Anna Mwasyoke: Miaka 15 Katika Taaluma ya Uandishi wa Habari

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
617
1,800
Hii ni simulizi ya miaka 15 ya maisha ya Anna Mwasyoke katika fani ya uandishi wa habari ambayo imetimia tarehe 02/01/2023. Mwasyoke, kupitia ukurasa wake wa Instagram, ameona ni vema kuushirikisha umma japo kwa ufupi kuhusu safari yake hii anayoieleza kuwa ni “nzuri na tamu isiyochosha" ili kuwavutia wengine wanaotamani hii fani au mashabiki wanaopenda kujua alipotokea, alipo na anapoelekea.

FB_IMG_1673556323164.jpg

Anna akiwa katika studio ya TBC.

Safari yangu rasmi katika Shirika la Utangazaji Tanzania TBC ilianza 02/01/2008 ambapo nilianza rasmi kazi ya uandishi na utangazaji katika idhaa ya lugha ya Kingereza, yaani TBC International.

Ilikuwaje nikapata hiyo kazi?

Kuna watu wawili siwezi kamwe kuwasahau nao ni Joseph Burra na Anicet Mwesa, hawa vijana nilisoma nao Chuo Kikuu cha Tumaini - Iringa (sasa Chuo Kikuu cha Iringa) na niliwatangulia mwaka mmoja mbele.

Tangazo la kazi la idhaa ya Kingereza lilitoka mwishoni mwa mwaka 2007 na wala sikubahatika kuliona, wao walikuwa field TBC wakati linatoka. Basi bwana, wakanitafuta kweli kunijulisha kwamba niombe kazi tu na deadline ilikuwa imepita kidogo, nikawaambia mi simjui mtu yeyote ntapata kweli, wakasisitiza we omba tu.

Basi bwana, nikaomba hiyo kazi ikawa bahati nikaitwa kwenye usaili na nikapata kazi ambapo tulianza watu kumi wakati huo akiwemo mtangazaji mwenzangu wa kipindi cha asubuhi Paul Alphonce na shoga yangu Mwamini Andrew, basi tukaanza kazi pamoja yaani siku moja.

FB_IMG_1673557675929.jpg

Anna na Essero Mafuru. Wote wahitimu wa Tumaini University - Iringa.

Lilikuwa jambo la furaha kupata kazi, tukapitishwa kwenye ofisi na tukafahamishwa mambo mbalimbali kuhusu TBC na nakumbuka mama Edda Sanga mtangazaji nguli alikuwepo wakati huo.

Baadaye kazi ikaanza rasmi ya kubuni vipindi maana sisi ndio tulianzisha hiyo redio kwa mara ya pili ukiacha ile iliyoitwa External Service na ndipo sasa tukakaa pamoja kufikiria vipindi gani vingekuwa vizuri kwa ajili ya hiyo idhaa na ilikuwa kazi yenye mafanikio makubwa ya kubuni vipindi sasa.

Safari ya kwanza nje ya nchi

Mkurugenzi Mkuu wakati huo Tido Mhando baada ya kuona mawazo yetu akatupa fursa ya kwenda Nairobi kwa wiki tatu kujifunza katika idhaa ya BBC na KBC na nikwambie tu hiyo ndio ilikuwa mara ya kwanza kusafiri nje ya nchi basi moyo ukalipuka paaaa!

Basi bwana nikaenda nyumbani siku hiyo nikamwambia baba na mama kwamba tunakwenda Nairobi kwa furaha kubwa sana na wote pamoja walifurahi sana, yaani kama unavyofahamu wazazi wanavyofurahia jambo zuri kwa watoto wao.

Basi wakati ukawadia tukaenda Nairobi na tulipanda basi enzi hizo hadi Nairobi, tukafikia hoteli nzuri tu na kesho yake tukapelekwa Shirika la Utangazaji la Kenya ambako tulikuwa na shauku mno mno ya kutaka kujifunza wanavyofanya kazi. Pale KBC walikuwa na matangazo ya Kiswahili, Kingereza na idhaa iliyotangaza lugha za makabila. Kwa siku kadhaa tulijifunza pale KBC.

Baada ya kumaliza KBC tulikwenda Idhaa ya Kiswahili ya BBC ambako pia tulijifunza utayarishaji na utangazaji wa matangazo yao ya asubuhi na baadaye sasa kikao ambacho kililenga kutathmini kipindi kilichopita na maandalizi ya kipindi kijacho.

Nakumbuka wakati huo tulishangaa sana namna watayarishaji wa kipindi walivyoamka alfajiri na walivyotangaza kwa umahiri, yaani enzi hizo nisingewaza kama ntafikia huo umahiri ambao hapana shaka nimeuvuka kwa mbali tu.

