Mhindi, dereva wa daladala ambaye alikuwa akipinda kona kuiacha Umoja wa wanawake aingie Maktaba, alijikuta akisimamisha gari ghafla na kushuka chini huku akitetemeka. Aliamini kuwa amegongana au kagongwa. Alipoona gari likiwa halina dosari, huku kila mtu kaduwaa akauliza, “Nini hiko nalia?”
Hakupata jibu.
***
Jibu alikuwa nalo mtu mmoja tu, Joram Kiango. Ni yeye aliyeona na kujua kilichotokea. Kakakuona alikuwa ameuawa! Mlio uliosikika ni silaha ya aina yake, ambayo tangu ilipogundulika iliaminika kuwa ilikuwa imekwisha tumiwa mara mbili tu. Mara ya kwanza ilitumika nchini Urusi, kwa amri ya Stalin. Ilitumiwa kumwondoa duniani mjerumani mmoja ambaye alijipenyeza hadi katika jeshi la Urusi , miaka nenda miaka rudi akiiba siri mbalimbali ambazo alikusudia kuzipeleka kwao. Wakati huohuo Urusi na Ujerumani ikiwa katika vita, Stalin aliamuru bunduki hiyo itumike juu yake ikiwa pia kama sehemu za majaribio kwa silaha hiyo. Matokeo yake yaliwasisimua sana warusi.
Lakini matokeo hayo yaliwavutia pia Wamarekani ambao walifanya jitihada zote hadi baada ya miaka kumi wakawa wameiba mbinu za kuitengeneza. Na walijikuta wakilazimika kuitumia miaka saba baadaye.
Kijana mmoja aliibuka kusikojulikana na kutangaza kuwa aliwahi kufanya mapenzi ya kimwili na mke wa Rais wa Marekani ambaye alikuwa madarakani wakati huo. Alidai kuwa anamtaka Rais huyo ajiuzulu, vinginevyo angezitoa hadharani picha za video alizopiga akifanya mapenzi na mama huyo. Siku chache baada ya madai hayo, kijana huyo alipokuwa akitoka nje ya nyumba yake, alisikia akiitwa na watu waliokuwa ndani ya gari lililosimama mbele ya nyumba hiyo. Wakati akilisogelea ulisikika mlio kama huu. Ukawa mwisho wake na mwisho wa madai yake.
Silaha hii, ambayo wenyewe huiita ‘kifutio’ ilikuwa kali kiasi kwamba mara unapopokea kipigo chake unasambaratika katika vipande vidogovidogo zaidi ya milioni mbili.Matokeo yake ni kwamba hakionekani kipande cha mfupa, nyama wala tone la damu. Unakuwa umefutika katika uso wa dunia kana kwamba hukuwai kuwepo.
Ni silaha hiyo iliyotumiwa kwa Kakakuona, mbele ya macho ya Joram Kiango. Sekunde moja alikuwa hai mbele ya macho yake, sekunde iliyofuata haikuwepo hata dalili yake.
Joram alilitazama jengo hilo kwa makini. Hakuona mtu wala kitu. Yeyote Yule aliyeifyatua bunduki hiyo alitumia mfadhahiko uliowakumba. Joram pia aliamua kuitumia fursa hiyo. Alitumia funguo zake Malaya, akalifungua gari la Kakakuona na kuichukua ile briefcase yake aliyokuwa nayo mkononi. Akaurudishia mlango na kuondoka taratibu.
***
Akiwa na shahuku kubwa ya kufahamu chochote ambacho angeweza kufahamu juu ya hayati Kakakuona, Joram Kiango hakwenda mbali. Aliivuka barabara hiyo ya UWT na kuingia katika moja ya majengo ya SIDO ambayo baadhi yamepangishwa kwa watu wanayoyatumia kama ofisi.
