Halisi
JF-Expert Member
- Jan 16, 2007
- 2,802
- 612
Pamoja na kukosewa kwa headline ya ajali ya helikopta, swali langu ni je, helikopta za jeshi zinakodishwa? Je, walikuwa watalii ama wageni wa jeshi/serikali? Niliwahi kumsikia KAtibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Blandina Nyoni, akisema, wageni wetu wamepata ajali ya helikopta lakini hawajafa. Je ni watalii ama wageni wa serikali? Lakini mbona kuna muongoza watalii na si ofisa wa serikali? Je, ni zile helikopta ambazo walizileta akina VITHLANI na mwenzake Tanil Somaiya wa kesi ya RADA?
Walionusurika ajali ya Helikopta ya jeshi watajwa
na David Frank, Arusha
Walionusurika ajali ya Helikopta ya jeshi watajwa
na David Frank, Arusha
MAJINA ya watu saba walionusurika kufa baada ya helikopta ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliyokuwa wakisafiria kuanguka, yamefahamika.
Helikopta hiyo ilianguka na kuwaka moto juzi kwenye Ziwa Natron mkoani Arusha.
Kamanda wa Polisi mkoani Arusha, Matei Basilio, alisema ajali hiyo mbaya ilitokea juzi asubuhi majira ya saa 3:30, baada ya helikopta hiyo, ambayo namba zake za usajili hazijafahamika, kuruka na dakika chache baadaye ikiwa angani kutoa moshi mzito mweusi, kabla ya kuanguka ndani ya Ziwa Natron.
Kamanda Basilio alitaja walionusurika kifo na nchi wanazotoka kwenye mabano kuwa ni pamoja na Jeffrey Sibbery (Canada), Forest Sowyer (Marekani), Ben Herberston (Australia) na Mark Berker (Uingereza), mkazi wa Kisongo wilayani Arumeru, ambaye inasadikiwa kuwa mwenyeji wa watalii hao.
Watanzania walionusurika katika ajali hiyo ni pamoja na rubani wa helikopta hiyo ya jeshi, Luteni Kanali Mayenga, ambaye amevunjika mguu na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC Moshi, msaidizi wake, Luteni Edward, fundi wa helikopta, Gabriel Majala na mwongoza watalii, Issaya ole Poruo.
Aidha, kamanda huyo alisema kuwa Jeffrey na Forest wamepelekwa Kenya kwa ndege ya kukodi kwa matibabu zaidi baada ya hali zao kuonekana haziridhishi.
Akisimulia ajali hiyo, Kamanda Matei alisema mara baada ya helikopta hiyo kuanguka, wakazi wa Kijiji cha Engusero, waliwahi eneo la tukio na kufanikiwa kuwaoka abiria hao, waliokuwa katika helikopta hiyo kabla hawajapata madhara ya moto uliolipuka.
Watalii hao walikwenda katika eneo hilo kwa lengo la kupiga picha maeneo ya vivutio vya utalii, likiwemo Ziwa Natron na Mlima Oldonyo Lengai, ambao una sifa ya kutoa volkano hai na unaosifika kwa kulipuka mara kwa mara.
Wakati huo huo, Alli Waziri (45), alifariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea jana katika eneo la Ndemwa ndani ya hifadhi ya Ngorongoro baada ya gari walilokuwa wakisafiria aina ya Toyota Land Cruiser, lenye namba za usajili T 241 ATC, kupinduka.
Kamanda Basilio alisema gari hiyo ilipinduka baada ya gurudumu la mbele upande wa kushoto kupasuka wakati gari ikiwa katika mwendo mkali. Gari hilo lilikuwa likiendeshwa na Gerald Msaki (45).