Alibaba na wezi 40

SEHEMU YA KUMI

07014989.png

Kutoka sehemu ya tisa:

Baada ya mpango wa mwizi wa kwanza kufeli, ikatokea mwizi wa pili kwenda kujaribu kuitafuta nyumba ya Kassim. Kwa utaratibu uleule, mwizi wa pili alimlipa Mustafa dhahabu ili apate msaada wa kupelekwa kwenye hiyo nyumba. Sasa safari hii mwizi wa pili aliweka alama ndogo sana nyekundu ambayo si rahisi kwa mtu kuiona na kwa furaha kabisa akarudi msituni kwenda kutoa taarifa kwa kiongozi wao.

Endelea sehemu ya Kumi.


Jioni ile, Marjane alikuwa akiandaa chakula cha jioni kwa aajili ya familia ya Alibaba na wenzake nyumbani. Aliandaa nyama ya kuku, kachumbari na mchanganyiko wa mbogamboga mbalimbali, alipomaliza kuandaa mchuzi ule wa kuku na mbogamboga akaanza kuandaa upishi wa wali, alichukua sufuria na kuweka maji kiasi, kisha akaweka sufuria hiyo kwenye jiko. Baada ya hapo alienda mpaka stoo kuchukua mchele ili aweze kuchambua na kuusafisha kabla ya kuutosa kwenye maji, kwa bahati mbaya sasa, akakuta mchele hakuna.

35667032.png

“Itabidi tu niende kununua mchele” alijisemea moyoni. Marjane akachukua kapu lake la sokoni na kuelekea mjini sokoni.

Alipokuwa akirudi aliona alama ndogo nyekundu kwenye fremu ya dirisha, macho ya Marjane yalikuwa mazuri sana, hakuwa na matatizo ya macho hata kidogo.

“Hii alama haikuwa hapa kabla” Marjane alijisemea moyoni. “Mara ya kwanza alama nyeupe, na mara hii tena alama nyekundu!! Vizuri sana! Nitafanya kama nilivyofanya mara ya kwanza.”

Aliingia ndani na kwenda kuchukua chaki nyekundu. Kisha akarudi nje na kuweka alama nyekundu katika kila fremu ya dirisha kwenye nyumba zote za mtaa ule.

“Hii lazima imchanganye huyu aliyeweka ile alama nyekundu pale.” Alijisemea huku akicheka. Kisha akarudi nyumbani kuendelea kuandaa chakula cha jioni, lakini hakumwambia yeyote kuhusu alama ile nyekundu.

Yule mwizi aliyeweka ile alama nyekundu alifika msituni, alipowakaribia wezi wenzake akaanza kupiga kelele za furaha, “Nimeiona! Nimeipata nyumba ambayo suti ya marehemu ilishonwa!!”

Kiongozi wao alimfurahia sana. “Umefanya kazi nzuri!” Alisema. “Umefanya kazi muhimu sana! Sasa tunaweza kumpata aliyetuibia dhahabu zetu.”

“Nilienda mpaka kwa fundi nguo, Mustafa.” Mwizi alisema kwa kujisifu. “Alikubali kunisaidia kama ningempa dhahabu. Nikamfunga macho na kitambaa kama alivyofanya awali, na akanipeleka mpaka kwenye hiyo nyumba. Nikaweka alama ndogo sana nyekundu kwenye fremu ya dirisha ili tuweze kuipata hiyo nyumba tena.”

Wezi wakampigapiga mgongoni kama ishara ya kumpongeza huku wakishangilia. Kisha kiongozi wao akasema, “Nipeleke huko sasa hivi.”

Hivyo basi, wawili hao wakaondoka kuelekea mjini. Baada ya kufika tu mwizi mmoja akamuonesha mkuu wake nyumba ambayo kwenye dirisha kuna alama nyekundu kwenye fremu.

“Hii hapa sasa!” mwizi alimwambia mkuu wake. “hii ndiyo nyumba yenyewe! Unaona alama nyekundu kwenye fremu ya dirisha?”

Kiongozi wa wezi alienda mpaka karibu na kuiangalia alama ile.

“Ndiyo, naiona! alijibu mkuu wa wezi. “pia naona kuna alama kama hii katika fremu ya dirisha katika nyumba ile, na ile pia! Na ile na ile! Kwanini alama hiyo ipo kila dirisha katika nyumba za mtaa huu? Nani atakuwa ameziweka hizo?”

“sijui, “ alisema mwizi yule akiwa hana furaha tena. “Mimi niliweka alama kwenye dirisha moja tu”

“wewe ni mjinga wa pili!!” alifoka mkuu wao. “haya haraka sana turudi msituni!!”

Asubuhi iliyofuata, kiongozi wao aliwaita wezi wote katika eneo lao la kukutana.

“Wawili wenu walishindwa kuitafuta nyumba tunayoihitaji” aliwaambia. “Sasa nitakwenda na kuitafuta nyumba mimi mwenyewe. Nisubirini hapa”

Hivyo basi, kiongozi wao akaondoka kuelekea mjini mwenyewe. Akaonana na Mustafa katika kibanda chake, akampa sarafu ya dhahabu. Mustafa akamuongoza kiongozi huyo wa wezi kulekea kwenye ile nyumbaya Kassim.

Kama kawaida alivaa kitambaa kufunika macho, na kwa kutumia msaada wa harufu na sauti mbalimbali, Mustafa alifanikiwa kumfikisha kiongozi wa wale wezi mpaka kwenye ile nyumba.

“Nasikia harufu ya maua mazuri sana, natumaini hapa ndipo mahala penyewe.” Alisema Mustafa.

15265345.png

“Sitaweka alama yoyote ya chaki,” kiongozi yule alijisemea moyoni. “Alama za chaki zote zilizowekwa hazikuweza kufaa kabisa hapo kabla. Nitaitizama nyumba hii kwa umakini kabisa na kukariri kila kitu ili niweze kukumbuka ninachokiona.

Hivyo basi, Kiongozi yule aliangalia madirisha mazuri ya nyumba ile, pia aliangalia milango iliyopakwa rangi ya samawati na mapazia mekundu yaliyoning’inizwa kwenye madirisha. Aliangalia mimea mirefu iliyopandwa ndani ya mitungi mikubwa meupe na paka wa rangi ya machungwa mwenye macho ya njano akiwa kwenye dirisha akimtazama.

Baada ya kuangalia yote hayo, alimchukua mzee Mustafa na kumrudisha kwenye kibanda chake kisha akarudi msituni kuonana na watu wake.

“ninaifahamu nyumba ile sasa,” Alisema alipofika. “Hatuwezi kuamini alama za chaki tena, hivyo nitaamini kumbukumbu yangu. Nimeangalia kwa undani sana ile nyumba, ina madirisha mazuri sana na milango ya nje iliyopakwa rangi ya samawati, pia kuna mapazia mekundu kwenye madirisha. Nje kuna mimea mirefu iliyopandwa katika mitungi mikubwa yenye rangi nyeupe na kuna paka wa rangi ya machungwa mwenye macho ya njano anaishi humo. Itakuwa rahisi sana kuipata hiyo nyumba.”