“Naomba kwenda haja,” alimweleza mtu wa kwanza ambaye alimkuta mbele ya ofisi mojawapo, msichana mtanashati ambaye alimchekea na kisha kumwelekeza kwa mkono.
Joram aliufuata mkono huo na kujikuta katika choo ambacho bila shaka hakikuwa na mwangalizi kwa jinsi kilivyokuwa kichafu. Hata hivyo, alijifungia kwa komeo, kisha akajibanza nyuma ya mlango huo na kuanza kuishughulikia ile briefcase ya Kakakuona. Kwa mtu wa kawaida, briefcase hizi zinafunguliwa kwa namna maalumu, ingemchukua miaka kuifungua. Lakini si kwa Joram Kiango. Yeye alikuwa na mbinu zake ambazo alizitumia kucheza na namba hizo. Dakika mbili baadaye tayari ilikuwa wazi ikimchekea.
Kati ya yote aliyoyategemea katika mfuko huo, kamwe hakutegemea kukuta mabunda mengi ya pesa za kigeni kiasi hicho. Kwa hesabu ya harakaharaka zilikuwa paundi za kiingereza laki moja. Zaidi ya pesa hizo ilikuwemo hati ya kusafiria yenye jina la Bruno Malapaka ambaye alielezewa kuwa raia wa Naijeria ambaye alikuwa ni mfanyabiashara. Picha ilikuwa ya Kakakuona. Chini ya vitu hivyo kulikuwa na bastola.
Joram alivitazama vitu hivyo kwa mshangao. Kwa kiasi fulani, mategemeo yake katika kuuchukua mfuko huo yalididimia. Alitegemea kupata maelezo ya kutosha ambayo yangemwezesha kufahamu mengi juu ya Kakakuona; aliajiriwa na nani, mwajiri yuko wapi, kwa nini anafanya mauaji hayo, na mengine mengi. Badala yake alichoambulia ni hati ya usafiri ambayo bila shaka yoyote ni ya bandia, bastola ambayo hakuihitaji sana na pesa ambazo bila ya Nuru kupatikana mapema, akiwa hai, kamwe zisingeweza kumfariji.
Kulifikiria kwake jina la Nuru kulimrejeshea hasira na hofu aliyokuwanayo juu ya usalama wake. Hisia zilimfanya ashuku kuwa waliomuua Kakakuona ni watu haohao waliotumwa kumkamata Nuru. Hisia zilionyesha kuwa mara baada ya Kakakuona kumfikisha Nuru mikononi mwao hawakuuona tena umuhimu wake. Hivyo, walichofanya ilikuwa kumlipa malipo waliomwahidi na kisha kumshawishi aondoke mara moja. Wakati akiondoka ndipo walipoamua kumfuta duniani kwa matumaini kuwa hakuna ambaye angeona wala kuelewa kilichotokea, jambo ambalo lingewafanya polisi waendelee kumsaka Kakakuona ambaye hayuko tena duniani hali wao wakiwa wametulia zao raha mustarehe.
Kuwa kwao na silaha hatari kama hiyo, ambayo ni wachache tu waliowahi kuisikia na uwezo wao kiuchumi, ni miongoni mwa mambo yaliyomfanya Joram azidi kuamini kuwa hawa hawakuwa watu wa kawaida. Licha ya kujizatiti kwao kwa kiwango hicho bado walikuwa wakatili kupindukia. Kitendo chao cha kumwua mtumishi wao, Kakakuona, kikatili kiasi kile, na kupuuza mamilioni ya pesa walizompa kulimfanya Joram aamini kuwa walikuwepo kwa kazi moja tu, kuua.
Hali hiyo ilimfanya ataabike sana moyoni kila alipowaza kuwa Nuru yuko mikononi mwao, mikononi mwa viumbe wasihofahamika, katili kuliko shetani mwenyewe.
