Historia ya Kanisa Katoliki Tanzania

bagamoyo

JF-Expert Member
Jan 14, 2010
21,287
24,162
HISTORIA YA KANISA KATOLIKI TANZANIA

Jubilei ya Miaka 150 ya uinjilishaji Tanzania: Furaha ya Injili
Jubilei ya Miaka 150 ya uinjilishaji Tanzania: Furaha ya Injili
KANISA

Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania: Furaha ya Injili​

Kanisa lililo hai ni lile, linalojiweza katika uinjilishaji, utawala na kujitegemeza. Kanisa la Tanzania limepiga hatua kubwa sana katika mambo mawili ya kwanza na pole pole linaanza kijitegemea katika shughuli zake za uinjilishaji. Wamisonari na baadaye Mt. Papa Yohane XXIII tulipoupata uhuru mwaka 1961 alilikabidhi taifa letu kwa Mama Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili.

Na Askofu Method Kilaini - Bagamoyo​

Utangulizi:

Madhumuni ya kanisa ni kujenga ufalme wa Mungu. Hivyo jubilei ya miaka 150 ni kuadhimisha jinsi gani kanisa limeweza kujenga ufalme wa Mungu katika Tanzania. Kuona jinsi gani Neno la Mungu ambalo liko kamili na takatifu limepandikizwa katika ulimwengu ya binadamu hususan hapa Tanzania, kwa kutumia binadamu ambao wana mapungufu yao. Uinjilishaji ni kumwongoa binadamu mzima roho na mwili.

Katika kutazama tunachofurahia tutafakari pamoja juu ya historia ya uenezaji wa Habari Njema. Tuonyeshe mchango kutoka kwa wamisionari, mapadre na watawa wazawa, makatekista na watu wote kwa ujumla. Nafasi ya walei na ukomavu wake katika historia ya kanisa, maisha ya ibada, mchango wa kanisa katika ustawi wa watu. Kanisa kama sauti ya kinabii katika ulimwengu. Katika miaka 150 kanisa limepitia katika changamoto na majaribu mengi. Siyo kila mara mambo yalikwenda mteremko lakini kanisa kila mara lilijifunga na kuamka bila kukata tamaa.

Kanisa linaweka mizizi: Shirika la Roho Mtakatifu
Ingawa Fr. Fava kutoka Reunion aliingia Zanzibar mwaka 1860 na pole pole misioni ikaanza humo viziwani na baadaye kuwatuma wamiaionari mwaka 1863, ni ukweli kwamba hicho kisiwa kilikuwa mapitio, kanisa lake halikuweza kushika mizizi imara. Tunaongelea juu ya Zanzibar kama sehemu ya matayarisho ingelikuwa shule tungeliita ya awali kabla ya daraza la kwanza. Baada ya kazi kubwa hadi leo Wakatoliki hawafikii 1% ya wakazi wa Zanzibar ni kama 10,00 tu. Zanzibar inatufundisha ustahimilivu na ushuhuda. Wamisionari hawakutingisha kiberiti bali walitunza uhusiano wao mzuri na sultani na wenyeji wao, Waislamu.

Historia yetu inaanza tarehe 4 Machi 1868, kwa ruhusa na msaada wa Sultani Seyyid Majid wa Zanzibar, wamisionari wa shirika la Roho Mtakatifu, wakiongozwa na Padre Antoine Horner akiwa na Padre Ettien Baur, walizindua misioni ya Bagamoyo. Hali ya Bagamoyo haikuwa tofauti na Zanzibar ila pale walipata ardhi ya kutosha na ilikuwa rahisi kupanuka nje ya mji. Mji ulikuwa na utamaduni wa Kiarabu na Kiislamu na wenye kituo kikubwa cha biashara ya utumwa. Wamisionari walitumia fursa wakawakomboa watumwa na kutengeneza kijiji cha wahuru. Kijiji cha watumwa huru kiliunda kundi la vijana ambao utambulisho wao ulikuwa ukristu wao. Vijana waliokombolewa walipata hadhi na motisha pamoja na kujiamini kutoka kwa wamisionari kwa sababu hawakuwa na ukoo mwingine. Hili lilikuwa jeshi lililoshirikiana na wamisionari katika uinjilishaji katika kanda nzima ya mashariki na kaskazini. Hapo Bagamoyo waliwapata masista Mabinti wa Maria wa Mtakatifu Denis kutoka reunon waliowasaidia kutunza na kuelemisha watoto, kusaidia wagonjwa na wanawake. Misioni yoyote ile isipokuwa na watenda kazi wa jinsia zote mbili haifanikiwi hata kidogo. Walijifunza lugha ya Kiswahili, tamaduni mbali mbali za watu, wakatayarisha na mazao mbali mbali ikiwemo kahawa.

Wamisionari walipoimarika walitembelea makabila mbali mbali wakiwemo Wazigua, Wadoe, Wakami, Wanguru na Wasagara wakitafuta pa kupanulia. Mwaka 1877 walifungua Mhonda na misioni nyingine Morogoro zikiwemo Mandera (1881), Morogoro (1882), Tunuguo (1884), Ilonga (1885), Matombo (1892). Mwaka 1890, 14 Agosti wakipitia Mombasa walifika chini ya Mlima Kilimanjaro na kufungua misioni za Kilema, Kibosho (1895) na Rombo Mkuu (1898). Kutoka kilema imani ileenea sehemu zote za kaskazini, Tanga (1983), Kondoa Irangi (1907), Kuryo (1908), Kilomeni Same (1909), mwanzoni Arusha ilishindikana hadi mwaka 1926.

