Dunia haina usawa

Dunia haina usawa

SEHEMU YA 51

Hapo alipokaa kwenye ndege alikuwa na mwanaume mmoja, alikuwa mtu mzima kidogo, walianza kupiga stori na kuzungumza mambo mengi. Walichangamkiana na mzee yule aliposikia kwamba alikuwa mwandishi wa habari, alifurahi zaidi.

“Nitataka kuanzisha gazeti langu la siasa, nadhani nitafanya mawasiliano na wewe ili uje kunipa mawazo juu ya nini cha kufanya,” alisema mzee huyo huku akiwa kwenye tabasamu pana.
Wakakubaliana, walipofika Dar es Salaam, ndege ikaanza kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere. Iliposimama, wakainuka na kuanza kuelekeea nje.

“Nina mizigo mingi sana, unaweza kunibebea mmoja hadi nje?” aliuliza mzee huyo.
“Hakuna shida.”
Wakaelekea sehemu ya kuchunguzia mizigo yao, walipoichukua, mzee yule akampa begi lake Matamshi ili amsaidie mpaka nje ambapo angechukua teksi na kuelekea nyumbani.

Huku akiwa na begi lile na kupiga hatua nje, ghafla akashtuka akisimamishwa na polisi wawili waliokuja mbele yake. Mzee yule hakusimama, aliendelea kupiga hatua kwenda mbele, na hata alipoitwa, hakugeuka.

“Simama hapo,” alisema polisi mmoja.
“Kuna nini?”
“Tunahitaji kukuchunguza!”
“Ili?”
“Tunahisi umebeba madawa yya kulevya!”
“Nimebeba madawa ya kulevya?”
“Ndiyo! Twende kwenye chumba kile,” alisema polisi mmoja na polisi wengine watatu kuongezeka.

Matamshi hakuonekana kuwa na hofu, alijua kabisa kwamba hakuwa muuzaji wa madawa ya kulevya, hakuwahi kuyatumia, hakutaka kupinga, akaondoka nao na kwenda kwenye chumba kimoja na kukaa huko.

Polisi wale wakaanza kuangalia mizigo yake, hakukuwa na kitu. Hapo ndipo walipoanza kulipekua begi lile alilopewa na mzee yule. Muda wote Matamshi alikuwa akitabasamu, alijijua kwamba alikuwa mtu msafi na hakuhusika kabisa na biashara hiyo haramu.

“Umejitetea sana kwamba hujabeba madawa ya kulevya, na haya ni nini?” aliuliza polisi mmoja huku akitoa mfuko wa madawa ya kulevya, Matamshi akapigwa na mshtuko, hakuamini kuona mzigo wa madawa ya kulevya ukitolewa ndani ya begi.

“Hapana! Huo mzigo siyo wangu! Ni wa mzee aliyeniambia nimbebee,” alijitetea huku macho yakiwa yamemtoka.
 
SEHEMU YA 52

“Hapana! Huo mzigo siyo wangu! Ni wa mzee aliyeniambia nimbebee,” alijitetea huku macho yakiwa yamemtoka.
“Hahah! Wenzako wote wanaokamatwa husema hivyohivyo! Upo chini ya ulinzi,” alisema polisi mmoja na polisi mwingine kuchukua pingu na kumfunga mwanaume huyo.

“Jamani! Mimi siyo mzigo wangu huo!” aliendelea kujitetea huku akianza kulia.
“Sawa. Ila si ndiyo begi jingine ulilokuwa nalo!”
“Nilikuwa namsaidia yule mzee. Jamani! Nisikilizeni, mimi sihusiki na madawa, sijawahi kutumia wala kuuza. Jamani! Mimi ni mwandishi wa habari!” alisema Matamshi huku akilia kama mtoto.

“Utamwambia hakimu mahakamani! Ila miaka ishirini inakuhusu,” alisema polisi mmoja huku wakimchukua na kuondoka naye ndani ya chumba hicho. *** Mapoto aliendelea kumuuguza mtoto wake, Irene aliyekuwa hoi kitandani. Kila siku katika maisha yake ilikuwa ni siku ya maombolezo, hakuacha kulia, alifarijiana na mkewe kwa kuamini kwamba kuna siku mtoto wao angesimama tena lakini kikafika kipindi mioyo yao ikakata tamaa kwa kuhisi kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa kumuona mtoto wao akiwa hai.

