KERO Halmashauri ya Bunda Mji: Watumishi Wapya Bado Hawajalipwa Fedha za Kujikimu na Mshahara wa Kwanza tangu Julai 2025

KERO Halmashauri ya Bunda Mji: Watumishi Wapya Bado Hawajalipwa Fedha za Kujikimu na Mshahara wa Kwanza tangu Julai 2025

Hii ni kero ambayo mwananchi ameiwasilisha JF akitaka wahusika kuchukua hatua
A

Anonymous

Guest
Ninaandika ujumbe huu nikiwa mtumishi wa umma niliyeajiriwa ajira mpya mwezi wa saba (Julai) mwaka 2025 katika Halmashauri ya Bunda Mji.

Kwa masikitiko makubwa, hadi leo hii bado hatujalipwa fedha za kujikimu kama ilivyoelekezwa kisheria. Aidha, baadhi yetu bado hatujalipwa hata mshahara wa kwanza, huku waliolipwa wakipata malipo pungufu yasiyoendana na haki zao.

Hali hii inaharibu ari ya kazi, hasa pale tunapolinganishwa na wenzetu tuliyeajiriwa pamoja katika halmashauri nyingine ambao tayari wamelipwa fedha zao zote kwa ukamilifu. Tofauti na wao, sisi wa Halmashauri ya Bunda Mji bado tunadai fedha za kujikimu, ambazo kisheria mtumishi anatakiwa kupewa mara moja ili aweze kujikimu kimaisha anapoanza kazi.

Idara ambazo bado hazijalipwa fedha hizo ni Elimu Sekondari na Afya, na hata miongoni mwa waliolipwa, baadhi wamepewa nusu ya kiasi, jambo ambalo ni kinyume kabisa na taratibu za kiutumishi.

Hapa tunajiuliza kwa masikitiko makubwa:

Je, Serikali ya Tanzania ina utaratibu wa kulipa nusu ya stahiki za mtumishi mpya, au ni maamuzi ya baadhi ya halmashauri binafsi?

Tumekuwa tukifuatilia mara kwa mara katika ofisi husika, lakini majibu tunayopata ni yale yale:
"hela itaingia" — bila tarehe, bila maelezo, bila uwajibikaji.

Hali hii:
Inakatisha morali ya kazi
Inawaumiza watumishi kimaisha
Inasababisha madeni na msongo wa mawazo
Inapunguza ufanisi wa utoaji wa huduma kwa wananchi
Inavunja imani kwa mfumo wa ajira serikalini

Watumishi wapya wengi tunaendelea kufanya kazi kwa uadilifu na uzalendo, huku tukipambana na changamoto za maisha bila stahiki zetu za msingi.

Tunaomba kwa heshima lakini kwa msisitizo mkubwa, mamlaka husika ikiwemo TAMISEMI, Ofisi ya Rais – Utumishi, Wizara ya Elimu na Wizara ya Afya, kufuatilia kwa dhati suala hili na kuhakikisha:

Fedha za kujikimu zinalipwa kikamilifu.
Mishahara yote ya awali inalipwa bila kucheleweshwa.
Taratibu za kiutumishi zinafuatwa kwa usawa katika Halmashauri zote.
Hatuombi hisani — tunaomba haki yetu ya msingi.

Jamii ikikaa kimya, uovu unaendelea. Tumaini letu ni haki itendeke!
 
Back
Top Bottom