Hadithi: Roho ya paka. (Ben R. Mtobwa)

nameless girl

JF-Expert Member
Apr 22, 2012
4,195
2,675
1
ILIKUWA ghafla, kama pigo la kisu ambalo lilipenya mwilini na kuujeruhi moyo wa Inspekta Kombora. Kati ya yote aliyoyatarajia jioni ya leo, simu kama hiyo, ya maafa, haikuwamo kabisa akilini mwake. Kwa jumla, ilikuwa kama iliyopigwa muda huu kwa ajili ya kumsimanga au kumdhihaki.
Muda mfupi uliopita alikuwa akiitazama kwa furaha kubwa chati yake ya taarifa za wizi, ujambazi na mauaji nchini. Ingawa tabasamu ni kitu ambacho huutembelea uso wa Kombora kwa nadra sana, lakini leo liliutawala uso huo kwa muda mrefu wakati akiitazama chati hiyo. Furaha iliyotokana na jinsi idadi ya vitendo hivyo ilivyokuwa ikishuka kwa kasi. Ukiacha udokozi mdogomdogo, wizi wa kuaminiana na ule wa kalamu vinginevyo rekodi hiyo ilikuwa ikielekea kwenye sifuri. Wakati wowote Tanzania ingeweza kujitangaza duniani kama taifa pekee ambalo limeushinda kabisa ujambazi.
Kombora alikuwa mtu wa kwanza aliyestahili kuifurahia hali hiyo kwani alikuwa mstari wa mbele kati ya wale wachache ambao huumiza vichwa vyao na kukesha usiku na mchana pindi linapotokea tukio lolote ambalo hutishia usalama wa taifa hili. Hivyo, alichekelea huku akimpongeza kimoyomoyo Waziri wa Mambo ya Ndani, Augustine Mrema, ambaye alisimamia kwa dhati ulinzi wa sungusungu ambao uliwajumuisha raia wenyewe kujilinda usiku. Kombora aliamini kabisa kuwa hilo lilichangia sana kupunguza wizi, uvunjaji wa majumba na mauaji ambayo yalifikia kiwango cha kukatisha tamaa.
Hata hivyo, tabasamu la Kombora lilitoweka. Lile wazo lililokuwa likimpekecha ubongo mara kwa mara lilipomjia tena, wazo la kwamba, kama imefikia hatua ya raia wenyewe kukesha nje wakijilinda, vyombo ambavyo vina jukumu hilo vinafanya nini? Havitoshi? Haviwezi? Havifai? Haviaminiki? Na kama jibu limo katika moja ya maswali hayo kuna umuhimu gani wa kuwa na vyombo hivyo na kuvitengea mamilioni ya pesa kila mwaka?
Akiwa askari mwaminifu, anayeipenda na kuiamini kazi yake Kombora alijisikia haya. Angefurahi zaidi kama idadi hiyo ya matukio ya kijambazi ingekuwa inashuka kutokana na uwezo wa polisi au usalama. Angefurahi zaidi kama raia wote wangelala usingizi wao kwa amani kama ilivyokuwa miaka michache iliyopita. Pamoja na hayo, aliendelea kuifurahia hali ya usalama. Alijiona kama kwamba wanausalama wako mapumzikoni au chuoni wakiandaa mkakati ambao utawafanya warudipo kazini watimize jukumu lao kwa uhakika zaidi.
Ni wakati alipotoka mbele ya jedwali hilo na kuketi juu ya kiti chake pindi ilipolia simu hii na kuupasua moyo wake kwa habari za mauaji. “Unasema unaitwa nani vile?” Kombora aliuliza kwa ukali kidogo.
“Sajini Brashi, mzee. Wa kituo Kikuu… Ni kweli hunifahamu. Lakini mimi nakufahamu…”
Kombora alimkatiza tena, safari hii kwa ukali zaidi, “Kwa nini unipigie mimi? Huna mkuu wako wa kazi? Sikiliza, Sajini. Kama hadi leo hujafahamu taratibu za kazi yako nadhani njoo zako hapa tukupe barua ili urudi tena chuoni.”

“Sivyo, mzee,” upande wa pili ulijibu, kiasi sauti yake ikiwa na hofu. “Naufahamu wajibu wangu. Lakini kuna jambo katika mauaji haya, ambalo nadhani ungependa kuliona kabla ya mtu mwingine yeyote.”
“Jambo lipi hilo?”
“Labda nikuombe uje mara moja. Ni mwendo wa dakika tano tu, mzee…”

