Halafu alianza kuipunga mikono yake, akaanza kuimba kwa sauti iliyosikika hekaluni mwote.
Maneno aliyoimba yalikuwa yakulisifu jua.
Yalikuwa kama haya yanayofuata:
Kuna kimya juu ya uso wa Dunia na wa maji yake, Ndiyo kimya imeukalia uso wa maji kama ndege akaaye juu ya kiota chake.
Na kimya imekali kifua cha giza nene, juu sana angani tu nyota zinasema na nyota.
Dunia anataka kuzimia kwa kutamani na machozi yake yanatoka kwa ajili ya tamaa yake.
Usiku mwenye ukanda wa nyota huikumbatia isiridhike.
Imelala imefunikwa kwa ukungu kama maiti katika sanda, Imeinyosha mikono yake kuendelea masharikini.
Tazama! Mbali masharini iko dalili ya mwangaza.
Dunia imeiona na kujiinua, Inatazama toka chini ya kitanga cha mkono wake.
Ndipo malaika wako wakuu hutoka katika mahali pako Patakatifu, ee jua.
Huzitupa panga zao zenye moto katika jua na kuliunguza.
Hupanda mbinguni na kuzitupa chini nyota toka viti vyao vya kifalme.
Ndiyo, huzirudisha nyota ziinemetazo katika giza la usiku.
Hufanya mwezi kufifia kama uso wa mtu anayekufa.
Na tazama! Utukufu wako huja, ee jua!
Ee wewe uliye mzuri, hujivika kwa moto.
Mbingu pana ni njia yako, hupita juu yake kama gari.
Dunia ni bibi arusi wako. Huikumbatia nayo huzaa watoto, ndiyo, humpendeza naye hutoa mazao yake.
Wewe ni Baba wa wote na mtoaji uzima ee jua.
Watoto wadogo huinyosha mikono yao na kukua katika mwangaza wake, Wazee nao hutokea na wakikuona hukumbuka nguvu zao.
Wafu tu, ndio wanaokusahau, ee jua.
Ukasirikapo ndipo huficha uso wako.
Hujifunika na pazia la vivuli.
Ndipo Dunia huona baridi na Mbingu hufadhaika; Hutetemeka, na sauti yake ni kama sauti ya ngurumo Hulia, na machozi yao humiminika katika mvua;
Huguna, na pepo kali ni sauti ya kuguna kwao.
Maua hufifia, mashamba yenye mauuno husinyaa na kunyauka.
Wazee na watoto huenda mahali panapo wahusu.
Uchapo mwangaza wako, ee jua!
‘’Sema, u nini, ee uzuri usio na mfano nani aliyekuweka juu sana, ee kitisho cha joto?
Ulianza lini, na siku ya mwisho wako itakuwa lini?
Wewe ni vazi la roho mwenye uhai.
Hakuna aliyekuweka juu maana wewe ndiyo mwanzo.
Huna mwisho hata watoto wako watakapo sahauliwa .
Ndiyo, huna mwisho kabisa, maana wakati wako ni wa milele.
Umekaa juu katika nyumba yako ya dhahabu na kupima wakati.
Ee Baba Wa Uzima! Ee Jua Mfukuzaji wa Giza!’’
Basi, aliacha kuimba na ingawa maneno niliyotafsiri huoonekana kama si mazuri sana, lakini yale aliyoyasema yalikuwa mazuri ajabu; kisha, akatazama juu katika kipepeo cha kuba, akasema.
‘’Ee jua, ushuke juu ya madhabahu yako!’’
Aliposema maneno hayo, jambo zuri la ajabu lilitokea.
Mwali mmoja wa nuru ulipenya lile tundu katika kuba kama upanga wa moto mkali.
Ulitua juu ya milango ya dhahabu iliyofungwa juu ya madhabahu, ukatiririka juu yake, na ua lile tukufu lilifunuka kama kwamba limefunuliwa na mwangaza wake.
Lilifunuka polepole na milango ile ilipokuwa ikifunuliwa, na kuonyesha madhabahu ya dhahabu ambayo juu yake moto huwaka daima, makuhani walipiga panda zao, na watu wote walipaaza sauti zao, na sauti zao za kusifu zikapanda juu zikapiga kuba ya dari zikarudishwa tena katika kuta za marumaru.
