CHADEMA walikwishatamka toka mwanzo kuwa wapo tayari kushirikiana na chama chochote alimradi chama hicho kiwe ni chama cha upinzani kweli. CHADEMA isikubali kushirikiana na vyama vingine kwa msukumo wa kuwa na wabunge wengi wa upinzani bungeni bali iwe ni kwa sababu imeridhika kuwa wote nia yao kuu ni moja. Maana ni aheri kuwa wachache wenye lengo moja kuliko kuwa wengi lakini ndani ya huo uwingi ukawa na maadui wa ndani. Vyama vingine vya upinzani vinavyotaka kuingia kwenye umoja wa upinzani vipimwe kwa malengo yao, yakionekana yanawianika na ya CHADEMA, washirikishwe lakini yakionekana kutofautiana sana, basi waachwe, wakae nje ya serikali kivuli. Katika kuwapima, ni lazima waulizwe kwa nini muda wote wamekuwa maadui wa CHADEMA, na kwa nini sasa wanataka kushirikiana na CHADEMA. CHADEMA ikiwakubalia ni lazima kuwepo mwongozo uliokubalika na vyama vyote vilivyokubaliana kuingia katika umoja ili kukiwa na chama chochote kikaenda kinyume na mwongozo huo kifukuzwe kutoka serikali katika umoja.
Kutokana na mwenendo wa CUF na marafiki zake kuwa wa kutatanisha, ni vema wakawekewa masharti na vigezo maalum ili kupima dhamira yao halisi. Wakikidhi, na wote tukaridhika, kunaweza hata kufanyika makubaliano maalum ya ushirikiano kati ya CHADEMA na CUF kwa sababu hivi vyama vyote viwili adui yao mkubwa CCM amewafanyia propoganda nyingi sana za udini ambayo kuweza kuishinda ni lazima vyama hivi, kwa kutumia viongozi wenye busara wanaojua mbinu mbaya ambayo CCM inapandikiza, kuweza kuwa na ushirikiano wa kuaminika, na hiyo iwe ni pamoja na kuangalia uwezekano wa CUF kuvunja ndoa yake na CCM japo CUF Zanzibar inaweza kuendelea kuwa na Makamu wa Rais asiyewajibika kwa Rais, iwe ni hadhi tu lakini siyo katika maana ya ushirikiano na serikali, na wala asiteuliwe na Rais ili aweze kuwa huru kwa sababu hawezi kuwa na ndoa na CCM halafu na CHADEMA ambaye sasa ndiye inayeonekana mpinzani mwenye nguvu dhidi ya CCM. Haya yakishindikana, ni aheri CHADEMA waendelee pekee yao maana kwa na wapinzani wasioeleweka, faida ya kuwa nao itakuwa ni ndogo kuliko hasara inayoweza kupatikana.