‘Lazima atoke mikononi mwao… mapema iwezekanavyo…’ Joram aliwaza huku akiyasaga meno yake kwa hasira. Hata hivyo, alijirudi mara moja na kujaribu kuituliza hasira yake alipojikumbusha, kwa mara nyingine, kuwa dhamira kubwa ya watu hao, kwa kila aina ya ukatili wanaoufanya, ilikuwa kumtia uchungu na hasira, ili ashindwe kufikiri kikamilifu, jambo ambalo litamfanya akurupuke na kuangukia katika mikono yao kama kinda la ndege.
‘Lazima nitulie… nipange kila kitu kwa tuo…’ alijinong’oneza moyoni.
Akiwa ameituliza akili yake alijiuliza anafahamu nini juu ya maadui hao. Hakuna! Aliwaza kwa uchungu muda wote alikuwa akihangaika na Kakakuona ambaye sasa ni marehemu. Hivyo, alikuwa hajui chochote zaidi ya ukweli kuwa anapambana na watu wenye nguvu zote: kiuchumi, kiulinzi na kiukatili.
Chanzo pekee cha kufahamu juu ya watu hao ni katika jengo hilo la kampuni ya Kangaroo ambamo silaha iliyomwua Kakakuona ilitokea. Alijua kuwa jumba hilo au chumba katika jumba hilo kilihusika, kwa namna moja au nyingine, na mkasa huu. Ni hapo ambapo angeanzia. Hata hivyo, Joram alifahamu fika asingekurupuka na kwenda huko kwani ingekuwa sawa na kujitumbukiza wakati moto anauona, hakuwa na shaka kuwa maadui hao wanamsubiri kwa hamu.
Kwamba angehitajika kushughulika mara moja ili kumtoa Nuru katika mikono yao, hilo halikumsumbua tena. Alikuwa na uhakika kuwa Nuru alikuwa akitumiwa kama chambo cha kumfanya aharakishe kuwaendea, jambo ambalo lilimtia moyo kuwa wasingemdhuru kabla hajatokea.
‘Nitatokea… nikiwa tayari…’ aliwaza.
Wazo lake lilikatizwa kwa mlango kusukumwa kwa nguvu nyuma yake. Kitendo hicho kilifuatiwa na sauti nzito ya kiume iliyoita toka njeikiuliza, “vipi braza, bado tu?”
Ndio kwanza Joram akakumbuka kuwa alikuwa chooni. Akaitazama saa yake na kugundua kuwa alikuwa ametumia zaidi ya robo saa, akiwa amejifungia katika choo hicho cha watu. Sasa aliweza hata kusikia harufu kali ya mchanganyiko wa kinyesi na mkojo chooni humo.
Akahakikisha kuwa ameifunga briefcase hiyo kama ilivyokuwa na kutoka nje ya choo huku akijitia kufunga vifungo vya suruali yake. “samahani ndugu yangu.” Alimwambia kijana wa kiume aliyekuwa amenyoa panki, ambaye alikuwa kasimama nje ya choo hicho katika hali ya kubanwa sana na haja ndogo. “Tumbo lilikuwa likinisumbua sana,” alimlaghai.
“Shauri ya bia za Mtikila.” Kijana huyo alimjibu akiingia na kujifungia.
Joram aliduwaa hapo nje kwa muda. Kisha, akajiwashia sigara na kuipachika mdomoni. Kwa mwendo wa utulivu, alivuta hatua moja baada ya nyingine akielekea katika hoteli ya Mawenzi ambako alipanga achukue chumba na kuziifadhi zile pesa. Mengine yangefuata baadaye.
***
Wakati Joram Kiango alipokuwa ameduwaa chooni, Inspekta Kombora alikuwa pia ameduwaa robo kilomita toka hapo. Yeye aliduwaa akiwa ameliegemea gari lake kwa mgongo, katika hali ya kukata tamaa.