Tukiwa Nairobi pia tulipata fursa ya kuwatembelea wenzetu ambao walipelekwa kule na gazeti la Mwananchi Communications Limited kwa ajili ya kupikwa kupitia Daily Nation ambalo ndio gazeti lao mama. Namkumbuka zaidi Orton Kishweko ingawa walikuwepo na wengine. Tulijifunza mengi pia kupitia kwao na tukabadilishana uzoefu.

Pia, tulipata fursa ya kutembelea vivutio vya utalii, maduka makubwa na maeneo mengine mengi, yaani kwa ujumla tulipata uzoefu mkubwa, tuliona mengi na hatimaye tukarejea nyumbani kuanza kazi rasmi ya kuijenga idhaa ya Kingereza TBC International.

FB_IMG_1673560466233.jpg

Anna akiendesha kipindi katika studio ya redio ya TBC.

Maisha ya kazi yakaanza rasmi sasa baada ya wiki tatu tulizokaa Nairobi. Nakumbuka tukapitia upya sasa mawazo ya vipindi tulivyobuni na kuviweka vizuri kwenye maandishi na pia tukaanza kupewa uzoefu zaidi wa kutafsiri habari za Kiswahili kwenda kwenye lugha ya Kingereza.

Kushamiri njaa ya kujifunza

Wakati nikiendelea na majukumu hayo njaa yangu ya kujifunza na kutaka kufahamu mambo zaidi ikanifanya pia nianze kujitolea muda wa ziada kujifunza zaidi kwenye idhaa yetu ya vijana ya redio, yaani TBC FM sasa.

Nakumbuka wakati huo nilijifunza kupitia kipindi cha Busati kikiendeshwa na Annastazia Willherick, dada mwenye moyo wake wa dhahabu na mwenye historia kubwa na umahiri wangu katika utangazaji. Hapana shaka historia yangu itamkumbuka daima. Anna nakushehimu mno, ulijua sana kunitia moyo, vilevile alikuwepo partner wangu wa maisha yote Paul Alphonce ambaye nilijifunza mengi sana kwake.

Kipindi kingine ambacho nilijitolea kujifunza kilikuwa ni Njozi Njema kikiongozwa na Jocelyn Kitakwa na mara nyingine Ahmed Salum ambaye pia tulianza kazi pamoja, baadae nikaja kumudu vema sana kipindi cha usiku cha Njozi Njema na sauti yangu mujarab ikanogesha mno kipindi. Jocelyn Kitakwa mwenyezi Mungu akubariki sana sana ulinifundisha kwa upendo sana.

Kusema ukweli wa moyoni kabisa TBC FM lilikuwa darasa kubwa sana katika maisha yangu ya utangazaji na nakumbuka Annastazia Willherick alikuwa akiniambia, ‘Anna una kitu kikubwa sana ndani yako’, na wakati akiniambia hayo hakuna ambaye angewaza ningekuja kufikia hatua ya kuwa miongoni mwa watangazaji bora hapa Tanzania.

Sina haja ya kusimulia mengi sana hapa ila safari yangu ya utangazaji katika miaka miwili ya mwanzo ilikuwa na changamoto nyingi mno!

Niliendelea kujifunza kwa nguvu na bidii sana pale TBC FM, mara nyingine nililazimika kulala siku mbili hadi tatu kazini bila kurejea nyumbani ili nitumie muda wa ziada kujifunza utangazaji kwa maana kumbuka kwamba nilikuwa na majukumu yangu ya msingi TBC International, kwa hivyo nikimaliza kazi zangu International ndio nahamia FM. Kwa hivyo nilikuwa nabeba nguo zangu za siku mbili hadi tatu mara nyingine.

Hapa somo kubwa ninalowapa ni kwamba kuna nguvu na baraka kubwa katika bidii kazini, maana ratiba hiyo ngumu ilinifanya nijifunze mno.

Kuhamia Mikocheni

Wakati hayo yakiendelea nilikuwa pia na shauku ya kufanya kazi katika ulimwengu wa habari na matukio ambayo ndio dunia yangu mpaka leo, na nakumbuka Annastazia akaniambia, ‘wewe itabidi uombe kuhamia Mikocheni, utaweza kwa hakika’.

Basi bwana, nikamtafuta Mkurugenzi Mkuu Tido Mhando wakati huo na nikamwambia natamani kufanya kazi katika Idara ya Habari na Matukio Mikocheni, akanihoji maswali mengi na nikamuelezea ni kwa nini.

Basi baada ya miezi kadhaa nikahamishiwa Idara ya Habari na Matukio Mikocheni na mwenzagu Ahmed Salum na huo ulikuwa mwaka 2009 ambapo pia ndio mwaka tuliopata ajira rasmi ya serikali maana mwanzo tulikuwa kwenye ajira ya mkataba.

Maisha mapya yakaanza katika ofisi mpya Mikocheni katika Idara ya Habari na Matukio na hiyo ilimaanisha kujifunza upya kila kitu na waandishi wenzangu mnajua maisha yalivyo kwenye vyumba vya habari, mara nyingi tunajifunza kwa njia ngumu (tough way) ila ndio inakufanya uwe bora zaidi. Kwa kipindi cha mwaka mmoja nilipitia mengi na changamoto zilikuwa nyingi.

