Askofu Mwamakula na matembezi ya hiyari Nchi nzima

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,015
Mheshimiwa Dkt. John Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania!

Amani iwe kwako!

Mheshimiwa Rais! Mimi Askofu Emmaus Bandekile Mwamakula, nisimamaye katika zamu yangu kama Mtumishi wa Mungu katika zamani hizi za utawala wako kama Sauti ya Haki katika nchi, ninatuma ujumbe huu kwako, washauri wako na Watanzania kwa ujumla wao (Habakuki 2:1).

Kwamba mimi Askofu Mwamakula nimesukumwa kutoka moyo wangu na nafsi yangu kuongoza "Matembezi ya Hiyari" katika nchi nzima yenye lengo la kuuhamasisha Umma wa Tanzania kuhusu umuhimu wa Kuunda Tume Huru ya Uchaguzi na Kuandika Katiba Mpya. "Matembezi ya Hiyari" yatafanyika katika mikoa yote ya Tanzania na wilaya zake zote katika kipindi chote cha mwaka 2021.

Ikumbukwe kuwa mara baada ya Uchaguzi Mkuu wa 28 Oktoba 2020, mimi nilitoa tamko kupitia Vyombo vya Habari kuwa Uchaguzi haukuwa Huru na wala haukuwa wa Haki. Hivyo, pamoja na mambo mengine nikatoa wito wa Kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi itakayosimamia Uchaguzi mwingine na chaguzi nyingine zitakazofuata. Ni dhahiri kuwa tunapozungumzia Tume Huru ya Uchaguzi suala la Katiba Mpya haliwezi kuepukika!

Ninapenda Mheshimiwa Rais utambue kuwa kwa mtazamo wetu, tangu matokeo ya Uchaguzi yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) pamekuwa na maumivu makubwa, uhasama mkubwa na chuki isiyoelezeka miongoni mwa Watanzania! Ukweli huu hauwezi kuelezwa kwako wazi na watu wako wa karibu kwa sababu ya unafiki walionao kwako kwa lengo la kulinda maslahi yao binafsi, nk. Hata hivyo, Vyombo vya Usalama (ikiwemo Taasisi ya Usalama wa Taifa) vinajua ukweli huo na hata viongozi wa dini walio karibu na utawala wako wanajua kuhusu ukweli huo. Ushahidi mmojawapo wa hayo ni mamia ya wapinzani waliorundikwa katika Magereza karibu katika kila Mkoa au Wilaya nchini.

Mheshimiwa Rais, hali hii ya uhasama, chuki na hofu katika nchi haiwezi kuachwa kuendelea. Ni lazima sote kwa pamoja tutafute njia nzuri ya kuliponya taifa. Lakini kama kila mtu na kila taasisi wana hofu ya kutoa sauti na kuelezea hisia na ukweli hadharani, tutakuwa taifa gani sisi? Je, ni kweli kuwa sisi sote tu wanafiki katika nchi? Je, ni kweli kuwa sisi sote tupo kwa ajili ya kutafuta maslahi binafsi katika nchi? Je, ni kweli kuwa sisi sote hatuwezi kuuona uhalisia wa mambo katika nchi? Je, ni kweli kuwa sisi sote tunaogopa kuuawa na watu wasiojulikana endapo tutausema ukweli pasipo kuogopa? Je ni kweli kuwa sisi tunaogopa kuandamwa taasisi zetu endapo tutapaza sauti? Je, ni kweli kuwa sisi sote tunaogopa mali zetu kuguswa na familia zetu kutikiswa endapo tutasema ukweli? Je, ni kweli kuwa sisi sote tunaogopa 'kung'olewa' katika nafasi zetu za uongozi katika taasisi zetu endapo tutafumbua vinywa vyetu? Je, ni kweli kuwa sisi wengine ambao tutachukua hatua za kuieleza jamii ukweli tutakuwa sio wazalendo kwa nchi? Je, uzalendo kwa nchi ni pamoja na kutokumueleza ukweli kiongozi? Je, ni kweli kuwa Mheshimiwa Rais hawezi kupokea ushauri nje ya washauri wake? Sisi wengine tunaamini kuwa jibu la maswali hayo hapo juu ni HAPANA!

Ni kwa sababu hiyo, tunaamini kuwa "Matembezi ya Hiyari" yatatoa fursa kwa umma kutoa hisia zao kuhusiana na jambo muhimu sana katika nchi. Kwamba suala la Mjadala wa Kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Kuandikwa kwa Katiba Mpya litaleta umoja wa kitaifa ambao kwa sasa haupo lakini pia litawapa matumaini watu kuhusu kushiriki kwa Uchaguzi mwingine. Matumaini hayo yataleta utulivu katika nchi lakini pia yataupa utulivu utawala wako katika ngwe hii ya mwisho kwako! Kinyume na hapo utakuwa ni muendelezo wa uhasama, chuki, vitisho, vurugu na kuathiriwa kwa uchumi wa nchi.

"Matembezi ya Hiyari" hayana lengo la kuvuruga utulivu na shughuli za uzalishaji katika nchi kwa kuwa yatakuwa na nguvu kubwa ya kimaadili na hayapita katika njia au barabara ambazo zinaendelea kujengwa, nk. Ndio maana tumeelekeza watembeaji kutokuzidi 20 kwa kundi moja na kuwapo kwa nafasi ya umbali wa nusu kilomita au kilomita moja katika ya kundi na kundi.

Ni kwa sababu hiyo, tunatarajia kuwa Vyombo vya Dola havitatumiwa kuzuia au kuvuruga Matembezi hayo iwe kwa kumsumbua Askofu au kuwasumbua watakaokuwa wanaambatana na Askofu au watembeaji wengine! Tunatumaini pia kuwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya, Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Wakuu wa Polisi wa Wilaya hawatatumika kuzuia Matembezi hayo bali wanaweza kuwa sehemu kwa kuhudhuria na kuangalia usalama pale inapobidi.

Tunaamini kuwa kama Serikali yako na Vyombo vya Dola hawatatumia nguvu kuzuia vuguvugu hili la umma linaloongozwa na Askofu, basi Mheshimiwa Rais utaweza kumaliza muda wa uongozi wako salama. Lakini kama Serikali na Vyombo vya Dola watatumia mamlaka yao vibaya kwa kumzuia Askofu na kuwadhuru washiriki ambao wanakusudia kutembea kwa amani basi Serikali yako haiwezi kuwa na mwisho mwema na hata baada ya mwisho wenu kufika hamtaweza kufurahia maisha baada ya utawala wenu kumalizika!

Mwisho ninapenda kukujulisha kuwa nitazindua "Matembezi ya Hiyari" katika Majimbo ya Uchaguzi ya Ubungo na Kibamba katika Wilaya ya Ubungo katika tarehe nitakayoitangaza! Matembezi haya yanajulikana pia na Jumuiya ya Kimataifa ambayo itayafuatilia kwa ukaribu sana kutokea ndani na nje ya nchi!

Ni imani yangu kuwa Mungu atasema na nafsi ya Rais na kwamba Mungu atanilinda sawasawa na Neno lake (Zaburi 121). Lakini hata hivyo, hata kama Mungu katika hekima yake isiyoweza kuhojiwa ataruhusu mabaya yanaipate sitaweza kuogopa na nitaongoza Matembezi ya Hiyari kwa kuwa dhamiri yangu mbele za Mungu hailaumiki kuhusiana na jambo hili (Isaya 6:8-13).

Mwana Kondoo Ameshinda! Tumfuate!

Askofu Mkuu Emmaus Bandekile Mwamakula
 
Watanzania tumejawa na unafiki wa kiwango chs lami. Tundu Lissu aliitisha maandamano ya amani nchi nzima, watu wakasusa kisha wakakimbilia kulalamika kwenye mitandao ya kijamii uonevu unaofanywa na serikali.

Haya nafasi ya pili imepatikana ya kutoa yote yaliyopo moyoni mwa watanzania. Na hii isusiwe tena.
 
Back
Top Bottom