Hadithi ya umslopagaas

Hadithi ya umslopagaas

Hivi humu jamii forum yote hamna hadithi za alfu ulela... Kama zipo mtu atuekee link hapa tupate jimwaya mwaya
 
SURA YA NANE


Basi, vita vilikwisha. Mahali mbele ya mlango mkubwa wa boma palikuwa pa kutisha sana. Mauaji yalikwisha na mlango ulikuwa umezibwa kwa maiti.

Sisi tulipigana tukiwa na watu thelathini, na katika hao, kumi na watano tu waliobaki hai. Basi, tulipanda mlimani kwa shida na maumivu, na pale mlangoni Bibi Mackenzie alikuwa anatungojea analia kwa ajili ya hofu ya mambo yaliyokuwa yametokea.

Nikasimulia habari za vita kwa maneno machache lakini Yule mtoto Flossie ambaye alikuwa amekwisha fika nyumbani salama amekwisha mwambia mengine.

Tukaingia nyumbani tukavua nguo zetu, tukaganga majeraha. Nafurahi kusema ya kuwa mimi sikujeruhiwa, na Sir Henry na Bwana Good waliumia kidogo tu. Lakini Bwana Mackenzie aliumia vibaya sana.

Tulipokwisha kula chakula cha asubuhi, tulilala, wala hatukuamka tena mpaka wakati wa chakula cha mchana, kisha, tuliwakusanya watu wote wanaume, na wanawake, na vijana, waje kwenye mauaji ya asubuhi ili kuzika maiti. Tukazitupa maiti za Wajivuni katika mto Tana.

Basi, tulipoitupa maiti ya mwisho mtoni, mambo mabaya ya asubuhi ya kuishambulia kambi ya Wajivuni yalikwisha.
 
SURA YA TISA

Zilipopita siku saba, tulikuwa tumekaa tukila chakula cha jioni mezani mwa mission. Tulikuwa tukihuzunika sana, maana kesho yake na mapema tutaagana na rafiki zetu wema akina Mackenzie, na kuendelea katika safari yetu.

Hatukusikia wala kuona tena habari za Wajivuni, na kwa kweli isipokuwa kwa mikuki miwili mitatu iliyoachwa katika majani nje ya boma la ng’ombe, na maganda machache ya risasi, hakuna alama iliyobaki kuonyesha kuwa vita vikali vimepiganwa huko.

Bwana Mackenzie alikuwa anaendelea vizuri katika kupona kwa sababu ni mtu wa kiasi; na wale waliojeruhiwa walikuwa nao wanaendelea vizuri isipokuwa mtu mmoja aliyekufa kwa sababu jeraha lake lilioza.

Tena, watu wa Bwana Mackenzie walikuwa wamekwisha toka pwani, kwa hiyo walitosha sasa kuilinda nyumba yake.

Basi kwa kuwa mambo yalikuwa hivi, ingawa tulikaribishwa tukae siku nyingi zaidi, lakini tuliona lazima tuendelee mbele, kwanza mpaka mlima Kenya, kisha, katika nchi isiyojulikana, kutafuta taifa lile la watu weupe tuliokusudia kuligundua.


Tulikuwa tumefanya shauri la kuchukua punda kumi na wawili katika safari yetu badala ya wapagazi kuichukua mizigo yetu na sisi pia ikitokea haja.

Sasa tulikuwa na Wakazi wawili tu waliobaki kuwa watumishi, wala hatukuweza kupata wenyeji wengine kufuatana nasi kuiendea nchi isiyojulikana tuliyokusudia kuigundua na nani aliweza kuwalaumu walipokataa?

Basi, ilipopata saa moja asubuhi tulikuwa tumekwisha pakia mizigo yetu, na wakati wa kuagana ulifika.

Tuliona huzuni nyingi tulipoagana na rafiki zetu, na hasa tulipoagana na Yule mtoto mdogo Flossie, naye alilia sana.

Basi, baada ya kupeana mikono mara nyingi na kuagana na wenyeji wa huko, tuliondoka, nahii ilikuwa mara ya mwisho kuiona ile nyumba ya mission. Lakini mara nyingi nawakumbuka wale akina Mackenzie.

Basi, tuliendelea bila kupingwa sana mpaka tulipofika chini ya mlima Kenya, kisha tulilipita ziwa linalokaa peke yake liitwalo Baringo, na huko Mkazi mmoja katika wale wawili waliosalia alikufa.

Aliumwa na nyoka aitwaye pofu aliyemkanyaga, na ingawa tulijaribu tuwezavyo kumwokoa lakini hatukuweza.