FB_IMG_1673559222280.jpg

Anna na Gabriel Zacharia

Maisha mapya yakaanza Mikocheni na nakumbuka nilikabidhiwa kwa Gabriel Zacharia miongoni mwa watangazaji wazuri Tanzania kuwahi kutokea, kwa sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Busega, Simiyu.

Mimi na wenzangu Ahmed Salum na Asha Haji tukaanza kupikwa kuandaa vipindi vya habari na matukio na hapa pia haikuwa rahisi maana mimi ndio nilionekana nina slow pace kuliko wote katika kujifunza, kwa hivyo changamoto zilikuwa nyingi ikiwemo kusimamishwa kwa takribani mwaka mzima kuweka sauti kwenye chochote kile. Nilihuzunika sana na nakumbuka nilienda chini ya mti mmoja hapa TBC nikalia sana na alikuja Agnes Mbapu akanibembeleza sana akiniambia, ‘mdogo wangu futa machozi, endelea kuchapa kazi’.

Kwa hivyo nikaendelea tu kutayarisha vipindi bila kuweka sauti yeyote kwa usimamizi wa Gabriel Zacharia. Sasa baada ya mwaka Gabby siku moja akaniambia umeshakaa muda mrefu sana bila kutangaza; leo nakuandalia kipindi. Nakumbuka kilikuwa cha Matukio ya Wiki. ‘Utatangaza na ikitokea mtu anauliza mi ndo nitajibu’.

Basi bwana, akaandaa mapema akanipa script nikapitia vizuri mapema kisha nikatangaza vizuri na hakuna aliyeuliza na ndio safari ikaanzia hapo na nikasema iwe mvua liwe jua nitatangaza.

Jamani, nilifanya mazoezi mno ya kutangaza na nilikaa kazini muda mwingi sana kujifunza na watu wa TV na radio mnajua akija mtu mpya na anapenda vipindi basi watu wanamtegea balaa, sasa nikawa naachiwa vipindi na watangazaji wa wakati huo (nawashikia) na ndio vikanifanya niwe bora zaidi. Gabby nakushukuru ulijua kunipambania na uliupiga mwingi mnooo.

Bosi wangu Assumpta ulinibalasa mwanzo ila baadae ulinifundisha kwa bidii sana pia. Nikaanza kupewa kazi za sauti sasa ikiwemo makala. Nikaanza kuwika mno baadaye nikahamishiwa kipindi cha Asubuhi ambapo nikakabidhiwa kwa Shaaban Kissu mwenye moyo wa dhahabu. Nakumbuka tulikuwa tukiingia saa sita usiku hadi asubuhi kwa siku tatu mfululizo kuandaa kipindi na baadaye kukirusha kuanzia saa kumi na mbili hadi saa mbili na nusu.

FB_IMG_1673560159081.jpg

Anna katika majukumu ya kiuanahabari.

Shaban Kissu na Juma Nkamia walitufundisha kwa upendo sana na hebu nikuibie siri kidogo. Hapa sasa ndoto yangu ya siku nyingi ilitimia maana ni kipindi ambacho nilikipenda tangu kikiitwa Majira hadi sasa kinaitwa Asubuhi Hii, ila nilipenda zaidi wakati kikifanywa na Zawadi Machibya wakati nikiwa chuo na nikamwambia Mungu siku moja natamani nifanye hicho kipindi. Basi hiyo ikawa mwanzo ya ndoto yangu kutimia maana baadae zaidi nikawa mtangazaji wa Asubuhi hii pamoja na mwenzangu Paul Alphonce kwa miaka karibu minne. Nakwambia ndoto ukizifanyia kazi hutimia.

Majukumu kuongezeka

Asubuhi Hii ilikuwa nyota angavu kwangu maana ndio ilikuwa mwanzo sasa wa kuaminika na baadae kipaji kikaonekana nikaanza kufanya kazi nyingine nyingi za utangazaji ikiwa ni pamoja na kutangaza vipindi vya mahojiano vya radio na TV, kusoma habari radio na TV, kuweka sauti kwenye makala ndani na nje ya TBC.

Nakumbuka niliweka sauti hadi kwenye mchezo wa radio wa DW, kuweka sauti kwenye matangazo ya biashara, matangazo ya nje OB. Sasa miaka hiyo ya 2013 na kuendelea nakumbuka kwa upcoming generation mimi nikawa miongoni mwa wale wa mwanzo kabisa kuaminiwa na kupelekwa kwenye matangazo ya nje OB na nikabahatika kufanya matukio mengi makubwa ya viongozi wakubwa na kazi hiyo ikanifanya nitembee Tanzania yote na nje ya Tanzania pia, maeneo niliyotembea Duniani nayo ni series ya siku nyingine.

