Ujumbe wa Prof Anna Tibaijuka
MAWAKILI WA CHADEMA WAKIWASILI DODOMA KUTETEA CHAMA CHAO: Ni haki kwa mlalamikaji yeyote kutafuta haki yake mahakamani ila historia inaonesha matumizi ya mifumo ya mahakama kutatua migogoro ya vyama vya siasa hayajaonesha mafanikio ya kudumu barani Afrika. Mfano mashuhuri ni ANC iliyopigwa marufuku mwaka 1960 na Makaburu, ikalazimika kufanya shughuli zake kwa siri, takriban miaka 32 viongozi wake wakifungwa au kukaa uhamishoni.
Matokeo ANC ikajijengea uhalali mkubwa ndani na nje ya nchi na hatimaye, Mfumo wa ubaguzi ulipoanguka, ANC iliibuka ikiwa na nguvu zaidi na kushinda uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia mwaka 1994 chini ya uongozi wa Nelson Mandela. Jaribio la kukiondoa chama hicho kupitia sheria liliishia kukiimarisha.
Pili ni Senegal, chama cha PASTEF kilipigwa marufuku mwaka 2023. Hatua hiyo ilichochea hisia za wananchi dhidi ya kile kilichoonekana kama ukandamizaji wa kisiasa, na mwaka mmoja tu baadaye, 2024, viongozi wanaohusishwa na chama hicho walishinda urais. Tukio hili linaonyesha jinsi hatua za kisheria zinavyoweza kubadili chama cha upinzani kuwa alama ya mapambano ya kisiasa.
Tatu, Gambia, wakati wa utawala wa Yahya Jammeh, vyama vya upinzani vilikumbana na vizuizi vikali, ikiwa ni pamoja na kupigwa marufuku. Hata hivyo, vyama hivyo vilijipanga upya, vikaungana, na hatimaye kushinda uchaguzi wa mwaka 2016. Hivyo basi, ukandamizaji haukuondoa nguvu zao bali uliwafanya wawe na mshikamano zaidi.
Tanzania tunatambuliwa kuvisaidia vyama vya ukombozi wa Afrika hadi uhuru wao, huku vikiwa vimepigwa marufuku na tawala za kikoloni ikiwemo: ZANU-PF ya Zimbabwe, MPLA ya Angola, na FRELIMO ya Msumbiji.
Matumizi ya mahakama katika ushindani wa kisiasa hakulipi. USHAURI WANGU TUJISAHIHISHE NDANI NA NJE YA VYAMA VYETU kushindania uongozi bora hasa wakati huu tunapohitaji MARIDHIANO na MSHIKAMANO ili kulileta taifa letu Pamoja.