Hakutaka kuamini kuwa Kakakuona alimponyoka katikati kabisa ya mtego wake kama samaki katika mdomo wa mamba. Hakupenda kuamini ingawa hali iliashiria hivyo. Upekuzi wa hali ya juu kupita kiasi tayari ulikuwa umefanyika katika jengo zima.
Tayari Kombora alikuwa na malalamiko ya baadhi ya wapangaji hao, mmoja akidai kuwa alilazimishwa kutoka bafuni akiwa uchi,mwingine akidai kuwa kapigwa ngwara bila sababu; watatu wakilalamika kusukumwa na kusachiwa bila maelezo. Halikadhalika, kulikuwa na malalamiko ya kuvunjwa kwa kabati moja ambalo funguo wake ulichelewa kupatikana, kubomolewa kwa tundu la ndege, kuharibiwa kwa mafriji matatu na friza moja; kuchanwa kwa mazulia na mapazia yasiyo na idadi, n.k. yote hayo Kombora alijua yangeletwa kwake kwa maandishi. Hakujali.
Ambacho alijali, ambacho kilimtisha ni kule kutopatikana kwa dalili yoyote ya Kakakuona. Alikuwa ametoweka! Nuru akiwa mikononi mwake! Ni hilo lililomfanya Kombora aduwae, Na kwa mara ya kwanza maishani mwake alijikuta akiwa hajui la kufanya kwa dakika kadhaa.
Alipotanabai kuwa karibu vijana wake wote walikuwa wamerejea na kumzunguka kwa namna ya kusubiri maelekezo zaidi ndipo alipojiinua toka kwenye gari na kupiga hatua mbili tatu za taratibu, huku akiwaza. Mara akagundua kuwa hakujua awaze lipi zaidi. Ndipo ikamjia akilini kuwa alihitaji kupata muda wa kutuliza akili yake ili aweze kuwaza kwa makini zaidi.
“Wanne wabaki hapa na kulilinda jengo hili kwa uangalifu mkubwa kila dakika, kila upande wa nyumba uwe katika macho yenu; mpo?” alisema.
“Tupo.” Msaidizi wake wa karibu alijibu
“Vizuri. Nitarudi ofisini kwa muda. Baadaye nitaleta maelekezo mapya. Bado naamini mshenzi huyu yupo humuhumu ndani. Na sitamruhusu aiachie nyumba hii akiwa hai, alisema akigeuka kuliendea gari lake.
“Hayumo mzee, kama angekuwemo hata kama angekuwa amejigeuza sisimizi tungempata. Naamini hayo…” kachero kijana aliyeyasema hayo alilazimika kusita ghafla huku akiulaani ulimi wake baada ya kuona Kombora akimgeukia na kumtupia jicho kali, ambalo lilipenya uso wake na kuunyanyasa moyo wake kiasi cha kumfanya atetemeke miguu, jicho ambalo kamwe hatalisahau.
Kombora alipanda gari na kumwamuru dereva kuelekea ofisini. Lakini kabla dereva hajalitia moto wazo jipya lilimjia. Akashuka garini na kumwita tena sajini Kangua, msaidizi wake wa karibu “Nadhani tunahaja ya kutupia macho majumba ya jirani kabla ya kuendelea na ulinzi wa nyumba hizi. Unasemaje?”
“Wazo zuri afande,” Kanguru alimjibu “Kwasababu kama angekuwa humu ndani kwa vyovyote angekuwa amepatikana.”
Walifuatana kuiendea nyumba iliyokuwa kushoto mwa jengo hilo. Lilikuwa duka kubwa, la Mhindi mmoja aliyenenepa kupita kiasi. Mhindi huyo, ambaye bila shaka yoyote alikuwa anafahamu kuwa kwa jirani kuna jambo, alijizoazoa kwa tabu na kumfuata Kombora kaunta.
“Ndio bana kuba, iko taka nini?”
Kombora alimvuta nje ya wateja na watumishi wake, ambao walitega masikio yao kwa makini ili wasikie kinachoendelea. “Tungependa kuikagua nyumba yako hii.”