Shirika la Wamisionari wa Afrika (Mapadre Weupe)
Mwaka 1878 walifika wamisionari wa Afrika kutoka Algiers, wakitumwa na Kardinali Lavigerie. Hao walikuwa wamepewa sehemu yote ya magharibi mwa Tanzania, Rwanda, Burundi, Uganda na Kongo. Baada ya kufanya maandalizi Zanzibar na Bagamoyo wakisaidiwa na wamisionari wa Roho Mtakatifu walielekea Tabora kwa taabu nyingi hata mmojawapo alifariki njiani karibu na Dodoma. Tabora kundi moja likaelekea magharibi na kusini na lingine likaelekea kaskazini ziwa Nyanza na Uganda. Kundi la magharibi baada ya kushidwa Ujiji walikouawa mapadre wawili na mmisionari mlei, mwaka 1884 liliweka makao yake Karema ukingoni mwa ziwa Tanganyika. Hii ilikuwa kama ngome ya kujikinga na wafanyabiashara ya watumwa. Tokea Karema injili ilienea kwa kasi kati ya wafipa kwa ushirikiano na watemi wao, Kapufi wa Kirando (188), Kala (1892), Mwaka 1897 mtemi Mwene Kapere, akiwa na miaka 18, aliwapokea Zimba katika bonde la Rukwa, na kufadhilia sana wamisionari. Zilifuata misioni nyingine. Mwaka 1903 ilifunguliwa misioni ya Urwira karibu na Mpanda, Kate 1906; Chala 1912, Mwambani (1901) Mbeya na Kigoma mwaka 1914.

Unyamwezi ikiwa na wafanyabiashara chini ya chifu Mirambo haikuwa rahisi kupenya na hivyo kwa muda mrefu ilikuwa sehemu ya mapito tu. Mwaka 1891 kwa msaada wa mtemi Ndega walifungua misioni ya Ushirombo, mama wa uinjilishaji Unyanyemmbe. Baadaye zilifuata Ngaya (1893), Ndala (1896) kwa mtemi Ntabo, Tabota 1900 na Itaga (1914). Kipalapala tangu mwaka 1882 ilikuwa inasuasua hadi mwaka 1945 ilipoimarika. Wamisionari wa Afrika waliokwenda kaskazini mwanzoni walivuka na kwenda Buganda na upande wa Tanzania ilikuwa sehemu ya mapito tu na kimbilio walipopata shida. Misioni ya kwanza ya kudumu Tanzania ilikuwa Bukumbi (1883) kwa Mtemi Kiganga. Kutokea Bukumbi walifungua misioni za Kagunguli (1895) na Murutunguru (1909) huko visiwani Ukerewe; Kome huko Geita (1900); Nyegezi na Sumve (1911) Mwanza, na Nyegina Musoma (1911). Misioni na kituo cha pili ilikuwa Kashozi (1892) huko Bukoba iliyofungua misioni za Katoke (1897) huko Biharamulo; Kagondo (1904) Rubya (1904), Mugana (1904) na Bunena (1910) zote zikiwa Bukoba.

Wabenediktini wa Mt. Otillien

Kundi la tatu la wamisionari walikuwa Wabenediktini wa Mtakatifu Otilien kutoka Ujerumani. Hawa walifika baada ya serikali ya Ugerumani kuanza kutawala ambayo sasa ni Tanzania, Rwanda na Burundi. Kuwa taifa moja na watawala iliwapa shida kwa sababu watu waliwachanganya na watawala wakoloni. Misioni yao ya kwanza ilikuwa Pugu mwaka 1888 nje ya mji ili wawe mbali na wakoloni. Monasteri ilianza na wamisionari 14 wakiwemo padre, frateli, mabruda na masista wakiongozwa na padre Boniface.
Wabenediktini walipata majaribu makubwa licha ya wamisionari kufa wakiwa vijana kwa sababu ya maradhi mbali mbali hasa malaria kama mashirika mengine walishambuliwa mara kadhaa na kuuawa. Majaribu makubwa ya Wabenediktini Pugu yalikuwa tarehe 13 Januari 1889. Siku hiyo ya Jumapili wamisionari walishambuliwa na watu kama 150 wa jeshi la Bushiri waipiga risasi ovyo ovyo. walimwua Bruda Petro Michael hapo hapo Bruda Benedikti alikimbilia kanisani akipita katika mapigo ya risasi akafungua tabernakulo na kumeza sakramenti ya Ekatisti yote na akafuatwa akapigwa risasi na kufa hapo hapo mbele ya tabernakulo. Sr Marta Waising aliyemfuata kanisani naye alipigwa risasi na kufa. Pamoja naye waliwaua watoto wachanga wawili chini ya miaka miwili waliokuwa wanawatunza.

Misioni ilikuwa na watoto zaidi ya 40 wenye umri kati ya 6 na 12 nao walikimbia ovyo bila msaada au ulinzi. Wamisionari wengine wanne walishikwa na kufungwa kamba wakiwa wamejaa damu kwa sababu ya kukatwa kwa mapanga, kuchomwa visu na wengine kupigwa risasi. Nyumba na vitu vyote vilichomwa moto. Waliotekwa walikombolewa siyo kwa msaada wa wakoloni Wajerumani bali kwa nguvu na juhudi kubwa ya Padre Stefan Baur wa shirika la Roho Mtakatifu. Wawili tu, Bruda Joseph na Bruda Fridolin waliweza kukimbia na kujificha siku tatu porini wakitembea usiku hadi walipofika pwani.

