ya bega lake la kushoto iitwayo ''Yamba'' na juu ya bega lake la kushoto huweka fimbo yenye vichwa viwili inayomsaidia na shughuli zake zengine.

Mwanamke huvaa nguo ya kitamaduni iliyotengenezwa kwa pamba na huwa na miuzi mingi mizito iitwayo ''Hando'' na wanawake walioolewa hujifunga pambizoni mwa tumbo zao mkanda unaoitwa ''Magalia'' na juu ya shingo yake huvaa mkufu unaoitwa ''Ndale'' na kwenye miguu yake huvaa ''vikuku'' pamoja na kuvaa mapambo mengine yanayomfanya yeye kuwa tofauti na wenzake pia hujipaka wanja kenye macho yake na manukato kwenye mwili wake yaitwayo "Muranze".

Katika upande wa harusi jambo la kumchagua msichana huachiwa wazazi au Baba Mdogo ama Shangazi. Msichana huchaguliwa kutoka familia yenye kusifika na sifa ya kazi, uaminifu zikiwemo na sifa zengine njema.
Wakati wa kuposa mzazi wa kijana huandamana na baadhi ya watu katika familia pamoja na marafiki zake mpaka kwa wazazi wa binti anayehitajika kuposwa huku wamebeba chupa zilizojaa pombe ya mnazi na huitwa ''Kadzama''.

Wakifika nyumbani kwao husema maneno haya:''Namala mudzungu wa utsungu'' maana yake ni nimekuja nyumbani kwenu ili kumposa binti yenu kwaajili ya kijana wangu. Kama msichana hajaposwa Babake husema:''Mudzungu wa utsungu uhaha'' maana yake ni karibuni sana mnachokihitajia kipo.


Sacred-Mijikenda-Kaya-Forests-Kenya.jpg


Baba wa kijana hupeana pombe kwa Baba ya msichana ambaye humuita na kumuonyesha kama ishara kwamba wageni wamekuja kumposa.

Binti akiridhia, Babake hupeana ile pombe kwa Baba zake wadogo na Wajomba ili nao wanywe na kuonyesha kwamba wamekubali. Kisha Baba ya kijana humueleza mwanawe yote yaliyojiri na humtuma ili amwangalie msichana na kufahamiana nae huku wakisuhubiana na marafiki zao kwani hawaruhusiwi kukaa faragha kabla ya ndoa.

Baada ya mda wa wiki moja au mbili Baba ya kijana hurudi kwa mara ya pili ili kutoa Mahari yaitwayo ''Mahunda'' ambayo zamani ilikuwa ni ng'ombe au mbuzi tofauti na sasa.
 
umejitahidi kuelezea japo hujakidhi viwango stahiki,mimi ni mtanzania na ni mkaazi wa jiji la mombasa,nakaa north coast kisauni sunlight
 
Wacha aje atukosoe kma yuajua zaidi. Hivi kaka un'kaa bamburi au Mtwapa au Kikambala? Mimi mkaazi wa Kiembeni sio mbali na Mwembekuku mitaa ya Bamburi
 
....Nadharia nyengine ambayo ni ya wasemavyo wenyeji wa asili ya Mombasa ni kuwa jina hilo latokana na "Manpasa" hususan wazee hupaita Mambasa. Kuhusiana na usuli wa neno hilo kwa bahati mbaya sijafanikiwa kujua undani wake.

Kuhusu usuli wa majina mengine ya mji huu mkongwe ni kama ifwatavyo; Kongoweya ni jina linalotokamana na neno la Kiswahili "Kongoni"- yaani karibuni na hini ni kwa ajili ya ukarimu wa wenyeji wa mji huu kwa kukaribisha wageni. Gongwa nalo ni neno la kingozi (Kiswahili cha kwanza) kwa maana ya ukuta.

Kama ilivyokuwa katika miji ya pwani hapo kale yalizungukwa na kuta ndefu ambazo zilikuwa ni kinga dhidi ya mashambulizi kutoka kwa jamii zilokurubiana nazo. Kutokana na mapokezi ya mzee mmoja wa Mombasa (Ustadh Ahmad nassir Juma Bhalo) ni kuwa ukuta huo ulijengwa kwa ajili ya kuwazuwiya kabila moja iliyojulikana kwa jina la Warimba ambalo lilikuwa likila nyama za binadamu.
 
