kevylameck

Member
Nov 3, 2013
18
19
0EFDE22E-FB6F-43A7-8F04-19750F2D3F01.jpeg

Na Kevin Lameck

Tanzania itaingia katika chaguzi mbili muhimu kwa mustakabali wa maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla. Ni uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2024 na uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Kwa mara ya kwanza tutamshuhudia Samia Suluhu Hassan akipambana kwenye majukwaa ya kampeni ili kuweza kuchaguliwa kwa mara ya kwanza kama mgombea kamili wa nafasi ya Urais.

Bahati njema kwake ni kwamba kupitia uongozi alioachiwa na hayati Dr John Magufuli zipo turufu kadhaa zitakazokuwa upande wake kutokana na kazi kubwa anayoifanya katika kuendeleza yaliyoachwa na John Magufuli sambamba na mengi mapya aliyoyaanzisha tangu alipochukuwa kijiti cha urais 2021.

Tofauti na chaguzi mbili za nyuma, wakati huu huenda Samia akakutana na ushindani mkubwa kutokana na maamuzi yake ya kutengeneza mizania sawa katika siasa na kuruhusu tena uhuru wa kufanya siasa, kutengeneza mazingira sawia katika ulingo wa siasa na kuruhusu mikutano ya hadhara.

Bahati mbaya pia ushawishi wa Samia unaonekana kushuka kwa asilimia kubwa kulinganisha na wakati ule alipoichukua nchi.Hii inatoka na maamuzi kadhaa yanayochukuliwa na serikali yake.

Jinsia yake pia ni miongoni mwa mambo yanayoendelea kumpunguzia nguvu na sauti miongoni mwa wana jamii wengi na hata wanasiasa wenzake ndani na nje ya Chama anachokiongoza kutokana na mfumo dume uliokuwa umekita mizizi mirefu.

Mbaya zaidi ni kuwa mazuri yanayofanywa na Samia na serikali yake nayo hayapati muda wa kutosha kwenye majukwaa mbalimbali, kwenye vyombo vya habari na kwenye mitandao ya kijamii kama ilivyokuwa kwa Magufuli na serikali yake.

Kwa kulitambua suala hilo ndani ya chama chake pia zipo jitihada mbalimbali zinazofanyika hasa katika kuujuza umma kuhusu masuala kadhaa na maamuzi mbalimbali yanayochukuliwa na serikali kama ilivyokuwa kwenye mkataba 'tata' kuhusu Tanzania na DP World.

Ni muhimu zaidi pia kuendelea kuyasema na kuyatangaza mazuri mengi yanayofanywa na serikali ili kuweza kufahamu jitihada mbalimbali zinazotekelezwa na serikali ya Samia katika kuuleta umma pamoja na kutengeneza mazingira mazuri ya ushindi 2025.

Mengi hayafahamiki kumuhusu Samia na 'labda' ndicho pia kilichosababisha mabadiliko madogo ya siku kadhaa zilizopita kwa kumteua Mkurugenzi mpya wa idara ya Habari - MAELEZO na msemaji mkuu wa serikali.

Kupitia changamoto iliyopo, naamini mtu mwingine sahihi kwa Samia anayeweza kuwa mbele katika kumsaidia ni Mwanasiasa na Mkuu wa mkoa wa Dar Es salaam Bwana Albert Chalamila.

Albert ana sifa zote muhimu za kuwa Katibu wa Itikadi na uenezi wa Chama Cha mapinduzi - CCM. Chalamila kwangu ni chaguo na pendekezo namba moja akiwazidi wanasiasa wengi tulionao sasa ndani ya chama tawala.

Taaluma yake na ushawishi mkubwa alionao sambamba na mahaba makubwa waliyonayo wanahabari wengi na vyombo vingi vya habari kwake kutokana na kuamini kuwa ni mtengeneza habari mzuri (newsmaker), Chalamila ni kiungo muhimu kwa ushindi wa Samia na CCM.

Karama yake kubwa ya kukubalika haraka, uwezo wake mkubwa katika kuzungumza kwenye majukwaa mbalimbali na ushawishi mkubwa aliouonesha kwenye miaka yake michache ya sisi kumfahamu kisiasa na kiuongozi, kunaweza kuwa na tija zaidi kwa CCM kuliko nafasi anayoitumikia kwa sasa.

Nimemfahamu tangu wakati huo akigombea ubunge Mufindi kabla ya kuwa meneja wa kampeni za mbunge wa sasa wa Mafinga Cosato Chumi na baadae kuwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa. Ana upekee ambao ni adimu kwa wanasiasa wengi wa umri wake.

Nayasema haya kwasababu Idara ya Itikadi na Uenezi ndani ya CCM ni kitengo nyeti na muhimu
na ni msingi wa chama hicho kuendelea kushikilia dola kwa miaka mingi ijayo ama lah!.

Miongoni mwa kazi za idara hiyo muhimu ni kushughulikia na kueneza masuala ya itikadi na Sera za Chama Cha Mapinduzi, kupanga na kusimamia mafunzo na maandalizi ya makada na wanachama na kusimamia vyombo vya habari ya Chama, mawasiliano na uhamasishaji wa umma.

Idara hii pia inawajibika kuongoza na kusimamia maandalizi ya sera, programu na ilani za uchaguzi za CCM pamoja na kusimamia utafiti, maktaba na nyaraka za Chama.

Makada kadhaa waliowahi kushika nafasi hiyo ni pamoja na Kingunge Ngombale Mwiru na Moses Nnauye.

Wamo pia Omar Ramadhan Mapuri, John Mgeja, Jackson Msome na John Chiligati pamoja na Humphrey Polepole, Shaka Hamdu Shaka na Mwanamama pekee anayeongoza mpaka sasa Sophia Mjema.

Kutokana na unyeti wa idara hiyo, CCM kwa miaka mingi huwa inaweka mtu makini anayeweza kusimamia na kupiga propaganda.

Kupitia majukumu hayo na unyeti wa idara hii naamini Chalamila ni mtu sahihi wa kueneza si tu itikadi za chama, bali pia kuyastawisha malengo na falsafa za Chama na kuijenga picha nzuri ya Chama kwa jamii.

Wasalaam!
 
Samia hana ushawishi wowote kuongea tu nje ya hotuba alizoandikiwa kunampa tabu

Huo ushawishi unaousema ni upi.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom