29
Walijua kusoma vizuri Kiingereza, waliweza vizuri sana somo la hesabu kiasi kwamba hata walimu wenyewe walishangaa na kubaki kujiuliza juu ya uwezo waliokuwa nao watoto hao.
“Haiwezekani! Mbona wana akili hivi?” aliuliza mwalimu Wilbert huku akionekana kushangaa.
“Hata mimi nashangaa! Wanaonekana ni hatari sana. Wana akili za kuzaliwa, haiwezekani kwa mwanafunzi kufahamu mambo kama haya, ni mapema mno lakini cha ajabu, wao wanafahamu sana,” alisema mwalimu mwingine huku uso wake ukiwa kwenye mshangao mkubwa.
Huyo ulikuwa mwezi wa kwanza, uwezo wao darasani uliendelea kujionyesha shuleni hapo na hata kipindi cha mitihani ya mwisho wa mwaka kilipofika, waliweza kushika nafasi ya kwanza kitu kilichowachanganya walimu wengi.
“Wamefaulu vizuri sana, zaidi ya wanafunzi wengine,” alisikika mwalimu mmoja, hakuamini kile alichokuwa akikiona.
“Wakina nani?”
“Wale watoto wa Kiafrika!”
“Godwin na Irene.”
“Hebu nione!”
Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa mabadiliko, shuleni, walikuwa wanafunzi hatari, hata mwaka huo ulipokatika na mwingine kuingia, bado walikuwa moto wa kuotea mbali.
Wale waliokuwa wakiwadharau watu weusi, wakaacha dharau zao kwani watoto hao wawili walizisafisha akili zao na kugundua kwamba si Wazungu peke yao waliokuwa na akili kuliko watu weusi, hata watu weusi wenyewe walikuwa na akili kuliko hao Wazungu.
“Ninaamini kwamba mnaweza kufanya vizuri zaidi ya hapa. Watoto wote mnaosoma nao, hakuna mtoto mwenye akili zaidi yenu. Hebu waonyesheeni kile ambacho Mungu amekiweka vichwani mwenu,” alisema Bwana Mapoto huku akiwaangalia watoto wake.
“Ninataka kuwa mchungaji baba,” alisema Godwin huku akimwangalia baba yake, kila siku katika maisha yake, hakukuwa na kitu chochote alichokuwa akikihitaji kama kuwa mchungaji kama alivyokuwa Reinhard Bonnke ambaye kila siku alimuona kama ‘role model’ wake.
Wakati hayo yote yakiendelea nchini Marekani, nchini Tanzania hali ilikuwa imebadilika, kila mtu alionekana kukata tamaa ya maisha, hawakuamini kama kweli huo ndiyo ungekuwa mwisho wa Bwana Mapoto ambaye aliondoka na kuelekea nchini Marekani ambapo maisha yake yote yangeendelea kuwa huko.