Wakati maasi ya Prigozhin yalionekana kuipata Kremlin kwa ghafla mashirika ya kijasusi ya Marekani yalikuwa tayari yamepata ishara kwamba alikuwa akipanga kuchukua hatua na yalikuwa yamemjulisha Rais Biden pamoja na viongozi wakuu wa bunge mapema wiki hii, vyombo vya habari vya Marekani viliripoti.
Habari za kijasusi za Marekani ziligundua kuwa kiongozi wa kundi la mamluki alikuwa akikusanya silaha, risasi na vifaa vingine karibu na mpaka na Urusi, CNN iliripoti.
Gazeti la New York Times linaripoti kuwa Rais Biden alizungumza na viongozi wa Ufaransa, Ujerumani na Uingereza kwa sababu ya wasiwasi kwamba udhibiti wa Putin wa silaha kubwa za nyuklia za Urusi ungeweza kumponyoka katikati ya machafuko hayo.
Wakuu wa kijasusi wa Marekani walikuwa wakifuatilia uhusiano unaozidi kuzorota kati ya Prigozhin na maafisa wa ulinzi wa Urusi kwa miezi kadhaa na ujasusi ulibaini kuwa ni ishara kwamba vita vya Ukraine vinakwenda vibaya kwa Wagner na wanajeshi wa kawaida, gazeti hilo linasema.
BBC