Sasa madhabahu ya ua ilikuwa imefunuka , mwangaza wa jua ulitua juu ya ulimi wa moto mtakatifu, ukaupiga chini hata ukapepesuka na kuzama na kutoweka katika shimo ulimotokea.
Ulipokuwa ukitoweka , sauti za panda zilipaa tena, na Yule kuhani mzee aliinua mikono yake juu tena, akasema kwa sauti kubwa
‘’Twakutolea kafara ee Jua!’’
Nilimtazama Nyleptha tena; nikaona ya kuwa macho yake yamekazwa kuutazama mlango ule wa shaba wa chini, mbele ya madhabahu.
Nikasema, ‘’Jihadharini!’’ na nilipokuwa nikisema, nilimwona Agon anainama mbele na kugusa kitu juu ya madhabahu.
Na alipofanya hivyo, nyuso za watu wote ziligeuka nyekundu, kisha zikageuka nyeupe tena, nikasikia sauti ya kuvuta pumzi kutoka kwa watu wote.
Nyleptha aliinama mbele, akajificha macho yake kwa mikono yake kama hawezi kujizuia.
Sorais aligeuka akamnong’oneza mkubwa wa walinzi wa kifalme, ndipo sauti ya kukwaruza ilisikika, na mlango ule wa shaba katika sakafu ulifunguka mbele ya miguu yetu, na mahali pake palikuwapo shimo lenye moto mkubwa mkali sana chini ya madhabahu.
Tulitoa sauti ya hofu, tukaruka nyuma. Mara kukawa na ghasia nyingi sana, na sisi tulijipanga mgongo kwa mgongo.
Sote tulikuwa na bastola maana ingawa tulipokuwa tukitoka jumbani, tulinyang’anywa bunduki zetu, bastola tulikuwa nazo maungoni mwetu.
Watu hawa hawakujua bastola ni kitu gani. Tena, Umslopogaas alikuwa na shoka lake la vita, na sasa alilizungusha kichwani akatoa ukulele wa vita wa Kizulu uliozunguka zunguka hekaluni.
Basi, hapa makuhani ambao walikuwa wamenyang’anywa mawindo yao walifuta panga zao toka chini ya mavazi yao meupe, wakaturukia kama mbwa mwitu wanavyowarukia wanyama wanaojitetea.
Nikatambua ya kuwa ingawa iko hatari katika kutenda jambo lolote, lakini hata hivyo, lazima tujaribu kujitetea au tupotee.
Basi, mtu wa kwanza alipotujia naye alikuwa mtu mrefu mkubwa nilimpiga risasi ikampata, akaanguka mbele ya lile shimo la moto, akatumbukia ndani ya lile shimo la moto tulilowekewa sisi, na huku anapiga kelele.
Sijui kama ilikuwa kwa sababu ya kelele alizofanya au kwa sababu ya kishindo cha bastola na matokeo yake wale makuhani wengine walisimama kama wamepooza na kufadhaika kabisa.
Na kabla hawajaweza kujongea mbele tena, Sorais alitoa amri, na mara ile sisi pamoja na Malkia wawili na watu wakuu tulizungukwa na kundi la askari wenye silaha.
Basi, hata hapo makuhani walisita, na watu wote walisimama kama wanyama walioshtushwa, wasifanye hivi wala vile.
Sauti ya mwisho ya Yule kuhani aliyeangukia motoni ilififia, kukawa kimya kabisa katika hekalu.
Ndipo kuhani mkuu Agon alipogeuka, na uso wake ulikuwa kama wa shetani! Akawapigia ukulele wale Malkia akasema, ‘’Kafara itolewe.
Kufuru iliyotendeka na wageni hawa haitoshi na ninyi Malkia mtaingia nyinyi kama mnataka kuwaokoa watu hawa walio tenda uovu ule wa kuwaua wanyama wale waliowekwa wakfu.
Na sasa kuhani wa Jua pia amekufa, wamemuuawa kwa uchawi wao. Wageni hawa waliofika kama pepo za mbinguni toka wapi hatujui, wala hatuwajui ni nani!
Jihadharini ninyi Malkia namna mnavyojiingiza na kushughulika na utukufu wa mungu, hata mbele ya madhabahu yake.
Iko nguvu iliyo kuu kuliko nguvu zenu; iko haki iliyo juu kuliko haki yenu. Jihadharini wala msiinue mikono ya kufuru kuzipinga. Enyi Malkia, kafara itolewe.’’
