Hadithi: Roho ya paka. (Ben R. Mtobwa)

Hadithi: Roho ya paka. (Ben R. Mtobwa)

jamani hizi simulizi mi zinanikosha kweli.nimejitahidi kuchangia kidogo kwa kunua nakala mbili sasa.za Ben.1tutarudi na roho zetu na 2 salamu toka kuzimu.vyote nimenunua kariakoo.asanteni wadau mlionielekeza sehemu ya kuvipata.
 
9

Penye wengi hapakosi mengi. Katika mkusanyiko wa wasafiri waliokuwa wakiisubiri Sea Express bandarini Dar es Salaam, ili iwapeleke Zanzibar kulikuwa na pilikapilika nyingi ambazo hazikuwa na msingi wowote. Kwa mfano, pamoja na ukweli kwamba kila msafiri alikuwa na tiketi yake mkononi, yenye namba ya kiti chake, bado kuna wale waliojifanya kuwa wana haraka zaidi ya wengine. Hawa walikuwa wakikimbia huku na huko, mizigo mikononi, na kisha hukaa katika ukingo wa kivuko tayari kuivamia meli hiyo ambayo ndio kwanza ilikuwa inatia nanga.

Milango ilipofunguliwa na abiria watokao Zanzibar kuanza kushuka taratibu abiria hawa “wenye haraka” walikuwa kikwazo kwa jinsi walivyosababisha msongamano mkubwa mlangoni hapo. Watumishi wa Bandari walifanya kazi ya ziada kuwadhibiti abiria hao ili wenzao washuke kwa utaratibu.

Kati ya abiria hao wenye haraka alikuwamo Joram Kiango. Pengine yeye alikuwa na haraka zaidi ya watu wote katika msafara huo. Lakini, kama kawaida yake haraka au shauku yake ya safari hiyo ilikuwa siri yake binafsi. Usoni alionekana mtulivu, ambaye isingekuwa rahisi kufahamu kama anasafiri, amekuja kupokea mgeni, au anasindikiza.

Aliketi juu ya kiti cha mbao, ambacho wasafiri wengi walikiacha na kusimama wima na mizigo yao. Akiwa katika mavazi yake yaliyomfanya awe mtu asiyetazamika sana, yaani kanzu ya kawaida, kijikoti juu ya kanzu hiyo, kilemba kichwani na ndevu za bandia huku kijimfuko kidogo kikiwa miguuni pake, hakuna aliyejisumbua naye.

Lakini yeye alikuwa akijisumbua na kila mtu. Macho yake yenye uzoefu yalimpitia karibu kila mtu katika umati huo. Watu wawili katika umati huo walimsumbua. Ingawa walikuwa wageni kwake, lakini macho yao na tazama yao ilimfanya Joram aone kuwa si wasafiri wa kawaida. Neno “kachero” lilikuwa wazi katika tazama yao, zungumza yao na simama yao.

Joram alihisi kuwa hawa pia wako safarini kwenda Zanzibar kumfuatilia Kakakuona, jambo ambalo halikumpendeza kwani alitamani sana ngoma hiyo aicheze peke yake. Hata hivyo, alitulia kimya, akiendelea kutazama kwa makini zaidi, aone nani mwingine yumo katika msafara huo.

Kwa uzoefu wake wa upelelezi hiyo haikuwa kazi kubwa kwake. Alifuatilia tazama ya makachero hao wawili. Kila walipoelekeza macho yao kwa hila, yeye pia aliyaelekeza huko kwa mbinu, akichunguza ishara zote.

Haukupita muda mrefu kabla Joram hajakipata hicho alichokusudia. Macho ya makachero hao yalikosea kulitazama gari moja, aina ya Toyota Land Cruiser, lililokuwa limepaki nje kidogo yabandari, ndani yake mkiwa na watu watatu. Joram Kiango alimtambua mmoja kati yao mara moja. Alikuwa Inspekta Kombora.

‘Kombora pia anakwenda Zanzibar!’ Joram alijiuliza kwa mshangao. Ndio kwanza akahisi kuwa Kakakuona ni mtu hatari sana. Awali ya hapo alimchukulia kama mtu kichaa tu, ambaye anaua watu wanyonge na kumteka mtu asiye na hatia, kama Nuru, kwa sababu zake anazozijua yeye mwenyewe, ambazo Joram Kiango hakuona kama angepata muda wa kuzifahamu kwani alichokusudia, mara tu baada ya kukutana na kichaa huyo ana kwa ana, ilikuwa kumuua kwanza, kumuuliza maswali baadaye.

