SoC02 Fahari ya jamii ni kilimo cha kisasa

Stories of Change - 2022 Competition

Kaka Ibrah

Member
Sep 6, 2022
83
63
Kilimo ni kitendo cha kupanda ama kuotesha mbegu ya zao husika na kuvuna mazao kwa wakati muafaka. Kitendo hiki huambatana na jukumu la kuulea mmea katika kipindi chote cha kukua kwake hadi pale utakapo toa mazao na kukomaa.

Ukiachilia mbali nguvu ya teknolojia, viwanda, biashara na ajira ikiwa ni kama ni vyanzo vya mtu kujiingizia kipato; kilimo pia ni moja kati ya shughuli mahususi sana kwa maisha ya mwanadamu ikizingatia kwamba huweza kumpatia mtu chakula na pesa kwa wakati mmoja iwapo mtu ataifanya kwa kuzingatia kanuni zinazo shauriwa na wataalamu. Zama tulizopo sasa si za kuendelea kung'ang'ana na kilimo giza, bali sisi waafrika tunapaswa kufanya kilimo mwangaza (kilimo cha kisasa) na ni vyema zaidi hasa sisi watanzania tukawa mstari wa mbele kwa ajiri ya manufaa na maendeleo ya jamii zetu na nchi yetu kwa ujumla.

Mabadiliko ya tabia ya nchi kwa sasa imekuwa ni kikwazo kikubwa hasa kwa upande wa kilimo cha mazoea. Tanzania na watu wake sasa twapaswa tushtuke na kujikita katika kilimo cha kisasa, kwani kilimo cha aina hii huzingatia zaidi matumizi ya mbolea, dawa ya sumu dhidi ya wadudu, kupura magugu na kumwagilia iwapo eneo lina changamoto ya mvua. Pia katika hili teknolojia imerahisisha sana ikiwa ni sambamba na muongozo wa kikatiba hapa nchi ambapo walau mtu mwenye uwezo aweza fanya kilimo cha mkataba kupitia kampuni kadha wa kadha zilizo sajiliwa kisheria hapa nchini.

shamba.jpg

Chanzo cha picha; www.eatv.tv
(Aina ya kilimo kilicho fanywa pasipo kuzingatia njia bora za kisasa za kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi).


kilimo.jpg

Chanzo cha picha; mtanzania.co.tz
(Aina ya kilimo kilicho fanywa kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo/kilimo cha kisasa chenye uwezo wa kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi).


Twaona mifano mingi kupitia nchi za wenzetu ambazo zimepiga hatua kubwa katika nyanja ya kilimo na kuinua uchumi wa nchi zao na kuboresha maisha yao, na kupunguza kwa kiwango kikubwa tatizo la njaa na utegemezi wa misaada ya chakula kutoka kwa mataifa ya Ulaya na Amerika. Hii ni kutokana na kwamba mataifa hayo yameweza kuzingatia kilimo cha kisasa. Mfano wa mataifa hayo ni Botswana, Uganda, Zambia, Misri, Ghana pia Afrika ya Kusini.

Sidhani kama nitakuwa sahihi kusema kwamba zao flani ndilo lafaa zaidi kulimwa kuliko zao jingine, la hasha; Bali kila aina ya zao lafaa kwa kulimwa kulingana na hali ya hewa ya eneo husika. Kila aina ya zao ni muhimu (mazao ya chakula na mazao ya biashara), ili mladi tu eneo maalumu kwa uzalishaji wa zao husika lizingatiwe.

Lakini kwa zama tulizopo kwa sasa kilimo cha mazao ya chakula hatuna budi kujikita zaidi kwacho. Takwimu zinaonesha kuwa idadi ya watu wanao zaliwa kila siku ni kubwa zaidi ukilinganisha na ile ya wanao kufa kila siku. Kwahiyo hapa tunaona kabisa kwamba hitaji la chakula kwa watu duniani lazima liongezeke (tuchangamkie zaidi fursa ya mazao ya chakula). Mfano wa mazao ya chakula ambayo yaweza kulimwa na kustawi vizuri hapa nchini ni kama vile mpunga, mahindi, mtama, karanga, uwele, maharage, kunde, njugu, nakadharika.

shamba-la-mpunga.jpg

Chanzo cha picha; www.mogriculture.com
(Zao la mpunga likiwa linaelekea kukomaa shambani/jarubani).

Kung%27oa+karanga.jpg

Chanzo cha picha; www.mogriculture.com
(Hizi ni karanga zikiwa katika hatua ya kwanza ya kuvunwa, hatua ya pili ni kuzichambua na kuzikausha juani).


Katika ukulima mtu hutarajia mazao kwa ajiri ya mahitaji makuu muhimu mawili, kwa ajiri ya chakula vilevile pia mazao kwa ajiri ya biashara. Shauku kubwa ya wakulima wengi ndani ya nchi yetu imekuwa ni kufikisha mazao yao katika soko la uhakika ili kwamba waweze kufikia malengo ya ndoto zao, lakini hilo limekuwa ni changamoto kwao kutokana na kwamba baadhi yao hawafahamu namna jinsi wanavyo weza kuyafikia masoko. Kuna njia nyingi za kuyafikia masoko na kuonesha mazao yako, kwa mfano; kwa kutumia mitandao ya kijamii, kwa kutumia mawakala, lakini pia kwa kushiriki matamasha mbalimbali ambayo huwaleta wakulima pamoja kama vile sikukuu za nanenane ambako mkulima hupata fursa ya kutangaza mazao yake pasipo gharama yoyote.

thumb_437_800x420_0_0_auto.jpg

Chanzo cha picha; www.arusha.go.tz
(Sherehe za wakulima zilizo waleta pamoja ili kupata fursa ya kuonesha mazao yao mbalimbali, pia kuuza mbegu za mazao, mazao menyewe na pia hapa hupata wasaa mzuri wa kuelezena wapi yalipo masoko mazuri kulingana na aina ya zao husika).


Nyanja ya kilimo ni nyanja nyeti sana kwani ndiko twapata vitu viwili kwa wakati mmoja, yaani chakula na pesa. Hivyo basi; serikali ya nchi yetu pia nayo inajukumu kubwa la kuhakikisha inashirikiana na bodi za kilimo nchini kwa ukaribu zaidi ili kumuwezesha mkulima wa kitanzania kupata manufaa zaidi na kupata hamasa ya kuwekeza zaidi katika kilimo. Hii inaendana na kuweka bei yenye tija kwa mazao ya mkulima pindi yatakapoingizwa sokoni.

Hivyo basi; Ni wakati sahihi kwa mtanzania kulitazama hili swala la kilimo kwa jicho la upembuzi na kuchukua hatua kwalo, kwani chakula kwa mwanadamu ni muhimu zaidi. Kwa mfano; Mtu akiwa amebakiwa na Tshs: 10,000/= mfukoni na hana unga ama mchele ndani halafu akakumbuka kuwa hana umeme (LUKU) ndani mwake, sidhani kama atasitisha kununua unga halafu anunue umeme. Kilimo cha kisasa ndicho chenye tija kwa karne ya sasa kwa kutokomeza njaa, utegemezi wa misaada ya chakula kutoka kwa mataifa ya watu weupe na itapelekea kunyanyua zaidi kiwango cha ubora wa maisha yetu na kuuweka uchumi wa taifa letu katika viwango vya ushindani wa kimataifa.


Shukrani za dhati kwa kila mmoja, nawasilisha.
 
Back
Top Bottom