SoC04 Athari za kiafya na kiuchumi zitokanazo na bidhaa zitakanazo na zao la tumbaku ni nyingi kuliko faida za uzalishaji; tunahitaji sera mpya kwenye hili

Tanzania Tuitakayo competition threads

Martinszjr0042

New Member
Dec 1, 2018
3
2
Zao la tumbaku ni miongoni mwa mazao ya biashara ambayo kwa kiasi kikubwa iliaminika kwa miaka mingi kuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi. Hili sio jambo la kufichika kutokana na ukweli kuwa maeneo mengi ambayo watu huzalisha tumbaku, wengi wameamini kuwa ukuaji wao kiuchumi umechangiwa Sana na uzalishaji wa zao la tumbaku. Hata sasa ukienda mikoa kama vile Tabora na Mara ambayo ina wakulima wengi wa zao hili utapata shuhuda mbalimbali kwa namna zao hili limesaidia sana ukuaji wa uchumi kuanzia ngazi ya Kaya ambazo zinazalisha zao hili.

Hii haipingiki kwa wale wanaozalisha tu na sio watumiaji wa bidhaa zitokanazo na tumbaku. Pengine kutokana na soko kubwa la tumbaku na kukosekana kwa elimu mbadala juu ya kilimo cha aina zingine za mazao ya biashara katika maeneo hayo ndio sababu iliyopelekea zao hili la tumbaku kubaki kuwa miongoni mwa mazao muhimu ya kibiashara yanayochangia ukuaji wa uchumi kuanzia ngazi ya Kaya na hata taifa kwa ujumla. Je, ni kweli tumbaku ni zao la kulitegemea na kuliendeleza?. Ili kuweza kujibu hili, tuangalie pia matumizi ya tumbaku na bidhaa zitokanazo na tumbaku. Bila Shaka tutakubaliana kuwa bidhaa zitokanazo na tumbaku licha ya kuchangia ukuaji wa uchumi, bidhaa hizi ni hatarishi kwa afya kwa watumiaji wake.

Kwa nini bidhaa zitokanazo na tumbaku ni hatari?
Inatuhitaji kwanza kuwa na ufahamu juu ya bidhaa zitokanazo na tumbaku na matumizi yake. Kwa bahati mbaya matumizi ya bidhaa hizi hata kama zinachangia kwa kiasi kikubwa kwenye kukuza uchumi, hayana tija kwa taifa la Tanzania. Hebu angalia, tumbaku inatumika kwenye starehe kwa namna mbali mbali kwa mfano kwa kuvuta moshi wake au kwa kutafunwa au kumung'unywa. Njia zote hizo au namna zote hizo hakuna ambayo ina tija kwa afya ya watumiaji wake. Watu wengi wameanza kupata uelewa juu ya athari za uvutaji wa sigara au bidhaa za tumbaku unavyoongeza hatari ya kupata aina mbalimbali za saratani kwa watumiaji wake.

Pia tafiti mbali mbali juu ya athari za tumbaku, zimebaini kuwepo kwa aina zaidi ya 7000 za kemikali kwenye moshi utokanao na tumbaku ambazo huchangia kutokea kwa saratani kwa mtumiaji wa tumbaku. Kemikali hizi husababisha mtu kuwa kwenye hatari ya kupata saratani kwa kuharibu mfumo sahihi wa vinasaba vya seli za mtu unaoruhusu utengenezwaji wa seli mpya na kupelekea kuzalishwa kwa seli zisizo za kawaida na hivyo kupelekea kutokea kwa saratani. Kutokana na athari hii tumeona kuwa watu wengi ambao wanatumia bidhaa za tumbaku wako kwenye hatari ya kupata aina mbalimbali za saratani ukilinganisha na wale wasiotumia. Athari hii haipo kwenye ngazi ya mtumiaji pekee, bali familia au Kaya na taifa kwa ujumla. Unaweza sema ni kivipi familia nzima na taifa linaathirika?

Chukua hii, pale inapotokea familia imepata mgonjwa wa saratani, huwa kuna gharama zisizotarajiwa hasa kwenye kumhudumia mgonjwa mwenye saratani. Hapa itahitajika pesa nyingi za kugundua aina ya saratani aliyonayo na pia pesa kwa ajili ya matibabu ambayo pia hutegemea hatua ya saratani aliyonayo. Hii inaweza kudidimiza uchumi wa mtu binafsi, Kaya au familia na taifa kwa ujumla kutokana na ukweli kuwa nguvukazi itaelekezwa kwenye kumuhudumia huyu mtumiaji wa bidhaa za tumbaku ambaye imempelekea kupata saratani. Kwa ngazi ya taifa, fedha nyingi zinatumika kwenye kuratibu na kuendesha miradi mbalimbali inayolenga kutoa matibabu ya saratani hivyo kuathiri ukuaji wa uchumi.