“Iko kosa gani? Mimi niko fanya biashara lali bana kuba. Bana Rema iko jua ivo. Iko toa michango mingi. Iko lipa kodi pato. Iko…” alisema huku akitetemeka.
Kombora angeweza kumwacha aropoke hadi mwisho wa maelezo yake, akiwa na hakika kuwa wafanyabiashara hawa hawakosi madhambi. Lakini kwa kuwa hakuwa na nafasi hiyo alimkatiza kwa kumwambia kwa upole, “Hatuna haja na wewe wala biashara zako. Tunataka tuone kama kuna uwezekano wowote wa mtu kupenya toka jengo hilo la jirani yako kupitia hapa kwako.”
“Hakuna mitu pita hapa,” alijitetea
“Tunajua. Lakini tunataka kuwa na hakika,” Kombora alisema akianza kuingia ndani. Mhindi huyo alimzuia kwa kono lake zito lililolowa jasho.
“Hapana taka… Ngoja mimi iko piga simu kwa waziri Rema ulizia yeye. Iko subiri.”
Kauli yake ilipandisha hasira za Kombora. Aliutoa mkono huo kifuani pake kwa pigo moja la kiganjakwa mkono wake wa kushoto. “Sikia,” baadae alifoka huku kamkazia macho makali mhindi huyo, “Ukiendelea kunipotezea muda wangu nitaruhusu vijana wangu ishirini waingie humu na kuipekua nyumba hii. Na nakuhakikishia baada ya dakika ishirini tu utakuwa mahabusu kwa makosa yasiyo na idadi.”
Ukali wa Kombora ulifikisha ujumbe katika kichwa cha Mhindi huyo. Kwa unyonge, huku akijitia kutabasamu, alimpisha Kombora na kumfuata taratibu huku akisema, “Mimi iko mitu mema iko penda saidia…”
Kombora hakumsikiliza alimwita hadi uwani akifuatiwa na msaidizi wake. Huko walikutana na ukuta mnene, mrefu ambao ulikingwa na vipande vya chupa. Kombora hakuona uwezekano wa mtu kuupanda ukuta huo katika muda mfupi kama ule. Akageuka kumtazama msaidizi wake ambaye macho yake yalionekana kuwa na wazo hilohilo.
“Kwa mtu kama Kakakuona ukuta huu unapandika. Lakini apande yeye, ampandishe na mateka wake kwa nguvu, huku akiwa na bastola mkononi sio rahisi.”
Hata hivyo, Kombora na msaidizi wake, bastola zikiwatangulia, walianza ziara ya chumba hadi chumba. Mhindi huyo ambaye tayari alikuwa ameamuru kufunga duka alikuwa akiwafuata nyuma huku akitetemeka na kulalamika kwa maneno mengi ambayo Kombora aliyapuuza.
Karibu kila chumba kilikuwa na vitu mbalimbali vya thamani kubwa kama mashine za kupozea hewa, TV, deki za video, mazulia, nguo na vitu mbalimbali. Kwa jinsi Mhindi huyo alivyokuwa akitetemeka Kombora alijua fika kuwa kama angehoji mengi juu ya vitu hivyo angegundua kuwa nyingi zilikuwa mali za magendo au hazikulipiwa ushuru bandarini, au zimelipiwa nusu n.k. hata hivyo hakuwa na muda huo hadi alipofikia chumba ambacho Mhindi alitetemeka hadi kutokwa na machozi wakati Kombora akimshurutisha kukifungua.
“Iko kupa pesa milioni, sawa?” alibembeleza.
Kombora alimshika ukosi wa shati na kumsukasuka kwa hasira hadi funguo zikamtoka mkononi. Sajin kangua alizidaka na kuufungua mlango huo. Huku bastola ikimtangulia alitangulia kuingia, Kombora akimfuatia, na kumvuta mhindi huyo ambaye baada ya kuona hana hila alijikaza kisabuni na kuendea sefu la chuma lililokuwa katika kona moja ya chumba hicho. Alilifungua na kutoa mabunda ya pesa za kigeni na kumkabidhi Kombora.
