Binadamu hatuwezi kufikiri kama Mungu anavyofikiri. Au ufahamu au maarifa ya mwanadamu ni tofauti na maarifa ya Mungu.
Mathalani unatizama movie ambayo kwako ni mpya hujawahi kuiona, ufahamu au maarifa ya mwanadamu hayawezi kujua mwanzo wa movie utakuwaje, katikati ya movie itakuaje na mwisho wa movie utakuwaje.
Kwa mfano huu wa movie kwa jinsi mwanadamu anavyoyaangazia mambo basi anamkadiria Mungu wake naye ufahamu wake wa kuangazia mambo upo kama aliyonao yeye binadamu.
Na hapa ndipo tunapofeli! Binadamu hawezi kufikiri kama Mungu! Na ufahamu au maarifa ya binadamu ni tofauti na Mungu!
Mungu anafahamu mwanzo wa jambo utakuwaje hata kabla ya hilo jambo kuzuka, na katikati ya jambo litakuwaje na mwisho litakuaje. Si hivyo tu! Bali Mungu anafahamu litatokea wakati/muda upi na hata baada ya wakati/muda Mungu anafahamu ni nini kitakachotokea.
Maamuzi ya maisha yako ya kwamba utakua wa peponi au wa motoni Mungu hajayapanga. Bali wewe mwenyewe binadamu ndiye uliyeyapanga. Ndiyo, Mungu ameshaandika kila kitu kitakavyokuwa na mwenendo wake utakavyokuwa na mwisho wake utakavyokua.
Kwa nini Mungu kajua hivyo? Kwa sababu Mungu elimu yake, ufahamu wake na ujuzi wake umetangulia nyakati. Elimu yake Mungu imetangulia kabla hata ya nyakati kutokea, baada ya nyakati kutokea, nyakati iliyopita, nyakati ya sasa na nyakati ijayo, na baada ya nyakati.
Ndiyo maana yeye Mungu anafahamu kwamba yule atakuwa wa motoni na yule atakuwa wa peponi. Kwa sababu yeye tayari alishaona kabla mwenendo wa hao viumbe wake utakuaje...