Kisha, walimtazama Umslopogaas kwa ushangao! Naye akaliinua shoka lake kuwasalimu.
Kisha walimtazama Bwana Good, wakavutwa na mavazi yake mazuri, kisha walimtazama Sir Henry aliyesimama na huku mwangaza wa jua unazing’arisha nywele na ndevu zake.
Sir Henry aliyainua macho yake yakakutana na macho ya Nyleptha, na hivyo kwa mara ya kwanza mwanaume mzuri kupita wote na mwanamke mzuri kupita wote niliopata kuwaona walionana.
Nikafikiri moyoni, ‘’Sasa nadhali wanawake wameyaingilia matata yetu, basi pengine mambo yataenda vizuri zaidi,’’ Nikaguna kimya nikijua ya kuwa uzuri wa mwanamke ni kama uzuri wa umeme kitu kinachoharibu na kufanya ukiwa.
Basi nilipokwisha kufikiri hivyo, Malkia wote wawili walikuwa wamekwisha kaa vitini mwao, na panda zililia tena, na watu wote walikaa, na Malkia Sorais alituashiria tufanye vile vile.
Kisha, Yule mtu aliyetuongoza ambaye alikuwa amerudi nyuma katika kundi la watu, alijitokeza amemshika mkono Yule mwanamke tuliyemtoa katika hatari ya kiboko.
Alijiinamisha mbele ya Malkia, kisha alianza kusema. Hakosi alikuwa anasimulia habari za namna walivyotukuta.
Lilikuwa jambo la kuchekesha kuzitazama nyuso za Malkia walipokuwa wakisikiliza habari hizo, na namna zilivyoonyesha ushangao na hofu.
Ikawa dhahiri kuwa hawakufahamu namna tulivyolifikia ziwa lile na kuonekana tunaelea juu yake, wakaelekea kusadiki kuwa hatukufika kwa njia za kibinadamu.
Basi, Yule kiongozi aliendelea kusimulia habari, na kwa jinsi alivyomuuliza Yule mwanamke mara kwa mara nilitambua ya kuwa anasimulia habari za jinsi tulivyowapiga viboko wale.
Nikaona ya kuwa mambo yamekwenda upande wa habari za viboko, maana wale makuhani walidakiza maneno mara kwa mara kama kwamba wameudhika sana, na wale Malkia wawili walisikiliza na huku nyuso zao zimejaa ushangao, na hasa Yule kiongozi alipowaonyesha bunduki zetu na kueleza ya kuwa ndizo zilizowaua wale viboko.
Basi, ni afadhali nieleze hapa ya kuwa Wazuvendi huliabudu jua, naya kuwa viboko ni mwiko kwao, wanahifadhiwa nao.
Si kwamba hawawauwi viboko, bali pengine huwaua wengi sana nao hutumia ngozi zao kufanyia ngao za askari.
Basi, kwa bahati mbaya, wale viboko tuliowaua walikuwa wamefungwa, nao walikaa mlangoni mwa bandari na kulishwa kila mara na makuhani ambao ulikuwa wajibu wao kuwaangalia.
Tulipokuwa tuna wapiga niliona kuwa walionekana kama kwamba ni wakufugwa, basi hii ndiyo iliyokuwa sababu yake.
Hivyo katika matendo yetu ya kuwaonyesha wenyeji nguvu zetu, kumbe , tumefanya jambo la kufukuru kuu kabisa.
Basi, kiongozi wetu alipokwisha simulia habari, Yule kuhani mkuu Agon alisimama akatoa hotuba ndefu ya hasira.
Sikupenda namna alivyotukazia macho yake baridi ya kijivu, na kwakweli ningalimchukia zaidi kama ningalifahamu ya kuwa anadai kwa jina la Mungu wao, ya kuwa lazima tutolewe kafara kwa kuchomwa moto tungali hai.
Alipokwisha sema, Malkia Sorais alisema naye kwa sauti nzuri ya upole ikawa kama kwamba anashindana naye na kumweleza upande mwingine wa jambo.
Kisha Nyleptha, akasema kwa sauti nzuri, lakini hatukujua ya kuwa anasihi kwa ajili ya maisha yetu, ndipo pale alipo akasema na mtu mrefu mwenye umbo la kiaskari, ana ndevu nyeusi na upanga mrefu, ambaye tulipata kujua baadaye jina lake ni Nasta.
Naye ni mkuu wa nchi kubwa, akawa kama anamsihi amsaidie. Lakini ilitokea ya kuwa Sir Henry alipomtazama Nyleptha rangi ya uso wake iligeuka, na Nasta aliliona jambo hilo, akajiuma mdomo akaushika upanga wake imara zaidi.
Baadaye tulipata habari ya kuwa Nasta anataka kumwoa Yule Malkia. Basi, ni dhahiri si mtu wa kumwomba msaada, na alipojibu alisema kwa sauti nzito kama kwamba anakubali shauri la kuhani mkuu Agon.
Alipokuwa akisema, Sorais alikuwa amekaa na huku ameshika tama, akamtazama Nasta na huku anacheka kidogo kama kwamba anazijua fikira zake, naye amekaza nia asishindwe naye.
Lakini Nyleptha alikasirika, na uso wake ulibadilika, na macho yake yaling’aa. Kisha aligeuka akamtazama Agon, ikaonekana kwamba anayakubali kidogo maneno yake, maana alikiinamisha kichwa chake; na alipokuwa akisema alipunga mikono yake ili kuyakaza zaidi maneno yake, na huku Sorais amekaa vile vile anacheka kidogo.
Kisha, Nyleptha alifanya ishara ghafla na panda zililia tena, na watu wote walisimama wakatoka sebuleni isipokuwa sisi na askari walinzi, maana alifanya ishara sisi tukae.