“Sasa tunaweza kumpata mtu aliyetuibia dhahabu zetu,” kiongozi aliendelea kusema. “Na lazima tumuadhibu! Lakini kwanza, lazima tuingie ndani ya nyumba ile. Nina mpango. Tutaenda huko usiku wa leo. Njooni hapa karibu, vijana wangu, na nisikilizeni kwa makini kabisa.”

Wezi wote wakasogea karibu kusingia mpango wa kiongozi wao.

“Mtajua wenyewe mjipange vipi,” Kiongozi wao alianza kuwaambia. “Nendeni mjini na kiasi cha kutosha cha dhahabu. Jaribuni kupita kila sehemu ambayo kuna wafanyabiashara wakubwa wakubwa ambao wanatumia punda katika kazi zao. Jaribuni kuongea nao wawauzie punda, hakikisheni mnanunua punda ishirini na mniletee hapa msituni.”

Baada ya hapo wezi wakachukua kiasi cha kutosha cha dhahabu na kulekea mjini.
 
SEHEMU YA KUMI NA MOJA

WEZI THELATHINI NA TISA


Kutoka sehemu ya kumi:

Baada ya mpango wa mwizi wa pili kufeli, sasa kiongozi wa wezi akaamua kutumia mbinu zake mwenyewe kwenda kuitafuta nyumba ya Kassim, na hatimaye akaipata. Sasa kiongozi wa wezi akapanga mpango wa kwenda kwa Alibaba.....

Endelea sehemu ya Kumi na moja.


Wezi walipofika mjini wakaanza kazi ya kutafuta punda kama walivyoagizwa na kiongozi wao.

“Ishirini? Unahitaji punda ishirini?” aliuliza mtu mmoja kwa mshangao.

“Ndio, hivyo ndivyo nilivyosema, ishirini,” mwizi alijibu.

“vizuri, sina punda ishirini,” alijibu yule mtu, “lakini nitakuuzia wawili. Wako kwenye uwanja wangu, nyumba ya nyumba. Njoo nikuoneshe.”

Wezi walikuwa wakifuata mpango mzima wa kiongozi wao. Kwanza, walizunguka mji mzima kutafuta wenye punda. Wenye punda walipooneshwa sarafu za dhahabu kwenye mikono ya wezi wale, wengi wao walifurahi sana na kutaka kuwauzia.

54302708.png

Mwisho wa wiki ile, wezi wote walinunua punda wote ishirini kama walivyoagizwa na kiongozi wao. Punda wakubwa, punda wadogo na waliozeeka, wenye rangi ya kijivu, weusi na weupe.

“Hivi kwanini kiongozi wetu anataka punda hawa?” mwizi mmoja alimuuliza mwenzie. “amechanganyikiwa nini?”

“Mh! Sijui..” mwizi wa pili alijibu. “sisi tufanye tu kama alivyotuagiza.

Wakati wezi wakiwa mjini wakinunua punda, kiongozi wao alikuwa akitembelea kwa watengeneza vyungu na mitungi nje ya mji kidogo. Fundi mmoja alikuwa akipaka rangi katika mtungi mmoja mkubwa uliotengenezwa kwa udongo wa mfinyanzi.

“Unahitaji mtungi, rafiki yangu?” aliuliza mtengeneza mitungi.

“Ndiyo nahitaji.” Alijibu kiongozi wa wezi. “lakini nahitaji unitengenezee mitungi mikubwa arobaini ya kuwekea mafuta. Yote lazima iwe na mifuniko, lakini mifuniko hiyo isiwe yenye kukaza sana wakati wa kufunika mitungi. Mitungi lazima iwe imekamilika ifikapo mwisho wa wiki hii. Ni muhimu sana!”

Mtengeneza mitungi akamuangalia sana kiongozi wa wale wezi. “Wiki moja haitoshi kutengeneza mitungi yote arobaini.” Alimjibu. “Sina uhakika kama naweza kuifanya kazi hii.”

“ukiweza, nitakulipa mfuko mzima wa dhahabu,” alisema yule kiongozi wa wezi. Akanyanyua lile fuko la dhahabu juu kisha akanyanyua upanga wake mkali juu. “lakini usipoifanya kazi hii, unajua mwenyewe kitakachotokea.”

Mtengeneza mitungi akatikisa kichwa kwa ishara ya kukubali na haraka sana akaanza kuifanya ile kazi ya kutengeneza mitungi arobaini.

“nitamuomba kaka yangu anisaidie,” mtengeneza mitungi alijisemea moyoni. “ na shemeji yangu pia atanisaidia. Kama tukifanya kazi hii kwa juhudi, natumaini tutaimaliza ndani ya huu muda wa wiki moja.”

Baada ya wiki moja mitungi ile ilikuwa tayari, kiongozi wa wezi akaenda kwa muuza mafuta mkubwa sokoni na kujaza mtungi mmoja mafuta. Kisha akamtuma mmoja wa wezi akawalete wale punda ishirini aliowanunua.

Kiongozi wa wezi akapakia kwa kila punda mitungi miwili miwili. Kisha akawapeleka mpaka kule msituni kukutana na wezi wengine waliobakia huko.

“Sasa ni sehemu ya pili ya mpango wangu,” alisema kiongozi wa wezi. “Kila mmoja wenu aingie ndani ya mtungi mmoja.”

“Tuingie kwenye mitungi? Kwanini?” aliuliza mmoja wa wezi . “Na tutapumuaje?”

“mifuniko yake haikazi sana.” Alijibu kiongozi wa wezi. “Msihofu – mtaweza kupumua. Chukueni panga zenu na ngao muingie nazo ndani ya mitungi kwasababu zina kazi yake maalumu huko. Tutaenda kwenye ile nyumba mkiwa nyote thelathini na tisa ndani ya mitungi thelathini na tisa.”

“Na vipi kuhusu huo mtungi wa arobaini? Utaingia wewe?” mmoja aliuliza.

“Hapana!” alijibu kiongozi wao. “Nitavaa mavazi ya kuficha uso na nitawaongoza punda wote mpaka huko. Huu mtungi wa arobaini umejaa mafuta – ni moja ya mpango wangu, nitajifanya ni muuza mafuta. Nitawaongoza punda wote mpaka kwenye nyumba ambayo Mustafa alinionesha. Nitawaomba watu wa nyumba ile kama watanipa msaada wa kulala usiku mmoja kwasababu niko kwenye safari ndefu na ninapoelekea ni mbali sana. Kisha akiniruhusu tu na kunipa nafasi ya kuwaingiza punda hawa ndani, sasa itakuwa ni nafasi yenu nzuri ya kujitokeza na kumaliza kazi. Hapo atajuta kutuibia mali zetu.”

Baada ya kusema hayo kila mwizi alichukua upanga na kuingia ndani ya ile mitungi.

Kiongozi akavaa mavazi ambayo uso wake hauwezi kuonekana vizuri, kisha akaanza safari ya kuelekea mjini na punda ishirini waliobeba mitungi arobaini.