***​
PONGWE Hotel ni moja kati ya yale mamia ya hoteli za kitalii ambazo ziliibuka kama uyoga huku na huko nchini, mara baada ya kutangaza ule uhuru wa kiuchumi. Hii ipo katika Mtaa wa Livingstone, Kariakoo. Ina ghorofa sita, vyumba mia na ishirini vya kulala, vyote vikiwa vinajitegemea kwa bafu, choo na mashine ya kurekebisha hewa.
Kwa nje hoteli hii inaonekana kama hoteli nyingine nyingi za mji huu, kana kwamba wajenzi wake walikusudia kumfanya mpitanjia asivutiwe kabisa na majengo, rangi wala mandhari yake. Lakini ndani, hali ilikuwa tofauti kabisa. Utaalamu na utajiri vilijumuishwa kiasi cha kumfanya Kombora, ambaye hapati nafasi ya kutembelea hoteli mara kwa mara, atikise kichwa chake.
Zilimchukua dakika tisa, badala ya tano, kutoka ofisini kwake hadi hapa, hali ambayo ilisababishwa na msongamano wa magari na ubovu wa barabara. Alimkuta Brashi, kijana mwembamba, mrefu, mwenye nywele nyingi aliyevalia kiraia, akimsubiri mlangoni.
“Hadi sasa, zaidi ya mhudumu wa chumba hicho na meneja wa hoteli, hamna mtu mwingine anayejua kilichotokea,” Brashi alimweleza Inspekta akimwongoza ndani. “Ni katika ghorofa ya tano, chumba namba 108.”
Walipita mapokezi ambapo mhudumu wa kike alikuwa akiwakaribisha wageni wanne kwa maneno na tabasamu lililotosha kabisa kuwashawishi wakae hotelini hapo kwa miaka. Kutoka hapo waliingia chumba cha vinywaji. Huko nusu ya viti vyote tayari ilimezwa na wateja walioonekana wachangamfu zaidi kutokana na bia nyingi zilizokuwa wazi mbele yao. Wawili kati ya wateja hao waligeuza nyuso zao kuwatazama Brashi na Inspekta Kombora, waliokuwa katika mavazi yao ya kawaida. Watumiaji hao waliwapuuza mara moja kwa kuwachukulia kama wanywaji wenzao. Brashi alimwongoza Kombora kuifuata ngazi ya kupandia juu.
Mbele ya chumba walichokihitaji walimkuta meneja akinong’ona na mzee mmoja mwenye tumbo nene na uso wa mtoto mdogo ambaye, kwa kumtazama tu, Kombora alifahamu kuwa ni Mchaga. Nyuso zao zilijawa na wasiwasi.
“Karibu mzee,” Meneja aliwakaribisha. “Huyu hapa ni bwana Mmari, ndiye tajiri wa hoteli hii. Nilikuwa nikimfahamisha mkasa uliotukuta.”
Walishikana mikono. Kisha, wote wakaingia katika chumba hicho ambacho kwa mtazamo wa kawaida kilikuwa kama kawaida. Shuka zilitandikwa vizuri kitandani. Juu ya kitanda hicho alilala kifudifudi msichana mwembamba, mweupe, ambaye huhitaji kumtazama usoni ili ujue kuwa ni mzuri. Alivaa nguo zake zote; gauni jepesi, refu japo lilifunua paja moja na kuonekana kutokana na kulala vibaya. Mikono yake laini ilijaa bangili na pete ya dhahabu. Shingoni pia alikuwa na mkufu wa dhahabu ambao ulioana na nywele zake ambazo pia zilibeba rangi ya dhahabu. Kwa kila hali alikuwa msichana mzuri wa kileo.
Angeweza kuwa amelala… angeweza kuwa amejipumzisha. Kombora alimtazama Brashi kama anayetaka ufafanuzi wa hayo.
“Amekufa mzee,” Brashi alijibu swali hilo ambalo alilisoma katika macho ya kombora. “Amekufa kifo cha kikatili kupita kiasi.”
Kombora hakuelewa. Alimwonyesha hivyo Brashi katika macho yake.
“Labda nikuonyeshe, mzee,” alisema akimsogelea marehemu. “Nikuonyeshe jeraha mzee?” Kombora alipotikisa kichwa kukubali, Brashi alichukua kitambaa cha meza ndogo kando ya kitanda hicho na kukifunga katika mkono wake wa kushoto. Kisha, akautia mkono wake tumboni mwa marehemu na kumgeuza taratibu huku akiyafumba macho yake na kusema taratibu, “Jiandae kwa mshituko.”
Kwanza Kombora hakuelewa. Ilikuwa kama anaota ndoto ya ajabuajabu inayotisha kuliko vitisho vyote. Kisha, akadhani kuwa haoti, bali anatazama sinema ya kuogofya kupita kiasi. Alipotanabahi kuwa hayuko pichani wala ndotoni alihisi alishikwa na kichefuchefu. Hakuhitaji kutapika kwani bwana Mmari alikuwa akitapika badala yake huku akitokwa na sauti ya kilio cha ghafla.
Ilikuwa picha ya kutisha, picha isiyoelezeka wala kutazamika. Yeyote aliyefanya kitendo hiki hakuwa binadamu wa kawaida isipokuwa mnyama. Vinginevyo, hangewezaje kuthubutu? Angewezaje kufikiria hilo?
Bila kujua atendalo, Kombora alijikuta akimshika Sajini Brashi mkono kwa vidole vyake vikubwa na kumbana huku akimuuliza kwa sauti ndogo, “Mimi nahusika vipi na maiti hiyo Sajin? Kitu gani hapo ambacho uliona kitapendeza sana niskikiona?”
Brashi alijaribu kujitoa katika mkono wa kombora. Ilikuwa kama kujaribu kujikwatua toka katika pingu. Badala yake ndiyo kwanza vidole hivyo vilizidi kudidimia katika ngozi yake. Japo maumivu yalikuwa makali, lakini hayakumzuia kushangazwa na nguvu za mzee huyu. “Anakula nini?” alijiuliza akimtazama usoni.
“Kitu gani ulichodhani kitanipendeza hapa?” Kombora aliuliza tena.
“Unaniumiza Inspekta.”
Ndiyo kwanza Kombora akafahamu kuwa alikuwa amemshika Brashi mkono. Akamwachia na kuiona damu ambayo ilianza kutoka katika michubuko iliyosababishwa na vidole vyake. Angeweza kumwomba radhi, lakini hakufanya hivyo. Rohoni mwake, aliona adhabu hiyo ndogo inatosha kabisa kumfunza adabu sajini huyu kwa kosa lake la kuivuruga amani na starehe aliyokuwa nayo moyoni kwa siku chache zilizopita bila misukosuko ya kutisha.
Kumwita hili atazame maiti hii iliyokuwa katika taswira ya kutisha kupita kiasi, maiti ambayo haitamtoka akilini wala katika ndoto zake, kwa muda mrefu bila sababu ya maana, aliona ni ufedhuli wa hali ya juu. Alimkazia Brashi macho akifikiria adhabu ipi ya pili ambayo ingemfaa zaidi.
Brashi hawezi kuwa mbumbumbu kiasi hicho. Hawezi kuwa mtu pekee nchini na duniani ambaye hafahamu kuwa Kombora alikuwa akiongoza idara maalumu na pekee ambayo hushughulikia yale masuala mazito na yanayotishia usalama wa serikali na taifa, si masuala madogomadogo, ya kawaida ambayo yangeweza kushughulikiwa na polisi wa kawaida.
Kana kwamba anayasoma mawazo yake, Sajini Brashi alisema, “Samahani sana Inspekta, nilidhani wewe na Joram Kiango mna aina fulani ya uhusiano. Sijui namna yoyote ya kumpata Joram, ndipo nikaona nikuarifu wewe kabla ya kulipeleka suala hili kwa wakuu wangu ambako linaweza likatangazwa ovyo au kupuuzwa. Kama nimekosea, Inspekta, naomba radhi…”
“Sijakuelewa Joram anahusika vipi na huyu marehemu?” Kombora aliuliza, moyoni akitetemeka kidogo kwa jibu atakalopata.
“ Yawezekana huyu marehemu ni Nuru, yule mwenzi na mpenzi wake Joram Kiango. Kama ndiye…”
“Hukuona mzee?” Brashi alikatiza mawazo yake. “Hukuona? Basi nitalazimika kumfunua tena marehemu.”
“Kuona nini?”
Kombora alijaribu kumzuia, lakini alichelewa. Tayari alikwishamgeuza maiti chali. Kombora alilazimika kulitazama tena jeraha hilo.
Bado lilikuwa halitazamiki. Utalitazamaje jeraha ambalo lilikuwa zaidi ya jeraha? Pale ambapo palitakiwa kuwa na uso wa msichana huyo, toka sikio hadi sikio, na paji la uso hadi kidevu, badala yake palikuwa na shimo la kutisha lililokuwa limekula nyama zote na kuacha mifupa mitupu. Pale yalipostahili kuwepo macho, pua, midomo na ulimi sasa yalikuwa mashimo ambayo yaliacha wekundu wa nyama na damu uonekane kiasi cha kutisha zaidi ya fuvu lolote la binadamu.
Safari hii, akitazama kwa makini zaidi, Kombora aliweza kubuni kilichokula nyama hiyo. Kama si biological weapon ya kisasa zaidi ambayo inatoa wadudu wadogo na wengi sana ambao wanashambulia nyama ya binadamu kwa dakika kadhaa kabla ya kufa, basi ni aina kali sana ya asidi ambayo ilimchoma binti huyo uso mzima na kuacha mifupa mitupu.
“Unaona mzee?” Brashi alimzindua.
“Nini?”
“Tazama hapa,” alielekeza mkono wake pale ambapo palistahili kuwa kinywa, ambapo sasa palikuwa na meno yaliyotokeza kana kwamba yanalia au yanacheka. Kombora aliinama na kuchungulia. Ndipo alipoweza kukiona kipande cha karatasi kilichokuwa kimelazwa humo kinywani. Kilikuwa na maandishi. Kombora aliinama na kuyasoma.
“TUNAMTAKA JORAM KIANGO”
Kombora aliyasoma kwa mara ya pili kabla hajaupata ujumbe huo. Alipoupata aliingiza mkono wake mfukoni na kutoa kitambaa. Akakizungushia katika vidole vyake na kuvididimiza humo kinywani hadi alipofikia hicho kipande cha karatasi. Alikichukua na kukizungushia katika kitambaa hicho na kisha kukitia mfukoni mwake.
Baada ya hapo alimgeukia Brashi na kumwambia, “Sikia sajini, umefanya kazi nzuri. Wanamtaka Joram Kiango. Tutampa ujumbe wao.” Alimkazia macho kabla hajaendelea, “Sasa unaweza ukaendelea na taratibu zako zote, kama kawaida. Tafadhali nitaomba unipe taarifa kamili ya upelelezi wenu juu ya mauaji haya mara mtakapokuwa tayari. Sawa?”
Brashi alitikisa kichwa.
“Na unajua sajini? Sikio la mtu yeyote nje ya chumba hiki lisisikie kuwa mauaji haya ni salamu tu kwa Joram Kiango. Nataka iwe siri, tafadhali.”
“Bila shaka Inspekta.”
“Ngoja nikuonyeshe,” alisema akiinama tena kitandani na kumshika maiti.

