Boti ya Seagull ifanyayo safari zake kati ya Dar es Salaam na Zanzibar ikiwa imegonga Jahazi lililokuwa likitokea ng`ambo ya pili kwa upande wa Kigamboni.
Mabaharia kumi waliokuwa kwenye jahazi lijulikanalo kama Asilojua wamenusurika kufa baada ya kugongwa na boti ya abiria ya Seagull na kuzama eneo la Feri, jijini Dar es Salaam.
Akisimulia tukio hilo, nahodha wa jahazi hilo, Musa Machano (35), alisema kuwa, ajali hiyo ilitokea jana saa 6:00 mchana wakati wakitokea Visiwani Zanzibar kuja Dar es Salaam.
Alisema boti hiyo ilikuwa ikitokea Dar es Salaam kuelekea Zanzibar.
Aliwataja mabaharia walionusurikia kuwa ni Nassor Mohamed (18), Hamis Shauri (20), Hamis Makame, Faki Shauri (30), Haji Shaban (24), Kaimu Amri, Mati Shauri (32), Rashid Fumu maarufu kama Chidi (15), Haji Musa (25) na mwingine aliyetambuliwa kwa jina moja la Hamisi.
Machano alisema wakati jahazi lake likiwa upande wa Kigamboni aliona boti hiyo ikija kwa kasi mbele yake na alijaribu kutoa ishara kwa naodha wa boti ya Seagull ili apite nyuma yao lakini hakufanya hivyo.
"Alitugonga ubavuni na kutukokota kama mita kadhaa na hatimaye tulizama," alisema.
Alisema baada ya kuwagonga boti hiyo iliendelea na safari.
Alisema watu wanane akiwemo yeye walifanikiwa kuogelea na kuokolewa na wavuvi wa samaki wa eneo hilo.
"Kuna wenzetu watatu akiwemo mmoja ni mtu wa makamo ambao tumeambiwa walidandia boti ya Seagull, bado hatuna uhakika kama wapo humo au la," alisema.
Alisema jahazi walilokuwa wakilitumia ni la kubeba mizigo na kwamba walitoka visiwani humo Jumamosi iliyopita.
Alisema wakati wa tukio hilo walikuwa na kreti tupu za bia na soda zaidi ya 1500 ambazo walikuwa wanazileta Dar es Salaam kwa ajili ya kununua vinywaji.
Alisema mali nyingine walizozipoteza ni pamoja na simu za mikononi ambazo Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, aliyekuwa eneo hilo, aliahidi kuwapa simu mpya.
Alisema mali nyingine ni pamoja na fedha pamoja na mabegi yao ya nguo
Akizungumza na waandishi wa habari eneo la tukio, Kamanda Kova, alisema wanaendelea kufanya mawasiliano na upande wa Zanzibar ili kujua kama ni kweli mabaharia watatu walipanda boti ya Seagull baada ya ajali.
CHANZO: NIPASHE
Boti inagonga Jahazi kisha inaondoka kama hapajatokea kitu? Huu Kweli ni Ubinadamu?