Muda ambao alikuwa ameshafika mjini, tayari giza lilikua limeshaanza kutanda.

94430394.png



Muda mfupi tu akafika katika nyumba ile yenye maua mazuri na paka wa rangi ya machungwa. Kulikuwa na mtu aliyekaa kwenye stuli nje ya nyumba hiyo. Alikuwa akitazama watu wanaopita njia na akisikiliza sauti za ndege mbalimbali wakiwa wanatoa sauti za kujibembeleza kwaajili ya kulala.

Kiongozi wa wezi alipomuona yule mtu nje, alisimamisha punda wake wote.

“Habari ya saa hizi.” Kiongozi alimsalimia Alibaba.

“Nzuri,” alijibu Alibaba kwa hali ya kushangaa na kusimama kwa kuheshimu mgeni. “Naitwa Alibaba. Naweza kukusaidia nini rafiki yangu?”

“Mimi ni muuza mafuta, natokea mbali sana.” Alijibu yule kiongozi wa wezi. “Punda wangu wamechoka sana na hata mimi vilevile. Tunaweza kukaa kwako usiku huu tu kisha kesho asubuhi tutaondoka. Hatutakuwa na usumbufu wowote tafadhali.”

“Umesema wewe ni muuza mafuta. Mafuta hayo yako wapi?” aliuliza Alibaba kutaka kuhakikisha kwamba yule mtu ni mkweli.”

Yule kiongozi wa wezi akamuoneshea kwenye ule mtungi ambao alijaza mafuta. “Yapo kwenye mitungi hii, ni mafuta bora na mazuri sana kuliko ya aina yoyote ile. Ungependa kuyaona?”

Akafungua mfuniko wa ule mtungi wenye mafuta na Alibaba akachungulia ndani yake. Kisha akanyanyua macho kumtazama kiongozi na kutabasamu.

“Karibu sana ndani ukae,” alisema Alibaba. “ Walete punda wako uwani huku.”

“Ahsante sana. Una roho nzuri sana,” alisema kiongozi wa wezi. Kisha akawaongoza punda wale mpaka ndani.

“Naona pia punda hawa wanahitaji chakula na kupumzika,” Alibaba alimwambia kiongozi wa wezi. “Watue hiyo mizigo yao chini na wapeleke kwenye zizi. Wape nyasi huko na maji ya kutosha.”

Hivyo kiongozi wa wezi akashusha ile mitungi na kuwapeleka punda kwenye zizi. Akaiacha ile mitungi arobaini kwenye uwanja wa ndani wa nyumba ikiwa imepangika kwa mstari mmoja.

“Unaweza tu ukaiacha mitungi hii hapo uwanjani haina neno kwa usiku mmoja,” alisema Alibaba. “Twende ndani nikakupatie chochote ule ili upumzike.”

Akamkaribisha yule kiongozi wa wezi ndani na kumuita Marjane mtumishi wake.

“Mke wangu yuko wapi?” Alibaba alimuuliza Marjane.

“Wameenda kulala. Wote na mwanao pia leo wameingia ndani kulala mapema sana.” Alijibu Marjane.

“Sawa basi, Marjane. Mtengenezee chakula huyu mtu, tafadhali.” Alisema Alibaba. “Ni mgeni wetu na ni vema tukamkirimu.”

Marjane akavuta pumzi za kuonekana kuchoka. Alikuwa ameshachoka na kazi za siku ile na alikuwa anajiandaa kwenda kulala.

“Sawa bosi,” Alijibu Marjane na kuelekea jikoni. Muda mfupi tu chakula kilikuwa tayari.

Kiongozi wa wezi alikula vizuri sana usiku ule, Marjane alimuandalia wali wa njegere na nyama na alifaidi sana chakula kile.

92234655.png

“Mpango wangu unaenda vizuri sana.” Alijisemea moyoni. “Muda si mrefu Alibaba atakuwa mtuhumiwa wangu.”

Alibaba akaingia jikoni wakati Marjane akiosha vyombo vilivyotumika usiku ule.

“Naenda kulala sasa,” alimwambia. “Marjane, tafadhali hakikisha mgeni wetu anapata kila kinachohitajika. Asubuhi nitenda mapema sana kuoga hivyo nitahitaji sabuni na taulo.”

Hivyo Marjane akaenda kumchukulia sabuni na taulo na Alibaba akaenda kulala. Kiongozi wa wezi akamwambia Marjane kwamba angependakupata hewa safi ya nje kidogo kabla ya kwenda kulala.
 
SEHEMU YA KUMI NA MBILI

MARJANE NA MAFUTA

Kutoka sehemu ya kumi na moja:

Kiongozi wa wezi afanikiwa kuingia katika nyumba ya Alibaba na kutokana na mbinu zake Alibaba alimkaribisha kwa ukarimu kabisa na kupata chakula ch ausiku pamoja kwa furaha sana. Sasa alibaba na familia yote inaingia ndani kulala ila kiongozi wa wezi anaamua kuomba ruhusa ya kutoka uwani ili kupata hewa safi ya nje kidogo kabla ya kwenda kulala................

Endelea sehemu ya Kumi na mbili.


Kiongozi wa wezi akatoka nje mpaka uwani. Akasimama mlangoni kwa muda kidogo na akavuta pumzi, kisha kwa taratibu akaanza kuangalia huku na huku ili kuhakikisha kwamba hakuna mtu yeyote anayemtizama. Mbele yake ilikuwa ni ile safu ya mitungi yake aliyokuja nayo ambayo mifuniko yake ilikuwa iko wazi kidogo na ndani yake kuna wezi na walikuwa wamekaa kimya sana.

Akasogea karibu na mtungi wa kwanza, akainama kidogo kisha akaugonga pembeni kwa ishara ya kumuita aliye ndani yake, kisha akafungua mfuniko na kumnong’oneza mwizi wa kwanza kwenye ule mtungi.

“Sikiliza kwa makini!” alimwambia. “Hii ni sehemu inayofuata ya mpango wangu. Ukifika muda wa mashambulizi, nitarusha vijiwe kutoka katika dirisha la chumba nitakacholala. Vitaangukia huku uwani, mkivisikia tu tokeni na panga zenu na mkiwa tayari kushambulia. Nitakuja na mimi kuungana na nyinyi na kisha mwishowe tutamuua huyu Alibaba mwizi wa mali zetu!!”

Yule kiongozi wao alienda kwenye kila mtungi na kuugonga pembeni ili kumuita aliye ndani yake na kumwambia maneno yale yale kama aliyomwambia mwizi aliye kwenye mtungi wa kwanza. Kisha katabasamu na kupangusa mikono yake. Mpango ulikua unaenda vizuri sana.

Akaokota baadhi ya vijiwe na kuviweka mfukoni mwake kisha akarudi ndani ya nyumba na kumuita Marjane.

“Nakwenda kulala sasa,” alimwambia. “Nimechoka sana.”

“Nitakuonesha chumba cha kulala kilipo.” Marjane alijibu.