“Hivi kweli Irene atapona?” aliuliza Mapoto huku akimwangalia Dk. Phillips.
“Tunaamini hivyo!”
“Imani ni jambo la kiroho zaidi. Hebu niambie kibinadamu, kweli mnahisi atapona?” aliuliza Mapoto.

“Tunajitahidi sana kumrudisha katika hali ya kawaida, na ukweli ni kwamba atarudiwa na fahamu japokuwa hatujajua ni kwa muda gani. Hutakiwi kuwa na hofu, tumuachieni Mungu, kuna siku mtoto Irene atafumbua macho tena,” alisema Dk. Phillips.

Siku ziliendelea kwenda mbele, kitandani pale Irene hakuonyesha mabadiliko yoyote yale, alikuwa vilevile kama siku ya kwanza. Kula kwake, alikula kwa kutumia mipira huku hata kupumua alipumulia mashine ya oksijeni.

Kila siku walimu na wanafunzi wenzake walikuwa wakifika hospitalini hapo kumjulia hali. Godwin hakuwa na furaha tena, alitawaliwa na majonzi, kila alipokuwa akimuona dada yake akiwa kitandani alikuwa akilia tu.
 
SEHEMU YA 53

Hakuacha kuwauliza wazazi wake juu ya Irene, alitaka kujua ni siku gani ambayo dada yake angeamka lakini hakukuwa na mtu aliyempa majibu ya kuridhisha na hivyo kuhisi kwamba inawezekana Irene angekufa kitandani pale.

“Will she open her eyes again?” (atayafumbua macho yake tena?) aliuliza Godwin huku akimwangalia baba yake.
“Yes!” (ndiyo)
“When?” (lini?)
“Very soon.” (hivi karibuni)
Hakuwa na jinsi, kila alipomwangalia Godwin alimuonea huruma, kila siku alikuwa akilia, kama yeye na Rosemary walivyokuwa wamekata tamaa basi hata naye Godwin alikuwa amekata tamaa.

Alimfariji, alimdanganya kwamba Irene angefumbua macho hivi karibuni japokuwa hakuwa na uhakika juu ya hilo. Siku zikaendelea kukatika, baada ya mwezi mmoja kidogo hali ya Irene pale kitandani ikaanza kuonyesha mabadiliko, vidole vyake vikaanza kuchezacheza kitandani pale.

“Vidole vyake vimeanza kuchezacheza,” alisema nesi aliyekuwa akimuhudumia kila siku.
“Kweli?” aliuliza Dk. Phillips.
“Ndiyo!”
Daktari huyo akatoka ndani ya ofisi yake na kuelekea katika chumba kile. Alikuwa akikimbia kiasi kwamba hata Mapoto na familia yake waliokuwa nje ya chumba kile wakashangaa na kuhisi kwamba ndani kulikuwa na tatizo.

Dk. Phillips akaingia ndani ya chumba kile, alionekana kuchanganyikiwa kwa furaha, ni kweli Irene alianza kutingisha vidole vyake kuonyesha kwamba alikuwa amerudiwa na fahamu. Alisimama na kuumwangalia mtoto huyo kitandani, kwa mbali sana akaanza kuyafumbua macho yake kwa kuangalia huku na kule.

Hawakuamini, baada ya kukaa kitandani kwa mwezi mzima, hatimaye leo mtoto huyo alikuwa amefumbua macho na kuwaangalia. Alionekana kushangaa, ni kama hakujua sababu iliyomfanya kuwa mahali hapo, alimwangalia daktari, hakujua walikuwa wakina nani.

“I want to see my Godwin,” (nataka kumuona Godwin wangu) alisema Irene kwa sauti ya chini huku akimwangalia Dk. Phillips ambaye uso wake ulitawaliwa na tabasamu pana.
 
SEHEMU YA 54

“Doctor…tell us what is going on…you freaking us out…” (daktari tuambie ni kitu gani kinaendelea…umetutisha…) alisikika Mapoto nje ya chumba kile huku akigongagonga mlango, alionekana kuwa na hofu kubwa kwani kitendo cha kumuona daktari yule akikimbia kuelekea ndani ya chumba kile, alihisi kulikuwa na tatizo.

