Asema alijitakia mwenyewe
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Jakaya Kikwete, amesema kuwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana wa Chama Cha mapinduzi (UVCCM), Hamad Yusuf Masauni, hakuonewa wala kufanyiwa fitina bali alijiuzulu kutokana na kudanganya kuhusu umri wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu wa jumuiya hiyo mwaka 2008.
Rais Kikwete alisema kuwa Masauni alitamka kuwa alizaliwa mwaka 1979 wakati uchunguzi ulibaini kuwa alizaliwa Oktoba 5, 1973.
Akizungumza jana jioni baada ya kufungua kambi ya wiki moja ya UVCCM kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu katika Kijiji cha Ihemi, wilayani Iringa Vijijini, mkoa wa Iringa, Rais alisema Masauni hakuwa mkweli na kwamba uamuzi wake wa kujiuzulu usingeepukika.
Alisema kuwa suala la umri sio tukio la kwanza katika UVCCM kwa kuwa kuna baadhi ya wanachama wake waliozuiwa kugombea nafasi fulani za uongozi kutokana na kuzidi umri.
Ingawa hakuwataja kwa majina baadhi ya vijana waliokumbana na kikwazo hicho, lakini mmoja wao ni Nape Nnauye, ambaye katika uchaguzi wa mwaka 2008 aliomba kugombea uenyekiti wa Taifa, lakini juna lake likaondolewa.
Mwenyekiti huyo wa CCM alisema:Hakuna uchawi, ni kanuni na ni lazima kusimamia sheria na kanuni, hatutafumba macho.
Rais Kikwete alisema kwa kuwa Masauni ni kijana, atatafutiwa kazi nyingine inayolingana na umri wake.
Aidha, Rais alikemea makundi ndani ya jumuiya hiyo na kwamba makundi yasiyo na tija hayana nafasi ndani ya CCM.
Alisema alisikia kuna magenge ndani ya UVCCM akiwa mbali na kwamba sio vizuri kuwa nayo kwa kuwa hayakisaidii chama hicho.
Alisema njia pekee ya kumaliza tofauti ni vikao badala ya kuunda makundi.
Masauni na Naibu Katibu Mkuu UVCCM Zanzibar, Mohamed Moyo walitangaza uamuzi wao wa kujiuzulu nyadhifa zao katika kikao cha Baraza Kuu la jumuiya hiyo mjini Iringa juzi usiku.
Kabla ya kujiuzulu, Masauni alikuwa akituhumiwa kuwa uwezo wake wa kuiongoza jumuiya hiyo ni mdogo.
Masauni na Moyo waliwasilisha barua za kujiuzulu katika kikao cha Baraza Kuu ya UVCCM baada ya vikao vya sekretarieti na Kamati ya Utekelezaji.
Awali jana, Nipashe ilipomuuliza Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, kuhusu tuhuma kwamba Masauni aligushi vyeti na kudanganya umri, Makamba alisema:
Sijalisema mimi, hilo ni la kwako wewe. Katika chama hiki, kinachozingatiwa ni heshima na kuheshimu maamuzi yanayoamuliwa.
Makamba alisema kuwa kitu ambacho wajumbe walizingatia ni pamoja na heshima ya chama, jumuiya yao, na familia zao.
Katika hatua nyingine, UVCCM imesema itajaza nafasi ya Masauni na Moyo ambazo zilibakia wazi kufuatia uamuzi wao wa kujiuzulu.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za CCM mkoa wa Iringa jana, Katibu wa Umoja wa CCM mkoa huo, Roda George, alisema kwa sasa nafasi hizo ziko wazi kutokana na viongozi hao kujiuzulu kwa ridhaa yao wenyewe.
Alisema kuwa katika kikao cha juzi Masauni, aliandika barua na kuomba kujiuzulu rasmi uongozi huo.
Aidha, alisema kuwa katika barua hiyo, Masauni aliahidi kutoa ushirikiano na kukitumikia chama hicho kwa moyo.
Katibu huyo alisema Masauni katika barua hiyo, alieleza kuwa alifikia uamuzi huo bila kushinikizwa na mtu yeyote.
Roda alisema ombi hilo lilipokelewa na wajumbe baada ya kutangaziwa rasmi majira ya saa nne usiku katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo.
Masauni alipoulizwa kuhusiana na kujiuzulu, alikataa kuzungumza.
Migogoro ndani ya UVCCM imekuwa ikizuka mara kwa mara wakati wa michakato ya chaguzi, zikiwemo chaguzi zake.
Mwaka 1995 wakati wa mchakato wa uteuzi wa mgombea urais kupitia CCM, UVCCM iliitisha kikao na kuwapendekeza makada kadhaa kuwa ndio waliokuwa na sifa za kuteuliwa.
Hatua hiyo iliilazimisha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM kuipangua safu nzima ya uongozi wa taifa wa UVCCM.
Katika uchaguzi wa mwaka 1997 yaliibuka makundi ndani ya jumuiya hiyo yaliyowahusisha Emmanuel Nchimbi na Frank Uhahula.
Aidha, katika uchaguzi wa 2002 yalizuka makundi na mivutano ikiwa ni pamoja na kushutumiana hadharani miongoni mwa waliokuwa wakiwania nafasi ya uenyekiti.
Kadhalika, katika mchakato wa uchaguzi wa mwaka juzi, yalizuka makundi na kampeni chafu. Miongoni mwa matukio makubwa ni kuenguliwa kwa Nape Nnauye na vikao vya juu vya CCM kuengua majina ya waliogombea uenyekiti wa taifa na kuyaweka katika nafasi ya makamu mwenyekiti.
Miongoni mwa walioenguliwa katika nafasi ya uenyekiti ni Benno Malisa na Hussein Bashi wakati Masauni aliyekuwa ameomba kugombea umakamu mwenyekiti, jina lake lilihamishiwa nafasi ya uenyekiti na kuwa mgombea pekee.
Wachambuzi kadhaa wamekuwa wakiihusisha mivutano ndani ya UVCCM na mikakati ya wanasiasa ndani ya chama tawala kuitumia jumuiya hiyo nyeti kusaka uongozi wa juu wa dola.
Mvutano ulioibuka ndani ya jumuiya hiyo kabla na baada ya uchaguzi wa mwaka 2008, unachukuliwa kuwa ni mikakati ya wanasiasa kuanza mikakati ya kujipanga kutafuta uongozi wa dola katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
CHANZO: NIPASHE