Marjane akaweka vyombo vyake alivyokuwa akimalizia kuosha na kufuta mikono yake. Kisha akawasha mshumaa na kumuongoza kiongozi wa wezi juu ghorofani kwenye chumba chake. Akafungua mlango na kumkaribisha ndani.

“Natumai utakaa kwa faraja humu.” Alisema Marjane. “Je, kuna chochote kingine utakachohitaji?



“Hapana, Marjane. Nina furaha sana kulala katika kitanda hiki kizuri hivyo nadhani sihitaji kitu kingine. Nashukuru sana!.”

“usiku mwema,” alijibu Marjane. Kisha akarudi jikoni. Akaamua amenye vitunguu na karoti aviweke kwenye sufuria kwaajili ya mlo wa kesho kabisa. Lakini alipochukua kisu tu aanze kumenya mara giza likatanda jikoni.....

“Oooh, chemli imeisha mafuta,” Marjane alijisemea. Hivyo akachukua mshumaa na kwenda kwenye kabati. Kulikuwa na unga mwingi wa kutosha, mchele na sukari. Lakini kopo la mafuta lilikuwa tupu.

Marjane akavuta pumzi ya kuonesha kuchoka na hali ile ya kukosa mafuta ya kuwashia taa. “Nifanye nini sasa?” alifikiria. “ni usiku sasa maduka yote yamefungwa.

Kisha kapata wazo.

“Kuna mitungi arobaini ya mafuta nje!” alijisemea. “nina uhakika mgeni wetu hawezi kuchukia endapo nitachukua japo kidogo tu kwaajili yakuwashia taa pale nitakapomwambia kesho.” Kisha akachukua kopo la mafuta na mshumaa kisha akaelekea uwani kwenye ile mitungi arobaini. Alipofika akaenda kwenye mtungi wa kwanza uliokuwa karibu naye na kuanza kufungua taratibu mfuniko. Mara akasikia sauti itokayo ndani ya mtungi.

“Vipi muda tayari tutoke kwaajili ya mapambano?” sauti iliuliza kutoka kwenye mtungi.

Marjane alishtushwa na hali ile yenye kushangaza. Akasimama imara na kukaa kimya kwa umakini kabisa.

89023929.png

“Nifanye nini sasa?” alifikiria. “Kuna mtu kwenye huu mtungi wa mafuta!! Nadhani amekuja na huyu mgeni wetu muuza mafuta. Na sasa yuko tayari kwaajili ya mapambano, nafikiria bosi wangu Alibaba yuko hatarini, lazima nimuokoe.”

“Bado – ila muda mfupi tu nitawajulisha!” marjane alimjibu yule mwizi aliye ndani ya mtungi. Alitumia sauti ya kukaza ili ifanane na ya kiume kama ile ya muuza mafuta. Kisha akaenda kwenye mtungi unaofuata na mambo yakawa ni yaleyale kama ya kwenye mtungi wa kwanza. Kisha akaenda mtungi baada ya mtungi na maswali ya wezi yalikuwa ni yaleyale na majibu ya Marjane yakawa ni yaleyale. “Bado – ila muda mfupi tu nitawajulisha!”

Alipokwenda kwenye mtungi wa arobaini, kulikuwa kimya, hakuna sauti iliyouliza, “Vipi muda tayari tutoke kwaajili ya mapambano?” Marjane akafungua mfuniko na kuangalia ndani ya mtungi akakuta kuna mafuta na kuamua kuchota kwaajili ya taa yake.

Alipokuwa akijaza kopo lake mafuta yale alikuwa akifikiria, “kuna watu thelathini na tisa katika mitungi hii, wako tayari kumshambulia bosi wangu! Yule mgeni ndani atakuwa ni kiongozi wao!”

Kisha Marjane akaamua kuwa na mpango wa kumuokoa bosi wake, Alibaba.

Aliporudi jikoni, aliwasha taa yake na kuchukua sufuria kubwa kabisa na kuliweka jikoni, kisha akamimina mafuta yaliyobaki kwenye kopo. Akarudi kwenye mtungiwa arobaini kwa mara ya pili na kujazalile kopo mafuta na kwenda kuyamimina katika lile sufuria kubwa lililopo jikoni likiwa linaanza kupata moto. Alifanya hivi mara kadhaa mpaka sufuria likajaa mafuta.

Mafuta yalipoanza kuchemka akalitoa kwenye jiko na kulipeleka uwani ilipo ile mitungi. Akafunua mtungi wa kwanza na kumimina yale mafuta ya moto kiasi cha kutosha, kisha kafanya hivyo hivyo katika kila mtungi.

89699079.png

Marjane akarudi jikoni na kumalizia kazi zake za kuandaa mboga ya kesho. Kisha akazima moto na taa.

“Leo siendi kulala,” alijisemea. “ Nitakaa hapa nione nini kitatokea.” Akakaa kwenye stuli karibu na dirisha akitazama uwani kwenye ile mitungi.

Kiongozi wa wezi alijilaza kitandani kwa muda na kusubiri. Alisubiri kwa muda mrefu sana. Baadaye akajisemea, “kwa muda huu kila mtu ndani ya nyumba atakuwa ameshalala.” Kisha akatoka kitandani na kuelekea dirishani, kisha kwa ukimya kabisa akafungua dirisha. Akaangalia uwani ilipo mitungi na kusikiliza. “Sioni taa yoyote,” alijisemea. “Na sisikii sauti yoyote, sasa nina uhakika kila mtu amelala humu ndani, na sasa ni hatua inayofuata ya mpango wangu. Nitarusha vijiwe kwenye ile mitungi, watu wangu wakisikia tu watatoka na kuanza mashambulizi kama tulivyopanga na kumkamata Alibaba!!”

Akachukua vijiwe alivyokusanya kabla ya kuja kulala na kuvijaza kiganjani na kuvirusha chini kwenye mitungi na akasikia sauti ya vijiwe vikiangukia kwenye ile mitungi. Alisubiri lakini hakuna chochote kilochotokea! Hakuna hata mwizi mmoja aliyetoka kwenye mtungi.

Kiongozi wa wezi akarusha tena vijiwe kiasi cha kujaza kiganja, vikaanguka tena chini na sauti akaisikia lakini kwa mara nyingine tena hakuna kilichotokea na wala hakuna jibu lolote.

Kiongozi wa wezi akaanza kuingiwa na woga sasa. Alihisi tu kuna kitu kimetokea.

Akawasha mshumaa na kushuka taratibu kulekea uwani kwenye ile mitungi yake, akafika kwenye mtungi wa kwanza kisha akafunua mfuniko kidogo.

“Uko tayari?” akauliza. “uko tayari kwa mapambano?” Hakuna jibu. Akajaribu kuvuta harufu. “nahisi harufu ya mafuta humu,” alijisemea. “mafuta ya moto!!”

Akafunua mfuniko wote na kuangalia ndani ya mtungi. Mwizi aliyekuwepo mle ndani ya mtungi alikuwa ameshakufa!!

