Hisia Zangu-15
Pam alifungua mlango wa gari, Lilian naye akafanya hivyo. Wakashuka na kuibamiza kwa nguvu. Wakatembea wakiwa wameshikana mikono hadi Mapokezi ambapo Pam alichukua funguo.
Waliamua kutumia ngazi kupanda hadi ghorofa ya nne kilipokuwa chumba alichochukua Pam. Pam akafungua mlango. Lilian alishangazwa sana na namna chumba kile kilivyokuwa kimepambwa vizuri na kuvutia.
Zaidi alishangaa kuona kadi zikiwa zimezagaa kitandani. Pam akasimama nyuma yake kisha akamshika kiuno, akasema: Happy Birthday Lilian, Happy Birthday to you!
Lilian akashtuka sana!
Siamini Pam mpenzi wangu, leo ni birthday yangu?
Ndiyo mpenzi wangu. Hongera sana! akasema tena Pam.
Ahsante kwa kunijali. Yaani nilikuwa nimeshasahau kabisa, akasema Lilian huku akimwaga machozi.
Yalikuwa machozi ya furaha.
MARA zote huwa hakumbuki siku yake ya kuzaliwa. Aliyekuwa akimkumbusha kuhusu siku yake ya kuzaliwa alikuwa ni mpenzi wake Edo na wakati mwingine rafiki zake akina L (Latifa, Lucy na Leila) ambao humnunulia kadi na kumwimbia nyimbo za Birthday.
Siku hiyo Edo hakumkumbuka, wala hakumwambia kuwa ni siku yake ya kuzaliwa. Kitendo cha Pam kuonyesha kuikariri haraka ingawa penzi lao lilikuwa bado changa kulimchanganya sana Lilian na kuzidisha mapenzi kwa mwanaume huyo.
Lilian alimwangalia sana Pam kisha akamsogelea na kumbusu tena. Mashavu yake yalikuwa yamejaa machozi. Hakuamini macho yake.
Inanipasa nifanye hivi kwako, maana nakupenda kwa moyo wangu wote. Kwa nini unashangaa baby, mimi ndiye mwanaume wako, akasema Pam.
Unaniahidi Pam?
Ndiyo.
Nimefurahi sana kusikia hivyo.
Kilikuwa chumba nadhifu sana, kisafi chenye nakshi za kila aina ndani. Macho yao kwa pamoja yalifurahishwa na kila kilichokuwa ndani ya chumba kile.
Ingawa walikuwa wawili tu, Pam alikuwa ametayarisha shampeni. Alichukua chupa kisha akaifungua kwa ustadi, iliporuka ilikwenda kumlowanisha Lilian alipokuwa amesimama.
Wakamimiana kisha wakaanza kunywa kwa furaha. Baada ya kunywa glasi moja moja, kwa kuwa haikuwa yenye kilevi, Pam alifungua mvinyo mwekundu ambao ulikuwa na kilevi kisha akajaza glasi mbili.
Akampatia Lilian moja na moja akaishika yeye. Wote kwa pamoja wakagonganisha glasi zao na kuanza kunywa kwa furaha. Walikunywa taratibu, hadi walipoanza kuchangamka!
Baby sasa inabidi tupate chakula, utapenda kula nini? Pam akamwuliza Lilian.
Utakachokula wewe, nami nitakula hichohicho.
Sawa, natamani sana tule samaki, wewe unaonaje?
Samaki ni sawa, samaki gani lakini?
Unapenda wa ziwani au baharini?
Ziwani ni wa watamu zaidi, itakuwa vyema kama watakuwa sato na chipsi... akasema Lilian akitabasamu.
Sawa mpenzi, ni chaguo langu pia.
Pam akasogea kwenye meza ndogo iliyokuwa na simu, akanyanyua mkonga wa simu kisha akabonyeza namba za mapokezi na kuunganishwa na jikoni, akatoa oda yake.
Waliendelea kuzungumza mengi mle chumbani, Lilian akijihisi kuzidi kumpenda Pam kuliko awali.
Najisikia kukupenda sana Pam, akasema Lilian.