Akaamua kumpuuza Kombora na makachero wake wote na kuendelea kuwasubiri abiria waliokuwa wakiendelea kushuka kutoka katika chombo hicho waishe ili awe miongoni mwa watu wa kwanza kuingia.

Kama kawaida ya abiria wa meli, ile haraka yao ya kupanda waanzapo safari, haitofautiani sana na ile ya kushuka wanapofika mwisho wa safari. Hivyo, pilikapilika zilikuwa nyingi. Joram alitulia akiwatazama abiria hao, hali fikra zake zikiwa nje kabisa ya eneo hilo. Hakuwatilia maanani watu mbalimbali waliopita mbele yake, mizigo yao mikononi.

Lakini haukupita muda kabla hajashuka abiria mmoja aliyemfanya agutuke ghafla kama aliyenaswa na waya wa umeme. Kama si mzoefu katika masuala ya upelelezi angeweza kuinuka na kumkimbilia abiria huyo. Angeweza kumkumbatia na kumbusu. Lakini si yeye. Pamoja na kushtuka kwake, pamoja na kutoyaamini macho yake, alitulia kwa utulivu kana kwamba abiria huyo ni miongoni mwa abiria wa kawaida machoni mwake; kana kwamba hamfahamu na wala hajapata kumwona maishani mwake.

Abiria huyo alikuwa msichana mzuri kupita kiasi, mwenye umbo zuri kupindukia, alilolificha katika baibui alilojitanda juu ya mavazi yake. Mkono mmoja wa abiria huyo ulikuwa umeshika briefcase ya kiume hali mkono wa pili umeshikana na ule wa kijana mmoja ambaye alionekana kama mpenzi wake. Mkono wa pili wa kijana huyo wa kiume ulikuwa ndani ya mfuko wake wa koti.

Abiria huyo wa kike hakuwa mwingine zaidi ya Nuru.

Wala Joram hakuhitaji kuambiwa kwamba mtu huyo aliyeandamana naye alikuwa mtu baki zaidi ya Kakakuona.

Kwa mtazamo wa kawaida, mtu yeyote angepata hisia kuwa abiria hao walikuwa wapenzi wawili ambao ndio kwanza wameoana, hivyo, wanatoka zao Zanzibar kusheherekea ndoa yao. Lakini kwa mtazamo wa mtu kama Joram alifahamu fika kuwa uhusiano wa kimapenzi baina ya viumbe hao wawili ulikuwa sawa na ule wa kondoo na mbwa mwitu. Joram aliona wazi kuwa Nuru alikuwa ametekwa nyara na mtu huyo. Aliona wazi vilevile kuwa mkono wa mtu huyo uliofutikwa mfukoni ulikuwa umeshikilia bastola iliyomlenga Nuru kikamilifu na asingesita kuifyatua iwapo lolote lingetokea.

Adui huyo alikuwa akitembea kwa mwendo wa kujiamini kwa kiwango kilichomshangaza Joram. Hakutarajia muuaji mwoga, kiasi cha kuua watoto wa kike wasio na hatia, angeweza kuwa na moyo sugu kiasi hicho.

Macho ya Joram yaligongana na ya Nuru. Mavazi bandia aliyoyavaa hayakuwa kipingamizi cha kumfanya Nuru asimtambue mara moja. Joram alihisi kitu kama faraja ikichepuka ghafla katika macho yake mazuri.

Hata hivyo, akili yake ilikuwa nzuri vilevile kwa kiwango ambacho kilimfanya Joram Kiango azidi kumheshimu. Zaidi ya kumtupia jicho hilo moja la kawaida kama ilivyokuwa kwa watu wengine, Nuru aliendelea na safari yake kama kawaida.

Pamoja na uduni wa mavazi yake, Joram alikuwa kamili kikazi. Isingemchukua sekunde moja kuifikia bastola yake na kuufumua ubongo wa Kakakuona. Hali kadhalika, maungo yake yalikuwa yakichemka kwa hamu ya kumfanyia mazoezi ya judo mpuuzi huyo.

