Hoseah alonga
na Mwandishi Wetu
Tanzania Daima~Sauti ya Watu
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Dk. Edward Hoseah, ameamua kueleza kile kinachousononesha moyo wake.
Akizungumza wiki hii jijini Dar es Salaam, Dk. Hoseah alisema anaumia sana moyoni kutokana na watu wengi kumhusisha na kashfa za ufisadi.
Alibainisha kuwa, kinachouumiza sana moyo wake ni jamii kutompa sifa stahiki kutokana na juhudi anazotumia kupambana na rushwa nchini.
Mimi nitafaidika nini na ufisadi? alihoji Dk. Hoseah wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Hoteli ya Blue Pearl mapema wiki hii.
Nasikitika kuwa watu wanaonekana kukata tamaa mapema
lakini wanapaswa kufahamu kuwa kazi hii (ya kupambana na rushwa kubwa) ni ngumu na TAKUKURU ni chombo kinachojijenga hivi sasa, aliongeza.
Dk. Hoseah alieleza masikitiko yake hayo baada ya kurushiwa swali na Mwenyekiti wa wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), Reginald Mengi, aliyemtaka kueleza taasisi anayoiongoza imefanya nini hadi hivi sasa kukabiliana na rushwa nchini.
Katika maelezo aliyoyatoa kabla hajauliza swali hilo, Mengi alibainisha kuwa wananchi wengi wamepungukiwa na imani na chombo hicho kutokana na masuala mawili.
Kwanza, alisema, wananchi wengi wana shauku kubwa ya kufahamu au kuona kilichofanyika dhidi ya watu wanaotajwa kuhujumu nchi na mafisadi.
Pia, Mengi alisema wananchi wengi hawajui kwa uhakika muda unaotakiwa kwa taasisi kama TAKUKURU, kuchunguza tuhuma za rushwa kubwa na kuchukua hatua.
Kauli hii ya Mengi, bila shaka ni mwendelezo wa malalamiko kutoka katika jamii, ambayo inaonekana kukatishwa tamaa na kasi ndogo ya kuwashughulikia wala rushwa wakubwa na mafisadi nchini.
Dk. Hoseah, tumekupa imani kwa miaka miwili, tunaamini kuwa sasa ni wakati wa kuona matunda. Tukiona mwaka wa tatu unakatika, utakuwa umetuangusha na kifo chetu kitakuwa cha mende, alisema Mengi.
Mengi alisema kutokana na shauku hiyo, Watanzania hivi sasa wanatarajia kumuona Dk. Hoseah mpya na akaahidi kuwa MOAT na vyombo vya habari vitampatia ushirikiano wa kumwezesha kuyatekeleza majukumu yake vema.
Huko nyuma tulikuandika vibaya kwa sababu zile mbili. Sasa tunakupa muda wa kupumua tukisubiri kazi yako, alisema Mengi na kumuonya kuwa iwapo watu hawataona matunda ya kazi hizo, wanaweza kuanza kumwandika tena vibaya.
Akijibu hayo, Dk. Hoseah alifafanua kuwa kazi ya kupambana na rushwa kubwa, si rahisi kama watu wengi wanavyofikiria.
Aidha, alisema kuwa ni vema kwa taasisi kama TAKUKURU, kuwa na uhakika wa kile inachokifanya, hasa kufikia maamuzi ya kumfikisha mtu mahakamani kwa tuhuma za rushwa kubwa.
Alisema ni aibu kwa TAKUKURU kukurupuka na kumfungulia mtu mashitaka, lakini mahakama ikamwachia kutokana na kutokuwepo kwa ushahidi wa kutosha kumtia hatiani mtu huyo.
Dk. Hoseah alisema utaratibu wa uchunguzi unaondeshwa na taasisi yake unahusisha pia taasisi nyingine, kama vile Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kabla uamuzi wa kuifikisha kesi mahakamani haujafikiwa.
Aidha, Dk. Hoseah alibainisha kuwa sheria inamzuia kutangaza kesi ambazo TAKUKURU inazishughulikia, na hii inaweza kuwa sababu moja ya wananchi kudhani kuwa taasisi hiyo haifanyi lolote kushughulikia rushwa kubwa.
Lakini sisi TAKUKURU tumejiwekea malengo na kutokana na utendaji tunakamilisha malengo yetu. Kwa mfano, tumejiwekea malengo ya kukamilisha upelelezi wa kesi kumi za rushwa kubwa kila mwaka.
Ilipofika katikati ya mwaka huu tayari tulikuwa tumekamilisha uchunguzi wa kesi tano na majalada yake tuliyafikisha kwa DPP.
Baada ya kuyapitia, DPP ameturudishia majalada mawili kwa ajili ya kuyafanyia marekebisho
lengo letu ni kuhakikisha kuwa hadi mwisho wa mwaka tunakamilisha kesi kumi tulizojipangia, alisema.
Alibainisha kuwa urasimu huu, pamoja na ugumu wa kufuatilia masuala ya rushwa kubwa, ambayo mara nyingi yanahusisha pia tasisi za nje ya nchi, ndivyo vikwazo vinavyowafanya Watanzania wasijue kinachoendelea ndani ya taasisi hiyo.
Lakini aliwataka Watanzania kuwa wavumilivu na kuipatia TAKUKURU ushirikiano kwani kazi inayofanyika ni kubwa na itazaa matunda mazuri.