Vita vilipotulia kidogo maaskari Wajerumani walikwenda Pugu wakakusanya mifupa ya mashahidi na kuiweka katika sanduku na kuizika katika kaburi moja karibu na makaburi ya ndugu zao waliowatangulia bruda Wendelin na sista Lioba. Hawa ndio walikuwa mashahidi wa kwanza Wabenediktini, mashahidi wa Pugu. Miili yao ilichomwa pamoja na nyumba zao. Damu yao ndiyo mbegu ya imani Dar es Salaam na kusini yote ya Tanzania. Kwa miaka mingi Pugu ilifungwa na kubaki mahame. Kama alivyoandika mkuu wa misioni, Padre Bonifas: “Bwana alitoa na Bwana alichukua kwani tukikumbuka yote tuliyofanya pale tunatokwa machozi. Tulishajenga majengo mengi, tulikuwa na watoto na watu wazima na sasa hatutawaona tena. Yote tuyatoe kwa Mungu”. Baada ya hapo ilibidi wale waliobaki warudi nyumbani Ujerumani.

Desemba 1889 padre Boniface na mabruda walionusurika walirudi na mara hii wakanunua nyumba chakavu kwa rupia 10,500 mjini Dar es Salaam. Walipata na mashamba Kurasini, Mbagala na Msimbazi. Chini ya usimamizi wa Padre Maurus Hartman mwaka 1894 alifungua misioni za Lindi na Lukuledi; 19896 Nyangao mkoa wa mtwara; mwaka 1897 Tosamaganga na Madibira huko Iringa; mwaka 1898 Peramiho na Kisongera huko Songea; na mwaka 1902 Kwiro huko Mahenge.
Mwaka 1905 Wabenediktini walipata mkasa wa pili. Askofu wa kwanza wa vikariati ya Dar es Salaam, Askofu Cassian Spiess aliyewekwa wakfu mwaka 1902, akijiamini alisafiri kuelekea Peramiho wakati wa Vita vya Maji Maji (1905 -) aliuawa pale Mikuyumbu karibu na Liwale pamoja na masista wawili na mabruda wawili; Bruda Fransiscus akiwa Peramiho na Sr. Walburga akiwa Nyangao waliuawa. Misioni zote nje ya Dar es Salaam isipokuwa Tosamaganga na Madibira kati ya Wahehe ambao hawakushiriki zilichomwa moto. Abate Mkuu Nobert ambaye wakati huo alikuwa Pereamiho na akatoroka kupitia Malawi na Msumbiji alipofika nyumbani aliandika “Msalaba huu uliotukuta ni mzito. Mchungaji amepigwa, kundi lake limechinjwa au kutawanyika. Kazi ya miaka mingi imeharibika. Sisi sote tuligundua uzito huo, lakini tumetulia tulipokumbuka kwamba ni Mungu aliyedai sadaka hii; heshima na utukufu viwe kwake. Lakini wala hatari wala kifo haviwezi kuvunja moyo au ushujaa wa maaskari wa Kristu. Kinyume chake, tutasema kwa furaha zaidi: ‘mimi nipo”. Damu hii ndiyo mbegu ya ukristu kati ya wangoni na kanda ya kusini.

Baada ya vita vya maji maji wale wamisionari walionusurika kama Padre Yohanes ambaye misioni yake ya Kigonsera ilichomwa naye akajificha kwa miezi mitatu, ndio waliowatetea watu dhidi ya ukatili wa Wagerumani waliokuwa wanalipiza kisasi kwa kuwanyonga na kuwafanya watu wafe kwa njaa. Wamisionari waliwahubiri na kuwabatiza wengi wa watemi waliowaua wenzao na kuwabatiza kabla hawajanyongwa. Walijenga upya misioni zilizochomwa na dini iliimarika tena katika misioni zote. Hapa tunaadhimisha katika miaka 150 ya Uinjilishaji ushupavu, uvumilivu na imani ya hawa wamisionari wa kwanza ambao bila kujia lugha au watu walifika na kutuletea tunu waliokuwa nayo. Wengi wao walikufa wakiwa na umri mdogo sana lakini hili halikuwakatisha tamaa kadiri walivyokufa ndivyo na wengine walikuja kushika nafasi zao. Hata walipouawa kama mashahidi i bado wenzao walijaa imani na kuja. Kwa maneno ya Sr. Marta alipotumwa Afrika baada ya mashahidi wa Pugu aliandika hivi, “Kwa furaha na ujasiri navaa ukanda mwekundu unaonikumbusha daima ili niwe tayari kumwaga damu yangu kwa ajili ya imani takatifu.” Hili ndilo tunaloadhimisha tukimsifu na kumtukuza Mungu kwa zawadi hii ya waminsionari shupavu.

Vita Vikuu ya Kwanza ya Dunia.
Wakati wa Vita Vikuu vya Kwanza mwaka 1914 – 18;
Sehemu ya Shirika la Roho Mtakatifu, licha ya Zanzibar ambayo wakati huo ilikuwa imeuganushwa na Kenya wote wakiwa chini ya Waigereza; katika Tanganyika ilikuwa na vikariati mbili ile ya Bagamoyo na Vikariati ya Kilimanjaro. Sehemu ya Uinjilishaji wa Wamisionari wa Afrika ilikuwa na vikariati tatu’ Vikariati ya Tanganyika; Vikariati ya Unyanyembe na Vikariati ya Nyanza Kusini kabla ya Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia mwaka 1913. Kwa mfano Vikariati ya Nyanza ya Kusini ilikuwa na misioni 12, zikiwa Mwanza na Bukumbi, katika Jimbo Kuu la sasa la Mwanza, Kome katika Jimbo la Geita, na Ukerewe katika Jimbo la Bunda, Katoke katika jimbo la Rulenge-Ngara, Kashozi, Mugana, Kagondo, Rubya na Bukoba katika jimbo la Bukoba na Nyegina katika jimbo la Musoma. Walikuwa na wamisionari 51, masista 14 na makatekista 117. Waamini walikuwa 10,244 na wakatekumeni 7,406. Shule zilikuwa 97 zenye wanafunzi 2,010 na kati yao 688 wakiwa wasichana. Taasisi za hospitali, zahanati, nyumba za wenye ukoma na watoto yatima zilikuwa 20.

