Waziri: Tuliwaza kurejea umeme wa Dowans
2008-09-30 11:42:21
Na Waandishi Wetu
Serikali imesema kuwa kama matatizo ya mgawo wa umeme yaliyosababishwa na kuharibika kwa mitambo mitatu ya kampuni ya Songas yangeendelea bila kupata ufumbuzi wa haraka, ingelazimika kuutumia umeme wa kampuni ya Dowans.
Akizungumza na Nipashe jijini Dar es Salaam jana, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Malima, alisema kama tatizo la mitambo ya Songas lingeendelea ingelazimika kuchukua hatua hiyo kwa vile mitambo ya Dowans haina mushkeli.
``Hivi wewe nchi iko gizani, anajitokeza Dowans anasema kuna mitambo hapa ya umeme, ungekataa? Sisi tusingekataa,``alisema Malima.
Akifafanua, Malima alisema mgogoro kati ya serikali na Dowans haukutokana na kampuni hiyo kushindwa kufua umeme au kuwa na mitambo feki, bali tatizo lilikuwa kwenye mkataba.
``Tatizo la Dowans lilikuwa ubora wa mkataba, ule ulikuwa mbaya, lakini bidhaa zake (umeme) ni safi, wala hatujagombana nao kwa vile eti mitambo yao ni mibaya, hapana.
Mitambo ya Dowans ni safi na wana uwezo wa kuzalisha vema. Wangetupa ofa tusingekataa hata kidogo,``alisema Malima.
Malima alisema watu wenye wasiwasi juu ya suala hilo ni wale wanaochanganya na wasioelewa ugomvi kati ya Serikali na Dowans ulikuwa umesimama wapi.
``Dowans si haramu, mitambo yake si haramu wala umeme wake si haramu, haramu ulikuwa mkataba,`` alisema.
Malima alisema ni ukweli usiopingika kwamba Tanzania ina uhaba mkubwa wa umeme, hivyo serikali imepanga kuchukua hatua za haraka na za kudumu kujiongezea uwezo wa kuzalisha nishati hiyo.
Alisema njia hizo ziko nyingi, lakini moja wapo ni kununua mitambo ya Dowans kama itawezekana.
Malima alisema cha msingi katika kutafuta njia za kuongeza umeme katika gridi ya taifa, serikali inaangalia mikataba yenye maslahi kwa wananchi na wala sio historia ya kampuni yoyote.
Katika hatua nyingine, Shirika la Umeme nchini (Tanesco) jana limetangaza kwisha kwa mgawo wa umeme uliodumu kwa siku tano, kutokana na mtambo mmoja kati ya mitatu ya kuzalisha umeme ya kampuni ya Sangas `kupona`.
Akizungumza na Nipashe ofisini kwake jana, Meneja Mawasiliano wa Tanesco, Badra Masoud, alisema mgawo huo ambao uliamsha hisia za watu wengi, umefikia tamati jana, baada ya kazi ya kurekebisha mitambo ya kampuni ya Songas kuanza.
Alisema wataalam wa kampuni ya Kimarekani ya General Electrical waliwasili nchini usiku wa kuamkia jana, na moja kwa moja wakaanza kazi ya kurekebisha mitambo hiyo.
Badra alisema wataalam hao (hakuwataja majina) wamefanikiwa kutengeneza mtambo mmoja wenye uwezo wa kuzalisha megawati 40.
Alisema juhudi za kutengeneza mitambo miwili iliyobaki zinaendelea na Songas wametoa taarifa kwamba kazi itakamilika mapema iwezekanavyo.
``Ninawatangazia Watanzania wote wanaopata umeme kutoka katika gridi ya taifa kwamba kuanzia leo (jana) magawo wa umeme umekwisha, umeme utapatikana kama kawaida, na kama ikitokea sehemu moja haina umeme, yatakuwa matizo ya kawaida ya kiufundi, ambayo mara nyingi huwa tunayatolea taarifa,`` alisema.
Badra alisema hivi sasa Tanesco inapata jumla ya megawati 112 kutoka Songas, kiasi ambacho kinatosha kufuta mgawo.
Vilevile, mitambo yote inayomilikiwa na Tanesco nchini kote inafanya kazi nzuri.
Alipoulizwa kuwa Songas inastahili kufanywa nini baada ya kushindwa kuiuzia umeme Tanesco na kusababisha hasara kubwa, Badra alisema kwa kawaida lazima wapigwe faini.
``Unajua tunawalipa Songas kwa kadri wanavyotupa nishati, lazima kuna adhabu tutawapa katika mahesabu yetu ya malipo, lakini hilo tutalijua baadaye, sasa hivi ni mapema mno kulijadili,`` alisema.
Katika hatua nyingine Badra alisema Tanesco imeitisha mdahalo kati yake na wadau wanaotumia umeme, ili kuwapa fursa ya kutoa madukuduku yao.
Badra alisema mdahalo huo unafanyika leo katika Ukumbi wa Karimjee, jijini Dar es Salaam kuanzia saa 8 mchana.
Alisema mdahalo huo ni sehemu ya mikakati ya Tanesco kujiimarisha na kuwapa wateja wake fursa ya kutoa kero zao.
Kwa upande wake, kampuni ya Songas imesema kuwa mtambo wake mmoja aina ya UGT6 katika ya mitatu iliyoharika wenye uwezo wa kuzalisha megawati 40 za umeme, umetengemaa na kuanza kufanya kazi kama kawaida kuanzia juzi.
Taarifa iliyotolewa jana na Msemaji wa kampuni hiyo, Reuben Mwaikinda, ilisema mtambo huo ulifanyiwa matengenezo na wahandisi wa kampuni ya General Electric kutoka Marekani kwa kushirikiana na wa Songas na kwamba ilipofika saa 12 jioni juzi ulianza kufanya kazi na umeme wake kuingizwa moja kwa moja katika gridi ya taifa.
Imeandikwa na Simon Mhina na Abdallah Bawazir.
SOURCE: Nipashe