Bidii yangu kwenye kazi haikukoma, nikaanza pia kutafuta fursa za mafunzo ili nijiongezee thamani na ofisi pia ikanipa baadhi ya fursa. Sasa ukiacha ile ya Nairobi safari yangu ya pili ikawa ni mafunzo nchini Egypt, nakumbuka ilikuwa mwaka 2014.

FB_IMG_1673557547997.jpg

Anna akihitimu Shahada ya Uzamili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Mwaka 2014 nikiwa likizo nikapigiwa simu na ofisi ya HR nikaambiwa, ‘Anna kuna barua hapa unatakiwa kwenda Misri kwenye mafunzo ya miezi mitatu’. Yaani nikarukaruka kwa furaha mno, nakumbuka nilikuwa UDSM kwenye ofisi ya Supervisor wangu wa research ya Masters, basi nikafurahi mno.

Fursa huibuka na kupotea

Kesho yake nikaenda ofisini kwa ajili ya kuanza kufuatilia hiyo safari ambayo tulikuwa mimi, Steven Basheka na Upendo Mbelle, tukafuatilia hatua zote muhimu. Sasa siku ya mwisho ambayo ndio tulitarajia kupata visa na ticket tukiwa na mabegi yetu kabisa, kufika Ubalozini tukaambiwa kuna taratibu zilichelewa kidogo kwahiyo haiwezekani kwenda, siku hiyo naweza kuiweka kwenye historia kama miongoni mwa siku nilizohuzunika kupindukia.

Nakumbuka kaka yangu Nsape aliyenisindikiza na mama yangu wakaniambia usijali utapata fursa nyingine. Sasa kwanini nimesimulia hii, natamani kukwambia mara nyingine fursa zinaweza kutokea and it's okay.

Basi bwana, mwaka 2015 ulinifanya niamini kumbe kuna bahati maishani, maana ile fursa ikaja tena na mara hii nikapata fursa ya kwenda kwenye mafunzo na ndio ikawa mara yangu ya kwanza kupanda ndege (mwewe). Nakumbuka nilimsumbua baba yangu kunipeleka Airport maana nilitaka kwenda saa tano kabla ya safari, nikapanda Egyptian Airways saa sita usiku na asubuhi tukatua Cairo na wenzangu Fanuel Elia na Mbijima Mzungu wa ufundi.

Misri ni miongoni mwa maeneo ambayo yameacha alama kubwa mioyoni mwangu, tuliishi hoteli inaitwa Dar al Mudaraat ambayo ilikuwa na wageni wengi sana waliokuja kwa sababu mbalimbali zikiwemo michezo, mafunzo, kwa hivyo maisha kwenye hoteli yalinoga sana na ilikuwa kama Big Brother.

Ilikuwa sehemu ya kujifunza tamaduni zingine na nakumbuka kilichonifurahisha ni harusi za kila siku kwenye hoteli.

Mwisho wa wiki tulipata fursa ya kusafiri miji yote ya Misri, kwa kweli lilikuwa darasa kubwa sana kuishi Misri.

Baada ya kumaliza miezi mitatu nchini Misri, ukawadia wakati wa kurejea nyumbani Tanzania na pasipo chembe ya shaka elimu niliyoipata kule ilinivusha pakubwa mno.

Kuwasaidia wanataaluma wachanga

Nilirejea nyumbani Tanzania kuendelea na maisha sasa katika chumba cha habari na kingine sasa nikuibie siri kuhusu mimi, maisha yangu miaka miwili ya mwanzo kwenye tasnia na changamoto nilizopitia yalinifanya nidhamirie kwamba watu wote watakaopita mikononi mwangu nitawafundisha na kuwabeba kwa upendo wote. Kwahiyo ikawa passion yangu kufundisha na kuwafanya watu wakue kwenye career.

Nakumbuka nikarejea kwenye vipindi vya redio na sasa nikapewa kipindi cha Mchana Huu na Harakati na pia nikawa nasoma habari na vipindi vya mahojiano kwenye TV na matangazo ya nje OB.

Sasa passion yangu ya kufundisha vijana ikakua zaidi na zaidi na vijana wa field waliotoka kwenye vyuo mbalimbali walikuwa wakikabidhiwa kwangu na pia wale waliojiunga nasi waandishi wachanga nilikuwa nikawafundisha. Kwanini nasimulia hadithi, nataka nikwambie umuhimu wa kufahamu vipawa vingine ulivyo navyo na vinavyoweza kukufanya daraja la kusaidia wengine.

Leah Mushi, rafiki yangu mkubwa, na ingawa ni mdogo kiumri ila alinifundisha mengi na Mungu alimtumia kama daraja kwangu kwenye mafanikio ya career yangu.

Nakumbuka mwaka 2018 alinipigia simu kuna watu wanataka mtu anayeweza kumentor wanafunzi wa vyuo kwenye program maalumu inayoendeshwa na USAID basi akanitaja kwa sababu alikuwa akiniona TBC nilivyofundisha wengine kwa passion, akanitaja na nikaitwa na Internews ambao ndio waliratibu mradi huo.