Kisha tuliendelea kadiri ya maili mia moja na hamsini mpaka mlima mzuri mwingine wenye theluji juu ya kilele chake, uitwao Lekakisera, ambao mpaka wakati huo kadiri nijuavyo, haujafikiwa na Mzungu yeyote.

Tulipofika hapo tulipumzika muda wa siku kumi na nne, ndipo tulipoondoka tena, tukapita katika mwitu wa nchi iitwayo Elgumi, usio na njia wala watu, Katika mwitu huo wako tembo wengi zaidi kuliko niliopata kuona wakati wote wa maisha yangu.

Wanyama wakubwa hawa walikuwako kila mahali, nao hawakusumbuliwa na wanadamu. Hatukupiga wengi.

Kwanza kwa sababu hatukutaka kuzitupa bure risasi zetu ambazo zilikuwa zinaanza kupungua, maana punda mmoja aliyetwikwa mzigo wa risasi alichukuliwa na maji ya mto mmoja uliofurika, tena kwa sababu hatukuweza kuchukua pembe zao.

Nasi hatukutaka kuua kwa ajili ya kupenda tu. Basi, tuliwaacha isipokuwa wawili watatu tuliowapiga ili kujiinda. Wanyama wa kila namna pia walikuwako katika mwitu huo wa Elgumi.
 
Tena, walikuwako mainzi wabaya wengi sana waitwao mbung’o. Ilifikiriwa ya kuwa punda na wanadamu hawadhuriki wakiumwa na mbung’o lakini kwakweli punda wetu walidhurika, labda kwa sababu punda walikuwa wamedhoofu au labda kwa sababu mbung’o wa hapa wana sumu kupita kiasi, sijui, lakini punda wetu walikufa.


Kwa bahati hawakufa mpaka ilipopita miezi miwili baada ya kuumwa, na nilipowachuna niliona mistari yenye rangi ya manjano juu ya nyama, ndiyo dalili kuwa walikufa kwa kuumwa na mbung’o.

Tulipotoka mwitu wa Elgumi, tulizidi kuendelea upande wa kaskazini, maana ndiyo njia aliyoitaja Yule msafiri maskini aliyemfikia Bwana Mackenzie aliye kufa kwa namna ile ya kuhuzunisha niliyokwisha eleza.

Hatimaye tulilifikia lile ziwa liitwalo Laga, ambalo urefu wake wapata kadiri ya maili hamsini, na upana wake maili ishirini.

Ndipo tulipoendelea mbele kadiri ya mwezi mzima tulipita katika nchi yenye vilima vilima mfano wa mawimbi makubwa, na vichaka vilitapakaa huko na huko.

Wakati huo wote nchi ilikuwa imeinuka taratibu na kwa kweli ni mwinuko moja kwa moja mpaka kufika chini ya safu ya milima mingi yenye theluji juu ya vilele vyake.

Tulikuwa tukiiendea milima hiyo, maana tumepata habari ya kuwa ndiko liliko lile ziwa la pili ambalo Yule msafiri alisema halina mwisho wa kwenda chini.

Mwisho tulipafikia, na tulipohakikisha ya kuwa ziwa liko juu ya kilele cha mlima, tulipanda tena kadiri ya futi elfu tatu mpaka tulipofika kwenye genge linaloteremka ghafla.

Tukaona chini yetu kadiri ya futi elfu moja na mia tano, liko ziwa lenye umbo la mraba na upana na urefu wake ulipata kadiri ya maili ishirini, ambalo halitoshi ni shimo la volcano ya zamani.

Tuliona miji iko kando ya ziwa, basi tuliteremka kwa shida katika mwitu wa misonobari iliyofunika miteremko ya shimo lile, tukapokewa vizuri na wenyeji wa huko ambao ni watu wa amani. Wasiopata kuwaona watu weupe mpaka wakati huo; wakatutendea kwa heshima na wema, wakatupa chakula na maziwa kadiri tuliyotaka.


Siku tatu za kwanza tulizokaa huko, ilinyesha mvua, na mvua hii ndiyo iliyoanzisha sumu ya mbung’o katika punda wetu waliyobaki, na wote walikufa.

Msiba huu ulituweka katika shida, maana sasa tulikuwa hatuna njia ya kuchukulia mizigo yetu, lakini kwa kweli, hatukuwa na vitu vingi vilivyobaki kuchukuliwa. Tena, risasi na baruti zilikuwa zimepungua sana.

Tulikuwa na risasi kadiri ya mia moja na hamsini, na risasi za marisaa hamsini tu. Hatukujua namna ya kuendelea mbele, ikawa kama tumekwisha fika mwisho wa safari yetu.