Walipokwisha toka, alijiinamisha mbele akacheka vizuri na kwa sauti na ishara alitufahamisha kwamba anataka kujua mahali tulipotoka.
Shida ilikuwa namna ya kuelezana, lakini nilipata akili. Katika mfuko wangu nilikuwa na kitabu cha kuandikia na kalamu, nikavitoa, nikachora ramani ya ziwa, na kwa namna nilivyoweza nilichora picha ya mto chini ya ardhi na ziwa upande mwingine wa mlima.
Basi, nilipofanya hivyo alifahamu, akapiga makofi kwa furaha, akashuka katika kiti chake akakipeleka kitabu kwa dada yake Sorais, na yeye pia alifahamu.
Kisha, akaitwaa kalamu na baada ya kuitazama kwa udadisi, alianza kuchora picha ndogo ndogo.
Picha ya kwanza ilifanana na yeye mwenyewe ameinyosha mikono yake kutupokea, na mtu mwingine aliyefanana na Sir Henry, anaipokea mikono yake.
Kisha, alichora picha ya kiboko anagaagaa majini kama anakufa, na ya mtu aliyefanana na kuhani mkuu Agon ameiinua mikono yake kwa ghadhabu amesimama kando ya ziwa.
Kisha, alichora picha ya moto mkubwa unaowaka, na ya Yule Agon anatuchochea katika moto kwa fimbo.
Basi, picha hizo zilitujaza kihoro, lakini nilitulia kidogo alipoanza kuchora picha nyingine ya mtu kama Sir Henry, na ya wanawake wawili niliowatambua kuwa ni yeye mwenyewe na dada yake Sorais.
Na kila mmoja ameuweka mkono mmoja kumkumbatia Bwana Henry, na kwa mkono mwingine wameushika upanga ili kumlinda.
Basi, Sorais aliyekuwa akituangalia sote, na hata Sir Henry, akafanya ishara kuonyesha kuwa fikira zake zinapatana na zile za dada yake.
Nyleptha alichora picha ya jua linaloanza kuchomoza, akafanya ishara ya kuwa sasa lazima aende, na ya kuwa tutaonana tena asubuhi.
Basi, hapo uso wa Sir Henry ulikunjamana, na Nyleptha alimpa mkono wake aubusu ili kumfariji akaubusu kwa heshima.
Basi, huku Sorais ambaye Bwana Good alikuwa anamtazama tokea mwanzo, alimpa mkono wake aubusu, lakini macho yake, yalikuwa yanamtazama Sir Henry tu.
Nafurahi kusema ya kuwa mimi sikuwamo katika mambo hayo, wala hakuna mmojawapo aliyenipa mkono wake niubusu.
Kisha, Nyleptha aligeuka akasema na Yule mkubwa wa askari walinzi, ikaonekana kwa namna alivyopokea maneno kwa heshima, ya kuwa anatoa amri yenye nguvu; kisha, alituchekea akatoka sebuleni amefuatana na Sorais na wengine wa askari wa zamu.
Malkia walipokuwa wamekwisha toka, Yule askari mkubwa aliyepewa amri za Nyleptha alikuja mbele na kwa ishara nyingi za heshima alituongoza kutoka sebuleni, na katika vichochoro vinginevyo mpaka katika vyumba vingine vyenye vyombo vizuri sana na mazulia na vitanda vizuri vizuri.
Vyakula vilikuwa vimeandaliwa mezani katikati ya chumba, na meza ilipambwa kwa maua.
Watumishi wanaume na wanawake walikuwapo kutuhudumia na huku kinanda kilikuwa kinapigwa mahali nje, tukajiona kama kwamba tu katika pepo ya duniani, na jambo tu lililotuudhi ni kufikiri ya kuwa Yule kuhani mkuu anataka kukutupa motoni.
Lakini tulikuwa tumechoka sana hata tuliona shida tusishikwe na usingizi wakati tunapokula, na mara tulipokwisha kula tulifanya ishara ya kuwa tunataka kulala.
Basi, walituongoza wakataka kutupa kila mtu chumba chake peke yake, lakini tuliwaashiria ya kuwa tulala wote chumba kimoja.
Tena ili tusije tukashambuliwa ghafla, Umslopogaas alilala pamoja na shoka lake katika chumba kilichokuwa jirani.
Basi tulivua nguo zetu isipokuwa deraya za chuma tulizokuwa tumevaa ndani ya nguo zetu, tukajitupa vitandani tukajifunika kwa mashuka ya Hariri yenye nakshi.
Nilikuwa karibu kupata usingizi nilipoamshwa na sauti ya Bwana Good akasema, ‘’Je, Quatermain, ulipata kuyaona macho kama yale’’ nikajibu kwa haraka, ‘’Mcho! Macho gani’’ akajibu, ‘’Macho ya Malkia. Macho ya Sorais!’’ nikapiga miayo nikasema, ‘’Sijui mimi, sikuyaangalia sana, abda ni macho mazuri.’’
Basi, baada ya dakika tano hivi niliamshwa tena kwa sauti yake, ananiita tena.
Nikasema, na sasa nimekasirika sana kuamshwa hivi, ‘’Je, unataka nini sasa’’
Akajibu, ‘’Je, ulipata kuona visigino vya miguu yake namna vilivyo vizuri .''
Basi, hapa upuuzi wake ulinichosha kabisa. Nilikuwa nimeviweka viatu vyangu vizito karibu na kitanda nilicholalia, basi nilivitwaa nikavitupa vikampiga Bwana Good baraabara. Baada ya hayo nililala sana.
Sijui habari za Bwana Good, sijui kama alilala au kama aliendelea kuota habari za uzuri wa Sorais.