82884604.png

Kiongozi yule wa wezi akaangalia katika kila mtungi kwa hasira na kukuta wezi wote wamekufa!

“Sijui nini kimetokea,” alifikiri. “Yaani watu wangu wote wamekufa, ina maana kuna mtu amegundua mpango wangu kwa kumshambulia Alibaba. Akaamua kuwaua! Sasa atakuwa nani kafanya hivi?? Alibaba mwenyewe?? Mke wake?? Oooh siko salama tena kwenye nyumba hii yaani nimebaki peke yangu, lazima nikimbie kuokoa maisha yangu.

Kiongozi wa wezi akaacha mitungi yote na punda wote na kuruka kwenye ukuta wa uwani, akakimbia mbio zote kwa kadiri awezavyo. Lakini hakumsahau Alibaba. Alikuwa na hasira sana na bado alihitaji kumuua.

Asubuhi iliyofuata, Alibaba aliamka mapema sana, akachukua taulo yake na sabuni. Kisha akashuka chini na kukuta mitungi ile bado ipo.

“Ajabu! Hii mitungi bado ipo hapa sasa hivi” alijisemea. “Lakini bado mapema sana labda muuza mafuta bado amelala.”

Kisha Alibaba akaondoka kuelekea bafuni. Hakujua lolote lililotokea usiku ule.
 
SEHEMU YA KUMI NA TATU

JIHADHARI SANA ALIBABA!!!



Kutoka sehemu ya kumi na mbili:

Marjane agundua siri ya kiongozi wa wezi, kwa ujanja wake afanikiwa kuwauwa wezi wote thelathini na tisa bila ya kumjulisha yeyote ndani ya nyumba na bila hata ya vurugu yoyote kutokea ndani ya nyumba. Kiongozi wezi agundua kwamba wenzake wote wameshauliwa bila ya yeye kufahamu, sasa atambua kwamba hayuko salama ndani ya ile nyumba na kwa siri aamua kutoroka kwa kuruka ukuta wa nyuma ya nyumba ile. Alibaba asubuhi sana anatoka nje kuelekea bafuni na kukuta mitungi bado ipo na mategemeo yake ni kwamba mgeni ataondoka mapema sana. Lakini Alibaba aliamini kwamba huenda mgeni bado amelala kutokana na uchovu wa safari .............

Endelea sehemu ya Kumi na tatu.


Alibaba alipotoka bafuni bado aliiona mitungi ile arobaini pale uwani na muda ulikuwa umeenda kidogo, akilinganisha kauli ya mgeni wake kwamba angeondoka asubuhi sana kuelekea kwenye safari yake ya kuuza mafuta.

“Marjane!” Alibaba aliita, “Mbona muuza mafuta bado hajaondoka?”

Marjane akatoka jikoni. “Nitakuelezea kila kitu bosi wangu.”Marjane alisema. “Lakini kwanza hebu angalia ndani ya mitungi hiyo.”

Alibaba alichanganyikiwa kidogo kusikia hivyo. Akasogea na kufunua mfuniko wa mtungi mmoja.

“Kuna mtu humu!” alisema kwa mshtuko. “Tena amekufa!!”

Aliangalia katika kila mtungi. “Watu thelathini na tisa waliokufa ndani ya mitungi na mtungi mmoja una mafuta kidogo! Kumetokea nini Marjane?”

“Kuna mtu anajaribu kukuua, bosi,” Marjane alijibu. “Kuna siku niliona alama nyeupe ya chaki kwenye mlango wa mbele wa nyumba yetu. Nikajua huenda kuna mtu ameweka alama hiyo kwa siri na pia nikajua tu kwamba kuna kitu kibaya kinaendelea, hivyo nikaamua kuweka alama kama ile katika kila mlango wa mbele wa nyumba zote za mtaani hapa.”

“Siku nyingine nikaona alama ndogo nyekundu kwenye fremu ya dirisha. Basi nikafanya vilevile katika nyumba za mtaani.”

“Sasa jana,” Marjane aliendelea kuelezea. “Muuza mafuta alikuja na punda wake ishirini na mitungi ishirini ya mafuta kama unavyojua bosi. Usiku wa jana ulipokuwa umelala, niliamua kuandaa chakula cha leo mchana kabisa, hivyo nilihitaji mafuta zaidi kwaajili ya taa ya chemni, hivyo nilienda kule uwani kwenye mitungi ili nichukue mafuta kidogo tu kutoka katika ile mitungi. Sasa nilipoenda kwenye mtungi wa kwanza ili nichukue mafuta. Nikaanza kufunua mfuniko wa mtungi, mara nikasikia sauti ikitoka ndani ya mtungi ikiuliza, “Vipi muda tayari tutoke kwaajili ya mapambano?”

Marjane alinyamaza kidogo akimuangalia Alibaba. Kisha akaendelea kuelezea. “basi sikuwa na cha kufanya. Ila nikaijibu ile sauti iliyouliza nikasema ‘Bado – ila muda mfupi tu nitawajulisha!’ nikaenda kwenye mtungi wa pili, hali ikawa ni ileile, na wa tatu pia—na wa nne na wa tano mpaka mitungi thelathini na tisa hali ilikuwa ni ileile na mimi nikajibu vilevile kwa sauti nzito kidogo inayofanana na ya muuza mafuta. Isipokuwa mtungi wa arobaini ndio uliokuwa na mafuta ndani. Nikajua tu kwamba kwa hali ile bosi wangu uko hatarini hivyo nikachemsha mafuta mengi sana yaliyotoka kwenye ule mtungi wa arobaini na nikayamimina katika kila mtungi. Nafikiri bosi sasa unaelewa stori nzima.”

Alibaba alishtuka sana kusikia hivyo. Alisimama kwa muda kidogo kimya na kufikiri kwa haraka sana.

“Sina adui yoyote hapa mjini,” Alijisemea moyoni. “Lakini kuna hazina niliziiba kutoka kwenye lile pango la ajabu msituni na wezi walimuua kaka yangu Kassim. Sasa nafikiri wanajaribu kutaka kuniua na mimi. Lakini hawatafanikiwa!”

Kisha akasema, “Umefanya vizuri sana Marjane. Umeokoa maisha yangu. Nafikiri huyu muuza mafuta ni kiongozi wa wale wezi waliomuua Kassim, nafikir wanataka kuniua na mimi kwasababu nilichukua dhahabu zao. Lakini yuko wapi sasa huyo muuza mafuta?”

“Sijui, bosi,” Marjane alijibu. “Hata chumbani hayupo, nafikiri alikimbia usiku.”

Ulipoungia usiku, wakati mkewe amelala, Alibaba alimuita kijana wake Khalid na wakachukua masepetu mawili na kuchimba shimo kubwa sana chini ya bustani yao. Katika shimo hilo, waliwazika wezi wote thelathini na tisa pamoja na mitungi yote arobaini. Lakini walizificha panga zao na mikuki ndani ya nyumba kwasababu walijua kwamba huenda kuna siku watazihitaji.