“Welcome back to the world,” (karibu tena duniani) alisema Dk. Phillips huku uso wake ukiwa na furaha tele.
***
Rais Bokasa alichukia, kitendo cha kumuona mwandishi Matamshi akielekea chooni na Mapoto alihisi kabisa kulikuwa na kitu kilichokuwa kikiendelea. Moyo wake uliwaka kwa hasira na muda wote alikuwa akimwangalia mwandishi huyo huku akionekana kuwa na hasira kupita kawaida.

Hakukuwa na jambo jingine la kufanya zaidi ya kumuua mwandishi huyo kwani aliamini kwamba kama angemuacha akafika nchini Tanzania na kupelekea taarifa juu ya kile kilichokuwa kikiendelea basi hali ingekuwa ya hatari na watu wangeshinikiza mwanasiasa huyo kuandika barua ya kujiuzulu.

Ilikuwa ni lazima amuue, hakukuwa na jingine ambalo lingetakiwa kufanyika zaidi ya hilo. Akawapanga watu wake kwa ajili ya kummaliza kwa sababu tu alitaka kutetea kiti chake cha urais.
“Mkuu! Hatutakiwi kumuua! Nilikuwa na wazo moja,” alisema kijana wake aliyekuwa amempa kazi hiyo.

“Lipi?”
“Tumfunge. Tukifanikiwa katika hilo, basi tumemuweza. Kama tukimuua, kuna watu watahisi kwamba wewe ndiye umehusika, huyu ni lazima tumfanyie kitu ambacho kitawafanya watu kutokugundua kitu chochote kile,” alisema kijana huyo aliyeitwa kwa jina la Edson Pius.

“Sawa. Tutamfunga vipi?”
“Tumuwekee mzigo wa madawa ya kulevya, akifika uwanja wa ndege, akamatwe!” alishauri.
“Tutamuwekeaje?”
“Hapo ndiyo uniachie mimi!” alisema Edson.

“Sawa.”
Alimuamini kijana huyo, alikuwa miongoni mwa watu waliokuwa na uwezo mkubwa wa kufikiria, kazi hiyo akaiacha mikononi mwake kwa kuamini kwamba ingefanikiwa haraka iwezekanavyo.

Edson akamuandaa mwanaume mmoja ambaye alitakiwa kuondoka nchini Tanzania na kwenda Marekani haraka sana, huko alikuwa na kazi ya kurudi na mzigo mdogo wa madawa ya kulevya.
 
Jaman mbona hii kitu tamu sanaaa,daah shunie mama ahsante kwa kutupa raha
 
SEHEMU YA 55

Hilo halikuwa tatizo, mtu huyo aliyetumwa akaelekea huko. Alikuwa mzee wa makamo ambaye alikuwa rahisi sana kuaminika na mtu yeyote yule. Alipofika, mzigo wa madawa ya kulevya ulikuwa umeandaliwa na kupakiwa katika mfuko mmoja wa mzee huyo ambaye alipitishwa sehemu ya VIP kwa kuwa na kitambulisho kilichoonyesha ni mfanyakazi kutoka katika ikulu ya Tanzania.

Alipoingia ndani ya ndege, akamtafuta Matamshi na kwenda kukaa naye. Alihitaji kumchangamkia ili asimkatalie kwa kitu chochote kile ambacho angemwambia mwisho wa safari.
Kwa kipindi kifupi tu wakawa marafiki wakubwa kana kwamba waliwahi kuonana kipindi kirefu nyuma.

Matamshi hakugundua kama mzee huyo alikuwa na mambo yake, alimzoea kama abiria wengine na hata walipofika Dar es Salaam na kumwambia amshikie begi lake, mwandishi huyo hakuwa na hofu naye kabisa, alipofanya hivyo, akajikuta akikamatwa na polisi.

Polisi waliendelea kumshikilia Matamshi, wakamchukua na kuelekea naye katika kituo cha polisi kilichokuwa hapohapo uwanjani. Alikuwa akilia, aliendelea kuwaambia polisi kwamba hakuwa amehusika na madawa yale ya kulevya bali alikuwa amemsaidia mzee mmoja ambaye ndiye aliyempa begi lile lililokuwa na madawa hayo.