***​
HADITHI ilikuwa fupi na nyepesi. Kwa jina aliitwa Sofia Ali, mzaliwa wa huko Dodoma, wilayani Mpwapwa. Alikuja Dar es Salaam kama ilivyowatokea wasichana wenzake wengi wa hirimu yake. Amemaliza shule darasa la saba hana kazi wala mchumba. Jirani, mke wa bwana fulani huko Dodoma mjini anatokea na kumshahuri wafuatane naye mjini kumtunzia nyumba. Mshahara? Mia tano kwa mwezi. Chakula bure, malazi bure, nguo alizochoka nazo mama mwajiri bure, Akatae? Kama wengi wengine Sofia alijikuta yuko mjini.
Maji ya bomba ya mara kwa mara, chai ya maziwa kila asubuhi, chakula chenye viungo vyote; pamoja na ile dokoadokoa ya vipodozi vya mama ilifichua kiumbe mrembo aliyejificha katika umbo lile lililochakaa la Sofia Ali.
Badala yake, miaka miwili baadaye, aliyesimama mbele ya mama mwajiri alikuwa Sofia mwingine kabisa, Sofia aliyewiva, Sofia aliyejaza, Sofia ambaye alimfadhaisha baba mwenyenyumba na kumtisha mama. Matokeo yake Jumapili moja alipewa tiketi ya kurudi Mpwapwa. Kufanya nini? Kazi basi.
Hakurudi Mpwapwa. Akafuate nini? Jembe na mpini wake? Amwachie nani starehe za sinema na muziki ambazo ndio kwanza alikuwa ameanza kuzionjaonja? Rafiki yake aliyekuwa akiishi Tambuka Reli, ambaye alikuwa ameanza kujitegemea baada ya kupitia mkondo huohuo, alimpokea.
Chumba chao chenye upana wa futi tano kilibeba kitanda chao cha futi tatu na majukumu yote ya jiko, ghala; na mengineyo. Ungewatembelea mchana wakati wa joto, huku moshi ukiwaadhibu, usingekosa kuwahurumia. Lakini waone jioni, wakati tayari wameoga, wamevaa na kujitengeneza usingekosa kujiuliza kwa nini hawajatokea wachumba wakawaoa.
Mwaka mmoja baadaye, Sofia alikuwa Sofia hasa. Hata shoga zake walianza kumchukia kwa wivu. Hakujali, kwani alikuwa na marafiki wengi wa kiume kuliko wa kike. Na ni hao ambao aliwahitaji. Wakati huo hata jina alianza kulibadili. Badala ya Sofia sasa alijiita Soffy. Na alipenda sana baba yake aitwe Ally badala ya Ali. Hata lugha yake ilianza kubadilika. Katika kila sentensi alijikuta akiweka walau neno moja la Kiingereza. Hakujua kilipotokea hicho Kiingereza chake Lakini alikuwa na hakika nacho.
Sofia alifanya kosa. Mimba iliingia bila taarifa wala hiyari. Bwana hakumjua wala hakuhitaji mtoto. Alimeza vidonge mimba ikafa. Miezi miwili baadaye mimba ya pili ilimkamata. Hii haikusikia vidonge. Miezi mitatu, minne, mitano! Kila mtu alianza kumshuku. Elfu tatu zilimaliza kazi. Daktari mmoja asiye na huruma, alifanya kazi hiyo na kutupa mtoto anakokujua. Sofia aliponea chupuchupu. Baada ya miezi mitatu ya maumivu, afya yake ilimrudia. Mji wa Dodoma akauona nuksi. Huyoo, akaingia Dar es Salaam.
Dar ilimlaki juujuu. Rafiki yake mmoja wa Kinondoni, akijua kuwa umbo la Sofia lingemwongezea riziki, alimkaribisha kwake na kumwonyesha mji. Madisko ya Lang’ata na Ushirika yaliwakoma. Madansi ya DDC na Friend’s Corner yaliwatambua. Mabaa ya Sky Way na Kilimanjaro, yaliwaheshimu. Mabwana walikuwa tele, wa kila kabila na kila rangi. Sofia hakujua kumkataa mtu. Ni yeye aliyeanzisha msemo wa “… Ni pochi yako tu.”
Jioni ya leo alikuwa katika Hoteli ya Sky Way, ndipo alipomwona yule kijana mrefu, mnene, ambaye alikuwa akinunua vinywaji kwa fujo kuliko mtu mwingine yeyote hotelini hapo. Na mifuko yake bado ilionekana kuwa imetuna. Wasichana wengi waliokuwa wakimzengeazengea walipewa bia na kufukuzwa toka mezani pake. Sofia hakuwa mtu wa kuomba bia. Yeye huitwa au kufuatwa. Alimtupia jicho moja tu kijana huyo na kuona tayari ameimeza ndoano yake. Hakukosea kwani dakika mbili baadaye alianza kuletewa bia, oda ya kijana huyo. Na dakika kumi baadaye tayari waliketi pamoja, na kuanza kushikanashikana.
“Unasemaje?
“Pochi yako tu, darling.”
“Kiasi gani?”
“Hata wewe? Nilidhani umesoma, brother.”
Maongezi yao yaliishia katika kimojawapo cha vyumba vya hotelini. Baada ya nusu saa ya vilio na vicheko vya uongo na kweli Sofia alipokea “pochi” yake. Wakati akijiandaa kuondoka kijana huyo alimshika mkono na kumwambia, “Unajua Soffy, ni tamaa tu iliyonifanya niamue kuanguka nawe. Kwa kweli, nina rafiki yangu mpenzi, mwenye kitita cha pesa, kuliko hiki changu ambaye amenituma hapa Sky Way kumtafutia mwanamke mzuri. Kweli, hata hizi pesa nilizokuwa nikizinywa ni zake, kama hujachoka nikupeleke.”
“Kuchoka!” Sofia alicheka. “Nani aliwahi kuchoka kupokea pochi? Kama una wivu, I can understand, kama huna nipeleke.”
Kisha, Sofia alishituka na kusita kidogo wazo jipya lilipomjia. “Huyo, rafiki yako, What is his name?” aliuliza.
“Jina simfahamu.”
Why! Ni binadamu kweli?”
“Sema, maana mambo ya siku hizi you can’t understand. Mimi sijachoka kiasi cha kumvulia underware yangu mnyama.”
Kijana huyo alicheka. “Unadhani mimi ni crazy kiasi hicho? Huyo ni mtu mwenye hadhi na heshima zake. Naamini hujapata kukutana na mtu mzito kama huyo.”
Bado Sofia alisitasita kidogo. “Jina humjui. Wewe mwenyewe unaitwa nani, honey?”
“Niite Ram Shog.”
“Na huyo friend wako yuko wapi?”
Alipomalizia kuvaa, Ram alimshika mkono Sofia na kumwambia, “Twende nikupeleke. Amepata chumba katika Hoteli ya Pongwe.”