“One hundred thousand dollars. Please…”
Kombora alizichukua fedha hizo na kuzikabidhi kwa msaidizi, “Yaani hata benki ya fedha za kigeni unayo katika chumba hikihiki, sio?” alimwuliza “Very well. Suala lako litamalizwa na polisi,” aliongeza akizungumza katika redio call yake na kuombwa aunganishwe na kituo kikuu cha polisi. Kilipopatikana aliwataka kuja kumchukua mtu wao mara moja.
Alipomgeukia Mhindi huyo nusura amhurumie kwa jinsi alivyolowa jasho na mkojo ambao ulikuwa ukimtoka kama mtoto hali mwenyewe hana habari. Kombora alimtazama kwa dharau na kumwacha mikononi mwa kachero wake mmoja kuwasubiri polisi. Kisha, akaongoza kutoka akiifuata nyumba ya upande wa kulia.
Nyumba hiyo haikuwasumbua. Lilikuwa jengo la ofisi ya idara moja ya serikali moja ambayo wafanyakazi wake wote tayari walikuwa wameondoka na kumwacha mlinzi ambaye hakuwa na funguo. Baada ya kutazama Kombora aliona mara moja kuwa Kakakuona hakuwa katika jengo hilo pia. Kuta zilikuwa ndefu, imara, ambazo pia zilipambwa kwa vipande vya chupa.
“Turudi ofisini,” aliamuru kwa sauti ya unyonge.
Nyumba hiyo haikuwasumbua. Lilikuwa jengo la ofisi ya Idara moja ya serikali ambayo wafanyakazi wake wote tayari walikuwa wameondoka na kumwacha mlinzi ambaye hakuwa na funguo. Baada ya kutazama Kombora aliona maramoja kuwa Kakakuona hakuwa ndani ya jengo hilo pia. Kuta zilikuwa ndefu, imara ambazo pia zilipambwa kwa vipande vya chupa.
“Turudi ofisini,” aliamuru kwa sauti ya unyonge.
Wakati wakipanda magari yao walipishana na polisi wengi wenye magwanda ambao walikuwa wakimburura Yule Mhindi mwenye duka huku tayari alikuwa ametiwa pingu “Tutawaandikieni ushahidi mdogo tulionao dhidi yake.” Kombora alimwambia kiongozi wao ambaye alikuwa amesimama kwa ukakamavu mbele yake baada ya kupiga saluti ambayo Kombora aliipuuza.
Msafara wa Kombora ulitanguliwa na gari lake. Waliuacha mtaa huo na kuingia barabara ya umoja wa wanawake. Walipopinda kushoto na kuelekea hatua kadhaa Kombora alitupa macho kulia na kuliona jengo ambalo kwake limekuwa kama fumbo la aina yake, fumbo lililomtia aibu na hasira kubwa kwa kushindwa kulifumbua.
Jengo hilo lilionekana nyuma ya jengo jingine la ghorofa mbili lililobeba maandishi yaliyosomeka Kangaroo Enterprises. Kampuni hiyo ilikuwa sambamba mgongo kwa mgongo na Sunrise Modern Club. Hisia zilimfanya Kombora ashuku kuwa inawezekana kabisa Kakakuona alitorokea katika jengo hilo. Akaamuru gari lisimamishwe mara moja. Huku akimwashiria Kanguru kumfuata, alishuka na kuliendea lango la kampuni hiyo.
Mlango ulifunguliwa hata kabla hawajaugusa. Aliyeufungua alikuwa askari aliyevaa magwanda ya mgambo ambayo ilionyesha ni moja ya kazi yake kuwafungulia wageni wote mlango waingiapo na watokapo.