Hata hivyo, kwa kuchelea kuyanadi maisha ya Nuru, hasa baada ya kukumbwa na misukosuko yote ile isiyokadirika, Joram aliamua kuacha mchezo huo uendelee kidogo.

Jambo lingine lililomfanya Joram aahirishe kumchukulia hatua muuaji huyo ni ile heshima au hadhi mpya ambayo alijikuta akimpatia muuaji huyo kutokana na kitendo chake hicho cha aina yake. Halikuwa jambo la kawaida muuaji ambaye anafahamu fika kuwa anawindwa zaidi ya kifaru mwenye kichaa, kujitokeza hadharani, mchana kweupe, akiwa na mateka ambaye ni mwanamke hatari zaidi ya nyoka aina ya swila. Hivyo, Joram alijikuta akiamua kujionea kitu kinachomtia ujeuri huo.

Kisha, akamkumbuka Kombora na makachero wake. Ndio kwanza akafahamu kuwa hawakuwa safarini, bali walikuja kwa ajili ya kumlaki mwuaji huyo kwa matumaini ya kumkamata.

Akageuka kuwatazama makachero hao. ‘Polisi ni polisi, avae magwanda asivae,’ Joram aliwaza alipoona hali ya makachero hao. Japo walijitahidi kujikaza, kana kwamba hakuna kinachoendelea, lakini hakushindwa kusoma ramani ya misukosuko katika nyuso zao.

Kila mara mikono yao ilichopoka na kupelekwa mifukoni, kuzipapasa bastola zao; miguu yao ikichezacheza kwa namna ya ukosefu wa utulivu mioyoni mwao. Mara kwa mara waliyatupa macho yao katika gari alilokuwemo Kombora kwa namna ya watu wanaosubiri amri ili wafanye jambo, amri ambayo Joram hakuona kama Kombora alikuwa tayari kuitoa kwa jinsi alivyopigwa butwaa ingawa alijifanya mtulivu; akivuta sigara yake, gazeti mkono wa pili.

Wakati huo Kakakuona na Nuru walikuwa wakimaliza ngazi na kuanza kutoka nje ya banda. Kakakuona aligeuka kumtazama mmoja kati ya makachero wa Kombora kwa namna ya kumwambia, “Nimekutambua.”

Joram alihisi kuona tabasamu la kebehi katika macho hayo.
 
***

Kama kuna siku ambayo Inspekta Kombora aliwahi kuhisi akili yake imeduwaa, huku fikra zake zikiwa zimedumaa, ni hii. Mwili mzima ulimlegea, mikono ikamtetemeka kwa kitu ambacho asingeweza kukipambanua kati ya hasira na aibu. Sigara ambayo aliiwasha kitambo iliendelea kuteketea mdomoni mwake.

“Mzee… anakwenda zake… Tufanye nini mzee?” mmoja kati ya wasaidizi wake, aliyekuwa kiti cha nyuma cha gari hilo alimuuliza Kombora akigeuka kumtazama, ingawa macho yake yalidhihirisha kuwa alikuwa hamwoni.

Akili yake bado ilikuwa imepaa au kuzama katika lindi refu la mshangao na kutoyaamini macho yake.

Zaidi ya saa moja iliyopita alipokea habari toka Zanzibar kuwa Kakakuona ambaye alitoweka ghafla, aliibuka toka katika mitaa ya mji huo akiwa amefuatana na msichana ambaye alionekana kama Nuru. Kombora aliwakumbusha waendelee kumchunguza bila kumshtua. Lakini dakika tano baadaye, alipoambiwa kuwa Kakakuona alikuwa akija Dar es Salaam kwa Sea Express na kwamba Nuru alionekana kama ambaye yuko chini ya ulinzi, aliongoza kikosi cha vijana wake wazuri, sita, ambao walikuwa tayari; wakisubiri amri yake.

Kombora alisita kuitoa amri baada ya kuona kile ambacho hakutarajia kukiona katika macho ya Kakakuona. Kitu kisichoelezeka kwa jinsi kilivyofungwa pamoja katika fungati la ukatili, dharau, unyama na dhihaka ya hali ya juu.

Kombora alishangaa alipoona kuwa Kakakuona alijua fika kuwa amezingirwa na makachero wengi, ambao walikuwa tayari kumuua mara tu wapewapo ishara, lakini bado alipita kwa kujiamini. Dharau yote hiyo ya Kakakuona ilitokana na ukweli kuwa asingekufa kabla hajamuua Nuru, jambo ambalo alifahamu kuwa yeyote duniani asingelifanya kwa urahisi.