Mwaka 2018 mwezi Julai nikaanza kufundisha Radio Journalism kwa wanachuo wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano ya Umma (SJMC). Kila siku nilikaa nao kwa saa nane nikiwafundisha kuandaa makala, kuandika habari, kusimulia, kutangaza na mengine mengi. Lilikuwa darasa zuri sana na binafsi nilikua sana kwenye fani na ilinifanya niwe na upendo zaidi maana uki-mentor watu unakuwa mama au baba wa watoto wengi na miongoni mwao nafanya nao kazi TBC kwa sasa.

FB_IMG_1673553747978.jpg

Anna akiwa na baadhi ya wanafunzi wa
SJMC.

Umuhimu wa kujiongezea thamani kwenye fani

Basi bwana mwaka 2018 baada ya kufanya kazi kwa umahiri mkubwa, mwaka 2019 nikapata fursa ya kufundisha tena na mara hii ikawa kwa miezi mitatu na somo kubwa nililojifunza ni upendo na furaha unapoona wengine wamefanikiwa na pia ukifanya kazi nzuri na kwa ufanisi unaonekana na ikitokea nafasi tena unafikiriwa na wahusika pia.

Vilevile, kazi ile ilijenga uhusiano mzuri pia kati yangu na Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC) maana walinipa pia nafasi nyingine nyingi ikiwa ni pamoja na kuwa judge kwenye shindano lao kubwa la utangazaji kwa wanafunzi.

Leo tamaa yangu kubwa ni kukwambia umuhimu wa kujiongezea thamani kwenye fani, hapa rafiki yangu Leah Mushi anatumika tena kama daraja, nakumbuka ulikuwa mwaka 2016 mwishoni baada ya Leah kuhitimu mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari wanawake katika fani na uongozi ambayo inatolewa na WANIFRA na chuo cha Witts cha Afrika Kusini akanishawishi na mimi kwa kuniambia, ‘Anna una uwezo mkubwa ni lazima usome hii course’, yaani alinikomalia mno hadi nikaomba na akanisaidia hadi baadhi ya vitu kwenye maombi yangu.

Chaguo la kwanza nikakosa na ndio maana huwa naamini kwenye bahati maana ikatokea mmoja kati ya waliochaguliwa hakujiunga na wenzake basi nikaitwa mimi wenzangu wakiwa wameshaanza sessions za mwanzo, nikajiunga nao na kwa usimamizi mzuri wa mentor na coach wetu Dkt Joyce Bazira nikapikwa nikawa sawa na wenzangu. Tulifanya sessions za ngazi ya kitaifa na coach wetu, sessions za mtu mmoja mmoja na coach na kisha tukaenda sessions za wenzetu kutoka maeneo mbalimbali Afrika na tulikutana South Africa.

Yaani nakwambia milango ya safari ikawa imefunguka na kusema ukweli huo ndio utamu wa tasnia ya habari.

Basi bwana, mafunzo hayo yalibadilisha maisha yangu kabisa maana yaliniongezea ujuzi, yalinijenga na kunifanya niwe mwandishi mwenye dira na dhima na pia kufahamu kusudi la mimi kuwepo kwenye tasnia ya habari.

Kubwa zaidi tulikwenda Afrika Kusini mara mbili, mara ya kwanza katika mji wa Johannesburg na mara ya pili ni Johannesburg na Durban ambapo tulipata pia fursa ya kushiriki mkutano mkuu wa waandishi wa habari Duniani, yaani nakwambia huko lilikuwa darasa na nusu, tulikutana na waandishi wa habari wakubwa, wamiliki wa vyombo vya habari na viongozi wa vyumba vya habari na wakapata fursa ya kutoa ushuhuda wao na kilichowafanya wafanikiwe.

Kwa kweli ilikuwa ni nafasi ya dhahabu kwangu na wenzangu kushiriki mkutano ule tukiwa pia na shoga yangu Leah Mushi na ndio maana nasisitiza maisha yangu yalibadilika kabisa na niliporejea sasa nikapanga mipango ya kujiboresha kabisa na nikasema sitokuwa wa kawaida kuanzia leo.

Nilipomaliza mkutano ule maisha yakaendelea katika chumba cha habari huku mara hii nikiwa na nia ya kupata mafanikio zaidi na kuwaza kuwavusha wengine zaidi, nikaanza kuandaa vipindi vyenye tija zaidi, nikaongeza ufanisi zaidi kwenye matangazo ya nje, nikatumia muda mwingi zaidi kuhakikisha najiboresha na navifanyia kazi zaidi vipawa vyangu vingine nilivyojaliwa na mwenyezi Mungu.

Sasa miongoni mwa vipawa nilivyojaliwa ni pamoja na kufundisha wengine, kutangaza, kuweka sauti (hapa nina mahaba napo sana) na mwenyezi Mungu amenibariki sauti kwa hakika.