Sehemu ya Wabenediktini ilikuwa va sehemu mbili Vikariati ya Dar es Salaam na Unyampara wa Lindi. Vikariati ya Dar es Salaam ilikuwa na vituo vya misioni 11: Dar es Salaam, Kurasini, Tosamaganga, Madiba, Kwiro, Ifakara, kipatimu, Bihawana, Sali, Sangi na Mchombe zikiwa na waamini 5536 na mashule 261. Unyampara wa Lindi ambao sasa majimbo ya sasa ya Lindi, Songea, Mbinga, Tunduru - Masasi, Njombe na Mtwara. Sehemu hii wakati huo ilikuwa na vituo vya misioni sita: Lukuledi (1895), Nyangao (1896), Peramiho (1898), Kigonsera (1899), Ndanda (1906) na Namupa (1909), vyenye waamini 6,873 na mashule 143. Makao makuu yalikuwa Namupa. Vita Vikuu vya Kwanza ilivuruga uinjilishaji kwa sababu wamisionari wote Wajerumani walikamatwa na kurudishwa nyumbani. Walioathirika kuliko wote ni Wabenediktini kwa sababu karibu wote walikuwa Wajerumani.

Hata hivyo vita hivi vilikuwa mtihani wa kuona jinsi gani walikuwa wamepanda mbegu nzuri na iliyokubaliwa. Ili kusaidia Roma mwaka 1917 iliwaomba Wamisionari wa Afrika wasaidie katika sehemu hii iliyoachwa na wabenediktini. Ilimteua Padre Joseph Laane, Mholanzi wa shirika la Wamisionari wa Afrika (Mapadre weupe) asimamie Vikariati ya Dar es salaam na Unyampaara wa Lindi. Alisaidiwa na mapadre 12 na bruda mmoja ambao walikuwa wachache mno kushika nafasi ya wamisionari zaidi ya 150. Lakini katika kipindi hicho imani ilibaki na hata kupanuka ikisimamiwa na makatekista.

Ni makatekista hawa walioendeleza uhai wa kanisa bila uhusiano wowote na mapadre au posho yo yote, walifundisha watoto na wakatekumeni na hata kutafuta wapya, walibatiza katika saa ya kufa, na kutunza mali ya kanisa. Maarufu kati yao ni Kostantini Yakobo Akitanda akiwa Matiri, Pauli Mlevi na Patro Ndunguru wa Litembo, Ambrose Ngombale wa Kipatimu, Joseph Ismail wa Chikundi, Paulo Yosef Holola wa Lupaso, Kassian Homahoma wa Litui kutaja wachache. Vile vile akina mama walijitolea na kujaza nafasi za masista katika kuwalea yatima, kutunza wakoma na kuwatunza wagonjwa. Vile vile katika sehemu nyingine. Watumwa huru waliofundishwa hapo Bagamoyo walifanya kazi kubwa kuziba mianya Vikariati za Bagamoyo na Kilimanjaro. Kule Kilimanjaro masista wengi walirudishwa nyumbani lakini wasichana waliotaka kuwa masista na walikuwa wakiishi nao walishika nafasi zao na kazi ikaendelea hadi wamisionari waliporudi. Hawa ndio baadaye walianzisha shirika la masista wa Mama Wetu wa Kilimanjaro. Kanisa lilijaribiwa na kubaki imara

Uinjilishaji baada ya Vita Vikuu vya kwanza ya Dunia: Utajiri wa Kanisa Katoliki ni kwamba ni Moja na Takatifu. Hakuna shirika lenye ukiritimba katika uinjlishaji bali ni kushirikiana. Baada ya Vita Vikuu vya Kwanza mashirika mengine yaliingilia kati kusaidia kujaza mapengo. Hili lilileta uhai mpya katika kanisa.

Shirika la Wakapuchuni wa Uswiss
Kwa sababu ya hali ngumu katika Vikariati ya Dar es Salaam baada ya Wamisionari Wabenediktini Wajerumani kurudishwa nyumbani, mwaka 1920 Roma shirika la Wakapuchni provinsi ya Uswiss kusimamia sehemu hiyo. Wakapuchini walifika mwaka 1921 wakiwa na masista wa shirika la ‘Divine Providence’ la Baldegg Uswiss. Waliongozwa na Padre Gabriel Zelger (1921-1929) ambaye mwaka 1923 alipewa daraja la uaskofu. Hii ilichukua sehemu ambayo sasa ni Jimbo Kuu la Dar es salaam, jimbo la Mahenge na jimbo la Ifakara.

Shirika la Wamisionari wa Consolata:

Askofu Spreiter alipofukuzwa nchini alimwomba Askofu Fillipo Perlo waVikariati ya Wakonsolata wa Kenya atume wamisionari kusaidia Tanzania. Shirila la Wakonsolata: Shirika la Wakonsolata lilianzishwa na Menye Heri Joseph Allamano, mwaka 1901 kule Torino Italia. Waliposhindwa kwenda kwa Wagalla Ethiopia walianzisha missioni Kenya. Mwaka 1919 wamisionari wanne walifika kushika misioni za Tosamaganga na Madibira. Mwaka 1922 Sehemu ya Iringa ilikabidhiwa rasmi na Roma kwa Shirika la Wakonsolata chini ya Mons. Francesco Cagliero (1922-35) makao makuu yakiwa Tosamaganga. Kama unyampara wa kitume ikiwa na sehemu ya Uhehe yenye misioni ya Tosamaganga; Usangu yenye misioni ya Madibira; Ugogo yenye misioni ya Bihawana na Pandangani; Ulanga na Masagati yenye vituo vya Mchombe, Merere na Sangi na vile vile Ubena na Ukinga ilikuwa bado bila misioni.Unyampara ulipandishwa kuwaVikariati mwaka 1948 na Mons Atillio Bertramino (1936 - 1965) alipewa uaskofu. Mwaka 1963 alihamishia makao ya jimbo Kihesa, Iringa mjini.