Lakini hata kama tungekuwa na nia ya kuliacha kusudi letu la kugundua yale tuliyokuwa tunayatafuta, ingekuwa jambo la upuuzi kufikiri habari za kurudi nyuma mwendo wa maili mia saba mpaka kufika pwani, hali hatuna zana za safari;

Basi, kwa kuwa wenyeji wa hapa ni wema, tulifanya shauri kukaa hapo tulipo na kungojea mambo yatakayotokea, na huku tunatafuta habari za nchi zilizo mbele.

Basi, tulinunua mtumbwi mkubwa mzuri wa kutosha kutuchukua sisi sote pamoja na vitu vyetu vilivyobaki, kwa mkubwa wa kijiji tulimokaa, tukaanza kusafiri ziwani kutafuta mahali pazuri pa kupiga kambi.

Kwa kuwa hatukujua kama tutakirudia tena kile kijiji, tulipakia mizigo yetu yote katika mtumbwi ule tena, tulichukua kipande cha nyama tuliyopika tayari, tukaondoka.

Wenyeji wengine walikuwa wametutangulia ili kuwaarifu wenyeji wa miji mingine kuwa tunakuja.

Tulipokuwa tukipiga kafi kwa taratibu, Bwana Good alisema jinsi maji ya ziwa yalivyo na rangi ya samawati, akasema.

Wenyeji, ambao ni wavuvi stadi wamemwambia kuwa ziwa hilo lina kina kirefu sana, tena lina tundu chini yake na maji yanatoka huku na kwenda kuuzima moto mkubwa sana unaowaka chini ardhini.

Nilisema kuwa habari hizi alizosikia, bila shaka ni mapekeo ya zamani sana, yalioanza wakati volcano za pande hizi zilipokuwa zingali zikitoa moto bado.

Tulipofika ng’ambo ya ziwa, tuliona ya kuwa kingo zake ni genge la mwamba linalopanda juu sana, wala hapana mahali linapoteremka kwa taratibu, basi, tuliliambaa genge hilo tukiuendea mwisho wa ziwa, maana tulijua ya kuwa kuna mji mkubwa huko.

Tulipokuwa tukienda tulianza kupita chungu nyingi za matete na majani na mashina ya miti na takataka nyingi zinazoelea juu ya maji, na Sir Henry alionyesha kundi la mabata weupe wakubwa waliokuwa wametua juu ya chungu nyingine, na sasa wanakula.

Nilikuwa nimekwishaona mabata wanarukaruka juu, nami sijaona namna yake katika nchi ya Afrika, nikataka kumkamata mmoja ili nimtazame vizuri.

Nilikuwa nimewauliza wenyeji habari za mabata hao, wakaniambia kuwa huja kutoka upande wa pili wa mlima majira Fulani ya mwaka, nao huja asubuhi, na kwa kuwa wamechoka, ni kazi nyepesi kuwakamata.

Niliuliza walitoka nchi ipi, lakini waliyatikisa mabega yao tu, wakasema kuwa juu ya genge lile ni nchi ya ukiwa, na kupita huko ni milima yenye theluji, imejaa wanyama wakali, wala hapana watu wanaokaa huko, na kupita milima ile ni mwitu mnene wa maili mia nyingi wa miti yenye miiba, hata tembo hawawezi kuupita, licha ya wanadamu.
 
Niliwauliza kama wamepata kusikia habari za watu weupe wanaokaa huko kupita milima na mwitu mnene wa miiba, wakanicheka tu.

Lakini baadaye mwanamke mzee sana alikuja akaniambia ya kuwa alipokuwa mtoto mdogo sana, babu yake alimwambia ya kuwa alipokuwa kijana, babu yake yeye alilivuka lile jangwa na milima, akaupenya mwitu ule mnene wa miiba, akaona watu weupe waliokuwa wakikaa katika nyumba za mawe.

Lakini wakati ule aliosimulia Yule mwanamke mzee ulikuwa zamani za miaka kadiri ya mia mbili na hamsini, na habari hazikuwa dhahiri sana lakini hata hivyo, habari zilikuwa zimetajwa tena, na nilipofikiri, niliona hakika habari nyingine tulizokwisha zisikia ni za kweli, nikakaza nia yangu lazima niigundue siri hii.

Wakati huo, sikusikia namna kusudi langu litakavyotimizwa kwa njia iliyokuwa kama muujiza.

Basi, tulianza kuwasaka wale mabata ambao walizidi kulikaribia lile genge, na mwishowe tulipeleka mtumbwi nyuma ya chungu ya takataka kadiri ya mwendo wa yadi arobaini kutoka mahali walipokuwapo, na Sir Henry aliitwaa bunduki yake ya marisaa, akailenga, akapiga wawili shingoni, wakafa.


Mara wale wengine waliopata thelathini au zaidi waliondoka kwa kishindo kikubwa na walipofanya hivyo alipiga tena, na mwingine alianguka amevunjika mbawa.

