Haki ya usawa nchini Tanzania

Abdul S Naumanga

JF-Expert Member
Jan 28, 2024
354
621
Wadau leo wacha nianze na hii story fupi kisha nitaingia moja kwa moja katika kuconnect story hii na mada tajwa hapo juu .

Ok let's start:),
Ilikua ni jioni tulivu katika kijiji cha Mazingira Salama, mkutano wa jamii ulikuwa umepangwa kujadili haki za wananchi chini ya Katiba ya Tanzania. Mzee Uwezo, mwenye hekima na maarifa ya sheria, alisimama mbele ya umati tayari kutema madini juu ya haki ya usawa nnchini Tanzania.

Alipoanza kuzungumza, sauti yake ilijaa uzito wa maarifa aliyoyabeba. "Ndugu zangu," alianza, "Katiba yetu inatupa haki ya usawa mbele ya sheria". Mzee Uwezo aliendelea, akielezea kwa kina kila haki iliyoorodheshwa katika Ibara ya 13(6) ya katiba ya Jamuhuri ya muungano wa Tanzania.

"Hii inamaanisha kwamba wakati haki na wajibu wa mtu yeyote vinahitaji kufanyiwa uamuzi wa mahakama au chombo kinginecho kinachohusika, basi mtu huyo atakuwa na haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa kwa ukamilifu" alisema.

"Na siyo hivyo tu," aliendelea, "ni marufuku kwa mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la jinai kutendewa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa anayo hatia..." Wanakijiji walitikisa vichwa vyao ikiwa ishara ya kuelewa na kukubali, wakifurahia haki hiyo yakikatiba.

Mzee Uwezo alipaza sauti yake, "ni marufuku kwa mtu kuadhibiwa kwa sababu ya kitendo chohote ambacho alipokitenda hakikuwa ni kosa chini ya sheria.." alisema, akisisitiza juu ya haki ya kutopewa adhabu isiyostahili.

Akizungumzia haki nyingine, Mzee Uwezo aliwaambia wanakijiji kwamba "ni marufuku kwa mtu kuteswa au kupewa adhabu zozote zinazomtweza au kumdhalilisha". Alisisitiza umuhimu wa kuheshimu haki za binadamu katika kila hatua ya mfumo wa sheria.

Alimalizia kwa kugusia haki ya mwisho, "kwa ajili ya kuhifadhi haki ya usawa wa binadamu, heshima ya mtu itatunzwa..." Wanakijiji walionekana kuguswa na maneno haya, wakielewa umuhimu wa heshima katika mchakato wa kisheria.

Mkutano ulipomalizika, kila mmoja aliondoka akiwa amejawa na ufahamu mpya na ujasiri wa kudai haki zao kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania. Mzee Uwezo alikuwa amewapa msingi thabiti wa kuelewa haki zao za kisheria, na sasa walikuwa tayari kuzitetea.
UFAFANUZI

Mzee Uwezo, mwenye hekima na maarifa ya sheria, alitoa mchanganuo mzuri wa haki zilizojumuishwa katika Ibara ya 13(6) ya Katiba ya Tanzania, akionyesha umuhimu na maana ya kila moja kwa wanakijiji wa Mazingira Salama (Watanzania).

Kuanzia na haki ya kupewa fursa ya kusikilizwa kwa ukamilifu kama ilivyoainishwa katika ibara ya 13(6)(a), Mzee Uwezo alielezea umuhimu wa kila mtu kupata fursa ya kueleza upande wake (kijitetea) mbele ya mahakama au vyombo vingine vya sheria au mamlaka yeyote (including maofisini). Hii inamaanisha kwamba katika mchakato wa kisheria, kila mtu anapaswa kupewa nafasi ya kusikilizwa kikamilifu kabla ya uamuzi wowote kufanyika.

Kwa mfano; Mwajiri anapotaka kumfukuza mfanyakazi wake kwa sababu fulani, mfanya kazi huyo anapaswa kupewa nafasi ya kusikilizwa na kueleza upande wake wa tukio (utetezi) kabla ya uamuzi kufanyika. Hii inazuia uwezekano wa mtu kutendewa kama mwenye hatia kabla ya kuthibitishwa na mahakama au chombo husika.

Kisha, Mzee Uwezo aliendelea kuelezea haki ya kutopewa adhabu isiyostahili, kama ilivyoainishwa katika sehemu ya (c) ya ibara hiyo. Hii inamaanisha kwamba ni marufuku kwa mtu kuadhibiwa kwa kitendo ambacho hakikuwa kosa chini ya sheria wakati akifanya kitendo hicho. Hii inalinda raia dhidi ya adhabu zisizostahili au zisizolingana na makosa waliyoyafanya.

Mfano; mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la kuuza bidhaa flani ambayo wakati akiuza bidhaa hiyo halikua kosa kisheria au adhabu ambayo anapewa ni kubwa kuliko adhabu iliyokuwapo wakati wa kutenda kosa hilo. Hii inahakikisha kuwa adhabu inalingana na makosa na haki ya mtuhumiwa inaheshimiwa.

Aidha, Mzee Uwezo alisisitiza juu ya haki ya kutotendewa kama mtu mwenye kosa mpaka ithibitike kuwa ana hatia, kulingana na sehemu ya (b) ya ibara hiyo. Hii inalinda haki za mtuhumiwa na inahakikisha kwamba hawatendewi kama watu wenye hatia kabla ya kuthibitishwa na mahakama.

Mfano ni mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la mauaji. Kwamba mtu huyo anapaswa kutendewa kwa heshima na usawa hadi pale itakapothibitika kuwa ana hatia ya kutenda kosa hilo. Hii inalinda haki ya mtuhumiwa na kuhakikisha kuwa anaendelea kuwa na hadhi yake mpaka ithibitike hatia yake.

Kuhusu sehemu ya (e) ya ibara hiyo, Mzee Uwezo alielezea umuhimu na haki ya kutoteswa au kupewa adhabu zinazomtweza au kumdhalilisha. Hii inalinda heshima na utu wa kila mtu katika mchakato wa kisheria, na inazuia matendo yoyote ya unyanyasaji au udhalilishaji.

Mfano; mtu aliyeshtakiwa kwa kosa la wizi, haki yake inalindwa dhidi ya adhabu yoyote ambayo inaweza kumtweza au kumdhalilisha, na kwamba mtuhumiwa huyo anapaswa kuheshimiwa kama binadamu katika kila hatua ya mchakato wa kisheria.

Hatimaye, alimalizia kwa kugusia haki ya kutunza heshima ya mtu kulingana na sehemu ya (d) ya ibara hiyo. Hii inamaanisha kwamba katika shughuli zote za kisheria, heshima ya kila mtu inapaswa kuheshimiwa na kutunzwa, kuhakikisha kwamba watu wanatendewa kwa haki na usawa.

Kwa ufafanuzi huu mzuri na wa kina, wanakijiji wa Mazingira Salama (Watanzania wote) sasa tutakuwa na ufahamu mpya na ujasiri wa kudai haki zetu kwa mujibu wa Katiba yetu pale zinapovunjwa ama inapohitajika. Mzee Uwezo ametupatia msingi imara wa kuelewa haki ya usawa kisheria na kikatiba, na sasa tupo tayari kuzitetea.

Screenshot_20240327-230612.jpg
 

Attachments

  • Screenshot_20240327-230612.png
    Screenshot_20240327-230612.png
    531.8 KB · Views: 1
Back
Top Bottom