Inastaajibasha kuona kuwa
Waziri Mkuu Mizengo Pinda hakutoa kauli yoyote
wakati huu ambao taifa linapita katika majaribu magumu Kama Kuuliwa
kwa RPC wa Mkoa wa Mwanza, Kuchomwa kwa makanisa huko mbagala, kupigwa
bomu kwa Katibu wa BAKWATA Arusha, Kutangazwa kwa baa la Njaa Mkoa wa
Tanga nk! Taifa linapitia wakati Mgumu na kibaya zaidi ni kuwa Serikali
imekuwa kama haina Waziri Mkuu. Amani imetoweka. Hofu katika mioyo ya
wananchi imetamalaki. Wananchi wanaishi katika wasiwasi mkubwa huku
kanisa likilia machozi! Kwa tishio kubwa kwa
amani ya nchi kama hili waziri mkuu kuwa kimya na kuonekana kama hayupo
haliwezi kunyamaziwa hata kidogo!
Msomaji mmoja kutoka Njiro, Arusha akaniandikia, alisema Umesema
kweli mwalimu mkuu wa watu, Pinda siyo kama hayupo ni hayupo kabisaa!
Mimi naona serikali yote haipo. Nchi imewashinda sasa wanyonge hatumwoni
wakumshika mkono! Pamoja na yote Edward Lowassa ndo waziri mkuu pekee
angalau alifanya kazi! Yaani haingii akilini mpaka sasa Pinda hajasema
chochote, ama ni mgonjwa wametuficha?
Rais Kikwete, Pinda lazima aliliwe hata kama mbingu zitaanguka kwasababu
alipoteuliwa kuwa waziri mkuu aliwapa matumaini makubwa wananchi ingawa
yeye mwenyewe hakujua! Wananchi walijawa na matumaini makubwa kwasababu
Mizengo Pinda wakati hila za kutafuta madaraka zilipokuwa zikifanywa na
baadhi ya viongozi waliopo madarakani hivi sasa yeye hakuwa mmoja wao!
Hivyo wananchi walidhani angekuwa na nafasi nzuri ya kuwa upande wao kwa
maana wametelekezwa! Yeye hakuwa katika
majadiliano na wafanya vurugu wa sasa! Hawamdai kitu chochote. Kama vile
haitoshi, serikali imetangaza balaa la njaa! Ukimya huu wa mtendaji
mkuu ukiendelea unadhani nini kitatokea? Siyo kwakutaka kwetu bali
tunalazimishwa kukumbuka balaa la njaa lililopita.
Tulishuhudia Waziri mkuu Edward Lowassa alivyokuwa wakihaha nchi nzima
kuhakikisha maisha ya Watanzania hayapotei kwa sababu ya njaa. Nani
asiyekumbuka ziara ya Waziri mkuu Edward Lowassa kule Same? Njaa
imeshika kasi, wananchi wanataabika kwa njaa, mkurugenzi kakaa na
mahindi ya njaa
ofisini! Eti Same yote hakukuwa na mtu mwenye uwezo wa kuyasafirisha.
Mtu huyu hakuwa na kile wadhaifu wanaita maamuzi magumu. Aliamua mahindi
yagawiwe kwa wananchi akiwepo! Wakati wakuondoka kurudi Dar es salaam
akaondoka na mkurugenzi; kazi ya mkurugenzi ikawa imeisha.
Mwangwi wake ukaenea katika masikio ya wakurugenzi wote nchi nzima! Nani
ataichezea serikali kwa kuwatesa wananchi? Kungekuwa na ukimya kama huu
kule Same wangekufa wananchi wangapi?
Lazima Waziri mkuu atokeze aseme na wananchi wanaoishi kwa wasiwasi
katika nchi yao. Atokeze awajibu Maaskofu wanaolia! Asimame akemee
ugaidi huu! Maaskofu wanahoji, Watu hawa wavamie nini ndipo hatua
zichukuliwe? Wachome nini ndipo viongozi wenye dhamana ya kulinda mali
na uhai washtuke? Wamuue nani ndipo iaminike kuwa watu hawa ni tishio
kwa usalama wa Taifa letu? Ni nini hiki wanachosema Maaskofu kuwa,
Katika mateso haya kanisa litaimarika zaidi; na katika majivu haya ya
Mbagala Tanzania mpya itazaliwa na ukombozi wa kweli utapatikana?
Labda Pinda anakuiga wewe Rais ulieahirisha safari ya kwenda nje
kutokana na kifo cha mwigizaji wa michezo huku ukitoa ubani wa milioni
kumi halafu ukaenda Oman wakati mauti yamemfika Kamanda wa Polisi wa
mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow? Au Labda ni Utamaduni wa
Serikali yote ya awamu ya nne- Serikali ya Tanzani ni Muungano wa Visiwa
Vya Zanzibar na Zimbabwe
PASCHALLY MAYEGA: KIPANDE CHA MAKALA GAZETI LA TANZANIA DAIMA
10-24-2012
TEL 0713334239