Kwa ajili ya unyama wa mtu huyo, kwa jinsi ambavyo alikuwa anaendelea kuteketeza maisha ya watu wasio na hatia, Kombora angekuwa tayari kutoa amri avamiwe na kuuawa bila kujali ambacho kingemtokea msichana huyo.

Ndiyo, angefanya hivyo, iwapo tu msichana huyo asingekuwa Nuru.


Nuru ni mmoja kati ya wasichana wachache wenye nafasi ya pekee katika moyo Kombora. Ingawa hakupata kumwambia hivyo waziwazi, lakini aliheshimu sana mchango wake katika harakati za yule mpenzi wake Joram Kiango.

Kombora asingeweza kusahau jinsi msichana huyo alivyobadilika kutoka katika umbile laini la kike na kuwa jabali la chuma tangu aliposhirikishwa katika ule mpango wa kinyama wa kuwaua viongozi wa nchi huru za Kiafrika mjini Arusha, mkasa ambao tayari umehifadhiwa katika kitabu kinachoitwa Salamu Toka Kuzimu ambao kwa jinsi unavyotisha hata baadhi ya watu wanauchukulia kama riwaya ya kubuni.

Baada ya hapo ndipo Nuru alipoamua kuudhihirisha uanamapinduzi wake katika visa na mikasa kadha wa kadha ambavyo pia vimetolewa vitabu vinavyoitwa Tutarudi na roho zetu? Malaika wa Shetani na vinginevyo.

Kazi ya Nuru katika mikasa hiyo ilikuwa kubwa kiasi kwamba bila ya yeye pengine Joram Kiango asingekuwapo duniani leo hii.

Kombora hakuona kama inayumkinika kutoa amri msichana kama huyo afe kwa ajili ya kumwogopa Kakakuona na unyama wake. Akaendelea kuduwaa.

“Mzee… wanaondoka,” msaidizi wake aliendelea kumkumbushia.

Wakati huo Kakakuona alikuwa akimaliza kuingia katika gari la kukodi, aina ya Datsun, baada ya kumtanguliza Nuru kukaa na dereva mbele, yeye, nyuma. Dereva akiwa haelewi lolote alitia gari moto na kuondoka taratibu.

Wakati gari hilo likiondoka, kijikaratasi cheupe kilidondoka toka dirisha la nyuma. Mmoja kati ya makachero wa Kombora alikiokota. Baada ya kusoma alikileta kwa Kombora huku akiwa na dalili za mshtuko mkubwa. Alimkuta Kombora akiongea katika Redio call kuwaarifu watu wake waliokuwa nje ya eneo hilo walifuate gari hilo kwa hila. Aliwapa namba za gari na rangi yake.

Kisha, aliitupa sigara yake ambayo ilikuwa imekwisha na kujiwashia nyingine.

“Ni nini?” alimuuliza askari huyo huku akipokea kipande cha karatasi.

“Ujumbe.”

“Ujumbe gani?”

Ulikuwa ujumbe mfupi ambao uliandikwa kwa peni ya wino mweusi;

Fanyeni upumbavu wa aina yoyote ile mtashangaa kuiokota maiti ya msichana huyu barabarani ikiwa na sura ya wale waliotangulia. Na sipendi kufuatwafuatwa.

Kakakuona.

Kombora aliisoma kwa mara ya pili. Kisha, akaitumbukiza katika mfuko wa koti, hasira zikichemka kichwani mwake, kutokana na dhihaka hiyo ya Kakakuona. Kombora alijikuta akizungumza peke yake kwa minong’ono, “It’s too much. Kama anajua anafuatwa ya nini kuendelea kujificha?”

Kwa sauti alikoroma, “Ok, twendeni.”

“Wapi?”

“Mfuateni,” aliamuru. “Usijali kama atafahamu kuwa anafuatwa au la,” alimwambia dereva. “Anaonekana kama anayetaka tumfuate.”

Magari mengine matatu ya polisi, yenye namba za kiraia, ambayo yaliegeshwa katika eneo hilo yalianza kuondoka moja baada ya jingine, kwa maelekezo ya Kombora kupitia Walkie talkie yake magari mawili kati ya hayo yalilipita gari la Kakakuona, ambalo lilikuwa likienda kwa mwendo wa wastani, na kulitangulia. Mbele ya safari gari moja lilichepuka kama vile halina habari na msafara huo, la pili likiendelea taratibu.