Eneo jingine ni la ushereheshaji wa shughuli rasmi na zile za harusi, nikaanza kuvifanyia kazi kwa bidii na kuweka mikakati zaidi ili viniongezee tija na pia niwasaidie wengine. Sasa nimeamua kusimulia umuhimu wa kufahamu vipawa vyako kwa sababu jambo hili litakufanya ujiboreshe, ujiongezee ujasiri na pia ujiongezee kipato zaidi, kwa hivyo hakikisha unatambua vipawa ulivyo navyo.

FB_IMG_1673560056526.jpg

Anna akisherehesha.

Matukio makubwa niliyoshiriki
Katika miaka hii 15 katika hii fani mwenyezi Mungu amenijalia nimetangaza kila kitu muhimu unachofahamu katika ulimwengu wa habari na matukio yaani kuanzia habari, vipindi, vipindi maalumu, matangazo mbashara na hasa kwa mwandishi unayekua.

Hebu nikupitishe katika baadhi ya matukio makubwa muhimu niliyowahi kuyafanya na nianze kwa kuwaambia kupewa kazi muhimu hakuji tu hivi hivi ni lazima uonyeshe bidii, uwezo na ujifunze bila kukoma.

Sasa miongoni mwa hayo ni pamoja na Uchaguzi Mkuu wa 2020, nimeshiriki katika chaguzi kadhaa ikiwemo 2010, 2015 nilikuwa mafunzo Cairo ila sasa 2020 ndio nikapata fursa ya kuzunguka na mgombea urais wa CCM Dkt John Magufuli ambaye kwa sasa ni marehemu.

Nakumbuka nilianza kutangaza kwa ajili ya TV na marehemu Elisha Eliah na baadae ikalazimika crew ipunguzwe na kwa hivyo mtangazaji aliyekuwa radio akarudishwa kwa hivyo ikabidi mi nihamie kutangaza radio mpaka kampeni zinaisha na nikiri kwamba ilikuwa experience ya aina yake ambayo nitakumbuka siku zote za maisha yangu.

Zilikuwa siku 42 zenye hisia mchanganyiko raha, kupigwa na jua, mvua, vumbi, baridi lakini kwa ujumla huo ndio utamu wa uandishi maana tulijifunza tamaduni mbalimbali kwa kuwa tulizunguka Tanzania nzima.

Kazi nyingine kubwa ilikuwa safari ya Beijing na Chenzhen nchini China, huko tulikwenda na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mwaka 2018, ilikuwa siku nane tu ila kama tulifanikiwa kulala muda mrefu ilikuwa ni kwa saa tatu pengine, kazi ilihitaji wanajeshi hasa. Nakumbuka nilikuwa na Franco Singaile, Nicholaus Mbaga, Fanuel Eliah. Aisee tuliupiga mwingi mno japokuwa tulikuwa busy sana tulifanikiwa kuleta stories nyingi na tuliruka live mara nyingi mno. Tulikwenda kuripoti ushiriki wa Tanzania katika mkutano wa Jukwaa la Ushirikiano wa Afrika na China.

Sasa kazi nyingine kubwa niliyobahatika kufanya ni kutangaza tukio la kuapishwa kwa Rais Yoweri Museveni wa Uganda mwaka 2021, nakumbuka mimi na ndugu yangu Victor Eliah tulikwenda nchini Uganda kwa lengo la kuandaa vipindi vya Kiswahili na kurusha matangazo mbashara ya shughuli mbalimbali za Kiswahili.

Tukiwa Uganda kwa ushirikiano na mwenyeji wetu balozi wa Tanzania Uganda Dkt Aziz Mlima tulifanikiwa kurekodi na kutangaza mbashara matangazo ya Kiswahili kwenye vilabu vya Kiswahili vyuo vikuu, ubalozini, mitaani kwa Waganda wanaozungumza Kiswahili na kwenye makazi ya watu na pia tulishiriki kutangaza katika idhaa ya Kiswahili ya UBC. Nakumbuka nilisoma habari UBC mara mbili na ilikuwa uzoefu wa aina yake.

FB_IMG_1673553617442.jpg

Anna akitangaza kwenye Kituo cha Televisheni cha Taifa Uganda - UBC.

Sasa tukiwa nchini Uganda zikiwa zimesalia siku mbili kuondoka, nakumbuka balozi Dkt Mlima akasema kwa nini msibaki kutangaza tukio la kuapishwa Museveni maana hii pia ina maana kidiplomasia kwetu na pia mmeonekana sana mko Uganda sasa msipotangaza itakuwa ajabu, nakwambia ndio tukapata fursa hiyo. Kwa hivyo kwa kushirikiana na ndugu yangu Victor Eliah, Evelyn Francis mpiga picha pamoja na watangazaji wa UBC tukafanya matangazo yale mbashara, ilikuwa amazing experience. Kwa nini nimeelezea hili, natamani waandishi wa habari wachanga waone umuhimu wa kujiongezea thamani ili wapate fursa ya kufanya kazi kubwa maana hii haiji tu hivi hivi, lazima uoneshe kwamba wakikutuma kazi kubwa watapata kitu, inabidi uaminike.

