SoC02 Elimu ya huduma ya kwanza kwa watoto wachanga itolewe kliniki ili kuepuka vifo vya ghafla vya watoto wachanga

Stories of Change - 2022 Competition
Aug 1, 2022
14
14
Huduma ya kwanza inamaanisha huduma au msaada Unaotolewa kwa mtu anayekabiliwa na ugonjwa au madhara ya ghafla wakati daktari anapokua hayupo karibu na kabla hajapelekwa hospitalini au kituo chochote cha afya kilichopo karibu kwa matibabu zaidi.

Vifo vya ghafla vya watoto wachanga au kwa lugha ya kitaalamu, “sudden infant death syndrome (SIDS)” ni aina ya kifo kwa mtoto ambacho hutokea kwa kushtukiza bila kutarajia kwa watoto walivo na umri chini ya mwaka mmoja.

Kwa kawaida mama mjamzito au ambaye ameshajifungua anahudhuria kliniki kila baada ya kipindi fulani wanachopangiwa na daktari ama wakungwa wao na huko ndiko wanakopata elimu juu ya lishe kwa ajili ya mama na mtoto, maendeleo na ukuaji wa mtoto na afya yake kiujumla

Mara zote mahudhurio ya kliniki utaratibu umekua ni ule ule kwamba unapofika Kama mzazi mtoto wako anapimwa kilo na kupewa chanjo kulingana na umri aliofikia vile vile muuguzi atakuuliza maswali machache kuhusiana na maendeleo ya mtoto kisha kurudi nyumbani.

Mbali na hayo pia hospitali nyingi katika kuta zao wamekua wakibandika mabango mbalimbali ya muhimu Kama kupasuka kwa midomo ya mtoto, dalili hatarishi kwa mama mjamzito, dalili hatarishi kwa mtoto Mchanga, UVIKO, VVU n.k lakini katika haya yote wanasahau kuweka mabango yanayoelimisha juu ya huduma ya kwanza ya kumpatia mtoto mdogo hususani alie chini ya umri wa mwaka mmoja kwani huyu hata kuongea hawezi.

Baadhi ya dharura hatarishi zinazoweza kumkuta mtoto mdogo na huduma yake ya kwanza.
Kuna mambo mengi hatarishi ambayo yanaweza kumkuta mtoto mdogo ambayo wazazi wengi wamekua hawajui cha kufanya yanapowapata kitu ambacho kinapelekea mtoto kupata matatizo makubwa ya kiafya na muda mwengine mpka kifo lakini mimi nitaongelea moja muhimu ambalo linawatokea watu wengi na kwa sababu hawana elimu ya kutosha yanawakuta matatizo makubwa zaidi ya walioyatarajia.

Moja, mtoto kukosa pumzi. Kuna sababu nyingi zinazoweza kusababisha mtoto kukosa pumzi ikiwemo, aina ya kumlaza kwa kulalia tumbo kunaweza mfanya abane pumzi, kuzama kwenye maji. Kupaliwa chakula au kimiminika, kubanwa na ziwa la mama wakati wa kunyonyeshwa, shoti ya umeme n.k.

Kuna baadhi ya wazazi nimeona wakitoa ushuhuda mfano mmoja alisema mtoto wao alitokwa na maziwa puani ghafla wakati amemlaza mpka akaacha kupumua na alichanganyikiwa na kushindwa kujua cha kufanya hivyo akamuwaisha hospitali japo ilikua mbali lakini mama huyu angekua ana elimu ya huduma ya kwanza katika hali kama hii angeweza kumfanyia mtoto huduma ya kwanza ambayo ingeweza kumsaidia mtoto hata kupona pale pale kabla hata ya kufika hospitali.

Kwa kawaida unapomuona mtoto wako haswa mchanga hapumui lazima uchanganyikiwe na kuweza kufanya jambo ambalo linaweza kumueka mtoto wako kwenye hatari kubwa zaidi ya aliyokua nayo.

Jambo muhimu la kufanya unapogundua mtoto amekosa pumzi ghafla kwanza ni kumfanyia Cardiopulmonary resuscitation (CPR) kwa bahati mbaya kamusi yetu ya kiswahili bado haina maana ya kiswahili ya utaratibu huu ila kwa lugha rahisi ni utaratibu wa dharura wa kumrudishia pumzi na kufanya damu iendelee kujisafirisha kwenda kwenye ubongo kwa mtu alieishiwa pumzi ghafla Kama kupitia mshtuko wa moyo n.k.

Mtu anaeweza kufanya utaratibu huu kwa usawa ni yule aliefanyiwa mafundisho ya kitaalamu lakini katika nchi za magharibi wenzetu wameweza kuwafundisha wananchi wao jinsi ya kufanya japo mambo msingi ili kujitahidi kumuokoa mtu aliepatwa na tatizo na hatua zifuatazo ni hatua chache unazoweza kufanya ambazo pia nitaziambatanisha na video za jinsi ya kumuokoa mtoto mwenye tatizo linalohitaji CPR.

Hatua ya kwanza ni Kutafuta msaada wa haraka kuelekea hospitali kama ni ndugu au mtu wa karibu yoyote atakayeweza kuwapeleka hospitali au jaribu kutumia namba hizi Za dharura. 112- Dharula, 115- Ambulance, 116- msaada wa watoto na 117- Afya.

