SoC02 Elimu ya uraia wa kidijitali mashuleni

Stories of Change - 2022 Competition

vannie12

New Member
Aug 23, 2022
1
0
Tunaishi katika ulimwengu unaounganishwa na teknolojia, ambapo teknolojia imewezesha shughuli nyingi za kielimu, kiafya, kibiashara n.k. Teknolojia ina athari kubwa kwa jinsi wanafunzi wanavyojifunza na jinsi wanavyojihusisha na elimu yao. Kwa kusudi hili, uraia wa kidijitali ni muhimu uhusishwe kama sehemu muhimu ya mpango wa elimu na maendeleo kwa watoto walio mashuleni na vijana kwa vijana.

Tafiti zinaonyesha kuwa uraia wa kidijitali umekuwa mada kuu kwa waelimishaji kwa takribani miaka kumi sasa, lakini mada hii imeibuka haraka katika miaka miwili iliyopita, na haswa mwaka jana ambapo masomo ya darasani na ya mseto yamehamia kwenye mifumo ya kijiditali kutokana na janga la COVID -19.

Ikiwa baadhi ya shule zimeanza kuzingatia uraia wa kidijitali kama njia ya kuwatayarisha wanafunzi katika ulimwengu wa kimtandao, Benki ya dunia nchini Tanzania inasisitiza utoaji wa elimu ya kidijitali kama njia mojawapo ya kukuza uchumi na kusaidia vizazi vijavyo katika ulimwengu wa teknolojia na mitandao.
Je ni nini hasa maana ya uraia wa kijiditali?

Uraia wa kidijitali ni matumizi ya teknolojia kwa njia sahihi. Kadhalika, ni mjumuiko wa maadili, tabia na majukumu ambayo yanaruhusu kila mtu kushiriki katika jumuiya za mtandaoni kwa tija, usalama na uwajibikaji.

Hapo awali, uraia wa kidijitali ulizingatia usalama na uhalali ikiwemo ulindaji wa nywila (passwords), utambulisho wa taarifa (profile creation) na mengineyo, lakini sasa inaangazia zaidi jinsi wanafunzi wanaweza kuwezeshwa kutumia zana na majukwaa ya kidijitali katika kunyakua fursa mbalimbali duniani. Kupitia ujuzi mbalimbali utokanao na elimu ya kidijitali, wanafunzi wanaweza kuwa salama mitandaoni na kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoambatana na mitandao.

Vipengele muhimu 5 vya uraia wa kidijitali ambavyo kila mwanafunzi anapaswa kujua, kuelewa, na kujifunza;
Upatikanaji/Uwezeshaji wa kidijitali. Licha ya kuongezeka na kuenea kwa huduma za mtandao, kuna changamoto ambazo zinazuia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa intaneti mashuleni. Zaidi ya hayo, shule nyingi za serikali hususani nchi zinazoendelea kama vile Tanzania hazina maabara za kompyuta kwa ajili ya wanafunzi kutumia.

Hadi sasa, Tigo kwa kushirikiana na programu ya Apps and girls imesaidia zaidi ya wanafunzi 64,000 katika upatikanaji wa intaneti bila malipo kote Tanzania. Lakini tujiulize. Je, ukiangalia hio idadi, unadhani imekidhi mahitaji ya intaneti kwa idadi ya wanafunzi wote nchini Tanzania?

Ujuzi wa kidijitali. Ni moja ya vichocheo vya maendeleo ya mifumo ya kidijitali. Na hivyo, husaidia katika ufahamu wa jinsi ya kutafuta fursa mbalimbali kupitia mitandao, na pia muhimu kwa kujifunza. Ujuzi wa kidijitali unaweza kuwasaidia wanafunzi katika kutafuta kazi au ajira endapo wakimaliza masomo yao, kujua ni taarifa gani watumie na programu zipi zenye manufaa katika ulimwengu wa mawasiliano.

Mfano mwaka 2019, Tigo ilizindua ujuzi wa uandishi wa programu za kompyuta (coding) kwa wanafunzi wa kike mashuleni ikiwa na lengo la kukuza elimu ya ujuzi wa kidijitali ili wanaweza kutumia mtandao vyema na kuweza kujisimamia katika maeneo tofauti katika majukwaa ya kidijitali.

Sambamba na hilo, hivi karibuni Kenya imekuwa nchi ya kwanza Afrika kuhalalisha uandishi wa programu za kompyuta “coding” kama moja wapo ya somo katika mitaala yao ya elimu. Lengo hasa ikiwa ni kusaida wanafunzi kupata ujuzi muhimu ambao utawasaidia katika kujiajiri.