Shirika la Wapasionisti:

Mwaka 1935 uliundwa unyampara wa Dodoma ukichukua sehemu ya Kusini toka Iringa, sehemu ya Mashariki na ya kati kutoka Bagamoyo na sehemu ya Kaskazini kutoka Kilimanjaro. Hii sehemu ilipewa wamissionari Wapassionisti kutoka Italia.Unyampala wa dodoma ulipandishwa na kuwaVikariati mwaka 1951 na kuwa jimbo mwaka 1953 chini ya Askofu Antony Pesce wa shirika hilo la Wapasionisti.

Shirika la Wapalotini

Shirika la Wapalotini walioanzishwa na Padre Vicent Mary Palotti mwaka 1835 walianza kazi katika Unyampala wa Mbulu mwaka 1943. Sehemu kubwa ya unyampara wa Mbulu ilikatwa kutokaVikariati ya Tabora na sehemu ya mashariki ilikatwa kutokaVikariati ya Kilimanjaro. Mwaka 1954 unyampara wa Mbulu ulipandishwa cheo na kuwa jimbo chini ya Askofu Patrick Joseph Winters wa shirika la Wapallotini.

Shirika la Warosimiani:

Shirika la Warosimiani kutoka Ireland lilipewa unyampara wa Tanga uliokatwa kutoka Vikariati ya Kilimanjaro mwaka 1950. Mwaka 1958 ulipandishwa cheo na kuwa jimbo chini ya Askofu Eugene Arthurs wa shirika hilo la Warosimiani.

Shirika la Wamaryknoll:

Mwaka 1946 Roma iliundaVikariati ya Musoma – Maswa ikikata Musoma kutokaVikariati ya mwanza na Shinyanga kutokaVikariati ya Tabora. Mwaka 1950 Vikariati hii walipewa shirika la Wamaryknoll kutoka Marekani. Mwaka huo Musoma na Maswa zilitengwa na kuwa naVikariati ya Maswa na unyampara wa Musoma.Vikariati ya Maswa mwaka 1956 ilipandishwa na kugeuzwa jina kuwa jimbo la Shinyanga chini ya Askofu Edward Aloysius McGurkin Mmarekani wa shirika la Wamaryknoll. Unyampara wa Musoma ulipandishwa cheo na kuwa jimbo la Musoma chini ya Askofu John Rudin naye Mmarekani wa shirila la Maryknoll.

Shirika la Wasalvatoriani

Shirika la Wasalvatoriani lilikuwa shirika la mwisho la kimisionari kupewa jimbo nchini Tanzania. Mwaka 1963 Roma ilikata sehemu kutoka Abasia Nullius ya Ndanda na kuunda jimbo la Nachingwea chini ya Askofu Mmarekani Arnold Cotey (1963-1984) ambalo sasa ni Jimbo la Tunduru Masasi. Baada ya hapo majimbo mapya yalipewa maaskofu wazawa na siyo tena shirika inagawa baadhi ya maaskofu wazawa walikuwa wanashirika.

Kanisa na Ustawi wa Jamaii

Toka mwanzo uinjilishaji uliendana na hudma za jamii kwa namna ya pekee Elimu na afya. Hadi leo kanisa limejikita katika kumhudumia binadami roho na mwili. Hili lilifanywa na mashirika yote. Huduma ya Elimu: Shirika la Roho Mtakatifu walipowakomboa watumwa jambo la kwanza walilolifanya lilikuwa kuwapa elimu dunia sambamba na elimu dini. Wamisionari wa Afrika kwa mfano askofu Hirth wa Vikariati ya Nyanza (kanda ya Ziwa Viktoria) aliamuru kwamba kila mkatekumeni chini ya umri wa miaka 40 asibatizwe kama hajajua kusoma na kuandika. Wabenediktina katika miaka yao 15 ya kwanza walikuwa na shule 32 zenye wanafunzi 914. Kabla ya Vita Vikuu vya kwanza mwaka 1913 misioni zote Tanzania bara zilikuwa na jumla ya wanafunzi 114,651.

Katika kipindi cha ukoloni wa Waingereza kulikuwepo ushirikiano mzuri na kanisa katika nyanja ya elimu. Papa Pio XI, Papa aliyependa sana misioni, alimtuma mjumbe wake Askofu Mkuu Arthur Hinsley kuwasisitizia maaskofu wakazanie kutoa elimu. Ikiwa wanapashwa kuchagua kujenga kanisa au shule wachague shule. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ushirikiano wake ulianzia katika sekta ya elimu. Mwaka 1958 Padre Joseph Sipendi alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Elimu kuwawakilisha maaskofu wote kwa serikali. Katika kipindi hiki hadi uhuru mafanikio yalikuwa makubwa. Mwaka 1968 Kanisa likiadhimisha jubilei ya miaka 100 kabla shule hazijataifishwa kanisa la Tanzania lilikuwa na shule za msingi 1,378; shule za sekondari 44, Vyuo vya ualimu 8; vyuo vya ufundi 15 na maarifa ya nyumbani 48, nk.

