Hatuwezi kwenda Uchaguzi wa 2024 na 2025 bila marekebisho ya Sheria za Uchaguzi

Rutashubanyuma

JF-Expert Member
Sep 24, 2010
219,470
911,174
HATUWEZI KWENDA UCHAGUZI WA 2024 NA 2025 BILA MAREKEBISHO YA SHERIA ZA UCHAGUZI

Watawala wamekuja na mbinu ya medani wengi hawaijui katiba iliyopo, vyama vya siasa siyo wamiliki wa Katiba na ubora wa katiba siyo lazima haki ikatendeka.

Hivi ni visingizio vya kukwepa kurekebisha mfumo wa uchaguzi na kutushinikiza tuendelee na dhuluma ambazo kwa kiwango kikubwa zimechangiwa na sheria za uchaguzi.

Maeneo yafuatayo ni vyema yakarekebishwa kwenye sheria za uchaguzi ili kulinda haki za mpigakura:-

Sheria inayowapa wakurugenzi wa halmashauri za majiji/ manispaa na wilaya kusimamia chaguzi zetu zifutwe na Tume ya Uchaguzi iajiri watendaji wake na kuwa na ofisi za wasimamizi wa uchaguzi kwenye kila jimbo.

Kanuni za uchaguzi zinazowataka wagombea wajaze fomu za kugombea baada ya kuteuliwa na vyama vyao vya siasa vilivyosajiliwa zifutwe. Makatibu wa vyama vya siasa tu wawe ndiyo wanawakilisha orodha ya majina ya wagombea wao katika nafasi zote nchi nzima. Hii itaondoa wimbi la vyombo vya dola kuwapora wagombea wa vyama vya upinzani fomu tajwa au wasimamizi kuzitumia fomu tajwa kuwaengua kwa sababu za kukosekana kwa picha au muhuri au dosari za kiapo au sahihi. Kwa kuwa vyama vya siasa vimesajiliwa hakuna uhaja ya wagombea kujaza fomu. Urasimu huu lengo lake ni kujenga mazingira haramu ya kuwavua wagombea wa upinzani haki yao ya kimsingi ya ushiriki wa kuchaguliwa. Pia wapigakura huporwa haki yao ya kuwachagua wagombea wafaao pale ambapo idadi ya wagombea inapunguzwa na warasimu na hata warasimu kufikia hatua ya kuwachagulia viongozi wasiowahitaji.

Tume ya uchaguzi kupitia waajiriwa wao kwenye majimbo ya uchaguzi ndiyo watawapa barua za mawakala wa vyama vya siasa badala ya wakurugenzi tajwa kufanya kazi hiyo. Uzoefu tulionao unaonyesha wakurugenzi tajwa hutumia madaraka yao haramu vibaya kwa sababu wengi wao ni makada wa CCM na pia wana mashinikizo ya mwajiri wao ambaye ana masilahi mazito kwenye chaguzi zetu kupindisha haki. Utaratibu ulivyo sasa unatoa mianya kwa wakurugenzi tajwa kugoma kutoa barua za mawakala na kwa kufanya hivyo kuharamisha chaguzi zetu kwa kutokuwa huru na za haki.

Vituo vya uchaguzi ambavyo mawakala wa chama chochote watazuiwa kushiriki na kuhakiki zoezi la kupiga kura basi chaguzi za kituo husika yatatenguliwa na uchaguzi wa vituo vilivyoathiriwa utarudiwa.

Tekinolojia ya kisasa itatumika katika kuyatuma matokeo kwenye tovuti ya Tume tajwa ambayo itakuwa wazi nyakati zote ikionyesha fomu za uchaguzi za kila kituo na jumla ya kura kwa kila jimbo yaliyotokana na yale ya kila kituo.

Majumlisho ya kura za kila jimbo yasiyoambatanishwa na matokeo kwenye fomu za kila kituo yatabatilishwa. Hili ni muhimu kwa sababu matamko mengi ya chaguzi za urais na wabunge yameonyesha hayana uhusiano wowote ule na yaliyomo kwenye fomu za vituoni. Kinachojitokeza wakurugenzi tajwa hutamka matokeo ya majimbo watakavyo kulingana na mashinikizo ya wale waliowateua kuzishika hizo nyadhifa.

Usafirishaji wa matokeo kutoka vituoni kwenda tovuti ya Tume ya uchaguzi yatumwe kwa tekinolojia ya kisasa badala kwa mikono ambako uzoefu umeonyesha ubadilishaji wa matokeo kwenye fomu za vituoni hufanywa na vyombo vya usalama ili kuhalalisha kutengua matakwa ya wapigakura yaliyojumuishwa kwenye fomu za kila kituo. Baada ya kuwaibia kura wagombea wa CCM kwa kubadilisha fomu za vituo vya uchaguzi wasimamizi wa majimbo hufanya majumuisho haramu yake na kutamka ya majimbo kinyume na matakwa ya wapigakura.

Matokeo yote ya uchaguzi yatangazwe ndani ya siku 7 ili kuondoa hisia za upangaji wa matokeo.

Mabadiliko ya uteuzi wa makamishina wa Tume ya uchaguzi inaweza kusubiri marekebisho ya katiba ili kuongeza sauti ya wapigakura kwenye utendaji wa Tume ya uchaguzi
 
Huu ndiyo ukweli wetu.
 

Attachments

  • IMG-20230913-WA0006.jpg
    IMG-20230913-WA0006.jpg
    34.8 KB · Views: 4
The Gospel truth before us.
 

Attachments

  • IMG-20230913-WA0005.jpg
    IMG-20230913-WA0005.jpg
    43.6 KB · Views: 2
Back
Top Bottom