Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAZECHA) Mkoa wa Mbeya, David Mwambigija, ametoa wito mzito kwa askari wa jeshi la polisi nchini kutojihusisha na matukio ya utekaji wa raia, akisisitiza kuwa wanapaswa kulinda haki badala ya kutekeleza maagizo haramu.
Mwambigija ametoa kauli hiyo jana, Juni 13, 2026, alipokuwa akihutubia mkutano mkubwa wa hadhara wa CHADEMA uliofanyika katika Viwanja vya Mwembetogwa mkoani Iringa, uliolenga pia kumkaribisha aliyekuwa Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, kurejea kikamilifu kwenye mapambano ya chama hicho.
Mwanasiasa huyo amewaasa askari hao ambao amewataja kama watoto wa wakulima, kuwa na hofu ya Mungu wanapoamriwa kutekeleza matukio yanayohatarisha usalama wa raia, akitolea mfano matukio ya utekaji yanayoripotiwa nchini.
"Ndugu zangu maaskari sikiliza, nyie watoto wa wakulima wadogo zetu, hivi mnapoambiwa maelezo ya juu kwani lazima ufanikishe dili? Ukimpigia simu kwamba nakuja, sogea mbele kidogo... kwani ukisema hili nimefeli shida iko wapi? Kazi kujipendekeza tu," amesema Mwambigija.
Akizungumzia kuhama na kurejea kwa viongozi ndani ya chama hicho, Mwambigija amesema kuwa CHADEMA ni taasisi imara ambayo haitikiswi na kuhama kwa mtu mmoja, akitolea mfano wanasiasa wakubwa waliowahi kuondoka na kurudi kama Edward Lowassa na Frederick Sumaye, huku akibainisha kuwa kuondoka kwa Msigwa huko nyuma kuliisaidia CHADEMA kujenga safu mpya imara.
Kuhusu afya na hali ya kisiasa ya Makamu Mwenyekiti Tundu Lissu, mzee huyo amewashangaza wanasheria wa Serikali na CCM wanaohangaika kumgandamiza kisheria, akieleza kuwa Lissu alinusurika kifo kwa miujiza mikubwa baada ya kupigwa risasi zaidi ya 16 mkoani Dodoma na kwamba amebaki kuwa nguzo imara ya chama hicho inayowaumiza kichwa watawala.
https://www.facebook.com/
View: https://www.facebook.com/share/v/1MgHcfLcsp/