Gari la Kakakuona liliifuata Barabara ya Sokoine na lilipoifikia Barabara ya Morogoro likaifuata, jambo ambalo lilifanya gari la makachero wa Kombora lililotangulia lipitilize hadi katika mzunguko wa Mnara wa Saa ambapo lilipinda na kuingia samora hadi walipopishana na Kombora, ambaye aliwaashiria kurudi ofisini kazi yao ilichukuliwa na teksi moja yenye namba za TX ambayo ilionekana kama imechukua abiria watatu.

Kichwa cha Kombora kiliendelea kusumbuliwa na hali ya kucheza na mtu kama Kakakuona. Alijihisi kuwa yeye na askari wake wote wako katika duru wakicheza ngoma wasiyoifahamu, ngoma ambayo mpigaji hakuwa mwingine zaidi ya Kakakuona mwenyewe. Jambo hilo lilizidisha hisia za hatari kichwani mwa Kombora.

Ingekuwa rahisi sana. Kati ya magari yake yaliyotangulia, moja lingeweza kusababisha ajali ya ghafla kwa lile lililomchukua Kakakuona, papohapo, yeye na askari wake kuivamia ili kumuua Kakakuona na kujaribu kumwokoa Nuru. Ni moja kati ya mambo ambayo yamekwishafanywa sana. Hata hivyo, ilikuwa kama kamari ambayo Kombora hakuwa tayari kuicheza. Hivyo, ikabidi aendelee kustahimili, akiruhusu magari yake yaendelee kumsindikiza Kakakuona kama shujaa anayepelekwa Ikulu kuchukua wadhifa wa nchi.
 
***

Kwa Joram Kiango ilikuwa kazi rahisi kuliko alivyotarajia. Mara tu alipomwona Inspekta Kombora akishindwa kuchukua hatua dhidi ya Kakakuona, badala yake akianzisha msafara wa kumfuata, yeye pia alifanya hima kuliendea mojawapo ya magari mengi yaliyokuwa yakisubiri abiria nje ya stesheni.

Alichagua gari jipya, aina ya Suzuki, lenye namba za Posta, ambalo ingawa dereva alidai kuwa yuko kazini, lakini Joram hakuchelewa kugundua kuwa alikuwa akisubiri abiria yeyote ambaye angemkodi ili ampatie chochote cha kutia mfukoni.

“Una petroli ya kutosha?” alimuuliza.

“Kwani unakwenda mbali mzee?”

“Itategemea,” Joram alijibu akizunguka upande wa pili ambako alifungua mlango na kuingia ndani. “Ifuate ile. Ifuate taratibu wasijue kuwa wanafuatwa.”

Dereva huyo alionyesha wasiwasi kidogo. “Gari ile, mzee! Kwa nini tuifuate? Unajua…” alisita kidogo. Lakini alipoona kitita cha shilingi elfu tano kikiwekwa juu ya mapaja yake alionekana kubadilika kidogo.

“Wakienda mbali zaidi nitakuongeza,” Joram alisisitiza, huku akimhimiza kuondoa gari.

“Tatizo ni kwamba ile gari naijua brother,” alisema akiondoka shingo upande. “Ile ni gari ya wenyewe ile. Inatumiwa na manjagu, pamoja na kuwa na namba za kiraia. Naogopa wasije wakaniletea matatizo wakijua kuwa wanafuatwa.”

“Usijali, hawatafahamu.”

Akili ya Kakakuona ikiwa juu ya magari ya Kombora ambayo alikwishayakariri namba zake vizuri sana kichwani, hakujishughulisha na gari dogo la Posta ambalo lilionekana kwa mbali sana miongoni mwa magari mengine.

Aidha, Kombora vilevile fikra na hisia zake zote zikiwa katika gari la mbele yake, ambalo lilimchukua muuaji hatari kama Kakakuona, hangeweza kulitazama gari hilo la Posta lililokuwa nyuma yao. Hali kadhalika, ikiwa tabia ya polisi ni kufuata badala ya kufuatwa, kusaka badala ya kusakwa, wazo la kugeuka nyuma mara kwa mara halikumjia akilini kabisa. Tabia hii ilifanya kazi ya Joram na dereva wake iwe nyepesi kama ilivyokuwa.

