Chifu
The Boss tatizo la msongamano wa magari Dar, kama walivyosema wadau hapa, linasababishwa na mpangilio mbovu wa mji. Dar imepangiliwa hovyo kuliko maelezo.
Baa kila mahala, showrooms za magari hata kwenye maeneo ya makazi; viwanda kuwekwa karibu na makazi; majengo marefu kujengwa yasipostahili; ofisi za serikali kuwa sehemu moja tu; njia za kuingia Kariakoo na Posta kwa watu wanaotoka eneo fulani kuwa moja tu, kwa mfano mtu anayekaa Mwenge ana route moja kubwa ya kumfikisha Posta,Ali Hassan Road, akitumia Shekilango-Morogoro road inakuwa maumivu kwake! Vilevile watu wanaokaa Gongolamboto, Segerea, Ukonga, Tabata na Vingunguti, nao njia zao za kwenda Posta na Kariakoo ni moja tu!
Vilevile hata mfumo wa incentives za usafiri kwa watumishi waandamizi wa umma ni wa kijinga. Hapa naongelea makatibu wakuu, wakurugenzi, wakuu wa vyuo na wasaidizi wao, wakuu wa idara za serikali n.k. Hawa wote wanapewa magari yao kuwapeleka ofisini na kuwarudisha majumbani kwao!! Kwa nyakati za asubuhi, hapo Dar, magari ya wakubwa hao hujaa barabarani!!!
Nini kifanyike sasa?
Kwa hali ilivyofikia sasa hivi, huwezi epuka suala la gharama katika kuja na mipango ya kuondoa msongamano wa magari hapo Dar. Hivyo basi, haya ni baadhi ya mapendekezo yangu, ambayo yataleta matokeo chanya kama yakitekelezwa sambamba:
1. Satellite towns: hii ni katika kutoa utegemezi wa wakaazi kwa mahitaji yao mbalimbali kutoka eneo moja. Mfano, Tegeta, Mbagala, Ukonga, Mbezi Juu/Kibamba na Tabata, zaweza kuendelezwa katika kiwango cha kuweka mahala pa kupata mahitaji yote ya msingi (hususani kwa yale yafuatwayo na watu wasio watumishi wa umma Posta na Kariakoo). Huduma za kibenki naona zimekuwa zikisogezwa karibu sana na hizo 'satellite towns'. Hii itaendana na kusimamisha ujenzi wa ofisi mpya za serikali na mashirika ya umma. Mfano mzuri, upo kwa TCRA; walivyoweka ofisi zao nje ya katikati mwa jiji ni vizuri sana. Hii itakuwa hivyo kama mpango wa kuhamia Dodoma utaendelea kusuasua. Ila kutekelezwa kwa mpango huo,kutakuwa ni moja ya masuluhisho makubwa ya msongamano Dar. Pia hili litaendana na kupiga marufuku ujenzi mpya wa majengo ya ofisi za mashirika binafsi katikati ya mji; majengo kwa ajili ya kuishi tu, ndiyo yanaweza kuruhusiwa.
2. Kuweka mfumo mpya wa usafiri wa umma. Katika hili mpango wa DART utakuwa ni moja ya suluhisho. Lakini hili litafanikiwa sana likienda sambamba na pendekezo la kwanza. Kuhusu hili mengi yameandikwa humu. Mfumo ukiwa mzuri, kuwepo na sheria kali juu ya matumizi na uingizaji wa magari binafsi katikati ya mji ili kudiscourage watumiaji wa magari hayo. Mfano, kuwe na ushuru mkubwa wa kuingiza gari binafsi katikati ya mji, na parking charges kuwa aghali kwa maeneo ya katikati ya mji. Hapa ni kutengeneza disincentives za mtu kutaka kuingia down town na gari binafsi na kuweka incentives kupitia mfumo mzuri wa usafiri wa umma. Hapa katika usafiri wa umma, nchi za Skandinavia zinatupa mfano bora kabisa wa mfumo mzuri wa usafiri wa umma.
3. Kuimarisha idara za mipango miji katika manispaa za Dar. Hapa jambo kubwa ni uwajibikaji wa watumishi wa idara hizi. Hawa wanapaswa kuwa makini katika kufuatilia matumizi ya ardhi na maeneo Dar. Baa kila kona ni tatizo; kwani nyingine, hazina parking, na kukuta kingo za barabara ndizo utumika kama parking! Kwa watumishi hawa, mkono wa sheria uwe wa chuma pale wanapotenda kinyume na mpangilio wa mji.
4. Ujenzi wa parking: kama alivyosema mdau mmoja humu, ukosefu wa parking spaces nao ni chanzo cha msongamano. Hii iendane na uwepo na ufuatiliaji wa sheria yenye kutaka kila jengo la ghorofa zaidi ya tano, ni sharti liwe na parking floor(s). Na ili kuleta kukubalika, mwenye jengo ndiye atakayekuwa akikusanya ushuru wa parking spaces, kwa wale watakaokua siyo wakaazi wa jengo hilo (kama ni la makazi) na watakaokua siyo watumishi (kama ni la ofisi).
5. Kubadilika kwa tabia za matumizi ya magari kwa watu binafsi na magari ya serikali. Kwa mfano, unakuta waziri wa nishati anatoka ofisini na kutaka kwenda ofisi za jiji pale, kwa ajabu ataenda kwa gari. Hii tabia pia ipo kwa watu binafsi wanaofanya kazi downtown. Ingekuwa vyema watu wakabadili tabia hizi; kwa mizunguko ya downtown, siyo lazima kuzunguka na gari. Kutembea kwa mguu kunapaswa kuwe ndiyo tabia. Ni jambo gumu, ila linawezekana kwa polepole.
Ni haya tu kwa sasa.