Matumizi ya bidhaa za tumbaku pia husababisha magonjwa mengine ambayo sio saratani. Magonjwa hutokana na athari za athari za kemikali zinazotokana na tumbaku kwenye mapafu, mishipa ya damu, figo, moyo na sehemu zingine za mwili. Hii pia huongeza gharama kwenye kumhudumia mtu aliyepata athari zitokanazo na utumiaji wa bidhaa za tumbaku. Matumizi ya bidhaa zitokanazo na tumbaku humuongezea mtumiaji hatari ya kupata shida ya kupumua kutokana kuharibiwa kwa mapafu na mfumo mzima wa upumuaji.

Hii hupeleka baadhi ya watu wenye shida hii kushindwa kupumua kwa kujitegemea hivyo kuhitaji kusaidiwa kwa mitungi maalumu ya oksijeni kwa sehemu kubwa ya maisha yao jambo ambalo pia ni gharama sana ili mtu aweze kujitegemea kwani wanapokosa hiyo mitungi maalumu ya kuwa nayo nyumbani basi itabidi maisha Yao yawe ni kushinda hospitali inapopatikana huduma ya oksijeni kwa muda wote. Je, ikiwa mtu amefikia hatua ya kuwa tegemezi kwa hatua hii, atakuwa na uwezo wa kuzalisha na kuongeza kipato kama hapo awali? Ni dhahiri hatoweza kufanya hivyo na hii huathiri uchumi kuanzia ngazi ya mtu binafsi hadi taifa kwa ujumla.

Licha ya tumbaku kuwa moja ya zao linalosaidia kukuza uchumi, kwa upande mwingine matumizi ya bidhaa zitokanazo na tumbaku hudidimiza uchumi kwa kusababisha athari mbalimbali za kiafya ambazo zinahitaji uwekezaji mkubwa kwenye kukabiloana na athari hizo.

Kwenye Tanzania mpya tunayoitamani ambayo kwa sasa imepiga hatua ya kupinga matumizi ya bidhaa zitokanazo na tumbaku hadharani, tunatamani kuwepo kwa mpango mkakati wa kupunguza uzalishaji wa zao hili kwa kiasi kikubwa. Hii itawezekana kwa kutoa elimu itakayowajengea uwezo watu ambao ni wazalishaji wakubwa wa tumbaku kuona fursa kwenye uzalishaji wa mazao mengine. Uzalishaji wa tumbaku ukopungua kwa kiasi kikubwa utasaidia kwa kiasi kikubwa kupungua kwa bidhaa zitokanazo na tumbaku zinazozalishwa ndani ya nchi na pia kuwepo kwa sera nzuri za kuthibiti uingizwaji wa bidhaa hizo ndani ya nchi.

Hakuna linaloshindikana kwa watanzania wenzangu, tunao wanataaluma wazuri wa maswala ya udongo na kilimo, na hivyo kupitia wao wanaweza kuzisaidia jamii ambazo zimekuwa tegemezi kwenye zao la tumbaku kuona fursa kwenye uzalishaji wa mazao mengine.
 
Bila Shaka tutakubaliana kuwa bidhaa zitokanazo na tumbaku licha ya kuchangia ukuaji wa uchumi, bidhaa hizi ni hatarishi kwa afya kwa watumiaji wake.

Kwa nini bidhaa zitokanazo na tumbaku ni hatari?
E eeh KWA NINI? Maana wote tunakubaliana kuwa ni hatari, sasa bro je unaonaje tukifanyia tafiti kuondoa huo uhatari wake tukaendelea kufaidi matunda yake bila matatizo?

hupeleka baadhi ya watu wenye shida hii kushindwa kupumua kwa kujitegemea hivyo kuhitaji kusaidiwa kwa mitungi maalumu ya oksijeni kwa sehemu kubwa ya maisha yao jambo ambalo pia ni gharama sana
Daaah ni masikitiko, mtu kushindwa kufanya kitu wengine wanakipata buuuuure kabisa. Kupumua imagine
 
athari mbaya haimaanishi kuwa haina faida kwa pato la taifa kuna madawa ya kulevya huko lakini bado yapo
 
E eeh KWA NINI? Maana wote tunakubaliana kuwa ni hatari, sasa bro je unaonaje tukifanyia tafiti kuondoa huo uhatari wake tukaendelea kufaidi matunda yake bila matatizo?


Daaah ni masikitiko, mtu kushindwa kufanya kitu wengine wanakipata buuuuure kabisa. Kupumua imagine
Sana asee,
 
Back
Top Bottom