***

Ulikuwa ni msafara usio na kona nyingi wala mizunguko mingi. Ilielekea kama Kakakuona alikuwa hana haja ya barabara nyingine zaidi ya ile ya Morogoro, Hata hivyo, walipofika Mtaa wa Jamhuri, gari hilo lilionekana likipinda kulia kuufuata mtaa huo. Gari la Kombora likafanya hivyohivyo. Joram pia akamwamuru dereva wake kuwafuata.


Njia hiyo ilikuwa na msongamano mkubwa wa magari hivyo, safari yao ilikuwa ya taratibu, jambo ambalo lilimtia hofu Kombora kuwa Kakakuona angeweza kuitumia fursa hiyo kuchepuka ghafla mahala ambapo asingekuwa mwepesi wa kuona alipoelekea.

Lakini Kakakuona hakuonekana kama mwenye haraka ya kufanya hivyo. Aliendelea na safari yake taratibu kama ambaye alikuwa na nia njema sana ya kumwongoza Kombora na msafara wake hadi alipoufikia uchochoro ambao unachepuka na kuunga mtaa huo hadi Mtaa wa Kisutu ambapo alionekana akisogea kulia na kuliingiza gari katika ukumbi wa jengo moja jipya, ambalo liliacha eneo zuri la kupaki magari chini yake kwa meta kama kumi ndani yake.

Kombora alilitazama gari hilo likipaki kwa utulivu. Alitumia dakika mbili tatu za kuduwaa, akijiuliza afanye lipi, kwa makini. Jengo hilo lenye ghorofa nne lilikuwa moja kati ya majengo mapya yaliyokuwa yakiibuka huko na huko jijini Dar es Salaam.

Vibao vya kampuni na biashara mbalimbali vilionekena katika kuta mbalimbali za jengo hili chini ya kibao kilichoandikwa Sunrise Modern Club. Kibao hiki kilimeza karibu robo ya ghorofa zima ya chini. Maandishi yake yalikuwa juu ya kioo kikubwa, kwa rangi mbalimbali ambazo usiku ziliwaka kwa namna ya kuchezacheza katika hali ya kuvutia macho. Kombora aliwahi kupita hapa mara nyingi usiku na kuvutiwa, kama watu wengine, lakini hakuwahi kuingia ndani. Kumwona Kakakuona akipaki hapo aliyakumbuka mauaji ambayo amekuwa akiyafanya katika hoteli na kumbi za starehe kama yale ya Lang’ata; akajikuta akipatwa na hisia za hatari kuliko awali.

“Liwalo na liwe,’ aliwaza. “Tunamfuata hukohuko ndani,” aliamuru, “Angalieni. La msingi ni kuyaokoa maisha ya Nuru. Hivyo, risasi za kwanza, kama itabidi, ziwe za kumvunja mabega, ili asiweze kuitumia mikono yake. Aliye kulia, alenge mkono wa …”

Kombora alilazimika kuyakatisha maongezi yake alipomwona Kakakuona akishuka huku akifuatiwa na Nuru ambaye alikumbatiwa kiuno kama wapenzi wa damu.

Walishuka harakaharaka na kuingia ndani ya jengo hilo.

Kombora, akiwaongoza askari wake wawili, pia alishuka na kumfuata. Alipolifikia gari lililokuwa likitumiwa na Kakakuona nusura atokwe na ukelele wa mshtuko, mshangao na hasira, alipomtazama dereva.

Alikuwa amelalia usukani wake akitapatapa; tundu kubwa la risasi likiwa limekifumua kichwa chake kisogoni, na kuruhusu damu nzito iliyochanganyika na ubongo iendelee kumwagika kama uji mwekundu unaomwagika toka katika birika.


“Haraka… ndani,” Kombora alinguruma akiitoa bastola yake na kutangulia ndani ya jengo hilo. Mlango uliwaongoza katika korido nyembamba iliyowafikisha katika chumba cha mapokezi, ambacho kilikuwa na makochi manne makubwa yaliyokuwa matupu. Makochi hayo yalikielekea chumba cha kioo ambamo hamkuwa na mtu. Kombora alitazama huku na huko kama anayeomba msaada. Aliiona lifti, na upande wa pili aliiona ngazi iendayo juu.

