SEHEMU YA 39
“Sawa. Ndiyo maana! Tumempa chumba apumzike kwanza. Mkitaka kumuona, mnaruhusiwa, ila mtatakiwa kuwa kimya, amepumzika,” alisema daktari.
“Sawa.”
Wakatoka ndani ya ofisi hiyo na kuanza kuelekea katika chumba alicholazwa Irene. Mapigo ya moyo wa Mapoto yalikuwa juu kwa kiwango kikubwa, alikuwa na hofu kubwa kwa kuhisi kwamba inawezekana mkewe angegundua kile kilichokuwa kimetokea Irene mara baada ya kumuona kitandani hapo.
Walipokifikia chumba hicho, wakaufungua mlango na kuingia ndani. Irene alikuwa kimya kitandani, waliambiwa kwamba alikuwa amepumzika hivyo hata Rosemary alivyomuona mtoto wake kitandani pale, hakuonekana kuwa na hofu kabisa.
“Nafikiri baadaye atakuwa kwenye hali ya kawaida,” alisema daktari.
“Tunashukuru sana!”
Mpaka kufikia hapo, wakawa na uhakika kwamba walifanikiwa kuutuliza moyo wa Rosemary, hakuonekana kuwa na presha, aliamini kile alichokisema mume wake.
Wakatoka na kukaa kwenye viti vilivyokuwa nje ya chumba kile, walikuwa wakizungumza huku Mapoto akijitahidi sana kujiweka katika hali ya kawaida.
Baada ya dakika kadhaa, dereva wake, James akafika hospitalini hapo akiwa na Godwin.
Alipomuona mama yake, akamkimbilia, alipomfikia, wakakumbatiana huku Godwin akilia kwa maumivu makali kiasi kwamba Rosemary alishangaa.
“Unalia nini?”
“Irene…Irene…”
“Amefanya nini?” aliuliza Rosemary.
“Anaumwa kichwa tu. Godwin njoo kwa baba,” alisema Mapoto huku akimchukua Godwin.
“Hebu subiri kwanza. Godwin, Irene amefanya nini?” aliuliza.
“Atakufa! Mwalimu amesema Irene atakufa, alianguka darasani,” alisema Godwin huku akimwangalia mama yake, Rosemary aliposikia maneno hayo, akahisi kama alipigwa na shoti ya umeme, akayapeleka macho kwa mume wake, Mapoto alibadilika, machozi yakaanza kumlenga, akayainamisha macho yake chini kwani hata kukutanisha macho na mkewe aliogopa.
“Irene alianguka darasani? Atakufa? Alianguka darasani au anaumwa kichwa?” aliuliza Rosemary huku akimwangalia mume wake.
“Nisamehe mke wangu!”
“Niambie! Ukweli ni upi?”
“Ire..Irene…Iren…”
“Niambie amefanya nini?” aliuliza mke wake kwa sauti ya juu, tayari machozi yalianza kumtoka, maumivu aliyoyasikia moyoni mwake kipindi hicho hayakuweza kuelezeka.
“Alianguka!”