SoC03 Chawa wa nafsi yangu

Stories of Change - 2023 Competition

ChrisantD44

New Member
May 31, 2023
1
4
“Zungu la wazungu nyayo zako uvungu wangu, usikanyage vumbi baba simama begani kwangu kichwa kiguse mawingu, baba hauna baya, baba ukifa hauozi, mbinguni njia yako ni ya lami na dhambi zako nachukua mimi, hata ukimtaka mke wang…..” Ayaa”,ninalalama kwa sauti nikiusoma ujumbe unaonitaarifu juu ya kifurushi kuisha. Licha ya kuwa tayari kumepambazuka, ninaamka kwa shingo upande nikijivuta huku nikitawaliwa na uchu wa kuimalizia video ile ya msifiaji mashuhuri almaarufu kama chawa akimwaga sifa huku akiokota noti zinazodondoshwa na bwanyenye msifiwaji mwenye ukwasi wa kuvuja.

Baada ya kujiandaa, ninashika njia kuelekea zahanati ya kijiji ninakofanyia kazi ya uuguzi. Nikiwa mita kadhaa kabla ya kufika, ninakutana na rafiki yangu wa kilabuni aitwae Zebedayo almaarufu kama Zebe mitungi ambae ananichangamkia kisha,

“Malaika katika mwili, mponyaji wa waponyaji. Unajua wewe kijiji kizima tunakukubali kwani unatuponyea watoto na wake zetu. Yaani bila wewe tungekuwa tunakufa kama nzige, Mungu akuweke baba” Zebe ananimwagia sifa na kunifanya nitabasamu huku moyo wangu ukifarijika.

Ndio, ninafarijika sana kwani maneno ya Zebe yanakinzana na malalamiko ambayo mimi na muuguzi mwenzangu bi Shadia tunapewa na wanakijiji juu ya utendaji kazi wetu. Lakini pia yanakinzana na onyo tulilopewa na mganga mkuu wa wilaya juu ya tabia ya uvivu na kutowajali wagonjwa ikiwa ni pamoja na kuchelewa kazini.

Kwa mbwembwe, ninampa Zebe shilingi elfu moja ambae anatoka mbio akiishika njia ielekeayo gulioni upande wa vilabuni kisha mimi ninaendelea na safari nikidunda kwa madaha.

Zahanati, ninawapita wagonjwa wengi waliowahi tangu alfajiri bila kuwasalimu na kuelekea kwenye ofisi yangu ambako ninamkuta bi Shadia akitazama video za ucheshi mtandaoni huku akiangua vicheko mfurulizo.

“Kawasikilize watu wako. Zamu yako leo” ninamwambia Shadia nikimkumbusha.

Ndio, ninamkumbusha kwani tumekuwa na utaratibu wa kupeana zamu. Yaani kama leo ni zamu yako basi utawahudumia wagonjwa peke yako huku mwenzio akiwa amekula kishoka na akijisikia anaweza kuondoka muda wowote.

Kwa shingo upande, Shadia anaweka simu kitini na kwenda mapokezi kutoa huduma huku mimi nikiketi na kutundika miguu juu ya meza kisha ninaunga kifurushi kingine na kuendelea kutazama video nizipendazo. Naam, ni zile za matajiri na watu mashuhuri wakimwagiwa sifa huku wao wakimwaga pesa.

“Duh, one day yes” Ninasema kwa sauti huku bi Shadia akiangua kicheko kwa mara ya kwanza tangu aanze kujibizana na kuwakaripia wagonjwa.

Majira ya alasiri, ninaondoka zangu nikielekea gulioni kunako vilabu ili nikaumwagilie moyo kama kawaida lakini mkusanyiko wa watu uwanjani kwenye mkutano wa kampeni wa diwani anaegombea kwa muhula wa tatu unaniteka huku maneno ya mpambe wake yakinivuta mkutanoni.

“Tulikuwa na muuguzi mmoja tu kwenye zahanati yetu. Mheshimiwa diwani amepambana tukaletewa kijana mwingine mzuri na mchapakazi na sasa wako wawili. Wanashirikiana vizuri na sasa tatizo la watu kusongamana na kukosa huduma limepungua sana. Jamani uongo kweli?” mpambe anasema huku sauti chache tu zisizoakisi wingi wa watu zikiitikia.

Zaidi ya mwitikio hafifu, kuna kitu kinamshangaza mpambe na wenzie walioko jukwaani. Ni jinsi watu wanavyogeuka nyuma na kunong’ona. Nikiungana na washangaaji, na mimi ninageuka nyuma nisikione cha ajabu na ndipo ninashtuka baada ya kugundua kuwa kumbe wapiga kura wale wenye sura chungu zinazotiririsha jasho la hasira wananitazama mimi.