***​

AKIWA mgeni katika hoteli hiyo, Sofia alivutiwa mara tu baada ya kushuka toka katika teksi iliyowaleta. Ram akamwongoza hadi mapokezi ambako aliomba ufunguo wa chumba namba 108. Walipanda ngazi hadi ghorofani ambako walifungua na kuingia hadi chumbani.
“Itabidi umsubiri,” Ram alimwambia Sofia ambaye alikwishajitupa juu ya kitanda na kujilaza. Usingizi wa pombe ukamchukua.
Hakuamka tena hadi majuzi, meneja wa hoteli alipojaribu kumwamsha na, hatimaye, Sajini Brashi alipomgeuza na kukutana na uso ule ambao aliokutana nao.
 
3


SALAMU… Zilimfikia Joram Kiango usiku wa siku hiyohiyo, japo kwa njia ya tofauti kidogo. Kwa zaidi ya miezi sita sasa Joram Kiango na mwenzi wake, Nuru walikuwa wameutoroka mji na kuhamia porini. Kama ilivyo kawaida ya Joram, safari hii ilifanyika kwa siri sana, kiasi kwamba hakuna mtu yeyote mwingine aliyefahamu wako wapi.

Kisa cha kuhama kwake kilikuwa kutafuta fursa nzuri ya kujitenga na dunia ya nje ili aweze kufanya mazoezi makali ya viungo, mbinu za mapambano na matumizi ya silaha, wazo ambalo lilimjia mara baada ya ule mkasa uliomfanya asafiri hadi huko nchini Pololo ambako yalitokea mambo mengi ya kutisha na kutatanisha kiasi kwamba alipoondoka huko aliacha yakifanyika mabadiliko makubwa katika ngazi za juu za uongozi; mkasa ambao tayari umeandikiwa kitabu kinachoitwa Malaika wa shetani baada ya juhudi zake kuwafanya wananchi waelewe nani malaika wa Mungu na nani wa shetani miongoni mwao.

Pamoja na kwamba Joram alishinda katika mkasa huo, pamoja na ukweli kuwa wahalifu wote aliwaacha maiti; bado ushindi huo haukumridhisha. Aliona kuwa mara nyingi aliponea chupuchupu kuliko ilivyomstahili na maadui zake, hasa lile dude lililokuwa na utaalamu wa ninja ambalo lilimwadhibu kama lilivyotaka hadi risasi ilipolituliza.

Jambo hili lilimfanya Joram ajisikie vibaya sana moyoni na akilini. Alijiona kama amekuwa mzembe na mvivu sana, ambaye anaishi kwa hisani ya wenye nguvu, kama ilivyo kwa binadamu wengi.

Hivyo, mara tu aliporudi Dar es Salaam alinunua mtumbwi na mashine yake kwa siri na kwa siri vilevile, wakapakia vitu vyao, chakula cha kutosha na vitu mbalimbali na kusafiri hadi katika kimojawapo cha visiwa vingi na vidogovidogo vilivyomo baharini kati ya Bara na Visiwani.

Alichagua kisiwa ambacho aliwahi kukichunguza huko nyuma, katika harakati zake za hapa na pale. Kisiwa hicho kilikuwa hakitumiwi na wavuvi, watalii wala picnic kwa vijana. Huko waliuficha mtumbwi wao ili usiweze kuonekana na wavuvi au wasafiri angani. Wakajenga kambi yao, kwa uficho vilevile, na kisha wakaanza mazoezi.

Mazoezi yao yalikuwa makali sana. Walijikumbusha kila walilolijua na kujifunza yote ambayo hawakuyajua. Walijifunza mbinu mpya ya kuficha silaha, kuitumia, kuikwepa, n.k. Zaidi, walijifunza mbinu mbalimbali za ninja. Wakisaidiwa na vitabu mbalimbali vya sanaa hiyo ya kale waliweza hata kugundua mbinu zao binafsi za hila na mazingaombwe, ambazo zinawafanya ninja waonekane kuwa si binadamu wa kawaida.

Joram aliunganisha mbinu za kale na za kileo, alioanisha utaalamu wa Mjapani, Mchina n.k. Baada ya miezi hiyo sita alikuwa amekamilika sawa na ninja yeyote aliyetoka katika chuo chochote kati ya vile vingi vya siri.

Naye Nuru sasa alikuwa amepikwa akapikika. Mwanzoni mwa mazoezi hayo alikuwa akiyafurahia na kushangilia. Lakini yalipopamba moto alianza kutokwa na machozi, huku jasho na damu ikimvuja ovyo mwilini. Kuna wakati alifikiria kutoroka, kuna wakati alitamani kufa na kuna wakati aliamini kuwa lazima angekufa kwa ugumu wa mafunzo hayo.

Wakati mwingine alitulia na kumtazama Joram kwa makini, mwili wake ukiwa na majeraha ambayo yalipona yenyewe, mikono yake ikiwa na makovu, kifua chake kikizidi kupanuka na mikono kukomaa. Alimtazama kwa makini, anavyoendelea na zoezi kwa ufundi akili yake yote ikiwa katika zoezi hilo.