“Atakayekuamini, nina hakika huyo atakuwa binadamu wa kwanza duniani kuwa mpumbavu,” alisema polisi mmoja huku akimwangalia Matamshi.

Kukamatwa kwa Matamshi ndiyo ilikuwa habari ya mjini, watu waliomuona akiwa mikononi mwa polisi hawakujua ni kitu gani kilikuwa kimemtokea, walimfahamu kama mtu mzuri ambaye hakuwa na uchafu wowote ule, alionekana kuwa mtu mwema kwa kuwa aliifanya kazi yake kwa ufasaha mkubwa kwa kuwahabarisha watu kila kitu kilichokuwa kikitokea nchini Tanzania.

Taarifa za kukamatwa kwake zikasambazwa, kila mtu aliyesikia alishangaa, hawakujua sababu iliyopelekea kukamatwa kwake hivyo watu kuanza kufuatilia na kugundua kwamba alikuwa amebeba mzigo wa madawa ya kulevya.

“Nini?”
“Eti alikuwa amebeba mzigo wa madawa ya kulevya!” alisema jamaa mmoja huku akionekana kushangaa.
 
SEHEMU YA 56

Walimfahamu mwanaume huyo, hakuwahi kujihusisha na biashara hiyo haramu, hawakujua nini kilitokea mpaka mwanaume huyo kubeba madawa ya kulevya na kukamatwa uwanja wa ndege.
Wengi walihisi kwamba kulikuwa na mchezo mchafu ulikuwa umechezwa, hawakujua mazingira ya mchezo huo na mtu pekee ambaye waliamini kwamba angewaambia ukweli ni Matamshi pekee ambaye alikuwa sero akilia.

Hakukuwa na mtu aliyeruhusiwa kumuona, si wafanyakazi wenzake wala familia, alishikiliwa huku akiandaliwa kupandishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kubeba madawa ya kulevya yaliyokuwa yakimkabili.

“Kazi imefanyika mkuu!” alisema Edson huku akionekana kuwa na furaha.
“Safi sana! Hicho ndicho nilichotaka kifanyike!” alisema Rais Bokasa kwa kuamini kwamba alimfunga mdomo mtu huyo na kusingekuwa na mtu yeyote ambaye angejua kile kilichokuwa kimetokea Marekani, hakujua kama habari iliandikwa hotelini na kutumwa kwa barua pepe.

*** Dk. Phillips akatoka ndani ya chumba kile, Mapoto na mkewe, Rosemary wakawa wakimwangalia kwa macho yaliyoonyesha walitaka kufahamu kile kilichokuwa kimeendelea ndani ya chumba kile.
Sura yake ilionyesha tabasamu pana, alionekana kuwa tofauti na siku nyingine, kwa muonekano huo tu ulionyesha kwamba kila kitru kilichokuwa kikiendelea ndani ya chumba kile kilikuwa salama.

“Kuna nini?” aliuliza Mapoto huku akimwangalia daktari huyo usoni.
“Mungu ametenda!”
“Imekuwaje? Amepona? Irene amepona?” aliuliza Rosemary huku akiwa amechanganyikiwa kwa furaha.
“Amefumbua macho, amepata nguvu na anazungumza,” alisema Dk. Phllips huku tabasamu lake likiendelea kuonekana usoni.

Mapoto akashindwa kuvumilia, palepale aliposimama akapiga magoti, akanyanyua mikono juu na kuanza kumshukuru Mungu.
Mwezi mzima walikuwa hospitalini hapo, alishindwa kufanya kazi zake, alikata tamaa kwa kuona kwamba huo ndiyo ungekuwa mwisho wa kumuona binti yake akiwa mzima tena lakini kwa nguvu za Mungu, hatimaye alipona na kuanza kuzungumza.

Hawakuamini kwa kusikia, waliona kwamba kulikuwa na uhitaji wa kuona kile walichoambiwa hivyo kumwambia Dk Phillips kwamba walitaka kumuona binti yao na kumsikia kwa masikio yao.
 