Ilikuwa moja ya zile ofisi nyingi ambazo unaweza kudhidharau kwa nje lakini ndani ukaziogopa. Ndio kwanza Kombora na msaidizi wake wakagundua kuwa walikuwa wamechakaa kwa jasho baada ya kujikuta katika chumba hicho cha mapokezi, chenye vioo kila upande ambavyo viliwafanya wajitazame. Chumba kilikuwa na hewa safi ambayo ilikuwa ikitokea katika vipozea hewa. Mbele yao, nyuma ya meza ya mapokezi kulikuwa na wasichana wazuri watatu. Kushoto kwao kulikuwa na msichana mwingine, nyuma ya ukuta wa kioo, ambaye alikuwa akiendelea kuwachekea huku akisema kwa mara nyingine, “Karibuni kwenye viti.”
Kombora alianza kujiona mpumbavu kwa uamuzi wake wa kuingia humo. Kati yao hakuna aliyeonekana kuwa na wasiwasi wowote juu ya lolote ambalo lilitokea nje ya ofisi hiyo.
Kakakuona hakuwa amepita hapo. Alishawishika kuketi kwenye makochi ya kuvutia chumbani humo, kutokana na uchovu aliokuwa nao.
“Kangaroo Enterprises shughuli zenu hasa ni zipi?” Alimwuliza msichana huyo ambaye alianza kupoteza tabasamu lake kutokana na jinsi alivyomwona mgeni wake.
Kabla ya kujibu msichana huyo aliinama na kuinuka huku mkono wake ukiwa umeshikilia kijitabu chenye kurasa zaidi ya ishirini zilizochapwa kwa rangi mbalimbali ndani na nje. Juu ya kijitabu hicho lilitajwa jina la kampuni hiyo na nenoCatalogue chini yake. Kombora alikipokea na kukididimiza mfukoni mwake. Msichana huyo alipoona hana walau nia ya kukitupia macho alisema kwa sauti ya kibiashara “Tuna fanya mambo mengi, tunajenga viwanda, tunasafirisha watalii, tunaagiza na kuingiza mali nje ya nchi, tuna maduka ya kubadili fedha n.k. Hii ni ofisi kuu hapa nchini. Ni tawi la kampuni ya Kangaroo yenye makao yake makuu nchini Marekani na matawi katika nchi mbalimbali za dunia” msichana huyo alieleza kwa ufasaha. Alipoona maelezo yake hayaelekei kumvutia. Kombora aliongeza harakaharaka.
“Sijui nikusaidie nini mzee wangu?”
“Naweza kumwona bosi wako?” lilikuwa jibu la Kombora
“Bosi huwa hapatikani kwa urahisi, labda ueleze shida yako ili tumwulize kama anahitaji kukuona..”
“Shida yangu ni kumwona yeye!” Kombora alijibu kwa sauti nzito iliyoonyesha madaraka. Alipomwona msichana huyo kaduwaa aligeuka na kuufuata mlango ulioandikwa Mkurugenzi Mkuu.
Akifuatana na msaidizi wake, walipanda ngazi ambazo ziliwachukua hadi ghorofa ya kwanza ambapo walijikuta ndani ya ofisi nyingine iliyojaa watu ambao pia walikuwa katika mishughuliko mingi. Alikuwepo msichana mwingine wa mapokezi. Kwa mshangao wa kombora msichana huyo aliwaelekeza kwa adabu katika chumba kilichoandikwa Mkurugenzi Mtendaji. Nje ya ofisi hiyo kulikuwa na chumba cha kusubiria chenye makochi bora zaidi, ambayo yaliizunguka meza ndogo iliyojaa makabrasha ya kujisomea. Kombora hakuketi. Aligonga mara moja mlango wa mkurugenzi na kisha kuusukuma. Ulifunguka na kumruhusu kuwa ndani ya chumba kipana nadhifu, ambacho kilinukia kila dalili ya pesa. Zulia lililotandikwa hapo sakafuni lingetosha kujenga madarasa matatu ya shule ya msingi, meza kubwa iliyokuwemo ingeweza kuwafanya ombaomba kuwa matajiri kwa miaka mitatu. Viti vilivoizunguka meza hiyo vingewafanya watoto wa mitaani wanane wasahau kuwa hawana wazazi.