Mwaka 1969/70 shule binafsi isipokuwa seminari zilitaifishwa. Kanisa liliondolewa katika elimu ya umma. Hili lilikuwa pigo kubwa sana kwa kanisa kwa sababu watoto na vijana ndio uhai wa kanisa. Hata hivyo kanisa halikukata tamaa. Bahati nzuri katika miaka ya 1980 serikali ilitambua kwamba peke yake haiwezi kukidhi mahitaji ya elimu na vile vile kiwango cha elimu kilikuwa kinashuka, hivyo ikaruhusu tena shule binafsi zikiwemo za mashirika ya dini. Kanisa bila kutazama nyuma ilijitupa tena katika kujenga na kuendesha mashule. Jimbo la Moshi lilikuwa mfano mkubwa katika hilo. Sasa hivi Kanisa Katoliki, katika ushirikiano kati ya majimbo na mashirika ya kitawa, linaendesha shule 56 za awali, 140 za msingi, 249 za sekondari, vyuo 6 vya ualimu na 51 vya ufundi. Kanisa lina Vyuo Vikuu 5 na Vyuo Vikuu vishiriki na Vituo 10. Mwaka 2013 Vyuo Vikuu vilikuwa na wanafunzi zaidi ya 20,000. Kama serikali itaruhusu na kuunga mkono kanisa liko tayari kupanua huduma hii kwa manufaa ya Watanzania.

Huduma ya Afya

Kama katika nyanja ya elimu kanisa katoliki lilitoa huduma ya afya toka mwanzo. Wamisionari walianza na vituo vya dawa katika misioni na pole pole hasa walipofika masista wakajenga zahanati na baadhi zikakua na kuwa hospitali. Serikali ya kikoloni haikuweka nguvu nyingi katika kutoa matibabu kwa watu na vile vile haikutoa msaada wowote kwa mashirika ya dini yaliyokuwa yanatoa huduma hiyo. Karibu huduma zote za matibabu vijijini ziliendeshwa na mashirika ya dini Kanisa Katoliki likiwa msitari wa mbele. Karibu kila shirika la watawa pamoja na mambo mengine lilijihusisha na huduma ya matibabu.
Kwa mfano wakati Kanisa linaadhimisha miaka 100 ya uinjilishaji mwaka 1968 Kanisa lilikuwa na hospitali 25 za kawaida na 8 kwa ajili ya kifua kikuu, zahanati 75, kliniki kwa ajili ya uzazi 74 na shule 11 za kufundisha wahudumu wa afya. Kati ya wahudumu kulikuwa na madaktari 36 na wauguzi wa kada mbali mbali 466. Huduma za afya hazikutaifishwa na hata nyingine ziliteuliwa kutoa rasmi huduma za serikali katika wilaya ambako hakuna hospitali ya serikali. Kufikia mwaka 1998 Kanisa lilikuwa na hospitali 36 ikiwemo hospitali ya rufaa ya Bugando na Vituo vya Afya na zahanati 223. Sasa hivi kuna hospitali kama 51 ikiwemo hospitali ya rufaa ya Bugando, Vituo vya afya 78 na zahanati 280. Huu ni mchango mkubwa sana wa kanisa katika huduma za jamii.

Wahudumu wazawa: Makatekista:
Wamisionari walifanya kazi kubwa saba lakini wasingelifanikiwa bila wahudumu wazawa. Tuliona Bagamoyo watumwa huru wenye uwezo walivyofundishwa vizuri na kuwa walimu na makatekista katika misioni mbali mbali. Walisindikiza na kusaida sana wamisionari wa Shirika la roho Mtakatifu kila walipoanzisha misioni mpya katika miaka ya kwanza hadi walipowapata makateskista mahalia. Wamisionari wa Afrika katika vikariati ya Nyanza walisaidiwa mwanzoni na makateklista waliotoka nao Uganda, wale wenza wa mashahidi wa Uganda kuinjilisha na kufundisha. Karema na Tabora mwanzoni kuna watumwa huru kutoka Malta kama Dr. Atman waliowasaidia sana. Kusini tumewaona makatekista shujaa waliowaficha wamisioanri wakati wa vita vya maji maji na vile vile kuendeleza imani baada ya Vita Vikuu vya kwanza wamisionari walipofukuzwa. Hadi leo makatekista ni wainjilishaji wenza wa mapadre na nafasi yao haiwezi kusifiwa vya kutosha.

Mapadre wazawa
Mashirika yote anzilishi yalijaribu kwa namma yao kupata mapadre wazawa. Siyo kila mara waliamini kwamba itawezekana kwa muda mfupi. Mmisionari shupavu kwa hilo kati ya wote ni Askofu Hirth wa Vikariati ya Nyanza Kusini (1894 – 912) ambaye aliwapenda na kuamini kwamba Waafrika wanaweza kuwa mapadre sawa na wazungu. Licha ya kupingwa na wamisionari wenzake alianzisha seminari Rubya Bukoba mwaka 1904 na mwaka 1917 akapata mapadre 4 wa kwanza Watanzania. Mapadre hawa na wale waiowafuata waifanya kazi nzuri sana ya kuigwa na hivyo kuonyesha uwezo wa Mwafrika siyo tu kama padre lakini katika nyanja zote. Mwaka jana tumiadhimisha hapo Dodoma kilele cha jubilei ya miaka 100 ya mapadre wa kwanza Tanzania. Kwa mfano wake, wamisionari wengine waliambiwa wajifunze kwake. Shirika la Roho Mtakatifu walimpata padre wao wa kwanza Alfonsi Mtana mwaka 1938 huko Moshi; Wabenediktini waliwapata mapadre wao wa kwanza mwaka 1943, Padre Gervas Ntara na Padre Simon Kapinga.
Tangu wakati huo juhudi nyingi zilifanywa kuwa na mapadre wazawa. Ni historia nzuri ya juhudi za mashirika ya kimisionari na baadaye ikaendelezwa na maaskofu wazawa kwa kuanzisha Seminari kubwa na ndogo kwa ajili ya kuwalea mapadre.