SEHEMU YA 57

Hilo halikuwa tatizo, wakapelekwa ndani ya chumba kile. Wakapiga hatua mpaka katika kile kitanda alicholala Irene na kuanza kumwangalia. Walichoambiwa ndicho walichokiona, binti yao alikuwa amefumbua macho, na alipowaona, aliwatambua kwamba walikuwa wazazi wake.

Rosemary akashindwa kuvumilia, akaanza kutokwa na machozi ya furaha, alijisikia nguvu mpya moyoni mwake, hakutegemea kumuona mtoto wake akirudi katika hali aliyokuwa nayo.

Hiyo ilikuwa hatua ya kwanza Irene, aliendelea kulala kitandani hapo huku akiendelea kupata nafuu kadiri siku zilivyozidi kwenda mbele. Moyo wa Mapoto ukafarijika, ukaanza kurudi katika hali yake ya kawaida, mawazo yakaisha na huo ukawa muda wa kurudi kazini kuendelea na kazi.

Alikutana na barua ile aliyotaka kuiandika kwa ajili ya kujiuzulu, hakujua ni kitu gani alitakiwa kufanya, ni kweli alitaka kufanya hivyo lakini tatizo lilikuwa moja tu, kama angejiuzulu inamaanisha kwamba angetakiwa kurudi nchini Tanzania.

Afya ya binti yake haikuwa imetengemaa, kama angerudi na kwenda kutibiwa nchini Tanzania, aliamini kwamba asingepata matibabu mazuri kama aliyokuwa akiyapata nchini Marekani, hivyo akaahirisha kwa muda zoezi lake la kujiuzulu.

“Rosemary! Nimeamua kuahirisha zoezi la kujiuzulu kwa ajili ya familia yangu,” alisema Mapoto, alikuwa akizungumza na mkewe walipokuwa nyumbani.

“Kwa nini?”
“Nimefikiria sana kuhusu matibabu! Kama tutarudi nchini Tanzania huku Irene akiwa kwenye hali hii, tunaweza kumpoteza, ni bora niendelee kubaki kama balozi kwa ajili ya Irene,” alisema Mapoto.

Wakakubaliana kwamba huo haukuwa muda wa kujiuzulu, akaachana na barua ile aliyokuwa ameiandika. Waliendelea kumuuguza Irene mpaka aliporudi shuleni na kuendelea na masomo na Rosemary kurudi nchini Tanzania.

Bado waliendelea kuwa vichwa darasani, walikuwa na akili nyingi mno, walimu hawakuisha kuwashangaa, kila siku watoto hao kwao walionekana kuwa na uwezo wa hali ya juu hali iliyowafanya Wazungu hao kushika vichwa, tena wakati mwingine walikuwa wakiumia kwa kuwa watoto waliokuwa wakiwaongoza walikuwa Waafrika na si Wazungu kama walivyotaka iwe.

Je, nini kitaendelea?
 
SEHEMU YA 58

“Ni kweli uulibeba madawa ya kulevya?” aliuliza mwanasheria wa kujitegemea wa Matamshi aliyeitwa Edwin Mwendapole.
“Hapana! Sikubeba madawa. Ningebeba vipi madawa na wakati siijui biashara hiyo? Sijui hata wateja wake ni wakina nani? Mwendapole, sikuwahi kubeba madawa,” alijitetea Matamshi.

“Sawa. Ila wanasema walikukuta na begi lenye madawa ya kulevya mikononi mwako,” alisema Mwendapole.
“Najua. Ngoja nikuhadithie ilivyokuwa,” alisema Matamshi na kisha kuanza kuhadithia.

Moyo wake ulimuuma mno, hakuamini kama safari yake ya kuelekea nchini Marekani ingemfanya kuwa katika hali hiyo. Alikuwa akilia, alihadithia huku akiwa na maumivu makali moyoni mwake, kila kitu kilibadilika, alikuwa na ndoto za kuwa mwandishi mkubwa barani Afrika lakini mwisho wa siku safari yake ya kwenda Marekani ikamfanya kuwa gerezani.

Kukamatwa kwake kwa madawa ya kulevya ikawa stori kila kona nchini Tanzania, wapo watu waliosema kwamba alipakaziwa lakini pia walikuwepo watu waliosema kwamba kweli alibeba mzigo wa madawa ya kulevya kwa kuwa mshahara wake haukuwa ukitosha.