B544E385-0E91-4948-9606-E22DF782B875.jpeg

Picha na Cartoonstock


Mawasiliano ya kidijitali. Hii inahusisha zana za mtandaoni kama vile majukwaa ya kijamii kama facebook, twita n.k, na barua pepe za kuwasiliana. Utafiti unaonyesha mawasiliano ya kidijitali yanaweza kuboresha uwezo wa kujisomea kwa wanafunzi kupitia kuandika na kuunda maudhui. Ni rahisi pia kwa walimu kutumia kama njia ya mawasiliano baina yao na wanafunzi katika kujadili madhumuni ya kujifunzia. Wanafunzi wanaweza pia kuwasiliana na kuunda magrupu ili kuzua mijadala ya kimasomo. Kwa mfano, baadhi ya shule nchini Tanzania, zimeweza kuwatengenezea wanafunzi barua pepe za binafsi ambazo hutumika kuwasiliana na walimu na kuuliza maswali tofauti kuhusu masomo yao.

Haki na wajibu wa kidijitali. Watu wengi ukiachilia mbali wanafunzi wamekuwa wakipata changamoto katika haki na wajibu wao wa kijiditali, na hivyo kupelekea wengi wao kuingia hatiani kwa makosa mbalimbali ya kimtandao kama vile wizi wa taarifa na maudhui, utambulisho wa mtu binafsi, hali kadhalika matusi na lugha zisizo na staha. Hivyo basi ikiwa wanafunzi wanaojihusisha na mitandao ni miongoni mwa watumiaji hai wa teknolojia ya kidijitali, ni muhimu kufundishwa jinsi ya kutii sheria, haki na wajibu wa nafasi zao wanapokuwa mitandaoni ili waweze kuepukana na athari ambazo kwa namna moja au nyingine zinaweza kupelekea uvunjaji wa haki na sheria.

Usalama wa Kidijitali. Kiujumla ni taratibu au zana zinazotekelezwa katika kulinda rasilimali zinazotumika kama utambulisho kwa watumiaji wa mitandao. Mfano wa rasilimali hizo ni kama nywila (passwords), taarifa binafsi za mtumiaji. Hii husaidia kuepukana na wizi/udukuzi wa taarifa, utambulisho wa mtu binafsi n.k. Vilevile, usalama wa kidijitali unahusishwa na uhalifu, utapeli na vitisho (attacks) vya mitandao. Hivyo ni vyema kuhakikisha walimu na wakufunzi wa teknolojia mashuleni wanawapa wanafunzi elimu ya jinsi ya kuambatana na vitisho na uhalifu wa mtandaoni na jinsi gani wanaweza kuepukana navyo. Mfano. Kuhakikisha wanafuta taarifa zao binafsi pindi wanapoingia mitandaoni, kutambua meseji za vitisho na kuripoti sehemu husika, kutoamini watu na taarifa zao mitandaoni n.k. Ili waweze kuwa salama pindi wanapotumia mitandao.

Aidha, mtaala wa elimu hapa nchini unaohusisha somo ya TEHAMA, lililojikita hasa katika kufundisha matumizi ya kawaida ya kompyuta kama kuwasha kompyuta, kufungua folda na n.k lakini tujiulize, je hivi vinamnufanisha vipi mwanafunzi katika ushindani wa soko la ajira pale ambapo anapomaliza masomo yake?

Sambamba na hilo, Team4tech inadhibitisha kuwa, chini ya 10% ya wanafunzi wa shule za msingi hupata nafasi ya awali ya kujifunza kusoma, kuandika, kuhesabu na stadi za maisha zinazohitajika kwa ajili ya elimu zaidi. Kwa sababu hii, upatikanaji wa elimu ya kidijitali nchini Tanzania ni mdogo. Tuchukue nchi kama Afrika ya Kusini ambako mfumo wao wa elimu umeonekana kuwa wa mafanikio kwani unasaidia wanafunzi kufaulu katika nyanja mbalimbali za maisha.

Ni wakati muafaka kwa Tanzania kuhusisha elimu jumuishi na kutengeneza programu na mitaala ya elimu ya jumla (holistic education) ili kuwasaidia wanafunzi kupata ujuzi tofauti tofauti ambao ni muhimu na utawasaidia katika fursa mbalimbali zenye maslahi katika Karne hii ya 21. Ujuzi kama vile uongozi, kujiamini, ubunifu na mawasiliano vinaweza kusaidia wanafunzi kukuza uwezo katika ulimwengu wa mtandaoni na maeneo halisi ukiachilia maarifa ya taaluma pekee wapatayo mashuleni.

Vyanzo vya habari:

Gazeti la mwananchi , 2020

Chapisho la Kreston global, 2022

https://africabusinesscommunities.com
 
Back
Top Bottom