Aaah napajua hapo. Hebu nisaidie kukidhi viwango hivyo unazodai
 
Jina lengine ni Mvita, na hili limetokana na hali ya mji ulipokuwa nyakati hizo.
Jina lenyewe latokamana na neno "vita" kwa kuwa mji wenyewe ulikuwa hauwishi vita- vita vya kupambana na wageni kama vile Wareno na Waarabu wa Oman waliokuja kuwatawala wenyeji, vita vya wenyewe kwa wenyewe na vita vya wenyeji wa Mvita na majirani zao (kwa mfano vita baina ya watu wa Mvita na watu wa Amu na vita baina ya Wapate na Wamvita).

Inasemekana katika tarehe yake mji huu uliteketezwa moto zaidi ya mara tatu (Tizama; JUSTUS STRANDES, PORTUGUESE PERIOD IN EAST AFRICA, KENYA LITERATURE BUREAU 1960) Basi hali hiyo ya vita na moto mkali ndipo likazaliwa jina la Nyali Kuu, yaani miale mikubwa.

 
Baadhi ya majina haya yapatikana katika mashairi ya Yule Shaha wa Malenga wa zamanai wa Mombasa, Muyaka wa Muhaji aliyeishi baina ya mwaka wa 1776 na 1840 (Tizama; MOHAMED H ABDULAZIZ, MUYAKA:19TH CENTURY SWAHILI POPULAR POETRY, KENYA LITERATURE BUREAU 1979 ukurasa, 19).
Na katika shairi hilo Muyaka asema;

Kongowea ja mvumo, Mvita Mji wa Kale
Isokoma mititimo, na mayowe na kelele
Ni ya ngao na mafumo, na mata na panga kule
Wafileo walifile, mwoleza mfu nnani?

Gongwa ni mji muovu, viovu siukalile
Hupomosha wenye nguvu, wakawa kama wawele
Ikawatia kivumvu, nyoyo zikajaa tele
Wafileo walifile, mwoleza mfu nnani?

Gongwa la Mwana Mkisi*, Mvita mji wa ole
Ina waume watesi, kondo hawaiketele
Wenye ghamidha na kasi, na hasira za milele
Wafileo walifile, mwoleza mfu nnani?

Kwamba mujile na kondo, kuteta na simba wale
Vumiliani vishindo, vyao msivikimbile
Simba wanayo magando, makucha wayatanule
Wafileo walifile, mwoleza mfu nnani?

Ndiswi Nyali Kuu ndiswi, ndiswi msambe tufile
Ndiswi mwapigana naswi, naswi msitutawale
Ni swiswi nguli ni swiswi, tuvundao miji mile
Wafileo walifile, mwoleza mfu nnani?

Kivumbi cha Kongowea, kivumapo ni ja ndwele
Walo mbali husikia, kingurumo chenda kule
Watambaji hutambia, kwa mwendo wa pole pole
Wafileo walifile, mwoleza mfu nnani?
 
Ambayo maana yake kwa Kiingereza ni:

Kongowea (Mombasa) is like a roaring surf; Mvita is a city of old
It is always seething (with trouble), with so much noise and endless cries
It is a place full of shields, lances, bows and arrows, and long
swords
The dead are dead and gone! There is no feigning death (i.e. one
dies only once).

Gongwa (Mombasa) is a city full of malice (towards its enemy), so
bear no spite against it!
It thrusts down powerful ones and renders them as helpless as the sick
It shatters them and fills their hearts with sorrow
The dead...

Gongwa is the land of Mwana Mkisi*; Mvita, what an awesome
place it is!
It has warlike men who spoil for a fight
Men who are intransigent and obdurate, possessed of everlasting
fury
The dead....

If you (Omanis) have come seeking a war with our mighty lions
Then bear their clamorous wrath, and do not flee!
These lions have terrible claws that are already stretched out
The dead....