“Hii Tanzania bwana! Hata mchungaji utakuta naye anabeba madawa, ndiyo sembushe mwandishi wa habari!” alisema jamaa mmoja.
“Umeona! Yaani hakuna kumuamini mtu kwa sasa, ukimwamini hata baba yako, kuna siku utajuta wallahi!” alisema jamaa mwingine.

Walichokifanya waandishi wa habari ni kuandika habari kuhusu Matamshi. Hawakuficha, waliandika kila kitu kilichokuwa kimetokea ndani ya ndege, iliandikwa kwa mfumo wa makala ambapo watu walipoisoma, wakahisi kulikuwa na kitu, mzee huyo alikuwa ametumwa na mtu ambaye hakufahamika.

Ilikuwaje mtu huyo apite bila kukamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa JFK? Ilikuwaje mtu huyo asionekana wakati akiingia? Ilikuwaje polisi wamtilie shaka sana Matamshi na wakati alikuwa mwandishi wa habari mkubwa tu?

Mbali na hayo, kwa nini Matamshi alipokuwa akimuita mzee yule, polisi hawakumfanya kitu mzee huyo na matokeo yake kumchukua na kumpeleka katika chumba cha uchunguzi?
 
SEHEMU YA 59

Kila swali ambalo watu walikuwa wakijiuliza, mwisho wa siku wakagundua kwamba huo ulikuwa ni mchezo uliopangwa, madawa ya kulevya yalipandikizwa kwa sababu fulani.
Uchunguzi ukaendelea kufanyika, watu walitaka kufahamu kile kilichokuwa kimetokea. Kwa kipindi hicho, suala hilo la madawa ya kulevya lilikuwa gumzo kila kona, kila mmoja alitaka kufahamu.

Gazeti la Kioo halikuishia hapo, likaandika kila kitu kilichotokea nchini Marekani kwamba Mapoto alitaka kuandika barua ya kutaka kujiuzulu lakini bahati mbaya mtoto wake alianguka na kupoteza fahamu, alishindwa kuandika kwa kuwa tu alikuwa kwenye hali ngumu ya kumuuguza mtoto wake.

Siku ambayo Matamshi alielekea hapo hospitali kumuona Mapoto, alikutana na Rais Bokasa ambaye alikuwa akimwangalia kwa jicho la chuki, na hiyo iliwezekana kuwa sababu kubwa ya kutaka kumpoteza mtu huyo kwa kuamini kwamba angesema ukweli juu ya kile kilichokuwa kikiendelea nchini Marekani.

“Huyu rais magumashi washikaji! Yeye ndiye atakuwa amehusika katika hili,” alisema jamaa mmoja huku akionekana kuwa na uhakika juu ya kile alichokuwa amekizungumza.
Hali ya hewa ikabadilika mitaani, kila mmoja akaanza kumshutumu rais kwamba alihusika katika shutuma ya usafirishaji wa madawa ya kulevya iliyokuwa ikimhusu mwandishi mashuhuri nchini, Matamshi.

Kelele zilikuwa nyingi kila kona, hata kabla mwandishi huyo hajapelekwa mahakamani tayari kukawa na tetesi kwamba wananchi walipanga kufanya fujo, kuchoma magari moto wakishinikiza mwandishi huyo aachiwe huru kwani kesi iliyokuwa ikimkabili ilikuwa imepandikizwa.

“Wananchi wanataka kuandamana na kufanya fujo,” alisema Waziri Mkuu, Bwana Donatius Marango.
“Wana nini hao wananchi?”
“Kivipi mkuu!”
“Wana bunduki?”
“Hapana.”
“Mabomu?”
“Hapana!”

“Sasa mnaogopa nini? Waambie polisi wawashambulie. Katika hili msilete kabisa mzaha, mtu yeyote akiingia mtaani kwa ajili ya kupambana, pambaneni naye, hii serikali yangu si ya masihara hata kidogo,” alisema Bokasa, alionekana kukasirika mno.

“Lakini mkuu…..”
“Marango! Unaogopa? Kama unaogopa acha niliambie jeshi liingie.”
“Hapana mkuu! Siogopi! Nitafanya hivyo! Nitawaambia polisi wafanye hivyo!”
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom