ILIPOISHIA :
Kutokana na hali zao ambazo hazikujulikana
kama wapo hai au wamekufa waliwawahisha
Muhimbili.
Gari alilokuwa akiendesha Colin liliendelea
kuteketea na hatimaye lilishika moto lote
kutokana na miundo mbinu mibovu ya kuzimia
moto.
SASA ENDELEA .. .
Liliteketea na kila kilichokuwepo pamoja na
simu zote za Colin na Cecy .
Msichana mmoja shoga wa Brenda rafiki wa
Mage ambaye alikuwa akimfahamu Colin
kutokana na kuwepo siku Colin alipomvisha
pete Mage , alikuwepo kwenye ajali ile baada ya
kuteremka kwenye daladala na kukuta watu
wakitolewa kwenye gari lililokuwa likiwaka
moto.
Kwa vile hakuijua namba ya simu ya mama
Colin aliamua kumpigia simu Brenda amweleze
Mage ili ampigie mama Colin kumjulisha ajali
ile. Baada ya kupigiwa simu Brenda alipokea
upande wa pili:
Haloo Loveness, niambie shoga !
Aisee kuna tatizo , alisema kwa sauti iliyojaa
wasiwasi .
Mbona unanitisha kuna nini? Brenda
alishtuka.
Colin kapata ajali mbaya sana .
Colin ! Yupi ?
Aliyekuwa mchumba wa Mage .
Wewe! Ajali ya nini tena Mungu wangu?
Gari alililokuwa akiendesha limepata ajali
barabara ya Sam Nujoma jirani na Mlimani City
kwa kugonga nguzo ya umeme .
Mungu wangu, vipi hali yake ?
Mmh ! Kwa kweli kuna taarifa nyingi japo si
rasmi.
Mungu wangu nisaidie mja wako , taarifa gani
tena Love ?
Wapo wanaosema wamekufa hapohapo.
Jamaniii! Kwani alikuwa na nani ?
Na msichana mmoja ambaye anaonekana
alikuwa na nguo za mazoezi.
He ! Yaani nimechoka , siamini kama Colin
amekufa kirahisi namna hiyo.
Sasa shoga nina imani Mage ana namba ya
mama yake , mpigie ili awajulishe nina imani
hawana taarifa.
Poa, lakini siamini mpaka niuone mwili wa
Colin kwenye jeneza.
Brenda akiwa amechanganyikiwa alimpigia
simu Mage aliyekuwa amekaa kwao huku
akichezea simu yake . Baada ya kumtumia
ujumbe Colin alipiga simu ambayo iliita bila
kupokelewa na mwisho ilizimwa kabisa.
Baada ya kuzimwa alijikuta akijiapiza :
Lazima nimpate Colin kwa hiyari kwa nguvu,
nitahakikisha nampoteza kinyago wake ili
niipate nafasi yangu bila hiyo sina maisha heri
ninywe sumu .
Akiwa katikati ya mawazo simu yake iliita ,
wazo lake alijua Colin alikuwa akitafuta sehemu
nzuri ili ampigie. Alipoangalia alikuta inatoka
kwa shoga yake Brenda , aliipokea .
Niambie shoga.
Mage kuna taarifa siyo nzuri .
Taarifa gani?
Zinamhusu zilipendwa wako .
Nani, Hans ?
Hapana, Colin.
He ! Colin kakupigia simu ?
Siyo kunipigia simu bali kapata ajali mbaya .
Acha utani , acha kunirusha roho unione kama
nampenda, sio siri Colin ndiye aliyebeba uhai
wangu.
Mage hebu tuliza akili unisilize.
Haya niambie mpenzi.
Colin amepata ajali mbaya barabara ya Sam
Nujoma jirani na Mlimani City na haijulikani
kama mzima au amekufa .
Brenda sipendi utani wa kujinga , nimetoka
kuzungumza na Colin hata robo saa haijapita.
Sasa wewe fanya utani naomba umpigie simu
mama yake sasa hivi , mweleze Colin amepata
ajali na amekimbizwa Muhimbili. Naomba
usiongeze lingine usije muua mama wa watu
kwa mshtuko . Najua anampenda sana
mwanaye ndiye kama mboni ya macho yake .
Japo siamini nitampigia tu.
Fanya haraka, unaambiwa hata gari alilokuwa
akiendesha limeteketea lote .
Mungu wangu! Brenda unasema kweli ? Mage
aliuliza kwa sauti ya kilio.
Kweli , siwezi kukutania kwa jambo zito kama
hili.
Mungu wangu hii nuksi gani ? Kama Colin akifa
nitakuwa na faida gani ya kuendelea kuishi,
Mage alizungumza peke yake huku macho
yamejaa machozi na mikono kumtetemeka
wakati wa kutafuta namba ya mama Colin .
Kila alivyokuwa akilitafuta machozi yalizidi
kuyafunika macho yake hata alipoyafuta kwa
mkono yalijaa tena. Alitoka chumbani na simu
mkononi hadi sebuleni na kumkuta mama yake.
Mage nini ? mama yake alishtuka na hali ya
mwanaye.
Colin mama, alisema huku akilia na kumpa
simu mama yake .
Colin ! Kafanya nini ?
Ajali.
He ! Lini ?
Sasa hivi .
Taarifa umezitoa wapi ?
Kanipigia Brenda sasa hivi ?
Dah! Vipi hali yake .
Na ..na. .sikia a ..a ..meku . .
Wewe mtoto ishia hapohapo, mama Mage
alimkata kauli mwanaye hakutaka kulisikia
neno la mwisho kwa vile aliamini litamuumiza
moyo wake .
Mama mpigie simu mama yake hana habari.
Mmh !
Mama Mage alichukua simu yake kutafuta
namba ya mama Colin huku naye mikono
ikimtetemeka. Baada ya kuipata alipiga simu
ambayo ilipokelewa upande wa pili .
Haloo dada vipi ?
Kwema , una habari gani?
Za nini ?
Kuhusu Colin .
Mmh ! Sina habari zozote.
Kuna taarifa kapata ajali.
Ajali!? mama Colin alishtuka .
Eeh , ndiyo , kuna mtu kampigia simu Mage na
kutaka tukujulishe kwa vile hakuwa na namba
yako ya simu .
Mungu wangu wee, yupo katika hali gani?
Hebu subiri , alisema na kuziba sehemu ya
kuzungumzia na kumgeukia Mage .
Eti Mage mwili wa Colin umepelekwa hospitali
gani?
Mama sijasema amekufa ila watu wanafikiria
hivyo, Mage alimgeuka mama yake .
Sasa kapelekwa wapi ?
Mama mwambie amekimbizwa Muhimbili, ila
usimwambie yupo vipi . .
Itaendelea Jumamosi ijayo .