sir.JAPHET
JF-Expert Member
- May 18, 2012
- 699
- 133
Alhamisi, Agosti 30, 2012 | Imeandikwa na Arodia Peter | Mtanzania
*Yalia polisi kuiruhusu CCM Lindi kuandamana
*Yaikataa tume ya kuchunguza mauaji Morogoro
WAKATI Jeshi la Polisi nchini, likisitisha mikutano na maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimeonekana wazi kuweweseka, baada ya wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoani Lindi kuandamana jana.
Habari kutoka mkoani Lindi, zinasema wafuasi wa CCM waliandamana wakati wakimsindikiza mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Wilaya wa chama hicho, Muhsin Rafi Ismail.
Kutokana na hali hiyo, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, aliitisha mkutano wa waandishi wa habari mjini Dar es Salaam jana na kusema maandamano hayo yameonekana wazi kukiuka maagizo ya Jeshi la Polisi.
"Tumeshangazwa sana na wenzetu wa CCM kufanya maandamano ya kumsindikiza mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Wilaya… kama tunavyokumbuka juzi polisi wamezuia vyama vyote kufanya mikutano hadi zoezi la Sensa ya Watu na Makazi litakapomalizika, jamani mbona hatutendawi haki.
"Ukiacha maandamano hayo, tunashangaa kuona Tume ya Kukusanya Maoni ya Katiba mpya, inaendelea na mikutano yake katika mikoa mbalimbali… je, suala hili haliingilii Sensa?" Alihoji Mnyika.
"Hapa hatuoni polisi wakiwazuia kwa kuwa Sensa inaendelea, zuio hilo linajitokeza wakati Chadema inapotaka kufanya shughuli zake za kisiasa kwa mujibu wa Katiba," alisema Mnyika.
Alisema wao kama chama, wanaheshimu mazungumzo na utawala wa sheria, ndiyo maana wameamua kuheshimu wito wa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Said Mwema, wa kusitisha mikutano na maandamano yao ili kupisha Sensa ikamilike.
Hata hivyo, alisema wanalitaka Jeshi la Polisi kutoa tamko ili umma ufahamu ni shughuli gani za kisiasa zinapaswa kuendelea ili kuepuka vikwazo.
MTANZANIA ilipomtafuta mgombea wa CCM Wilaya ya Lindi, Ismail kupata ukweli, alisema: "Ni kweli tumeandamana na wafuasi wangu wakati wa kurudisha fomu…sisi tunaona ni jambo la kawaida, hao wanaobeza wana lao jambo.
"Ni kweli maandamano yalifanyika, kimsingi ni marafiki zangu wameamua kunisindikiza, walikuwepo watembea kwa miguu, baiskeli, pikipiki na bajaji.
"Maandamano yalianzia nyumbani kwangu, Mtaa wa Uhuru, yakapita Soko Kuu, stendi ya mabasi kuelekea ofisi za chama eneo la Wailes," alisema Ismail.
Wakati huo huo, Mnyika alisema chama hicho kimeikataa tume iliyoundwa na Jeshi la Polisi kuchunguza kifo cha kijana Ally Zona, kilichotokea wakati wa kuzima maandamano yake mjini Morogoro.
Alisema, chama hicho kimefikia uamuzi wa kuikataa tume hiyo, kwa sababu tume nyingi ambazo zimeundwa na jeshi hilo, hazijawahi kutoa ripoti hadharani.
"Kama jeshi hili limeweza kumpotosha Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emanuel Nchimbi, kuhusu sababu za wao kuzuia maandamano yetu, watashindwaje kuhujumu uchunguzi huo?
"Tunatoa taarifa rasmi, tunapinga na hatuitambui timu iliyoundwa na Jeshi la Polisi kuchunguza kifo hicho, kwa kuwa pia wao ni watuhumiwa wa mauaji hayo.
"Kifo hiki kinapaswa kuchunguzwa na tume huru na siyo polisi ambao ni watuhumiwa wakuu wa suala hili," alisema Mnyika.
Aidha katika hatua nyingine, Chadema kimemwomba Rais Kikwete kutumia madaraka yake ya kikatiba, kutekeleza sheria (Enquest Act), Ibara ya 33 (3), kuunda tume huru ya kuchunguza kifo chochote chenye utata.