Mwaka 1967 sehemu kubwa ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania waliunganisha juhudi zao na kuunda Seminari kuu Moja yenye matawi matatu Kibosho Moshi na Ntungamo Bukoba kwa ajili ya Falsafa na Kipalapala kwa ajili ya Teologia. Kwa juhudi kubwa za Mwadhama laurean Kardinali Rugambwa mwaka 1984 iliongezwa Seminari Kuu ya nne ya Segerea Dar es Salaam kwa ajili ya Taalimungu. Kanda ya kusini ilibaki na Seminari ya Peramiho kwa ajili ya Falsafa na Taalimungu.

Licha ya Mapadre, Tanzania mwaka 1952 ilimpata Askofu wake wa kwanza mzalendo, Laurean Rugambwa wa vikariati ya Kagera ya Chini huko Bukoba ambayo baadaye ilipandishwa na kuwa Jimbo la Rutabo mwaka 1952. Pole pole majimbo yote yakashikwa na maaskofu wazawa la mwisho lilikuwa Arusha mwaka 1985. Mwaka 1960 Tanzania ilitunukiwa kumpata Kardinali wa kwanza Mwafrika, Laurean Kardinali Rugambwa wakati huo akiwa Bukoba na mwaka 1969 akahamishiwa Dar es Salaam. Sasa tunaye Kardinali wa pili Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na maaskofu wakuu 5. Sasa Kanisa la Tanzania lina mapadre wazawa wa jimbo zaidi ya 2, 000 bila kuhesabu mapadre wazawa walioingia mashirika mbali mbali ya kitawa. Na mwaka huu ni mwaka wa neema, Seminari zetu Kuu zimajaa na pamekosekana sehemu ya kupokea zaidi. Kule Ntungamo Seminari kumejaa na vijana wanalaa katika mabweni.

Mashirika ya Kitawa: Mashirika ya kimisionari

Wamisionari mwanzoni hawakutaka kuwaingiza wazawa katika mashirika yao. Yale yaliyojaribu palikuwepo hatari kwamba walipokuwa wanawalea mapadre wa jimbo wale wenye vipaji wangewashawishi waingie katika mashirika yao. Shirika la Roho Mtakatifu tayari mwaka 1973 liliwawapokea vijana 6 na kuwatuma Ufaransa ili wawe mabruda lakini hakuna aliyedumu. Mwaka 1950 walichagua wazuri kati ya mapadre wa jimbo, Padre Joseph Babu mwaka 1950, Padre Joseph Kilasara mwaka 1953; Padre Fransis Mketa mwaka 1956, Padre Bernard Ngaviliau mwaka 1957 na mseminari wa Moshi Josephat Msongore mwaka 1963. Mwaka 1971 walifungua nyumba ya malezi pale Usa River Arusha na sasa wana wanashirika wazawa 88 wakiwemo maaskofu wawili.

Wabenediktini badala ya kuwaingiza katika monasteri zao za Peramiho na Ndanda walianza monasteri tofauti ya Waafrika hapo Hanga ambayo imekua na kuzaa nyingine kule Mvimwa, Sumbawanga. Monasteri kongwe wazungu, Peramiho na Ndanda, kwa kukosa miito nyumbani sasa zinawapokea Waafrika na sasa Abate wa Ndanda ni Mtanzania. Wakapuchini sasa wanao mapadre 98 walio hai bila kuhesabu mabruda. Kwa sasa mashirika yote isipokuwa Wamaryknoll yanawapokea wazawa na ndiyo uhai wao. Mashirika ya kimisionari ya kike yalifuata mfano wa mashirika ya kiume na kuwapokea wanashirika wazawa. Mashirika yaliochelewa kuwapokea wazawa yana hali ngumu.

Mashirika ya Kike ya Jimbo

Wamisionari wa kike yalianza kukaa na wasichana walioyapenda maisha yao, lakini kihalisia walikuwa wanawake wacha Mungu bila mwelekeo maalum. Miaka ya mwanzo juhudi zilifanyika kuunda mashirika ya jimbo kutokana na hao wasichana lakini bila mafanikio. Askofu wa kwanza kufanikiwa alikuwa Askofu Lechaptois wa Vikariati ya Tanganyika (Sasa Sumbawanga) akisaidiwa na masista wawili wa Shirika la Mama Wetu wa Afrika, Sr. Philipa na Sr. Yakoba. Askofu alianza malezi mwaka 1903 na tarehe 3 Mei 1908 wasichana wawili waliweka nadhiri zao katika shirika la ‘Mtakatifu Petro Klaveri’ ambalo mwaka lilibadili jina na kuitwa “Shirika la Masista wa Mama Malkia wa Afrika”.
Mashirika mengine yalifuata baadaye: Shirika la Masista wa Mtakatifu Tereza wa Mtoto Yesu Bukoba (1933), Shirika la Masista wa Bibi Wetu wa Kilimanjaro (CDNK), Moshi (1934); Shirika la Mabinti wa Maria wa Tabora, (1935); Shirika la Masista wa Moyo Safi wa Maria (C.I.C.M), Morogoro (1938); Shirika la Masista Wabenediktini wa Mtakatifu Agnes wa Peramiho, Songea (1938); Shirika la Masista wa Upendo wa Mt. Fransisko wa Assisi, Mahenge, (1944); Shirika la Masista Wabenediktini wa Bikira Maria Msaada wa Wakristo, Ndanda, Mtwara (1946); Shirika la Masista wa Mama Yetu wa Usambara (COLU), Tanga (1956); Shirika la Masista wa Maria Malkia wa Mitume, Mbeya (1972), Mashirika mengine mengi yameanzishwa na yanaendelea kuanzishwa.
Mashirika ya Watawa Tanzania yaliunda umoja ambao sasa unaitwa TCAS. Mwaka 2015 walikuwa na mashirika wanachama 95 na kati yao mashirika ya kijimbo yalikuwa 40 na ya kimisionari 55 yote pamoja yakiwa na wanashirika zaidi ya 12,000. Tunaadhimsiha hili jeshi kubwa la kristu. Mabikira waliotoa maisha yao kujenga ufalme wa Mungu. Swali ni jinsi gani Kanisa linatumia jeshi hilo. Watawa wanaume wasiokuwa mapadre wengi wao wamo katika mashirika ya kimisionari yenye mchanganyiko wa mapadre na mabruda kama Wakapuchini, Wasalvatoriani, Wamisionari wa Afrika, Wabenedikitini nk. Mashirika ya jimbo kijumla hayakufanikiwa, machache yanayofanya vizuri ni Shirika la Moyo Mtakatifu wa Maria la Iringa.