Hatua ya pili ni Kuhakikisha mtoto umemlaza kwa kuangalia juu sehemu iliyo ngumu na Flati (hii ni muhimu sana na la kuzingatia japo wazazi wengi wa kitanzania wanaamini mtoto anakua salama zaidi akiwa amelala kwa tumbo, kutoa huduma ya kwanza ni lazima mtoto awe amelala huku anaangalia juu ndio njia safi na salama).

Hatua ya tatu ni utachukua vidole vyako viwili vya mkono wa kulia na kuvikandamiza katikati ya kifua cha mtoto chini kidogo ya mstari wa unaolinganisha chuchu kama inavyoonekana kwenye video

Hatua ya nne Utaanza kukandamiza na vidole vyako kwenda chini mara 30 kwa jina la kitaalamu hii inaitwa kumfanyia “compressions”.

Hatua ya tano Baada ya kumaliza hatua ya nne inabidi uwahi kuhamia kwenye kichwa cha mtoto ambapo utainua kichwa kidogo kama unakirudisha nyuma, kisha utamziba pua na mdomo kwa kutumia mdomo wako kisha utampumulia mara mbili kwa sekunde moja kisha utarudi kumfanyia compressions kama mwanzoni huku ukiwa unaangalia mapigo yake ya moyo kupitia kifundo cha mkono.

Hatua ya sita na ya mwisho Endelea kufanya hizi hatua mpaka msaada utakapokuja kwani kwa kufanya hivi unasaidia damu kuendelea kutiririka kuelekea kwenye ubongo na viungo vingine muhimu.

Dharura ya pili ni pamoja na Ajali za moto. Hizi ajali ziko tofauti mfano kuungua na vimiminika vya moto kama maji au mafuta ya kupikia, chai, maziwa n.k. Kuna siku moja nikiwa hospitali, mama mmoja aliingia na mwanae alieungua mkono na ngozi ilikua imening’inia. Baada ya kuongea na yule mmama na kunieleza ni kitu gani kimempata mwanae, alisema ya kwamba mwanae aliungua na mafuta ya samaki bahati mbaya na hakujua cha kufanya hivyo akamwagia maji na kujaribu kumfuta yale mafuta kumbe ndo alikua anamuondoa ngozi mwanae.

Kuna matukio mengi ya watoto kuungua na vitu vya moto Kwa sababu ya mazingira tunayoishi pia watoto wana asili ya udadisi na kwakua hakuna elimu ya kutosha kwa wazazi juu ya huduma ya kwanza, mtoto anakua kwenye hatari zaidi anapopatwa na tatizo hilo hivyo ni muhimu kupata elimu ya huduma ya kwanza.

Huduma ya kwanza kwa ajali za kuungua na moto hutegemea na aina gani ya kuungua mtoto amepata lakin kikubwa Kama mtoto ameunguzwa na kimiminika inabidi mzazi aangalie kwanza ni kwa kiasi gani mtoto ameungua Kama ni pakubwa au padogo.

Kama ameungua kawaida unaweza kumpatia huduma ya kwanza kisha uaendelea kumuangalia mtoto huyo kwa umakini mtoto huyo unaweza kumpatia huduma ya kwanza kwa njia zifuatazo:
  • mwagilizia maji kwa muendelezo kwenye jeraha kwa muda wa dakika 15. ikishindikana kufanya hivi
  • Pepea sehemu yenye jeraha, ila usitumie barafu kwani linaweza kusababisha athari zaidi.
  • Unaweza kumpa mtoto dawa za kupunguza maumivu Kama panado za watoto. Usimpatie mtoto dawa yoyote ile tofauti na dawa husika kwa watoto wachanga.
  • Unaweza kumpaka asali kwenye jeraha Kwani asali inasaidia vidonda kupona kwa haraka zaidi.
  • Lizibe jeraha kwa kulifunga na bendeji ama kitambaa kilicho safi na hakikisha hukazi sana wakati wa kufunga.
  • Angalia hali ya mtoto kisha umpeleke kituo cha afya kilicho karibu kwa uangalizi zaidi
Kwakua kliniki ndio sehemu ya lazima mama kwenda kwaajili ya kujua maendeleo ya mtoto katika miaka yake mitano ya mwanzo basi ndio sehemu nzuri ya kuwafundisha akina mama jinsi ya kutoa huduma za kwanza kwa dharura mbalimbali zinazowatokea watoto wachanga ili wanapokuja kujifungua wawe tayari na uelewa na Pia kwa wale ambao tayari wameshajifungua wanakua tayari wamejengewa ujasiri wa kukabiliana na changamoto hizo.

Ni muhimu sana kwa watanzania wote kujifunza mambo haya ya msingi kwani si mama mzazi tu ambae anaweza kukutwa na tatizo kama hili hata wewe ndugu, rafiki au mtu wa karibu inaweza kukukuta wakati upo karibu na mtoto wa mwenzako hivyo kupata elimu hii ni kuokoa maisha ya binadamu. Kwa mtazamo wangu nashauri elimu hii ingetolewa kwa ulazima sio tu kwenye mahudhurio ya kliniki bali hata mashuleni na sehemu nyengine nyingi kuanzia shule za msingi mpka awali.

Katika Uzi huu nimeambatanisha pia na dharula nyengine inayoweza kumkuta mtoto chanzo cha video ni mtandao wa kijamii wa tiktok account ya forwardmedicine.

Nawakaribisha wote kwa maoni na maswali ni furaha yangu kueza kuelimika pamoja na nyie asanteni.

View attachment 2356018
 
Back
Top Bottom