30120577.png

Asubuhi, Alibaba aliwaswaga punda wote ishirini sokoni na kuwauza wote.

“Nimewazika wezi wote thelathini na tisa na mitungi, na nimeficha silaha zao,” Alibaba alimwambia Marjane. “Pia nimeuza punda wote ishirini. Lakini bado kuna tatizo moja. Kiongozi wa wezi bado yuko huru! Huenda akajaribu kuniuwa tena!”

Wakati ule, kiongozi wa wezi alikuwa amejificha msituni ndani ya lile pango. Akiwa ameshika tama kwa huzuni.

Baada ya kukimbia kutoka kwa Alibaba, alielekea moja kwa moja mpaka msituni. Alikuwa na hasira na aibu pia kwasababu mpango wake ulishindikana.

Bado kulikuwa na hazina nyingi sana katika pango. Lakini hili halikumfurahisha. Alikuwa mpweke sana. Kwasababu watu wake wote waliuliwa kule kwa Alibaba. Hakuwa na mtu wa kuongea nae – hakuna mtu wa kumuheshimu – wala hakuna mtu wa kumwambia maneno mazuri. Alibaki tu kufikiria kwamba, ni lazima amuue Alibaba!!!!!

Hivyo basi kiongozi wa wezi alikaa pangoni kwa wiki kadhaa akitengeneza mpango mwingine.

“Lazima niwe mwerevu sana,” alijisema mwenyewe. “kuna mtu katika ile nyumba ni mwerevu pia. Na ndio maana sasa niko hapa peke yangu. Sasa lazima nifanye urafiki na Alibaba. Kwa njia hiyo nitaweza kuingia ndani ya nyumba ya Alibaba. Nitamuua hali ya kuwa hakutarajia. Huenda nikaamua wakati tunapata chakula cha jioni.”

Kiongozi wa wezi akaamua kujifunika uso kiasi ambacho hakuna mtu ndani ya nyumba ya Alibaba angeweza kumtambua. Alivaa ndefu za bandia na akanyoa nywele zake zote na kuwa na kipara.

Kisha, kiongozi wa wezi akaamua kutumia dhahabu zake kununua duka kubwa pale mjini. Akaanza kulijaza duka lake vitambaa mbalimbali vya hariri alivyokuwa amevihifadhi pangoni. Watu wengi sana walikuja dukani kwake na kununua vitambaa vile vizuri. Na muda mfupi tu kiongozi yule wa wezi akawa maarufu sana kama mfanya biashara mkubwa wa kuuza vitambaa vya hariri. Pia alijipatia jina na kujiita: Khoja Hussein.

85750454.png

Alipokuwa akiuza vitambaa kwa wateja wake, alikuwa pia akiwasikiliza wakizungumzia kuhusu watu tofauti wa pale mjini. Vilevile alifanya urafiki na wafanya biashara wakubwa wa pale mjini. Alitaka kwa hali yoyote ile kufahamu kwa undani kuhusu Alibaba na watu anaoishi nao katika ile nyumba. Siku moja alikwenda kumtembelea mfanya biashara mdogo wa mazulia aitwae Khalid. Duka la Khalid lilikuwa mtaa mmoja na duka lake.

“Habari za asubuhi,” Khoja alimsalimia kijana yule. Khalid alikuwa akikunjua zulia refu jekundu akimuonesha mteja wake pale dukani.

“Jina kangu ni Khoja Hussein na ni mgeni hapa mjini. Naona una mazulia mazuri sana!”

“Ahsante,” kijana alijibu. “Baba yangu mkubwa Kassim alianzisha biashara hii, lakini alikuja kuuawa katika mazingira ya kutisha sana.”

“Heh! Na ilikuwaje ikawa hivyo sasa?” Khoja aliuliza.

“Aliuliwa na wezi msituni!” Khalid alielezea.

Khoja alisogea mbele kidogo na kuonesha mshangao usoni.

“Kifo cha kutisha!” alisema. “umesema alikuwa ni baba yako mkubwa – ina maana ni kaka wa baba yako?”

“ndio,” Khalid alijibu.

“Na je baba yako yuko hai leo?” Khoja aliuliza.

“Oh , ndio,” Khalid alijibu. “Ninaishi naye sasa pamoja na mama yangu na mama yangu mkubwa ambaye ni mke wa marehemu baba yangu mkubwa.”

“Na baba yako anaitwa nani?” Khoja Hussein aliuliza.

“Jina lake ni Alibaba!” Khalid alijibu.

Siku inayofuata, Khoja Hussein alirudi pale dukani kwa Khalid.

“Nilifurahia mazungumzo yetu jana,” alimwambia muuza mazulia. “nafikiri tunaweza tukawa marafiki wazuri sana. Unaweza ukaja kwangu kupata chakula cha jioni leo.”

Hivyo wawili hao walipata chakula cha jioni pamoja na baada ya hapo wakawa ni wenye kuonana kila siku. Wakati mwingine Khalid alikwenda kwenye duka la Khoja Hussein na wakati mwingine Khoja Hussein alikwenda kwenye duka la Khalid na kuzungumzia mambo mbalimbali yahusuyo vitambaa vya hariri na mazulia na kuhusu wateja wao.

Siku moja, wakati Khoja Hussein amemtembelea rafiki yake Khalid katika duka lake la mazulia, kulikuwa na mtu mwingine pale dukani. Alikuwa akizungumzia kuhusu kununua zulia jipya kwaajili ya nyumbani kwao. Khoja Hussein akamuangali yule mtu kwa umakini kabisa. Alikuwa na uhakika kabisa kwamba huyo mtu ni yule adui yake, Alibaba!!! Kisha Khoja Hussein akaondoka pale dukani haraka sana. Hakutaka Alibaba amuone.

Siku iliyofuata, Khalid alimtembelea Khoja Hussein dukani kwake.

“Yule mtu aliyekuja kukuona jana,” alisema Khoja Hussein. “Anafanana sana na rafiki yangu. Alikuwa nani yule?”

“Yule ni baba yangu, Alibaba,” Khalid alijibu.

Baada ya hapo wote wakaenda kupata chakula cha jioni katika hoteli kubwa iliyoko maeneo ya pale mjini kama kawaida yao.

Jioni moja, wakati Khalid na Khoja Hussein wakiwa katika matembezi yao mjini pale, Khalid akasimama nje ya nyumba moja kubwa yenye mlango wa bluu.

86399652.png

“Hii ni nyumba ya baba yangu,” Khalid alimwambia rafiki yake. “Hapa ndipo tunapoishi. Nimemuelezea baba yote kuhusu wewe – duka lako, vitambaa unavyouza vizuri na upole wako na ukarimu wako kwangu. Anataka kuonana na wewe.”

“Ni mkarimu sana, Khalid,” Khoja alijibu. “Lakini huenda baba yako akawa na kazi nyingi sana jioni hii.”

“Hawezi kuwa na kazi nyingi kiasi cha kushindwa kumkaribisha rafiki yangu kipenzi,” Khalid alijibu.