Basi, tulikwenda tukawaokota wale wawili waliouawa, tukaanza kumsaka Yule aliyeangushwa akawahi kupita juu ya chungu ya takataka na kuingia katika maji wazi tena.

Kwa kuwa tuliona shida kupenya zile taka taka kwa mtumbwi wetu, nilimwambia Yule Mkazi aliyebaki, ambaye nilijua kuwa anaweza kuogelea vizuri, apige mbizi chini ya chungu ile ya takataka akamkamate Yule bata, maana nilijua hakuna mamba katika ziwa hilo, naye hawezi kudhurika.

Basi, yeye aliona kama ni mchezo tu akajitosa majini akamfuata Yule bata, na alipokuwa akimfuatia alilikaribia lile genge.

Mara nilimwona anaacha kuogelea kumfuata Yule bata, akaanza kupiga yowe ya kuwa anachukuliwa na maji na kweli tuliona yakuwa ingawa anaogelea kwa nguvu zake zote, lakini anavutwa kulikaribia lile genge.

Tulipiga kafi kwa nguvu tukapenya ile chungu ya takataka, tukamfuata kadiri tulivyoweza, lakini ingawa tulikwenda upesi sana, yeye alichukuliwa upesi zaidi kulikaribia lile genge.

Mara niliona mbele yetu kadiri ya nchi kumi na nane juu ya uso wa maji, liko tao kama ni mlango wa kuingilia pango linalopenya lile genge.

Basi, maskini mtumishi wetu alikuwa anavutwa na maji kuliendea pango lile kwa nguvu nyingi.

Nilipoliona lile pango, yeye alikuwa mbali nalo kadiri ya futi sitini, na sisi mbali kadiri ya futi mia moja na ishirini, na mtumbwi wetu ulikuwa unavutwa kasi bila sisi kutumia nguvu nyingi.

Alishindana kwa uhodari sana, nikadhani tutaweza kumuokoa, lakini mara niliona kuwa uso wake ya kuwa amekata tamaa , na mbele ya macho yetu alivutiwa katika lile pango akatoweka.

Mara ile he! Niliona kama kwamba mtumbwi wetu umeshikwa na mkono wenye nguvu nyingi mno na kuvutwa kwa nguvu isiyoweza kushindika kuliendea lile genge.

Sasa tuliona hatari iliyo mbele yetu, tukavuta kafi kwa nguvu ili tujiokoe tusivutwe katika maji yaliyokuwa yakizungukazunguka mbele ya mdomo wa pango.

Lakini juhudi yetu ilikuwa bure, na mara ile tulikuwa tunavutwa kuliendea lile pango kama mshale unaotoka kwenye upinde, nikafikiri tumekwisha potea.

Lakini kwa bahati sikushikwa na mfadhaiko, nikalia, ‘’Laleni chini!’’ nikajitupa chini katika mtumbwi, na wote walikuwa na akili kufanya vilevile.

Sasa tulisikia sauti ya kukwaruza, na mtumbwi ulisukumwa chini mpaka maji yalianza kuingia juu ya mbavu zake, nikafikiri huu ndiyo mwisho wetu, lakini kwa ghafla sauti ile ilikoma, nikaona kuwa mtumbwi ungali unaendele mbele.

Nilikigeuza kichwa changu kidogo sikuthubutu kukiinua nikatazama juu. Kwa mwangaza kidogo uliokuwako, niliona tumo pangoni, na juu yake ni mwamba wenye umbo la tao.

Baada ya kupita dakika, kama tano sikuweza kuliona, maana mwangaza ulitoweka, tukawa katika giza tupu.

Basi, kwa muda wa saa moja hivi tulilala, wala hatukuthubutu kuviinua vichwa vyetu visije vikapiga mwamba wa juu, nasi hata kusema hatukuweza kusema kwa sababu sauti ya maji yaliyokuwa yakipita kasi ilizimeza sauti zetu.

Na kwa kweli hatukuwa na moyo wa kusema, hali tumeshikwa na mashaka kwa hatari tuliyomo, na hofu ya kufa wakati wowote ama kwa kutupwa kwa nguvu kando ya pango, ama kuvutiwa chini katika maji yanayozunguka zunguka kwa nguvu, ama kusongwa kwa kutokuweza kuvuta pumzi.


Basi, namna hizi za kufa na nyingine nyingi zilipita katika fikra zangu nilipokuwa nimelala chini katika mtumbwi, nilisikiliza sauti kubwa ya maji yaliyokuwa yakienda kasi, sipajui wapi. Kweli hali zetu ilizipoozesha akili zangu, nikaanza kufikiri nimeshikwa na jinamizi la kutisha sana.
 
Back
Top Bottom