FB_IMG_1673558821832.jpg

Anna akiwa na Victor Eliah, Kampala, Uganda.

Kazi nyingine kubwa ni kutangaza mbashara matangazo ya ushiriki wa Tanzania kwenye maonesho makubwa ya Expo 2020 ambayo yalifanyika Dubai mwaka 2022, lengo la kufanyika mwaka 2022 badala ya 2020 ilikuwa ni kwa sababu 2020 kulikuwa na Corona kwa hivyo ikabidi yasubiri.

Darasa lilianzia kwenye uwanja wa ndege wa Dubai wenyewe, ama kwa hakika tuliosha macho haswaa kwa namna watu walivyokuwa wengi na hakukuwa na mtu anapoteza muda, tukapokelewa na majengo yaliyojengwa kwa ubunifu mkubwa na yenye mvuto wa aina yake kutoka uwanja wa ndege mpaka hotelini. Jamani ni kuzuri mashallah yaani barabara, madaraja ya juu, majengo na njia ya treni ya umeme vyote vilikuwa na mvuto wa aina yake.

Kiutamaduni tulichojifunza wageni ambao wametumia fursa ya kufanya kazi Dubai na namna walivyo serious na kazi.

Basi bwana, kesho yake sasa safari kuelekea Expo ilianza na tulifanikiwa kuingia salama kwenye geti la maonesho, binafsi sikuwa nimewahi kuhudhuria maonesho makubwa kiasi hicho ambayo yalifanyika kwa miezi sita na Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizoshiriki kwa kipindi chote hicho. Ndani ya lile eneo labda utumie mwaka mzima ndio unaweza kupamaliza, uwekezaji uliofanyika ilikuwa pia darasa tosha na hizi ndio fursa zinazopatikana katika fani yetu hii ya uandishi.

FB_IMG_1673556204805.jpg

Anna akiwa katika mitaa ya Dubai.

Tukiwa Dubai tulifanikiwa na wenzangu Joakim Kapembe (marehemu), Vumilia Mwasha na wenzetu wa nyuma ya camera tukaruka live kupitia Jambo Tanzania mara kadhaa, tukarekodi vipindi maalumu kikiwemo Lulu za Kiswahili, Wekeza Tanzania na tuliandika ripoti na kuja live kwenye Aridhio, kusema ukweli tulihakikisha kila kilichofanyika kwenye banda letu tunakirusha tena kwa ufanisi mkubwa kabisa.

Uandishi na utangazaji una utamu wake bwana, tulitembea na kununua bidhaa kwenye malls.

Ninavutiwa na Dunia ya Kiswahili
Bado naendelea kuzungumzia vipawa na namna ya kujiongezea thamani, na leo nawaambia chagua vitu vichache unavyovimudu vyema halafu vifanye kwa ufanisi. Binafsi miongoni mwa maeneo niliyoyachagua ambayo yananivutia ni Dunia ya Kiswahili.

Nakumbuka mwaka 2014 mtayarishaji mkuu wa Lulu za Kiswahili Victor Eliah alinifuata na kuniambia Anna uwe mtangazaji mwenzangu wa Lulu za Kiswahili akasisitiza naamini kitakuwa miongoni mwa vipindi bora kuwahi kutokea. Nikamwambia sawa, ingawa hekaheka zikanifanya nisianze mwaka huo na Victor na Flora Mwano wakaendelea na kipindi. Mwaka 2015 nikaungana nao kwenye Lulu za Kiswahili na baadae wakaja Godfriend Mbuya na Swaumu Mavura. Ila sisahau kumtaja Shaaban Kissu na Victor ambao walianza kipindi hicho siku za nyuma zaidi.

Basi bwana miongoni mwa vipindi vilivyonifanya nikue, nikutane na watu wengi muhimu na niende maeneo mengi ikiwemo nje ya Tanzania ni hiki na naamini siku moja mimi na wenzangu historia itatutaja na kutambua mchango wetu katika lugha yetu adhimu ya Kiswahili.

Kupitia LULU ZA KISWAHILI tumeshiriki na kuandaa makongano ya Kiswahili yaliyokutanisha pamoja washititi wa lugha ya Kiswahili na pengine nikutajie machache tu:

1. Kongamano la Idhaa za Kiswahili Duniani - Arusha 2022
2. Kongamano la miaka 61 ya uhuru wa Tanganyika sasa Tanzania Bara
3. Kongamano la Siku ya Kiswahili Ubalozi wa Marekani
4. Kongamano la Kiswahili Makerere Uganda na Chambogo.

Kupitia Kiswahili pia mimi ni miongoni mwa washiriki walioandika historia ya Tanzania katika maandimisho ya kwanza ya Siku ya Kiswahili 07/07/2022 katika kituo cha mikutano cha kimataifa cha JNICC.