“Jamani kuna nini? Geukieni huku tumsikilize mheshimiwa diwani sasa” mpambe anapaza sauti kwa msisitizo usiozaa matunda kwani wanakijiji wale wangali wamenitazama huku baadhi wakininyooshea vidole waziwazi.

“Dj, weka mziki tuchangamke kidogo” mpambe anatoa agizo na mara mziki unawekwa. Hii ndio inakuwa afadhali yangu kwani wanakijiji wanalipuka kwa shangwe na kuanza kuserebuka wasiniangalie tena.

Haraka huku nikigubikwa na hofu na majuto ya kujipeleka mkutanoni, ninaondoka mpaka kilabuni ambako ninapokelewa kwa shangwe na walionitangulia huku mama Kajoro ambae ndie mmiliki na muuzaji akinichangamkia na kunipimia bombonya lililojaa pombe kisha,

“Upe mwili pole dokta, kazi ya kutibu watu asubuhi mpaka jioni ni kubwa, piga hilo bombonya la pole kisha nikuletee jingine la pongezi kwa kazi yako kubwa. Hauna baya baba yangu, wewe ndo mponyaji wetu. Pigeni kelele kwa doktaaaaa” mama Kajoro anasema na kuanzisha shangwe huku wanywaji wote wakiitikia kwa sauti ya juu, wengine wakinifuata na kunipa mkono na wengine wakiniinua kucheza muziki lakini mimi ninagangamala na kuendelea kuketi.

Nisiizuie hali ya kutokuwa na furaha, ninapiga funda moja la pombe ambayo kinyume na siku zote, inapita kooni kwa tabu mpaka kufika tumboni. Ninapiga la pili ambalo linakutana na ukinzani zaidi kooni na kurudi kinywani na mimi bila hiana, ninalitema pembeni bila kuangalia kama kuna mtu ameketi.

“Ayaaaaaa, unanitemea pombe mimi? Ee, unatudharau sisi kwa kuwa wewe ni mganga? Halafu nilikuwa ninakuwinda muda mrefu mshenzi sana wewe. Mke wangu alikuja ukawa haumjali kidogo afe. Halafu mwisho wa mwezi unapokea mshahara. Shetani mkubwa wewe. Nakuonesha leo pumbafu” Ni sauti ya Zebe Mitungi akilalama huku akinisogelea.

Zaidi ya kuogopa, ninajikuta nikipigwa na butwaa nikishangazwa na maneno ya Zebe kwani hayaendani na sifa kedekede alizonimwagia asubuhi nikampatia buku ya pombe. Nikijiandaa kumuomba radhi, ananivamia kama radi na kunishushia ngumi mfurulizo usoni kabla hajadhibitiwa na kutolewa kilabuni.

Nikiwa na maumivu ya nje na ndani, ninakodi bodaboda na kuelekea nyumbani ambako ninajikanda kwa maji moto kwenye uvimbe kisha ninajilaza.

Kitandani, ninaingia katika tafakuri nzito nikiyawaza masaibu yaliyonikuta leo ambayo kwa hakika yamenifunulia uhalisia ambao sikuwa nimeung’amua hapo awali. Ni uhalisia tofauti na sifa kemkem ninazomwagiwa na watu mbalimbali mtaani hasa wale wanaoneemeka na vijisenti vyangu niwapavyo. Ninatafakari jinsi ulevi na kitendo cha kumtemea pombe Zebe kilivyomfanya ayatoe ya moyoni katika uhalisia wake huku akinishushia mvua ya makonde, jinsi mpambe yule alivyompamba mheshimiwa diwani kwa sifa zisizo halisi zinazonihusu kiasi cha kunifanya nitazamwe vibaya na wale watu pale mkutanoni na jinsi mama Kajoro anavyonisifiaga kila siku ili niendelee kununua ulabu na kuwazungushia wanywaji wengine kiasi cha kunifanya nipawaze kilabuni muda wote niwapo kazini.

Kwa msukumo nisiowahi kuuhisi, ninajiapiza kuwakwepa wasifiaji huku nikijiuliza moyo wangu ulio kipenzi cha sifa na ujiko utakuwa ukisuuzwa na nini? Baada ya kuwaza sana hatimae ninapata jawabu. Mimi mwenyewe nitakuwa chawa wa nafsi yangu na nitajihimiza kuyafanya yale yenye mchango chanya katika jamii.

“Wewe ni muuguzi mchapa kazi, mwenye upendo, muwajibikaji na asie mchelewaji, serikali na wanakijiji wanakutegemea” Ninajiambia na mara ninapata nguvu ya ajabu na kuondoka haraka kurudi zahanati.

Kule ninaanza kutoa huduma kwa moyo huku bi Shadia na wagonjwa waliosalia wakinishangaa wasiamini.
 
Back
Top Bottom