VITA YA WACHAWI-30
by-GLOBAL
10 hours ago
ILIPOISHIA:
Mganga hakutaka maiti ilale kwani ingemletea picha mbaya kwa wateja wengine, ilibidi kaburi lichimbwe usiku uleule na watu watatu kwa kupokezana mganga msaidizi wake na Amangise mwenyewe kwa vile wagonjwa waliokuwepo walikuwa wanawake watupu.
SASA ENDELEA...
Japokuwa Andendekisye alikuwa na uchungu wa kifo cha mkewe lakini alilazimishwa na mganga kusaidia kazi ya kuchimba kaburi kisha waliuchukua mwili wa mke wa Andendekisye na kwenda kuuzika watu watatu usiku uleule. Baada ya kuzika walirudi nyumbani kwa mganga ambaye kichwa kilimuuma kwa kilichotokea, toka aanze uganga hakuwahi kutokewa na kitu kama kile.
Alipofika kilingeni kwake aliangalia rada zake, ajabu kila alipoangali ilikuja sura yake kuonesha ndiyo iliyofanya vile. Kila njia alitumia ili aone nani aliyefanya vile hakukuwa na jibu lingine zaidi ya kujiona yeye kuwa ndiye mhusika wa kifo cha mke wa Andendekisye.
Baada ya kuchemka alimwambia Andendekisye:
Inaonekana jirani yako makombora ya mbali hayamuwezi nitaondoka na wewe mpaka kwako nikatege bomu langu karibu. Hawezi kunichezea akili sijawahi kuchezewa akili, naapa nikimshindwa naacha uganga.
Yaani siamini kama ukishindwa nitakwenda popote ili nimtie adabu hawezi kunitia hasara mara mbili, Andendekisye alisema kwa uchungu.
Tunaondoka muda huu ili mchana itukute Tanzania natega vyangu baada ya majibu naondoka usiku kurudi kwangu.
Yaani nipo radhi kutumia kiasi chochote cha fedha hata kuuza shamba langu lote ili nimtie adabu.
Wala hutaingia hasara yoyote majibu utayapata leo hii hii kama yeye anajua hivi sisi tunajua vile. Sijawahi kushindwa na kitu chochote, wachawi wote wanajua mimi ni nani. Kama kombora la mbali limemkosa sasa vita naihamishia Tanzania, kitu nitakachomfanya hakitasahaulika katika midomo kijijini Ibungu na vitongoji vyake- na Tanzania nzima.
Nataka pigo limalize mpaka kizazi chake chote hata kama kuna ndugu zake hakikisha unafagia mpaka sisimizi anayemuhusu.Hiyo kazi ndogo, hata jengo analoishi litageuka kichunguu, amenichokoza huwa sichezewi, mimi ndiye mchawi niliyeogopwa mpaka na shetani, mganga alijitapa kwa hasira.
Baada ya mganga kuchukua makombora ya maangamizi, waliondoka alifajiri ile na kuacha wagonjwa chini ya wasaidizi wao huku akiwaeleza atarudi usiku wa siku ile ili kuendeleza tiba zao na kama kuna mmoja atakuwa bado hajapata nafuu japokuwa aliamini dawa aliyowapa ilikuwa ni nzuri, wamuongezee dozi.
Walipanda magari mpaka mpakani na kuvuka mpaka hadi Tanzania na kupitia baikeli yake mpaka Ibungu ambako walifika saa saba mchana wakati huo watu walikuwa katika maandalizi ya mazishi ya Ambakisye. Alipofika alikwenda moja kwa moja hadi nyumbani kwake na kuingia ndani.
Mkuu taarifa wanazika saa kumi jioni, Andendekisye alimweleza mganga baada ya kudodosa habari za kijijini.
Basi kazi itaishia makaburini wote watarudi na pumzi lakini si Amangise na mkewe, hilo kombora ni moja ya silaha, huzitumia kwa nadra hasa kwa watu wenye kutaka kupimana nguvu na mimi.
Yaani nikisikia wamekufa mbona nitafanya sherehe, nitachinja ngombe wawili.
Hiyo kazi ndogo namaliza kazi yangu kachague hao ngombe kabisa.
Hilo halina tabu, yaani mpaka sasa nashindwa kulia kwa kifo cha mke wangu kipenzi, naona kama bado nipo ndotoni na asubuhi nikiamka naona kama zamelala pembeni yangu.
Najua, lakini moyo wako wa kuvumilia unanipa nguvu ya kuifanya kazi vizuri.
Nataka kilio changu kigeuke kicheko.
Jioni haipo mbali.
Sasa hivi sitasema kitu nasubiri majibu toka makaburi juu ya vifo cha Amangise na mkewe.
Mmh! Sasa kazi ndiyo inaanza kabla hawajaenda makaburini. Nipatie unga, ungo na chungu.
Andendekisye alifanya vile haraka kwa kumletea mganga alivyoomba kisha alikaa pembeni. Mganga alifungua makombora yake na kutoa- dawa aliyochanganya na unga na kipande cha ngozi ya chatu na kufunika kwa ungo.
Kisha alichukua dawa nyingine na kuchanganya na unga- na kucha ya bundi na kuvifunika na chungu, walitoka nje na kuomba chungu kingine kipya.
Nipatie kuku mwekundu.
Andendekisye aliingia bandani na kuchukua jogoo jekundu na kumpa- mganga ambaye alimchukua na kumlisha hirizi ndogo kisha alimzika akiwa hai. Chungu alikichukua na kukiweka nyuma ya nyumba na kuomba kisu.
Nichome tena kisu? Andendekisye alishtuka.
Hapana , kazi yote nafanya mimi kama bomu wacha linilipukie.
Mmh! Hapo sawa, maana sasa hivi kisu nakiogopa sidhani kama nitachinja hata kuku katika maisha yangu kwani sasa hivi nikishika kisu nitakuwa kama namuua mke wangu.
Ondoa wasi kazi yote nimeamua kuifanya mwenyewe wewe subiri majibu utajua huwa sibahatishi kwenye kazi yangu.Baada ya mganga kuchukua kisu na chungu kipya alikiweka nyuma ya nyumba na kukiweka kisu ndani ya chungu bila kitu chochote.
Kisha walirudi ndani na kumwambia- Andendekisye. Fungua kwenye chungu, alimwambia afunue chungu- kilichowekwa dawa na kucha ya bundi.--- -
Andendekisye alisogea kwenye chungu na kufungua, alishtuka na kusababisha kukidondosha chungu baada ya kumkuta bundi mkubwa ndani yake aliyetengenezwa na dawa alizochanganya mganga ambazo ziligeuka kuwa ndege huyo
He!
Unashangaa nini?
Siamini.
Kazi umeanza, hii ndiyo silaha itakayommaliza mke wa adui yako, mganga alisema huku akimtoa bundi na kumuweka pembeni kisha alimgeukia Andendekisye aliyekuwa bado amepigwa na butwaa baada ya kuona maajabu yale kwa mchanganyo wa dawa kutoa bundi.
Hii nitafunua mwenyewe kwa vile unaweza kufa kwa mshtuko, utakachokiona usishtuke ni silaha za maangamizi.
Kwani kuna nini?
Utaona tu.
Je, ni nini hicho, fuatilia wiki ijayo.