Unamaanisha kuwa mwanzoni hukuwa ukinipenda?
Siwezi kusema hivyo ila ukweli ni kwamba, kwa sasa nahisi kukupenda zaidi ya mwanzo. Nakupenda sana.
Ahsante sana Lilian, mimi nilikupenda kwa dhati tangu mwanzo.
Sasa nakukaribisha rasmi kwenye moyo wangu, uwe mwanaume wangu wa kweli, akasema tena Lilian.
Nimefurahi kusikia hivyo, nakuhakikishia nitakuwa mwanaume mwema kwako. Nitahakikisha unakuwa mwenye furaha siku zote. Narudia kukuambia tena, nilikupenda tangu mwanzo, tangu naonana na wewe mara ya kwanza nilikupenda na ninauamini moyo wangu, akasema Pam akiachia tabasamu.
Ahsante my love, akasema Lilian.
Mlango uligongwa, Pam akasimama na kwenda kufungua. Alikuwa ni mhudumu amefika na vyakula walivyoagiza. Pam akapokea na kuingia navyo ndani.
Waliketi mezani kisha wakaanza kula kwa furaha. Kama walivyotarajia ndivyo ilivyokuwa, chakula kilikuwa kitamu sana na wote walikifurahia sana.
Baada ya chakula wakaendelea na vinywaji. Lilian hakujua kitakachotokea baadaye, kilevi kilivyomkolea alijikuta akijiachia kihasarahasara, michezo ya kimapenzi ya hapa na pale ikaanza.
Hapo ukawa mwanzo wa kuelekea kwenye dimbwi la mahaba. Kwa ushawishi wa Pam, Lilian akajikuta akiharibiwa usichana wake. Kwa mara ya kwanza alikutana na mwanaume.
Alipata maumivu makali sana. Lilian alivunja ahadi aliyokuwa amewekeana na mpenzi wake Edo. Maumivu makali aliyopata, ukichanganya na ulevi aliokuwa nao, alijihisi mchovu sana.
Pam na Lilian walilala hadi asubuhi hotelini hapo.
***
Lilian aliamka asubuhi na mapema. Alipojigeuza na kufumbua macho, akamuona Pam amelala pembeni yake, hapo akagundua kuwa kweli alilala na Pam.
Akili za pombe zilimtoka, sasa akagundua thamani ya usichana wake. Alimkumbuka Edo na ahadi walizowekeana. Alimtingisha Pam aliyekuwa bado amelala pembeni yake.
Akashtuka!
Vipi mpenzi wangu? Pam akauliza mara baada ya kushtuka usingizi.
Pam, kwa nini umenifanyia hivi? akauliza Lilian kwa hasira.
Tuliza hasira basi, kwani kuna nini kibaya mpenzi wangu?
Huoni kama ni vibaya siyo? Huoni ubaya? Ona sasa umeharibu usichana wangu! akasema Lilian.
Wasiwasi wako ni nini wakati wewe ni mpenzi wangu? Nipo kwa ajili yako mpenzi. Mimi ni wako na wala si kwamba nimekuwa na wewe kwa siku moja tu, umeshakuwa wangu na utandelea kuwa wangu milele.
Hayo ni maneno ya wanaume, siku zote wamekuwa na maneno ya kudanganya tu baada ya kupata wanachotaka, wanaondoka!
Mimi nikuache wewe? Nani kasema? Sibahatishi, naujua moyo wangu. Najiamini kuwa nakupenda kwa dhati, akasema Pam.
Kweli?
Nakuhakikishia, akasema Pam.
Lilian akajivuta kwa Pam, akalala kifuani mwake. Penzi jipya lilifumuka kwa wawili hao.
Waliamka kwa pamoja na kuelekea bafuni kuoga kisha wakavaa na kuondoka. Pam alimrudisha Lilian mpaka chuoni.
Lilian alikuwa na jambo moja tu kichwani mwake; angemwambia nini Edo kuhusu usichana wake? Hakuwa na jibu!
Huo ndiyo mtihani mgumu uliokuwa mbele yake.
Itaendelea.