It is still we Mombasans, indeed it is. Do not think we are dead
It is us you are waging war against. We are fighting you so that
you may not rule over us
It is we demons who destroy yonder lands
The dead....

When Kongowea roars, it groans like someone suffering from a
terrible malady
Even those who are far away hear its rumblings
The warriors quietly take their positions and make their strategic
manoeuvres
The dead....
 
Masters Bamburi napajua ila kuna mambo ya pishori/ mchele kwa sana. Vischana vya kikuyu vya bara vimepotoa mji na kuleta usenge wa kinairobi. Mimi hupenda Samba Tudor, Pa pweza, Cheers Ya Wajerumani, Sheba na Tapas.
 
Wabongo wengi sana Mombasa ila wakija wanajikakamua sana hadi wanageuza lafudhi na kuongea kiMombasa ili wasijulikane. wengi haramia tu. Yaani wanabidii sana hata ile 'la - ra' inayowasumbua kila siku wanafanikiwa kuing'oa.

WaTanga, WaPemba na WaUnguja hawana neno kwa sababu lafudhi zao nzuri tu kama ya Kimvita au Jomvu. Wachagga nao wakija wanasema wantoka Taveta au taita. Wachagga wengi mno huku. :becky:
 
Peleka UAMSHO Zanzibari weye.
Pwani n Kenya ila Wapwani tuna matatizo makubwa ya kubaguliwa na serikali ya Kenya.

Tukiwa huru kama Pwani lazma Mwarabu akae chini la sivyo au anaweza geuza hali iwe kama enzi za kisultani wa zanzibari.
Kama twapata uhuru kama PWANI lazima ni mMIJIKENDA ndo awe JUU.

Hawa ndu'zetu Waswahili wameingizwa Uarabu hadi wakasahau asili yao .
Waswahili ( Kitambo wakiitwa Wangozi) ni mojawapo ya makabila ya Wa Midzi-Chenda.
Mswahili ni M'mtsi Kaya lakini saa hizi anajifanya Mwarabu. Hehehhehehe

Muone Joho gavana Mkauma asili siku hizi utadhani ni Mwarabu Manga toka Masqat Omani.
Bedzimba mbunge wetu harusi ya mwanae waweza dhani infanyika Sur au Salalah Omani kwa vile wanavovaa
 
Haya nimalize nadharia
...Mwana mkisi (Balqis) ni isimu ya aliyekuwa mtawala wa kale wa Mombasa, alikuwa mwanamke. Katika historia ya
Pwani ya Afrika ya Mashariki, kuna vipindi fulani ambapo utawala ulikua chini ya wanawake. Kwa mfano, Gongwa (Mombasa) kulikuwa na Mwana Mkisi (Balqis), Siu (kisiwa kilichoko kaskazini mwa

Pwani ya Kenya) kulikuwa na Mwana Musura, Unguja kulikuwa na

Mwana Aziza, Vumba kulikuwa na Mwana Shambi Shali, na kadhalika.
 
Peleka UAMSHO Zanzibari weye.
Pwani n Kenya ila Wapwani tuna matatizo makubwa ya kubaguliwa na serikali ya Kenya.
Tukiwa huru kama Pwani lazma Mwarabu akae chini la sivyo au anaweza geuza hali iwe kama enzi za kisultani wa zanzibari.
Kama twapata uhuru kama PWANI lazima ni mMIJIKENDA ndo awe JUU.
Hawa ndu'zetu Waswahili wameingizwa Uarabu hadi wakasahau asili yao .
Waswahili ( Kitambo wakiitwa Wangozi) ni mojawapo ya makabila ya Wa Midzi-Chenda.
Mswahili ni M'mtsi Kaya lakini saa hizi anajifanya Mwarabu. Hehehhehehe
Muone Joho gavana Mkauma asili siku hizi utadhani ni Mwarabu Manga toka Masqat Omani.
Bedzimba mbunge wetu harusi ya mwanae waweza dhani infanyika Sur au Salalah Omani kwa vile wanavovaa

Kwa nini Wamijikenda wawe juu?
 
Back
Top Bottom