[h=2][/h] Jumatatu, Agosti 27, 2012 06:35 Na Bakari Kimwanga, Dar es Salaam
*Ni baada ya kusema CHADEMA inafadhiliwa mabilioni
CHAMA Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kitamburuza mahakamani, Katibu wa Halmashauri Kuu, Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Jana, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, alisema Nape atafikishwa mahakamani baada ya kukituhumu chama hicho kuwa, kinapokea mabilioni ya fedha za misaada kutoka kwa wafadhili wa nje ya nchi.
Agosti 12, mwaka huu, Nape alisema sisi CHADEMA tunapokea misaada ya fedha kutoka kwa wafadhili walioko nje ya nchi.
Kutokana na kauli yake hiyo ambayo ilitangazwa na vyombo mbalimbali vya habari, tunaamini Nape ana ushahidi wa kutosha juu ya hilo.
Kwa hali hiyo, bodi ya udhamini ya Chadema, imetutaka kufanya kikao na kutoa maagizo kwa wanasheria wetu kuanza mchakato wa kumshtaki Nape.
Katika kutekeleza jambo hili, Agosti 24, wanasheria wetu wamemwandikia barua Nape na kumtaka kuomba radhi ndani ya siku 7, kwa uzito ule ule kupitia vyombo vya habari sambamba na kulipa fidia ya Sh bilioni 3 kutokana na kusema uongo.
Kauli yake hii ya propaganda chafu za kuikashifu na kuifitisha CHADEMA kwa umma wa Watanzania, ikiwamo kuzusha kuwa upo uwezekano wa chama chetu kupewa fedha hizo kwa mikataba yenye masharti ya kuiweka nchi rehani, tutataka athibitishe.
Eti Nape, alisema CHADEMA inawalaghai wananchi, sisi tuna viongozi wasio waaminifu na kwamba tuko tayari kuuza nchi kwa uroho wa madaraka, sisi tunasema kamwe hili hatuwezi kumvumilia kwa uongo wake huu.
Kipaumbele cha CHADEMA katika suala hili ni kuombwa radhi ingawa pia kiwango cha fidia ya fedha tunachokitaka kitakuwa ni fundisho kuwa uzushi na uongo unaolenga kuchafua watu bila sababu za msingi, alisema Mnyika.
Mkurugenzi huyo wa Habari, alisema kuwa, baada ya kutolewa kauli hiyo na Msemaji huyo wa CCM, alimtaka Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, kuwaeleza Watanzania iwapo propaganda hizo chafu zina baraka zake lakini hakufanya hivyo.
Ukimya wa Mwenyekiti wa CCM Taifa, unamaanisha kwamba, Nape hakutumwa na chama chake kutoa matamshi aliyoyatoa bali alifanya hivyo kwa matakwa yake.
Kwa maana hiyo, Chadema inachukua fursa hii kuutaarifu umma, kwamba Nape asipotekeleza maagizo hayo ndani ya siku saba kuanzia tarehe hiyo aliyopokea barua, hatua zingine ya kumfikisha mahakamani zitaanza, alisema Mnyika.
Pamoja na kudhamiria kuchukua hatua za kisheria, alisema CHADEMA inaendelea kusisitiza kwamba, ni chama imara, kitaleta uongozi bora, kina sera imara na hakuna sababu ya kukihofia.
Nape alipotakiwa kuzungumzia kauli hizo za CHADEMA, alisema atazitolea ufafanuzi leo.
Ndugu yangu naomba uniache, hayo madai ya CHADEMA nitayatolea ufafanuzi mzuri kesho (leo), katika mkutano ambao nitafanya na waandishi wa habari, alisema Nape kwa kifupi.
[h=4]Toa Maoni yako kwa habari hii[/h]