Sasa kwanini nimesimulia hii, najua vyumba vya habari vya Afrika waandishi wanafanya karibu kila kitu yaani kuandika, kupanga habari, kuandika habari za vitu karibu vyote, kuandika kwenye mitandao ya kijamii, sisemi ni kitu kibaya ila natamani pamoja na kujua vingi hebu chagua vichache na uvifanyie kazi kwa umahiri.

Hatimaye leo miaka 15 kamili imetimia tangu nilipoanza kuhudumu TBC na katika tasnia ya habari, imetimia huku hesabu zangu za mafanikio kwenye fani zikiwa sawa, namshukuru sana mwenyezi Mungu na naomba anijalie uzima nitimize ndoto kubwa zaidi zangu na za TBC.

Kama Kaimu Mhariri Mkuu

Sasa baada ya kutoa uzoefu wangu kwa takribani wiki mbili hivi, leo kipekee nizungumze nami kuhusu jambo kubwa zaidi nililopata kwa kipindi hiki cha miaka 15, namshukuru Dkt Ayub Rioba Chacha mwalimu wa wengi kwa kuona nafaa kuhudumu katika nafasi ya Kaimu Mhariri Mkuu wa TBC, ni nafasi iliyobeba majukumu mazito sana katika Idara ya Habari na matukio.

FB_IMG_1673553766234.jpg

Anna

Kwa miaka miwili na miezi sita niliyohudumu nikiri nimejifunza mengi na naendelea kujifunza sana, ni uzoefu wa kipekee maana unenifanya nimekua kila mahali, nimekuwa dada, rafiki, mama wa wengi katika Idara na imenifanya nijitambue zaidi hata katika maisha yangu binafsi na nashukuru pia nimepata uzoefu wa kuwa sehemu ya mabadiliko makubwa yaliyotokea kwenye idara.

Kwa dhati ya moyo wangu ni matamanio yangu kuona Idara ya Habari inakua, waandishi wanakua na wanatimiza ndoto zao, siku zote nimetamani kuwa daraja la mafanikio.

Shukrani

Nashukuru sana nimejifunza mengi kwenu pia wakati wote wa simulizi hii na niwaambie kama nikiulizwa miongoni mwa mambo nina mahaba nayo hapa Duniani ni tasnia ya habari, miongoni mwa waliochagua kazi za ndoto zao basi ni mimi. Naamini mmejifunza pia kupitia simulizi hii.

Kipekee leo unganeni na mimi kusherehekea miaka 15 tangu nianze kazi, ni jambo kubwa sana kwangu. Niambieni chochote kwenye ukurasa wangu.

MWISHO WA SIMULIZI
 
Hongera sana kwa huyu Binti Anna Mwasyoke kwa namna anavyofanya kazi yake kwa passion ya hali ya juu na kwa ufanisi mkubwa.

Huyu binti kutoka Mbeya Kata ya Ulenje, Kijiji cha Irambo, kabila la Wasafwa ni mfano wa kuigwa na wanahabari wengine
 
Hongera sana kwa huyu Binti Anna Mwasyoke kwa namna anavyofanya kazi yake kwa passion ya hali ya juu na kwa ufanisi mkubwa.

Huyu binti kutoka Mbeya Kata ya Ulenje, Kijiji cha Irambo, kabila la Wasafwa ni mfano wa kuigwa na wanahabari wengine
Acha ukabila mkuu! Ila Yuko vizuri na nimempenda alivyo maintain natural color yake, Kuna mwingine anaitwa kisa mwaipyana Yuko channel ten alianza kutangaza akiwa black beauty ila sasa ivi ni mzungu
 
Hongera sana kwa huyu Binti Anna Mwasyoke kwa namna anavyofanya kazi yake kwa passion ya hali ya juu na kwa ufanisi mkubwa.

Huyu binti kutoka Mbeya Kata ya Ulenje, Kijiji cha Irambo, kabila la Wasafwa ni mfano wa kuigwa na wanahabari wengine
Kumbe ni wa huko?

Basi hafai kuoa
 
Ila nadhani TBC ya Tido Muhando na Yao tofauti ni kubwa sana maana hii Yao Haina vipindi vizuri hata watazamaji sidhani kama ni wengi
 
Hongera sana dada Anna Mwasyoke

Ninakutakia kila la heri ,afya tele na busara zaidi aaamin aaaamin

SiempreJMT
 
Mbona hajasimulia kuhusu mahusiano ya kimapenzi?
hata mimi nimeshangaa,kwamba muda wote ni kazi tu hunyanduani??hujaolewa??huna mtoto??nami ni mwana habari mwenzako wa Makerere University Degree ya kwanza lakini sijawahi ku-practise mambo ya habari(Mass Communications) maana kwenye Masters na PhD nilibadili field kabisa
 
Back
Top Bottom