SEHEMU YA 40
“Alianguka? Alianguka? Ina maana atakufa? Irene mtoto wangu atak…” alisema Rosemary, hata kabla hajamalizia sentensi yake, presha ikapanda, akadondoka chini.
“Rose…Rose…Rose mke wangu,” aliita Mapoto huku akilia, manesi wakafika mahali hapo haraka sana, mapigo yake ya moyo yalianza kushuka, wakambeba na kumuweka kwenye machela, mwili wake ulimlegea, alionekana kama tayari alikwishakufa. Manesi wenyewe wakatingisha vichwa vyao kushoto na kulia kuonyesha kwamba inawezekana huo ulikuwa mwisho wa mwanamke huyo.
***
Mapoto alijipa moyo kwamba mtoto wake angeweza kupona na kurudi katika hali ya kawaida. Moyo wake ulikuwa na huzuni kubwa, kila alipokuwa akiikumbuka sauti ile ambayo aliamini kwamba ilikuwa ni sauti ya shetani, alijikuta akichukia moyoni mwake.
Hakuwa na tumaini jingine zaidi ya Mungu wake aliyekuwa akimuabudu. Kila saa alimwambia mke wake washikane mikono na kuanza kusali kwani aliamini kwamba Mungu angekwenda kufanya muujiza na hali waliyokuwa wakiipitia ilikuwa ni jaribu ambalo lilikuwa ni lazima walishinde.
“Mke wangu! Hili ni jaribu. Namuamini Mungu wangu, hawezi kukupa jaribu kubwa zaidi ya uwezo wako! Hili ni jaribu linalolingana na uwezo wetu, hatuna budi kulishinda,” alisema Mapoto huku akimwangalia mke wake ambaye macho yake yalikuwa mekundu mno kuonyesha ni kwa jinsi gani alikuwa amelia sana.
“Amen!” alijibu mkewe, hakutaka kuzungumza maneno mengi kwani kila alipotaka kufanya hivyo, moyo wake uliuma zaidi.
Upasuaji ukaanza, baada ya kukichana kichwa cha Irene, wakaanza kutoa kipande cha fuvu ambacho kitaalamu huitwa Bone Flap na kisha kukiweka pembeni kwa ajili ya kuangalia ndani ya ubongo kuona kulikuwa na nini.
Wakati wakiendelea kufanya upasuaji huo bado walikuwa wakizungumza huku wakikiangalia kichwa hicho kwa makini kabisa ambapo huko wakaliona donge la damu likiwa limeganda katika ubongo wake, tena kwa kujificha ndani ya ubongo kwa mbali.
“Ooh my God!” (Ohh Mungu wangu) alisema Dk. Phillips huku akionekana kushtuka kwani donge lile lilionekana kuwa kubwa tofauti na walivyodhani.