Kisha akafungua mlango na kumkaribisha Khoja Hussein ndani ya nyumba yao.
 
SEHEMU YA KUMI NA NNE

UCHEZAJI WA MARJANE




Kutoka sehemu ya kumi na tatu:

Baada ya kiongozi wa wezi kujifanya mfanya biashara mkubwa pale mjini na kupata umaarufu. Sasa afanya urafiki na kijana wa Alibaba ambaye ni Khalid muuza mazulia. Kutokana na urafiki wao kuwa ni wa ukaribu sana na hatimaye kuaminiana sana. Sasa Khalid aamua kumkaribisha kiongozi wa wezi ndani kwao........

Endelea sehemu ya Kumi na nne.


Alibaba alipomuona mgeni yule, alitabasamu na kumpa mkono. “Karibu sana nyumbani kwangu,” alisema kwa ukarimu. “ Kijana wangu aliniambia mambo yote kuhusu wewe,” aliendelea kusema. “Najua wewe ni muuza vitambaa vya hariri muhimu sana hapa mjini na pia ni rafiki mkubwa kipenzi wa mwanangu. Yeye ni kijana mdogo bado na anahitaji kujifunza mengi sana kuhusu mambo ya ulimwengu huu. Wazee kama sisi tunahitaji kuwaongoza vijana hawa katika njia nzuri.”

Khoja Hussein aliinamisha kichwa chake kisha akajibu. “Kijana wako ni kijana mzuri sana, na ninafurahia sana mazungumzo yetu, matembezi yetu na pia tunapopata chakula pamoja. Lakini nina uhakika wewe ni mtu mwenye kazi nyingi sana, Alibaba. Ninaondoka sasa ili niwaache wewe na familia yako mkiwa wenye amani.”

Alibaba alimshika mkono. “Tafadhali bado usiondoke,” alisema. “Ningependa tukae hapa kwa muda huu ili tupate chakula cha jioni pamoja mimi, wewe, Khalid, mke wa Kassim na mke wangu. Marjane yuko jikoni anaandaa kuku mkubwa sana na ataweza kututosha sote.”

“Nashukuru sana kwa kunikaribisha,” alijibu Khoja Hussein. “Lakini nina tatizo kubwa sana. Siwezi kula chakula chochote chenye chumvi.”

Alibaba aliposikia hivyo, alishangaa sana. Ni ajabu sana kusema hivi!!

Alibaba akafikiria kwa muda mfupi, kisha akajibu. “Sawa, hilo halina tatizo. Nitamwambia mfanyakazi asiweke chumvi katika chakula chetu cha jioni leo.”

Kisha Alibaba alienda jikoni na kumkuta Marjane.

“Tuna mgeni kwaajili ya chakula cha jioni leo,” alimwambia. “Jina lake ni Khoja Hussein, ni mfanyabiashara mkubwa sana wa vitambaa vya hariri. Ni rafiki wa Khalid pia. Hawezi kula chumvi, hivyo usiweke chumvi katika chakula. Tafadhali pia pika mbogamboga – na kumbuka kutokuweka chumvi kwenye mbogamboga pia.”

“Sawa bosi,” alijibu Marjane. Kisha akanyamaza kidogo. “Huyu Khojha Hussein ni nani?” alijisemea moyoni. “Kwanini hali chumvi?” kisha Marjane akakumbuka usemi wa kizamani unaosema kwamba: ukitaka kumwua mtu, usile chumvi nyumbani kwake. Ghafla Marjane akaingiwa na hofu. “Khoja Hussein amepanga kufanya nini?” alijiuliza. “Bosi wangu Alibaba yuko hatarini?”

Alipomaliza kuandaa chakula, alibeba sahani ya kuku mpaka mezani. Alipokuwa akiiweka mezani, Marjane alimuangalia Khoja Hussein kwa makini sana wakati akiwa anazungumza na Alibaba na mkewe.

“Huyu mtu mwenye ndevu ndefu nyeusi na upara,” Marjane alijisemea moyoni. “Lakini namtambua huyu mtu – ni kiongozi wa wezi – muuza mafuta – na sasa ni muuza vitambaa vya hariri!! Bosi wangu yuko hatarini tena – huyu mtu ana mpango wa kumuua bosi wangu usiku wa leo! Lazima nifikirie mpango madhubuti.”

Marjane akarudi jikoni na kuleta sahani ya mikate na bakuli kubwa la wali na mbogamboga. Alipokuwa akivitenga mezani, akamuangalia mgeni tena wakati akizungumza na Khalid na mke wa Kassim.

Ghafla Marjane akaona upanga. Ulikuwa umefichwa kwenye koti la mgeni! “amejaribu kuficha upanga,” Marjane alijisemea moyoni. “Lakini nimeweza kuuona.”

34233052.png


Alipokuwa anamalizia kutenga vyakula vilivyobaki, alizidi kufikiria zaidi kuhusu mpango wake.

Walipomaliza kula kuku, Alibaba akasema, “Kuleni matunda. Haya maembe ni mazuri sana.”

“Ahsante,” alijibu Khoja Hussein. Kisha akachukua embe moja kutoka kwenye bakuli na kuegemea kwenye kiti chake na kunyoosha miguu yake mbele na kutabasamu.

“Chakula cha leo ni kitamu sana,” alimwambia Marjane. “Wewe ni mpishi mzuri sana. Niambie, mbali na kupika nini kingine kizuri unaweza kufanya?”

Sasa Marjane akapata nafasi ya kutimiza mpango wake.

“Ninaweza kucheza,” Marjane alijibu. “Ungependa nicheze uone burudani wakati unakula matunda?”

“Unasema..??” alisema Khoja Hussein, akamgeukia Alibaba. “Je Marjane anaweza kucheza tumuone?”

Alibaba akatabasamu na kuitikia kwa ishara ya kichwa . Alikuwa na furaha kuona mgeni wake anaburudika jioni ile.

“Uhakika kabisa,” alisema Alibaba. “Na atatupigia dufu pia. Anajua sana kupiga dufu. Nenda kajiandae Marjane.”

“Sawa bosi,” Marjane alijibu.

Marjane akaenda chumbani kwake. Akavaa gauni refu la rangi ya fedha lenye kung’aa kwa juu. Akajifunga kitambaa mdomoni kuzunga kichwa chake. Akavaa mkanda mnene kiunoni. Kutoka kwenye mkanda ule akaweka ala ya kuwekea kisu, na katika ala ile akaweka kisu. Kisha akachukua dufu na kutoka chumbani kuelekea sebuleni kwaajili ya kucheza.

“Huyoooo amependeza!!” Alibaba alisema kwa furaha. “Sasa tutaburudika!”

Marjane akasimama katikati ya mlango na kuinama kidogo kama ishara ya kusalimia.

“Ingia! Cheza, Marjane!” Alibaba alisema kwa furaha. “ingia na ucheze! Mgeni wetu aone jinsi unavyojua kucheza!”

Marjane akaanza kupiga dufu taratibu na kuanza kucheza akizunguka chumba kile huku akitabasamu.