Katika nyakati kama hizo, Nuru alimwona Joram kama mwendawazimu. ‘Binadamu ana haki gani kujitesa kiasi hicho? ‘Anajitesa kwa ajili ya nani? Naye Joram ni nani?’ Nuru alijiuliza.

Hata hivyo, maswali haya yalitoweka kila alipojikumbusha kwa mhutasari tu kazi nzito ambayo Joram aliitendea nchi hii, Afrika na dunia kwa jumla. Alimwona kama malaika au nabii wa aina yake ambaye bila ya mchango wake ni dhahiri kuwa historia ya nchi hii ingekuwa nyingine na pengine ya kusikitisha sana.

Wazo hilo daima lilimtia Nuru faraja mpya, na juhudi mpya, hata akapambana na mazoezi yake kishujaa; kwa kiwango ambacho kilimshangaza hata Joram mwenyewe na zile nyakati za mapumziko ambazo alijipumzisha kando ya bahari mikono mikavu ya Joram ikimchezea hapa na pale, ulimi wake laini ukimtekenya hapa na pale, huku sauti yake kama muziki ukimfariji kwa neno hili na lile, Nuru aliisahau kabisa dunia ya nje na kutamani kisiwa hiki kitoweke katika ramani ya dunia hii ili waishi peke yao milele.

Walicheza na kucheka huku wakitaniana kama watoto wadogo, mapenzi yakiwa katika macho yao na kuzisaliti sauti zao.

Kipindi cha mazoezi kilipowadia utani uliwekwa kando, mapenzi yakasahauliwa.

Ili kuyapata mahitaji mbalimbali, kama chakula, vinywaji, magazeti na barua, Joram alikuwa na kawaida ya kuingia jijini kwa siri, mara moja kila wiki. Mara nyingi safari hizi alizifanya jioni, akiwa amejibadili kidogo kwa mavazi ambayo yasingeweza kumfanya afahamike mara moja.

Jioni ya leo alimuaga Nuru kama kawaida, baada ya kulipinga pendekezo lake la kufuatana naye, akichelea kuwa kufuatana kwao kungeifanya mbinu yao ya kujibadili isifanikiwe sana.

Akiwa amevaa shati pana, suruali iliyobana sana na kofia ya Kiarabu kichwani, alionekana kama kijana yeyote mhuni wa mitaani, pindi alipoiegesha boti yake ya pwani ya Ferry na kuifunga vizuri.

Baada ya kuhakikisha usalama wake waliondoka na kukodi gari lililomfikisha mjini, kituo chake cha kwanza kikiwa posta ya Sokoine Drive ambapo alimlipa mwenye gari, akashuka na kuingia eneo la masanduku ya barua.

Joram si mwandishi mzuri wa barua. Hivyo, si mtu ambaye hutarajia kupata barua nyingi. Mara nyingi barua zake huwa ni bili za umeme, simu na maji. Mara chache sana hupokea barua za ndugu, jamaa na marafiki, barua ambazo zinaadimika siku baada ya siku kwa ajili ya uvivu wa kuzijibu.

Hivyo, hakushangaa leo alipofungua sanduku lake na kukuta barua moja tu iliyokaa kama yatima. Lakini alishangaa mara baada ya kuitoa na kuiona kuwa japo ilikuwa na anuani yake kamili, badala yake haikuwa na stempu wala mhuri wa posta. Na alishangaa zaidi alipoifungua na kukuta, badala ya barua, ndani ya bahasha hiyo mlikuwa na picha mbili tu.

Kwanza, alidhani kuwa picha hizo ni za wasichana wawili wenye bahati mbaya. Baada ya kuangalia kwa utulivu zaidi aligundua kuwa mmoja alikuwa mwanamume japo alivaa shanga, na wa pili mwanamke. Walikuwa uchi kama walivyozaliwa. Hakuhitaji kufahamishwa kuwa walikuwa marehemu. Hakuna mtu anayeweza kuliwa nyama yote ya uso na kuachiwa mifupa mitupu akawa hai.

Joram alizitazama kwa makini kinyume na matakwa yake. Kwani zilimtisha na kumsikitisha. Kisha akajikuta akitetemeka kwa hasira, ngumi zake kazikunja kwa nguvu, meno kayasaga. Alikuwa ameyaona maandishi yaliyosomeka kwa shida kinywani mwa marehemu hao yakimdhihaki. Kwa Joram hili lilikuwa tusi kubwa na uchokozi wa waziwazi uliokusudiwa kumtia hasira.

Hakuitaji ujumbe zaidi kipindi ambacho yeye ametulia, huko kisiwani kuna mtu au kikundi cha watu ambacho kinamtafuta yeye kwa udi na uvumba na kwamba, ili kumchokonoa popote alipo ndipo walipobuni ila za kufanya mauaji haya; na kutumia funguo bandia kulifungua sanduku lake ambamo waliziweka picha hizi, ili azione.

Bila shaka yoyote vijana hawa hawakuwa na hatia, Joram aliwaza. ‘Itazame miili yao ilivyo laini! Haina dalili yoyote ya purukushani za dunia!’

Mawazo haya yaliongeza hasira kichwani mwake. Akalifunga sanduku lake la Posta na kutembea polepole hadi Hoteli ya Salammander ambako aliketi na kuagiza maji ya machungwa.

Wakati akiyasubiri aliwasha sigara na kuvuta taratibu huku akiwaza. Jambo la kwanza lililomjia akilini ni kwamba hakuwa na haja ya kuendelea kujificha. Hilo alikuwa ameamua kulifanya kwa sababu mbili. Ya kwanza, ni kule kuamini kwake kuwa maadui hao wangetafsiri kuwa anajificha kwa kuwaogopa.

Pili, alikuwa na hakika kuwa hata hapa alipo kuna mmojawao anayemtazama kwani baada ya kuweka barua au picha zile wangehitaji kujua kama amezipokea; na tangu hapo wasingemwacha huru. Zaidi, aliamua kuwa hadharani kwa kuhofia kuwa wasipomwona wangemuua mtu mwingine asiye na hatia, jambo ambalo hakupenda litokee kamwe.

Aliinywa juisi yake nusu ya glasi, akilini akiendelea kujiuliza kwa nguvu nani hasa anayeweza kutaka roho yake kwa nguvu kiasi hicho. Yeye ni mtu mwenye maadui wengi, lakini alikuwa na hakika kuwa kila adui yake ama alikuwa marehemu au kiwete moyoni baada ya kuvunjwa kiungo chake cha mwisho ambacho kingeweza kumfanya athubutu kurudia uzandiki wake.

Wazo la kuwa pengine hawa ni maadui wa taifa ambao wanatumia ila za kujifanya wanamtaka yeye binafsi hakulipa uzito. Dunia ikiwa kama ilivyo, katika kipindi hiki ambapo maadui wakubwa waliokuwa wanaketi katika meza moja na kuzungumzia umoja, haielekei kuwa kuna nchi ambayo inaweza ikaamua kuichokonoa Tanzania kwa kiwango hiki. Labda iwepo sababu nyingine nzuri sana, ambayo Joram hakuweza kuiona.