Lakini vitu hivyo havikumvuta Kombora kama alivyovutwa na mtu aliyeketi nyuma ya meza hiyo pana akiwatazama. Kombora alitegemea kumkuta Mkurugenzi wa kampuni iliyonona kama hiyokuwa mtu aliyenona, mtu ambaye hakuhitaji kujitambulisha ili umtambue.
Badala yake aliyeketi nyuma ya meza hiyo alikuwa mtu wa kutisha au kutatanisha. Haikuwa rahisi kujua kama alikuwa mzungu au mwafrika kutokana na kovu kubwa jeusi ambalo lilikula nusu ya uso wake, kuharibu jicho lake moja na kuchoma robo tatu ya nywele zake kiasi cha kumfanya awe katikati ya mataifa hayo mawili.
“Yes. Sir what can l do for you?” mwenyeji huyo alimwambia Kombora ambaye tayari alikuwa ameketi mbele ya kimojawapo ya viti hivyo.
Kabla hajajibu Kombora alitia mkono mfukoni mwake na kutoa moja ya kadi zake, ambazo humfanya awe na cheo kidogo kuliko kile cheo chake kamili, kile ambacho ni siri yake yeye pamoja na mkuu wa nchi. Meneja huyo alipokea kwa mkono wake wa kushoto, jambo lililomfanya Kombora aamue kuutazama mkono wa kulia na kugundua kuwa ulikuwa wa bandia ambao ulitengenezwa kwa mbao au plastiki kwa ufundi kiasi cha kufanana na ule wa kawaida.
“Vita… vita sio mchezo. Vita vya Angola ndiyo ilinifanya hivi,” alisema ghafla kana kwamba alikuwa akiyafuata macho na mawazo ya Kombora. “ Kwa hiyo wewe ndiyo Inspekta Kombora? Tumekuwa tukizisikia jitihada zako. Hongera sana.”
Kombora hakujua ni jitihada zipi hizo, na huyo bwana alizifahamu vipi, “Sijui na wewe mwenzangu unaitwa nani?” aliuliza badala yake.
“Naitwa Paul Powel. Ni mkurugenzi mwendeshaji wa kampuni hii. Sina budi kushukuru sana kutembelewa na mtu mzito kama wewe.”
Kombora alihisi kitu kama kebehi katika sauti yake. Naam, aliweza hata kuiona waziwazi katika jicho lake moja ambalo lilikuwa likimcheka ingawa mdomo wake ulikuwa hauna tabasamu lolote.
“Vizuri.” Alimjibu kwa utulivu. “Shida yetu ilikuwa ndogo sana. Kuna mtu wa hatari ambaye ametoroka jengo la jirani yenu upande wa pili wa mtaa. Tulichohitaji ni kukagua jengo zima ili tuwe na hakika kuwa hayuko humu ndani.”
Powel alicheka. “Jengo hili haliingiliki hovyo. Tuna biashara ya mamilioni hapa, hivyo tumelijenga kwa usalama wa hali ya juu. Mtu atakayeingia hapa itambidi kupitia mlangoni peke yake…”
“Hilo tunaelewa. Lakini kiutaratibu lazima tuhakikishe kwa macho yetu wenyewe, kwa usalama wenu…” Kombora alilazimika kusita ghafla alipoona pazia lililokuwa nyuma ya Powel likifunuka
taratibu na Powel mwingine kuingia ghafla kama kivuli na kuketi kwenye kiti kilichomuelekea Kombora.