Kisusi Mohammed
JF-Expert Member
- Aug 10, 2009
- 563
- 471
"Kumjali mteja kama ilivyo kiingereza Customer care" ni fumbo gumu sana Tanzania, na ni kwa sababu kubwa ya kukosa weledi katika sekta ya huduma, watu wengi waajiriwa kwenye sekta ya huduma huajiriwa kwa sababu tu anajuwa kuwasha computer na ana sura nzuri na lafudhi ya wiziwizi au ana undugu na wenye kampuni au shirika, hatuendi mbali na kupima uwezo wake wa kushughulika na wateja ama jinsi gani ana haiba ya biashara katika sekta ya kutoa huduma. Mnisamehe lakini natoa mfano kwa wenzetu wakenya; wanajua kumjali mteja bila kujali anaonekanaje, amevaaje, ana kitambi au la! Hii ni kwa sababu kwamba; mojawapo ya vigezo vya kupata ajira hizo ni kuwa na uwezo wa kujali mteja bila kujali amekujaje na anaonekanaje. Upande mwingine watanzania tuna tabia mbaya sana ya kusahau tulipotoka, unakuta mtu wakati anakuja kuomba ajira hiyo alikuwa mnyenyekevu kuliko maelezo, akishaipata kila mtu anakuwa mpuuzi kwake na mbaya zaidi akishaanza kujua kupaka lipstick na kufunga tai, inakuwa mitihani sana kwa wateja, yaani anajiona kana kwamba anamiliki hisa 51% kwenye kampuni. Najiuliza kila siku na sijawahi kupata jibu: Inawezekanaje mtu wa mapokezi au katibu muhtasi awe na kiburi cha kumnyanyapaa mteja kiasi cha kumkwaza? Wakati katika uhalisia wa huduma yule anaekutana na mteja kwa mara ya kwanza ndio anatakiwa kuwa kioo cha kampuni au shirika husika kwa kuonesha picha nzuri mwanzoni. Natoa shukrani zangu kwa watoa huduma wachache ambao nimewahi kukutana nao katika maisha wanaojua maana halisi ya "Huduma kwa mteja" na kwa tabia zao hizo wamekuwa na mafanikio makubwa sana makazini kwao. Natoa wito kwa watu wote wanaotoa huduma katika sekta yoyote; kumjali mteja ni kitu pekee kitakachokupa sifa zisizoelezeka lakini hakitakugharimu chochote katika maisha yako, na malipo yake utayaona hapa hapa duniani bila kificho.