Kisasi ni wazo pekee lililojitokeza katika fikra za Joram, hisia zilizomfanya ashuku kuwa kuna mtu mwenye kisasi naye ambaye ana kiu kubwa ya roho yake na lazima mtu huyu awe na roho ya shetani au ni shetani mwenyewe ambaye hafi mara moja, bali ameibuka toka kaburini na kuanza kumtafuta kwa vishindo vya kishenzi. Hasira zikizidi kuchemka mwilini mwake dhidi ya mtu huyo, Joram alitamani akutane naye papo kwa papo, ana kwa ana, ili amfunze adabu upya kwa kuvitawanya viungo vyake sakafuni na kumwacha mbwa wamle.

Akayamalizia maji hayo kwa fundo la pili. Kisha, akainuka na kuondoka; akaelekea kituo cha teksi.


***

Gari hilo lilimfikisha mbele ya nyumba yake Ilala. Haja yake ilikuwa kuchukua silaha zake muhimu za siri, kisha aende kisiwani ambako angemchukua Nuru na kumleta mjini. Hakuwa na haja ya kujificha tena. Na kama zoezi, lililokuwa mbele yake lingemtosha kabisa. Alikuwa na hakika kabisa kuwa tayari ameingia vitani dhidi ya binadamu katili wenye roho chafu, binadamu ambao ama ilikuwa yeye afe ama awateketeze.

Kabla ya kuutia ufunguo katika tundu la kitasa aliichunguza ile alama yake ya kawaida ambayo hutegesha kujua kama mlango huo umefunguliwa au la. Kama alivyotarajia, alama hiyo haikuwepo

‘Wamekwishanitembelea…’ Aliwaza huku akifungua na kuingia kwa hadhari. Jua likiwa limezama kitambo ilimlazimu kuwasha taa ili aweze kupata nuru ya kutosha. Aliichunguza swichi ya taa hiyo na balbu yake kabla ya kuwasha. Havikuwa na kasoro. Akawasha taa na kuingia ukumbini. Kila kitu kilikuwa kama alivyokiacha.

Chumbani pia hakukuwa na dalili yoyote ya upekuzi ambayo ingeweza kuonekana kwa urahisi, jambo ambalo lilimfanya aanze kuwahusudu adui hawa kwa umakini wao. Aliona wazi kuwa si kwamba walikuwa jeuri na wakatili tu bali pia watu makini ambao waliijua vilivyo kazi yao.

Joram alirudi ukumbini ambako aliinama na kufunua zulia ambalo, katikati ya chumba, lilifunika hifadhi yake madhubuti ya silaha.Wakati akihangaika kuchokonoa sakafu hiyo ambayo ilionekana ya kawaida kabisa, simu ililia. Joram aliitazama kwa mshangao. Nani anayejua kuwa yuko hapo, muda huo? Alijiuliza. Na anataka nini?

Simu iliendelea kulia. Baada ya kuwaza sana Joram aliamua kuipokea. Alichunguza mkono wa simu kwa makini kabla ya kuuinua na kuuweka sikioni.

“Joram Kiango?” upande wa pili uliuliza.


Joram alikaa kimya akimtafuta mwenye sauti hiyo

“Najua Joram Kiango unanisikiliza,” sauti iliongeza. “Sasa nisikilize kwa makini. Unanisikia?”

Joram akalazimika kujibu, “We nani?” alifoka.

Akasikia mtu huyo upande wa pili akicheka kidogo kabla ya kuendelea, “Huna haja ya kunifahamu kwa sasa. Lakini mimi ni rafiki yako mpenzi. Na ninayo nia njema sana nawe. Unasikia Joram?”

“Endelea,” Joram alifoka tena.

“Vizuri. Sasa nisikilize kwa makini sana. Ninayo habari kuwa salamu zetu za awali umekwishazipata. Au utakataa kuwa hukuona picha za warembo wawili wenye sura za malaika?”

Joram alianza kuchoshwa na kebehi za mtu huyo. “Haloo!” alifoka katika simu. “Sina muda wa kutosha kuzugumza na mpumbavu kama wewe unayekitafuta kitanzi kwa nguvu. Na kinakusubiri. Kwa hiyo, kama huna la kusema …”

“Ninalo,” mtu huyo alimkatiza harakaharaka. “Tena la maana sana. Kwa kweli ni habari ya kusikitisha sana kwako,” akasita. “Uko wima bwana Joram au umeketi?”

Swali hilo lilikuja ghafla. Likamshangaza Joram. Na alishangaa zaidi alipojikuta akijibu, “Niko wima. Kwa nini?”

“Keti tafadhali.”

“Kwa nini?”

“Keti kwenye kiti. Habari ninayotaka kukusimulia sasa ni ya kutisha sana, siwezi kukueleza ukiwa wima. Umeketi?”

Joram alizidi kushangaa. “Habari gani hiyo?”

“Umeketi?”

Simu ilikuwa juu ya meza. Kando ya meza palikuwa na kiti kimoja tu. Joram alitamani kuketi, lakini akiwa mtu ambaye hana mazoea ya kuwatii maadui zake, hasa adui kama huyo, ambaye anajificha kwenye simu, alijikuta akimpuuza. Hata hivyo, ili kufupisha maongezi hayo alimwambia, “Nimeketi haya nieleze…”

“Umeketi kweli?… unajua yule msichana wako, nani vile jina lake, Nuru sio unajua alikuwa na sura nzuri mno. Ulifanya makosa kumwacha kisiwani peke yake. Ukimwona sasa hivi… umeketi kweli, Joram?”

Joram alihisi akitetemeka. Moyo ukimdunda kwa kasi. Alitamani aketi na kufikiri. Kisha, alitamani akate simu na kuondoka mara moja. Kama kweli wamemkamata Nuru… Kama kweli wameiharibu sura yake… aliwaza, akisaga meno. Lakini kwa sauti tulivu, kama kawaida yake, alimuuliza mtu huyo kwenye simu, “Ni hayo tu? Kwa taarifa yako Nuru anajua kujilinda. Watu waoga kama wewe na wenzako mkithubutu kumsogelea mtashangaa… Nadhani sasa tuagane.”

“Bado!” ile sauti ilifoka upande wa pili. Ikafuatwa na kicheko kingine cha kebehi. “Bado rafiki yangu. Bado nnayo habari nyingine njema sana kwako,” Aliongeza kwa sauti ya kicheko. “Kiti hicho ulichokalia kimetegwa bomu. Ukithubutu kuinuka litalipuka na kugawanya viungo vyako vyote katika vipande milioni moja. Na sasa hivi simu yako tunaishughulikia isitoke nje. Kwa hiyo shujaa wetu mpenzi, Joram Kiango, tunakutakia mapumziko mema na marefu.”

Akakata simu, huku akiendelea kucheka; kicheko cha ushindi.

Joram alitamani kucheka naye lakini badala yake aliitua simu hiyo kwa utulivu na kuchungulia chini ya kiti. Bomu lilikuwa limefichwa vizuri sana chini ya kiti hicho. Nyaya mbili zilikuwa zimefungwa vizuri kwa namna ambayo kama angeketi uzito wake ungezifanya ziungane na kukamilisha mzunguko. Hivyo, kuinuka ingekuwa sawa na kulifyatua.

Kazi ya kulitegua bomu hilo ingehitaji muda. Joram hakuwa na muda huo. Aliinuka na kuingia chumbani kwake ambako alifanya haraka kubadili mavazi yake na kuvaa nguo zake nyepesi, za kazi. Kisha harakaharaka alizitia baadhi ya silaha zake katika mifuko yake ya siri. Silaha ambazo hakuzihitaji alizirejesha katika maficho yake na kurudisha kila kitu kama kilivyokuwa.

Akafunga milango na kuzima taa. Kisha, akatumia mlango wa nyuma kujipenyeza hadi nje ya nyumba. Dakika chache baadaye alikuwa ndani ya teksi akielekea ferry. Mashaka yake juu ya usalama wa Nuru yalizidi kuongezeka. Alimlipa mwenye gari hilo haki yake na kuharakisha kuuendea mtumbwi wake.

Hakuukuta. Mtumbwi ulikuwa umetoweka!

***

Ilimtokea Nuru kama muujiza. Sekunde iliyopita alikuwa binadamu pekee katika kisiwa hiki. Sekunde iliyofuata alikuwa amezungukwa na binadamu wengine wanne wenye silaha, ambao walimtazama kwa macho yenye kebehi na tamaa, tamaa ya kuua.

Aliwatazama adui hao kwa makini. Licha ya bastola zilizokuwa tayari mikononi mwao, sura zao zilitangaza shari na kiu ya damu. Macho yao wote yalikuwa kama bahari ambayo iliashiria dhoruba na misukosuko mingi ambayo wamekuwa wakipambana nayo katika maisha kiasi cha kuwafanya waone kuua na kufa ni kama jambo la kawaida sana.

Mmoja alikuwa hana jicho moja wala meno manne. Bila shaka, risasi zilifanya kazi hiyo. Lakini alitabasamu bila wasiwasi wowote. Mwingine uso wake ulikuwa unatisha na kuchekesha, kwa pamoja. Ulikuwa na vitu kama mapele na makovu, mfano wa mtu aliyepigwa chupping na fundi asiye mzoefu, bila shaka kazi ya bomu lililomlipukia usoni. Kilichomfanya abaki hai anajua muumba wake. Wawili waliosalia, zaidi ya macho yao kuashiria ushenzi, mioyoni mwao waliipenda aina hii ya maisha.

Bado wote walikuwa kimya. Walimtazama Nuru kwa tabasamu zao ambazo hazikusaidia chochote kuyafanya macho yao yapoteze walao kwa muda dalili za mauaji ambazo zilikuwa wazi kama ramani ya dunia.

Nuru alijua kuwa yuko hatarini, Pengine hatari kubwa kuliko zote zilizowahi kumkabili. Wanaume wanne, bastola nne, katikati ya kisiwa, maili nyingi toka nchi kavu! Wala hakuwa na shaka kuwa viumbe hawa wamehitimu mbinu zote za ukatili na mauaji. Kitendo chao cha kuweza kutua kisiwani hapo kimyakimya, na jinsi walivyoweza kumzingira kwa ukimya na utulivu kama mizimu ni dalili tosha ya ukomavu wao.

Hisia za hatari zilipomjia Nuru aliamua kutulia, kimya, chali, khanga moja tu ikiwa imefunika kifua chake. Hata hivyo kichwa chake kilikuwa kazini, ubongo wake ukichemka kwa makini, kutafuta namna na mbinu za kukabiliana na hatari hiyo.

Dakika nzima ilikuwa imepita tangu watu hao, walipomzingira Nuru, dakika nzima ya ukimya na utulivu, wakimtazama hali yeye pia akiwatazama kwa hila. Alipoona wameamua kutulia, wakimsubiri, Nuru alikitua kitabu chake kifuani na kuwatazama kwa zamu. Kisha, akawauliza kwa utulivu, “Kwa nini msiwe wastaarabu walao kidogo? Mnawezaje kumsimamia msichana ambaye amevaa kama nilivyovaa na kumtazama?”

“Msichana! Ha! Ha!” mmojawao alicheka.

“Kuvaa! He! Hee!” mwingine aliunga mkono.

Waliosalia walicheka tu huku wakizidi kumtazama. Ilikuwa kana kwamba ndio kwanza wanamwona Nuru katika hali hiyo, kama alikuwa akiwaalika walitazame vazi lake fupi, ambalo liliyaaacha mapaja yake manene, mekundu, nje kabisa ya vazi hilo. Kadhalika, matiti yake mekundu yaliyojaa, hayakuwa katika hifadhi yoyote ya haja ndani ya tabasamu laini ambalo aliliunda taratibu katika uso wake na kuwafanya maadui hao waduwae kwa muda, wakimtazama. Kisha, wakatazamana.

Mmoja alikohoa, mmoja aliguna. Mwingine alijaribu kucheka, kicheko ambacho hakikujitokeza. Kisha, mmoja alicheka ghafla na kusema, “Sikilizeni. Tulionywa kuwa msichana huyu ni mzuri kupita kiasi. Na tulionywa pia kuwa uzuri wake ni uchawi ambao unaweza kumtia wazimu rijali yeyote.

Zaidi ya hayo tunajua kuwa ana hila nyingi zaidi ya kinyonga. Na ni mtu hatari kama alivyo hawara yake. Kwa macho yangu nilishuhudia wakifanya mazoezi makali ya kutisha. Pamoja na kwamba nilikuwa mbali, nikitazama kwa darubini; lakini bado nilichoona ni kitu cha hatari sana kwa mwanamke huyu. Hivyo, natoa amri tufanye kazi yetu mara moja,” aliyeyasema hayo ni yule mwenye uso wa kutisha.

Mwenye chongo alicheka tena kidogo na kisha akasema, “Vizuri. Tunamtaka akiwa hai, sio?” Alimsogelea Nuru. “Ni kazi ndogo sana, na tamu sana kumshika msichana kama huyu na kumfunga pingu.” Aliinama na kumwinua Nuru.


“Twende huku,” msemaji wao alisema akimvuta Nuru kwa nguvu.

Nuru hakuwa msichana wa kuchukuliwa kikondoo kiasi hicho. Kwa jumla, hiyo ni hatua ambayo alikuwa akiisubiri kwa makini, hatua ambayo wao watadhani wamepata, huku wakiwa wamemshika kwa mkono mmoja, wa pili ukiwa na bastola. Kwa muda, alijilegeza mikononi mwao. Kisha, ghafla bila yeyote kati yao kutarajia alijikwanyua na kuruka juu huku akiachia mapigo manne ya judo, mapigo ambayo yalitoka katika mikono na miguu yake.

