Roving Journalist
JF Roving Journalist
- Apr 18, 2017
- 4,783
- 14,975
“Rekodi zinaonyesha ukuaji wa uchumi, lakini katika maisha halisi, wananchi wengi hawana fedha za kutosha. Vipato vyao ni vidogo sana, jambo linalowafanya kushindwa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya nchi,” amesema Mbunge Shigongo.
Mbunge huyo ameweka wazi kuwa tatizo la ukosefu wa fedha mkononi kwa wananchi ni la kimsingi na linahitaji suluhisho la haraka. Amesisitiza kuwa Watanzania wanahitaji fursa za kiuchumi ambazo zitawawezesha kuzalisha mapato yao wenyewe badala ya kutegemea misaada au mishahara midogo.
“Serikali lazima itengeze fursa zinazowawezesha wananchi kupata fedha kwa njia endelevu. Hii ni muhimu kwa ajili ya kuwaondolea umaskini na kuhakikisha kuwa ukuaji wa uchumi unaonekana kwa kila mwananchi, siyo tu kwa takwimu,” aliongeza Mbunge Shigongo.
Kauli hii inajitokeza wakati ambapo baadhi ya wananchi wanashikilia kuwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania hauonekani katika maisha yao ya kila siku, huku gharama za maisha zikiwa juu na fursa za ajira na biashara za kipato zinaonekana kuwa chache katika baadhi ya maeneo.