“Mmoja atumie lifti, mwingine apande kwa ngazi. Upesi. Kama nilivyosema, mkimwona msizungumze naye. Acheni risasi zizungumze. Ok?”

Wakati yule aliyeamriwa kwenda kwa miguu alipoanza kupanda ngazi harakaharaka na yule wa lifi akiita kwa kubonyeza tufe, Kombora aliitoa walkie talkie yake na kuwaamuru makachero wengine kuja mara moja. Kisha, akasogea kaunta bila kujua alihitaji nini. Kama awali alijisikia kupiga kelele, safari hii akijisikia kuzimia kwa kile ambacho alikiona chini ya meza hiyo ya kaunta.

Mzoga wa mtu ulikuwa umelala kifudifudi katika dimbwi la damu nyingi ambayo ilikuwa ikiendelea kujaa sakafuni. Dalili yoyote ya uhai haikuwamo katika umbile hilo ambalo sare alizovaa msichana huyo zilionyesha kuwa alikuwa mhudumu wa mapokezi.

Akili ya Kombora ilidumaa kwa kitambo cha robo dakika. Watu wawili, wasio na hatia, kuuawa huku yeye anashuhudia…! Aliwaza kwa uchungu. Alishindwa kuendelea kuwaza. Badala yake alikurupuka mbio kuiendea ngazi ambayo aliipanda kwa kuruka ngazi tatu tatu, bastola ikiwa imemtangulia.


***

Kwa Nuru ilikuwa kama mtu anayeshuhudia mchezo wa sinema ya kusisimua ambao yeye mwenyewe ndiye mtazamaji, wakati huohuo mwigizaji. Naam, ilikuwa kama ndoto tu; tangu alipojikuta akihama kutoka katika mikono ya yule muuaji Chongo na kuangukia katika milki ya Kakakuona. Kama kondoo, aliafiki kila alichoelekezwa. Aliafiki kuushika mkono wa muuaji huyo huku akitabasamu.

Kadhalika, aliafiki kupita kote huku akijua kabisa kuwa kila hatua anayopiga na muuaji huyo inamsogeza karibu zaidi na mauti yake mwenyewe.

Hata hivyo, ile kiu yake ya kufahamu kwa undani zaidi kiini cha mauaji haya ilikuwa sababu nyingine iliyomfanya aendelee na ukondoo huo. Aidha, ile bastola yake, ambayo aliificha vyema alipokuwa akioga bafuni ilimpa moyo na kumpa matumaini ya kupata fursa nzuri ambayo ingemwezesha kuyaokoa maisha yake mara mambo yatakapovuka kina.

Matumaini hayo yaliongezeka maradufu mara aliposhuka bandarini na kumwona Joram Kiango akimsubiri, bila ya Kakakuona kumtambua. Nuru alizidi kupata moyo.

Ilikuwa mara yake ya kwanza kumtia Joram Kiango machoni. Ile hofu yake kuwa tayari wauaji hawa wamempata ikatokomea. Ingawa hawakuongea wala kupeana ishara yoyote, lakini bado kule kumwona akiwa hai na kuyaona macho yake yaking’ara kama ilivyo kawaida yake kulimwongezea ari na kumpa matumaini makubwa ya ushindi.

Hivyo, hakuwa na hofu kubwa sana pindi walipochukua gari na kuondoka huku domo la bastola ya Kakakuona, iliyofichwa mfukoni, likiendelea kumtekenya ubavuni. Wala hakubabaika Kakakuona alipouandika ule ujumbe wa kejeli kwa Kombora, ambao ulikusudiwa kumwongezea hofu.

Lakini, mara tu baada ya gari kusimama hapa na Kakakuona kufanya kile kitendo ambacho Nuru hakukitarajia, alijikuta akiingiwa na hofu kubwa iliyochanganyika na hasira.

Ndiyo, Nuru ameshuhudia mara nyingi watu wakiuawa. Kamwe hakuwa mgeni kwa hilo. Lakini kuuawa kwa kijana huyu wa Kipemba, asiye na hatia, ambaye aliwaendesha bila hofu wala hisia zozote za hatari, kuliufanya moyo wake ukose baadhi ya mapigo yake, hasa pale alipoona kijana wa watu akianguka ghafla juu ya usukani kama mbuzi.
 
Back
Top Bottom