Ndipo Sorais alijibu, na sauti yake ilikuwa ya utulivu, na kama ilivyokuwa siku zote kama kwamba anadhihaki: ‘’Ee Agon umesema kama ulivyotaka, nawe umesema kweli. Lakini ni wewe unayetaka kuinua mkono wa kufuru juu ya haki ya Mungu.
Kafara ya saa sita imekwisha timizwa! Jua limechagua kuhani wake awe kafara.’’
Basi, wazo hili lilikuwa la kigeni, na watu wote wakalikubali.
Sorais akaendelea: ‘’Watu hawa ni nani? Ni wageni walioonekana wanaelea juu ya ziwa. Nani amewaleta hapa? Walifika hapa namna gani? Unajuaje ya kuwa si watumishi wa Jua?
Je, huu ndio ukarimu unaotaka taifa letu liwape watu ambao bahati imewaleta kwetu, Je, ni vyema kuwatupa motoni? Ole wako! Ole wako! Ukarimu ni nini? Kumpokea mgeni na kumkaribisha vizuri! Kuyaganga majeraha yake, kumpa mahali pa kulala, na chakula.
Lakini malazi yako ni shimo la moto, na chakula chako ni joto la moto. Ole wako, nasema!’’
Hapa alinyamaza kidogo ili aone namna watu wanavyoyapokea maneno yake, na alipoona wanayapokea vizuri, akabadili usemi wake, na sasa ulikuwa wa kutoa amri.
‘’Haya! Jitengeni; wapisheni Malkia na wale wanao funikwa na mavazi ya Malkia.’’
Agon akayakaza meno yake, akasema: ‘’Je, ee Malkia nikikataa?’’
Sorais akajibu kwa kiburi: ‘’Basi hapo nitakata njia kwa walinzi wangu, ndiyo, hata mbele ya madhabahu takatifu na katikati ya miili ya makuhani wako.’’
Agon akafura kwa gadhabu ya kushindwa. Akawatazama watu kama kwamba anawasii wamsaidie, lakini aliona ya kuwa wako upande wa Malkia.
Wazuvendi ni watu wenye udadisi, tena wakarimu, ingawa walifikiri ya kuwa kuwapiga wale viboko waliowekwa wakfu ni kosa kubwa, lakini hawakutaka wageni wa kwanza walioonekana katika nchi yao watupwe katika shimo la moto, na kwa hivyo kukomesha nafasi ya kupata habari zetu kwa kuzungumza juu yetu.
Agon alipoona hivyo akasita, kisha , Nyleptha alisema kwa sauti yake nzuri, akasema: ‘’Kumbuka Agon, kama dada yangu Malkia alivyosema, labda, watu hawa pia ni watumishi wa Jua.
Wao hawawezi kujitetea maana ndimi zao zimefungwa. Mambo haya yawekwe mpaka watakapojifunza lugha yetu.
Nani anayeweza kuhukumiwa bila kusikilizwa? Watu hawa watakapoweza kujitetea, basi hapo tutaweza kuwahukumu.’’
Basi, hii ilikuwa njia ya akili ya kuokoka ingawa Yule mzee mkali kuhani hakuipenda, hana njia nyingine, akasema: ‘’Vyema, Ee Malkia.
Watu na waende kwa amani, nao watakapo weza kusema lugha yetu watapata nafasi ya kujitetea. Na mimi, hata mimi, nitaomba mbele ya madhabahu maradhi yasiingie katika nchi yetu kwa ajili ya kufuru iliyotendeka.’’
Basi maneno yake yalikubaliwa na wote, tukatoka hekaluni tumezungukwa na askari wa kifalme.
Lakini hatukupata kujua kwa siku nyingi habari za mambo yaliyotokea siku ile, na jinsi maisha yetu yalivyookolewa kwa shida nyingi kwa mikono ya ukatili ya makuhani wa Zuvendi, ambao wana nguvu hata karibu kuzishinda nguvu za Malkia.
Kama Malkia hawakufanya bidii kutulinda, tungaliuawa hata kabla hatujaingi katika hekalu la Jua.
Ile hila ya kututumbukiza katika shimo la moto tuwe kafara, ilibuniwa baada ya kujaribu kutuangamiza kwa njia nyingi nyingine ambayo sisi hatukuwa na habari nazo.