KWELI Chips ni chakula kisicho na faida kubwa kwa afya ya binadamu pia ni chanzo cha Magonjwa

Taarifa hii imethibitika kuwa ya kweli baada ya kufanya tathmini ya kina
l-intro-1689785695.jpg

Chips ni chakula kinachotengenezwa kutoka kwenye viazi. Chakula hiki kimekuwa kinahusishwa na matatizo mengi ya kiafya ikiwemo magonjwa ya moyo.

Wataalam, tusaidieni ni kipi hasa kinachofanya chips iwe mbaya kiasi cha kuhusishwa na mambo mabaya.
 
Tunachokijua
Bila shaka wewe ni miongoni mwa watu waliowahi kutumia chips kwa nyakati tofauti kwenye Maisha yako. Umaarufu wa chakula hiki unazidi kuongezeka siku hadi siku.

Katika mahojiano madogo ambayo JamiiForums imefanya kwa baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es salaam, wengi wamekiri kuwahi kutumia chakula hiki cha haraka (fast food) ambacho kwa sababu za wengi, hutumika sana ili kuokoa muda na gharama.

Kwa jiji la Dar es salaam, tathimini ya kawaida inaonesha chips hugharimu kiasi cha Tsh. 1500/= hadi Tsh. 3000/=. Hizi ni bei za kawaida unazoweza kuzipata kwenye vibanda vingi vinavyoandaa chakula hiki pendwa na adhimu kwa watu wa umri na rika zote.

Virutubisho vyake
Achilia mbali utamu wake, chips huwa pia na virutubisho vinavyofaa kwa afya ya binadamu.

Mathalani, kwa mujibu wa My Food Data, kila gramu 100 za chips zilizokaangwa kwa kutumia viazi ulaya huwa na mjumuiko wa viambato vifuatavyo;

Virutubisho
Kiasi
Mafuta​
Gramu 34​
Sodium​
Miligramu 527​
Wanga​
Gramu 53.8​
Nyuzi lishe​
Gramu 3.1​
Sukari​
Gramu 0.33​
Protini​
Gramu 6.4​
Vitamini C​
Miligramu 21.6​
Madini chuma​
Miligramu 1.3​
Nishati​
Calories 532​

Hata hivyo, ni muhimu kufahamu kuwa vingi au uchache wa viazi hivi huathiriwa na mambo mengi ikiwemo sehemu vilipolimwa, aina ya mafuta yanayotumika kuvikaangia, muda wa kukaanga n.k

Faida za Chips
Kama ilivyofafanuliwa hapo juu, chips huwa na virutubisho muhimu vinavyofaa kwa mwili. Achilia mbali faida yake ya kuupa mwili nishati, husaidia kuongeza madini na vitamini zinazofaa kwa afya bora.

Aidha, chips ni chakula kisicho na Gluten, aina fulani ya protini yenye tabia zinazofanana na gundi ambayo kwa baadhi ya watu huwa sio nzuri kwao kwa kusababisha mzio (Allergy).

Pamoja na uwepo wa faida hizi, chips hutajwa kuwa chanzo cha madhara mengi kwenye afya ya binadamu ikiwemo upungufu wa nguvu za kiume, kusababisha upofu, kuongeza uzito wa mwili (kiribatumbo), magonjwa ya moyo na saratani.

TFNC wazungumza
JamiiForums imezungumza na Glory Benjamin, Mtafiti na Afisa lishe kutoka Taasisi ya Chakula na lishe Tanzania (TFNC) aliyefafanua kuwa shida sio viazi bali ni utaratibu unaotumika kuandaa chakula hiki.

Viazi vinavyopitishwa kwenye mafuta yenye moto mkali huharibu vitamini muhimu kwa afya, pia hufyonza mafuta na kumfanya mlaji atumie kiasi kikubwa cha mafuta na athari zake kwa baadae ni kama vile kuongezeka uzito, kuganda kwenye mishipa ya damu na kusababisha shinikizo la juu la damu.