Shingo ya adui mmoja, ambaye alikuwa kushoto kwake, ilivunjika na mwenyewe kuanguka chini kama mzoga. Kiuno cha aliyekuwa nyuma yake kiliteguka na bastola yake kupaa angani. Bastola hiyo sasa ilikuwa mikononi mwa Nuru ambaye alitua hatua kadhaa kando yao akiwalenga nayo.

Watu wawili hawakupokea kipigo cha Nuru kama kilivyokusudiwa. Yule mwenye uso wa ajabuajabu na yule mwenye chongo aliteremka kidogo tu na kisha kujitupa chini wakijificha nyuma ya miili ya wenzao waliokuwa wakitapatapa, bastola zao imara mikononi mwao zikimwelekea Nuru.

“Angusha bastola yako, msichana,” yule mwenye chongo alifoka. “Vinginevyo tutasahau wajibu wetu ni kukupeleka hai na badala yake tutaupeleka mzoga wako sawa?”

Nuru hakujibu. Habari hiyo ya kupelekwa hai ilimwongezea nguvu. Alijua kuwa wasingefanya haraka kumuua. Hivyo, alianza kutambaa kutafuta jabali lililokuwa kando, ambalo lingeweza kumuhifadhi. Risasi ya mwenye chongo ilimkosa kichwa kwa nusu inchi tu. Nuru alisikia mlio kama wa nyuki ambaye alipita kasi kando ya kichwa chake. Ili kuwaonyesha kuwa hana mzaha alimwaga risasi tatu tu harakaharaka huku akichupa na kujificha nyuma ya jabali alilokusudia.

Risasi moja kati ya alizomwaga Nuru ilikifikia kifua cha yule aliyeteguka kiuno, ambaye mwenye chongo alimfanya ngao. Alikoroma na kutapatapa kwa nguvu. Kisha, alikata roho.

“Bi mdogo, sasa tunakuua,” Chongo alifoka kwa hasira.

Walivuta miili ya marehemu hao wawili kwa hadhari na kujijengea ngao madhubuti zaidi. Kisha, waliisogelea na kunong’onezana jambo. Wakatabasamu na kutulia, macho yao yalitazama jua ambalo lilikuwa likizama magharibi.

Nuru pia alilitazama jua kwa makini. Akiwa mwenyeji katika kisiwa hiki alijua kuwa ni kiza tu ambacho kingeweza kumuokoa na maadui hao ambao sasa hawakutofautiana na simba aliyejeruhiwa. Hila yake ilikuwa moja tu, atoroke kwa chombo kilichowaleta na kuwaacha hapa kisiwani.

Hivyo, mara tu kiza kilipoanza kufunika kisiwa, Nuru kama nyoka, aliteleza kimyakimya kutoka jabali hadi jabali. Baada ya kila hatua kadhaa alitulia kuwasikiliza maadui zake wanafanya nini. Hakusikia chochote, kisiwa kizima kilikuwa kimya kana kwamba yeye ni kiumbe pekee hai kisiwani hapo. Ukimya huo ulimtisha kiasi kwa kutojua maadui zake wanafanya nini.

“Pengine wao pia wanafikiria kutoroka?” alijiuliza.


Haikuelekea. Watu kama wale, ambao kuua na kufa ni jambo la kawaida kwao, hakuona vipi wangefikiria kutoroka; na hasa kumtoroka mwanamke.

Aliamini kwa vyovyote walikuwa wakimwinda, jambo ambalo lilimfanya aongeze hadhari katika mwendo wake. Kama kivuli chenyewe Nuru aliendelea kunyata toka kichaka hadi kichaka, toka jabali hadi jabali. Macho yake, yaliyohitimu kuona gizani yalikuwa wazi kutazama kichaka na kila kivuli. Hakuiona dalili yoyote ya mtu hai katika maficho hayo. “Wako wapi maadui hawa?” alizidi kujiuliza, akianza kuwaogopa kiasi.

Binadamu wa aina gani hawa, ambao wanaweza kutembea kimyakimya kiasi hicho kama mizimu yenyewe? Alihisi wanamfuata na kuzisoma harakati zake zote. Jambo hilo lilimfanya akose raha.

Hata hivyo, aliendelea na safari yake na hatimaye, alifika pwani. Baada ya kutazama huku na huko kwa makini, aliweza kukiona chombo kilichoegeshwa nchi kavu. Ilikuwa boti yao. Kiasi Nuru aliduwaa. Kwa mara ya kwanza akautilia shaka usalama wa Joram Kiango. ‘Wamemkamata? Wamemuua?’ alijiuliza huku akitetemeka.

Hata hivyo, hakuwa na majibu yake. Badala yake aliendelea kunyata hadi alipoifikia boti hiyo na kuisukuma majini. Kisha, akapanda na kuanza kuishughulikia mashine. Mara tu ilipowaka aliisikia sauti yenye kicheko ikisema “Msichana mzuri … sasa n’takusaidia kuendesha.”

Ilikuwa sauti ya mwenye chongo. Wakati Nuru akigeuka kulenga bastola, alipigwa kwa kitako cha bastola ambacho kilitua barabara juu kidogo ya sikio lake. Pigo la pili hakulisikia. Tayari alikuwa ametekwa na fahamu, akaanguka kama mzoga. Mwenye chongo alicheka na kusema, “well done partner… umeona ilivyo rahisi? Ilikuwa kama kukamata kinda la ndege…”
endelea kuleta mambo tunakusubiria......!!!
 
Mkuu jana peterchoka Hiki kitabu jana nimekikuta maeneo ya posta mpya.. Sema nikanunua mtambo wa Mauti na Jumatatu nakwenda kukinunua hiki... Jana nimesoma Mtambo wa Mauti nikahisi Kueukaruka kwa Utamu na Hisia
 
Mkuu jana peterchoka Hiki kitabu jana nimekikuta maeneo ya posta mpya.. Sema nikanunua mtambo wa Mauti na Jumatatu nakwenda kukinunua hiki... Jana nimesoma Mtambo wa Mauti nikahisi Kueukaruka kwa Utamu na Hisia
posta mpya mtaa gani huo maana hivi vitabu adimu sana mtaani, inabidi tuvizie humuhumu
 
peterchoka pale kwenye sanamu la askari ukifika iwapo unatoka njia ya posta angalia upande wako wa kushoto utaona kituo cha tax kabla ya new africa hotel lakini upande ule ule utaviona pale....
 
au kama unatoka st joseph ipite new africa hotel and casino upande wako wa kulia utaona tax nenda na upande ule ule mbele kidogo utaviona vimepangwa vizuri.. Vipo vingi sana... Tutarudi na Roho zetu, mtambo wa mauti, roho ya paka. Mikononi mwa nunda, dimbwi la damu na Salamu toka kuzimu. Pia kuna vya watunzi na waandishi wengine
 
basi karibia pale ujichukulie... Jana nilitamani nichukue hata vitatu sema pesa niliyonayo ilikuwa ya mambo mengine
 
Back
Top Bottom