Miundo Mbinu ya Utawala

Kuanzia mwaka 1956 Maaskofu waliunda Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kwa ajili ya ushirikiano. Kwa pamoja wanapanga na kuweka sera za uinjilishaji, utoaji huduma za jamii na uhusiano na serikali na mashirika ya ndani na nje. Wanamiliki kwa pamoja tasisi kubwa kama Vyuo Vikuu, Hospitali ya Rufaa ya Bugando na taasisi nyingine.

Mahusinao na dini mbali mbali

Tanzania kumekuwepo na amani kwa sababu madhehebu ya dini yamefanya juhudi kubwa kuleta mahusiano mazuri. Mfano mzuri wa mahusuiano mazuri kati ya madhehebu ya Kikristu ni Tume ya Kikristu ya Huduma za Jamii (CSSC) ambapo TEC na CCT kwa pamoja wanaratibu huduma za jamii zinazotolewa na taasisi zao hasa Elimu na Afya. Kanisa linashiriki kwa dhati katika mazungumzano na dini nyingine hasa wale wenye mapenzi mema. Mara nyingi madhehebu ya Kikristo chini ya TEC na CCT yameshirikiana na Waislamu kupitia BAKWATA kutatua matatizo mengi ya pamoja.

Maisha ya Kiroho

Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulifungua milango mingi kwa kanisa katika Afrika. Ulialika kanisa liishi kama familia na kulisaidia liweke mizizi katika tamaduni za kiafrika. Kanisa la Tanzania kama makanisa mengine ulimwenguni lilijaribu kutamadunisha ujumbe wa Kristu. Bahati nzuri Tanzania ina lugha ya pamoja Kiswahili na mambo yote yanayowezekana yametafsiriwa katika Kiswahili. Mwaka 1976 nchi za AMECEA zilipitisha Jumuiya Ndogo Ndogo za Kikristu kama kipaumbele katika kuwa kanisa. Hii imekuwa neema kwa kanisa la Afrika chini ya Sahara. Maadhimisho ya liturgia yanaendeshwa katika lugha ya Kiswahili. Zaidi ya hapo kanisa la Tanzania lina bado kazi kubwa ya kupandikiza mizizi ya habari njema katika maisha ya kila siku ya Mtanzania. Utamadunisho katika liturgia unapashwa kwenda na maisha ya kila siku ya Mkristu mwafrika na hili ni zaidi ya nyimbo za Kiswahili na watoto wa utamadunisho. Kwa kuitikia Mtaguso wa pili wa Vatican licha vyama vya kitume vinavyokoleza uinjilishaji na ucha Mungu, kanisa katika Tanzania liliunda Halmashauri ya Walei na kwayo kufanikiwa kuwapa walei nafasi yao katika uongozi wa kansia kuanzia Jumuiya ndogo Ndogo hadi taifa.

Tuna haki ya kuadhimisha

Kanisa la Tanzania lina haki ya kiadhimisha kwa sababu kwa kiasi limekomaa. Lina wafanyakazi ingawa hawatoshi wengi walitaonea wivu mzuri, mapadre wa jimbo zaidi ya 2,000, watawa wazalendo ni zaidi ya 600 na wa kutoka nje wengi; watawa Wazawa zaidi ya 10,000 katika masirika mbali mbali. Tanzania imegawanywa katika majimbo 34 chini ya metropolitan 6 na aslimia 29% ya wakazi wa Tanzania ni Wakatoliki. Kanisa lina hamasa kila kona na linaendelea kukua na kustawi. Kanisa lililoinjilishwa sasa vijana wetu mapadre na masista wako nchi za nje wakiinjilisha. Tunawatoa wamisionari katika nchi mbali mbali za ulimwengu hasa walio katika mashirika mbali mbali. Kanisa lililo hai ni lile, linalojiweza katika uinjilishaji, utawala na kujitegemeza. Kanisa la Tanzania limepiga hatua kubwa sana katika mambo mawili ya kwanza na pole pole linaanza kijitegemea katika shughuli zake za uinjilishaji. Wamisonari na baadaye Mt. Papa Yohane XXIII tulipoupata uhuru mwaka 1961 alilikabidhi taifa letu kwa Mama Maria mkingiwa Dhambi ya Asili. Tumwombe Mama yetu aendelee kutubeba tunapoadhimisha miaka 150 ya uinjilishaji.
Source : Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania: Furaha ya Injili - | Vatican News
 
Pamoja na hayo yooote!! RC Ya Papa walifanya biashara ya utumwa ni hatareeee!! ,,,,mie huwa naona aibu sana Mtu mweusi tii!! au kisasa coloured anakwenda kusali kwa yesu muuza watu!! hakika yesu mzungu haji ng'ooo!! mtasubirisana!

wkt wenzenu wanatwaliwa mbinguni nyie mtakuwa mnaupiga mwingi tuu!.......wkt wa kirudi Duniani kugawiwa maeneno ya kuishi milele!! ndo mtashangaa!! hawa wametoka wapi??
 
Nashukuru kwa historia nzuri lakini ukweli haukwepeki waislam ndio wana historia kubwa juu ya uhuru wa Tanganyika wakristo walikuwa vibaraka wa wakoloni hilo halikwepeki
 
Back
Top Bottom