"Kiazi chenyewe kina kirutubisho kikubwa kinachoitwa sukari. Kwa hiyo hizo na zenyewe sio mbaya sababu zinaupatia mwili nguvu lakini inapozidi inaleta changamoto kwa kuwa kiasi cha ziada hubadilishwa kuwa mafuta na kutunzwa mwilini" amefafanua Glory.

Aidha, chips sio nzuri kwa watu wote, sio wanaume pekee. Chips huwa na virutubisho vingi vilivyo haribika ambavyo huwa havina faida kwa binadamu.

Kwa watu waliotumia chips kwa muda mrefu, Glory anashauri kutumia mlo kamili wenye kiasi kidogo cha wanga, mboga mboga, kupunguza matumizi ya chips na kutumia vyakula vingi vya asili.

Maelezo ya kitafiti
Machi 9, 2009, Jarida la Kitabibu la The American Journal of Clinical Nutrition lilichapisha utafiti unaotoa rejea muhimu inayofafanua chanzo pekee cha madhara yanayoweza kuambatana na ulaji wa chips.

Utafiti huo wa Naruszewucz et al. unaweka bayana kuwa vyakula vyenye kundi huru la kemikali za amino acids zinazoitwa Asparagine zikiungana na sukari wakati wa kuunguza (kukaanga/kuchoma) vyakula husika kwenye joto kali hutengeneza kemikali inayoitwa Acrylamide na chips ni miongoni mwa vyakula vyenye sifa na uwezo wa kutengeneza kemikali hii.

Vyakula vingine vinavyoweza kuzalisha kemikali hii ni mazao ya nafaka na kahawa.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Vyakula na Dawa (FDA), kemikali hii haizalishwi kiasili kutoka kwenye mazingira, bali hutokana na mwingiliano wa kikemikali wakati wa kukaanga au kuchoma kwa baadhi ya vyakula (Viazi vikiwemo) kwenye joto kali.

Mbali na ulaji wa vyakula (ikiwemo chips), mtu anaweza pia kuingiza mwilini kemikali hii kupitia uvutaji wa sigara.

Kwa mujibu wa Taasisi ya Udhibiti na Kinga ya Magonjwa (CDC), kemikali za Acrylamide huwa hazipatikani kwa kiwango kikubwa kinachoweza kuleta madhara hasi kwenye afya ya binadamu. Hata vyakula vinavyoizalisha (kama vile chips) huwa pia na kiwango kidogo sana ambacho mara nyingi huwa ni himilivu kwa mwili.

Lakini, kwa watu wanaotumia kiwango kikubwa cha kemikali hii huwafanya wapatwe na uchovu wa misuli, kuchoma choma kwa mikono na miguu Pamoja na kupunguza uwezo kwa viumbe vyenye jinsia ya kiume katika kurutubisha yai na kutungisha ujauzito.

Pia, tabia za mhusika na mtindo wake wa maisha huchangia ukubwa wa madhara.

Aidha, kemikali hii imekuwa chanzo cha aina mbalimbali za saratani kwa Wanyama waliofanyiwa majaribio kwenye maabara. Hata hivyo, hakuna uthibitisho wa moja kwa moja kuwa inaweza kusababisha saratani kwa binadamu.

Madhara mengine yanayotajwa kusababishwa na uwepo wa kemikali za Acrylamide ni kuongeza hatari ya kuugua magonjwa ya moyo na mfumo wa damu kama vile shinikizo kubwa la damu na kuziba au kupungua ukubwa kwa mishipa ya damu.

Ushauri
Ni muhimu kuhakikisha chips zimekaangwa na kukaushwa vizuri ili kuepuka ulaji wa mafuta yanayoweza kuwa chanzo cha magonjwa hasa yale yasiyoambukiza.

Pia, kama ilivyo kwa kila kitu, kula kwa kiasi. Mara nyingi madhara ya vyakula na madawa hutokea kwa watu wanaotumia kwa kiasi kikubwa kuliko kile kinachoweza kuvumiliwa na mwili.

Similar Discussions

0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom