Ghasia Afrika Kusini: Mtanzania apata hasara ya mil 300

Idugunde

JF-Expert Member
May 21, 2020
6,273
6,637
Vurugu zilizoibuka wiki iliyopita nchini Afrika Kusini zimemrudisha nyuma kimaisha Mtanzania Omari Juma, anayeishi na kufanya shughuli zake nchini humo.

Juma, aliyekuwa akimiliki studio na kiwanda cha kuchakata chupa za plastiki kwa kushirikiana na raia wa Cameroon, Alino Alino, amejikuta katika wakati mgumu baada ya jengo walilokuwa wanatumia kuhifadhi vifaa kuchomwa moto.

Juzi, balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Gaudence Milanzi alisema Watanzania waishio nchini humo wapo salama na hakuna aliyepata madhara kutokana na ghasia hizo.

Akizungumza na Mwananchi jana kwa simu, Juma, ambaye anaishi jijini Johannesburg, alisema jengo hilo ni ghala la kuhifadhi vifaa na mashine, upande mwingine walilitumia kwa ofisi na studio ya utayarishaji picha za video.

Alisema alfajiri ya Julai 10, alipigiwa simu kuwa jengo hilo limeteketezwa kwa moto na wafuasi wanaopinga kufungwa kwa Rais mstaafu wa Taifa hilo, Jacob Zuma.

Juma alibainisha kuwa wamepata hasara ya Randi 2 milioni sawa na Sh322 milioni walizowekeza kwa ajili ya ofisi na vifaa vilivyotekezwa ndani ya jengo hilo.

“Kwa kweli sijui naanzia wapi ni hasara kubwa tumepata, binafsi nilitumia miaka sita kuipata ile studio ikiwa imekamilika vifaa, mbia mwenzangu alikuwa na mashine za kubana makopo, kwa kifupi tumerudi nyuma.

Nina familia hapa Afrika Kusini na hata Tanzania wazazi wangu wananitegemea, jambo kama hili linapotokea linanipa wakati mgumu nisijue naanzia wapi. Kulikuwa na kazi za watu nimeshafanya, mipango ya kufanya kazi nyingine nayo ilikuwa imekamilika, kwa sasa sijui naanza vipi,” alisema Juma

Naye Rahim Mohamed, Mtanzania aishiye Jimbo la Gauteng, aliliambia Mwananchi kuwa vurugu hizo zimesababisha kuadimika kwa mahitaji muhimu, hivyo kulazimika kusafiri umbali mrefu kwenda kufuata mahitaji hayo.

“Watu wamevamia kwenye supermarkets na kuiba vitu, wamesababisha watu kwenda umbali mrefu kufuata mahitaji muhimu ya nyumbani. Kilichofanyika ni uhuni kwa sababu hata walivyochukua chakula kitaisha kisha watarudi kwenye maisha yao ya kawaida,” alisema Rahim.

Jana Rais Cyril Ramaphosa alitembelea majimbo ya KwaZulu-Natal na Ethekwini kwa ajili ya kuangalia athari za ghasia hizo.

Rais Ramaphosa alivipongeza vyombo mbalimbali vya usalama kwa kutuliza ghasia zilizojitokeza na kusema maandamano ni kinyume cha demokrasia.

Rais huyo alisema uporaji uliofanywa ulipangwa na watu ambao hawana nia njema na demokrasia ya Afrika Kusini.

Taarifa kutoka vyombo vya habari vya Afrika Kusini zinaeleza kuwa hadi sasa watu 117 wamefariki dunia, huku 2203 wamekamatwa kufuatia vurugu hizo.

Kaimu Waziri wa ofisi ya Rais nchini humo, Khumbudzo Ntshavheni alisema kati ya watu 117 waliouawa, 26 wanatoka Jimbo la Gauteng, na wengine 91 wanatoka Jimbo la KwaZulu-Natal.

Maduka mbalimbali yameporwa bidhaa na mengine kuchomwa moto.

Taarifa zinaeleza kuwa vurugu hizo zimesababisha maambukizi ya Covid-19 kuongezeka na takwimu zinaonyesha kuwa Julai 15, 2021 pekee yalitokea maambukizi mapya 16,435 na vifo 377.

Mwananchi
 
Back
Top Bottom