Alibaba na mgeni wake wakaanza kupiga makofi na mke wa Alibaba na mke wa Kassim wakaanza kuimba. Khalid alisimama dirishani akitabasamu tu.

Kisha Marjane akaanza kucheza haraka haraka. Alionekana kama anataka kupaa. Gauni lake lilikuwa likizunguka kama mwamvuli. Alishikilia dufu juu kupita usawa wa kichwa chake na kulitikisa ili vikengele vidogo vya kwenye dufu lile vitoe sauti. Kisha, kwa mkono wa pili, akatoa kisu kilichopo kwenye ile ala aliyoifunga kiunoni kwenye mkanda. Akaonesha kama ishara ya kukatakata vitu hewani, zote hizo ni mbwembwe mbalimbali za uchezaji.

Akaendelea kucheza mpaka akaenda kwa Alibaba na kujinyooshea kile kisu kifuani kwake mwenyewe na kisha kumnyooshea bosi wake. Akaendelea hivyohivyo kucheza mpaka kwa mke wa Alibaba na kwa mke wa Kassim, na kisha kwa Khalid.

Akazunguka na kunyoosha kisu kile hewani juu na kuendelea kucheza.

Kisha akacheza mpaka kwa Khoja Hussein na kumyooshea kisu kama alivyofanya kwa wengine huku akishusha dufu lile chini na kulishikilia kama sahani.

Alibaba alicheka na kutumbukiza baadhi ya sarafu za dhahabu kwenye lile dufu aliloshikilia Marjane.

“Unastahili kabisa kupata dhahabu hizi! Marjane” Alisema Alibaba. “Umetuburudisha vizuri sana jioni hii.”

34714313.png

Marjane huku ameshikilia dufu lile kama sahani ya chakula, akaendelea kucheza tena mpaka kwa wake wawili, nao wakatumbukiza sarafu za dhahabu katika dufu lile. Kisha ikawa ni zamu ya Khalid. Khalid alitabasamu wakati Marjane akimtazama na Khalid akatumbukiza sarafu za dhahabu kwenye dufu lile.

Mwishowe akafika kwa Khoja Hussein, Marjane akamuelekezea lile dufu.

Kiongozi wa wezi alitabasamu na kuingiza mkono wake mfukoni ili naye atoa japo sarafu kidogo kama wenzake walivyofanya. Muda uleule, Marjane akanyanyua kisu chake juu hewani na, kwa nguvu zake zote alikisukuma kisu kile mpaka kifuani mwa Khoja Hussein.

Khoja Hussein akaanguka nyumba ya sofa. Alibaba na Khalid wakakimbia haraka kwenda kumsaidia.

Alibaba akaweka mkono wake mdomoni kwa Khoja Hussein kuona kama anapumua, na kisha akashika kiganja chake ili kuona kama mapigo ya moyo yanaendelea.

“Hapumui tena!” Alifoka Alibaba. “Na moyo wake umesimama! Amekufa!! Wewe muovu, msichana muovu kabisa!! Kwanini umemwua??”

Kisha Marjane akausogelea mwili wa Khoja Hussein na kuchomoa ule upanga uliokuwa umejificha kwenye koti. Akamuoneshea Alibaba.

“Hakuja kukutembelea.” Marjane alimwambia Alibaba. “Alikuja kukuua. Nimeokoa maisha yako tena bosi.”

“Alikuja kuniua?” Alibaba aliuliza kwa mshangao mkubwa sana. “Kwanini rafiki wa mwanangu Khoja Hussein aje kuniua?”

“Huyu sio Khoja Hussein.” Marjane alielezea. “Huyu ni yule kiongozi wa wale wezi thelathini na tisa. Ametaka kukuua muda mrefu sana. Huyu ni yule muuza mafuta ambaye alikuja hapa kabla – na ni muuaji huyu!”

89871350.png

“Kiongozi wa wezi? Wezi waliomuua kaka yangu? Lakini umejuaje Marjane?” Alibaba aliuliza. “umemtambuaje?”

“Uliponiambia kwamba hali chumvi, nikaanza kumtilia mashaka,” Marjane alieleza. “Nikakumbuka usemi wa zamani wa wazee wetu ukisema: ukitaka kumwua mtu, usile chumvi nyumbani kwake. Hivyo nilipoenda mezani kutenga chakula nikamuangalia usoni kwa umakini kabisa, nikamtambua kuwa ni yule yule muuza mafuta ila amebadilika kwasababu amenyoa upara na ameweka ndevu za bandia, pia nikaona upanga ameuficha katika koti lake. Unaona sasa! Nilikuwa na uhakika kabisa kuwa ndiye mwenyewe”

Alibaba alifurahi sana kusikia hivyo.

“Marjane, umeokoa maisha yangu tena,” alisema. “Wewe ni muaminifu sana, ni msichana mjanja, na kuanzia sasa nakupa zawadi moja. Hautakuwa mfanyakazi wa ndani tena. Ningependa mwanangu Khalid akuoe na uwe mkwe wangu.”

Kisha Alibaba akamgeukia Khalid.

“Yule mtu muovu ametuchezea akili zetu sote wawili mwanangu. Kwanza, aliweka alama kwenye mlango na dirisha ili aweze kurudi nyumbani hapa na kuja kuniua. Kisha akaja na kujifanya ni muuza mafuta, kumbe ndani ya mitungi yake kulikuwa na watu wenye mapanga makali! Kisha akaja kwako kwa kujifanya mfanyabishara wa vitambaa vya hariri mpaka mkawa marafiki wakubwa ilia pate nafasi ya kuwa karibu na mimi na kutimiza lengo lake. Huyu msichana wa ajabu Marjane, ameokoa maisha yetu mara zote hizo. Je utakuwa tayari kumuoa?”

Khalid akatabasamu.

“Nitamuoa Marjane, baba, kama akikubali,” Khalid alijibu. “Ni msichana mzuri, mjanja na muaminifu pia”

Kisha Khalid akamsogelea Marjane na kumshika mkono kisha akamuuliza. “Utakuwa tayari nikuoe?”

“Sawa,” Marjane alijibu.

Kisha Marjane akaangalia juu na kutabasamu kwa familia yake mpya.
 
SEHEMU YA KUMI NA TANO

ALIBABA NI TAJIRI



Kutoka sehemu ya kumi na nne:

Baada ya kiongozi wa wezi kujulikana na Marjane baada ya kuingia ndani ya nyumba, Marjane aamua kutumia njia za ujanja na kufanikiwa kumwua. Alibaba alifurahi sana na kuamua kumuomba mwanaye Khalid amuoe Marjane iwe ni kama zawadi kwake, naye Marjane kwa upole akakubali........

Endelea sehemu ya Kumi na tano.


Hivyo basi, Khalid na Marjane wakafunga ndoa. Watu wengi walikuja kwenye sherehe. Wengi wao walikuwa ni majirani na rafiki zake Alibaba.

Katika sherehe hiyo, mmoja wa wageni alimwambia Alibaba, “Marjane ni masichana mzuri sana. lakini sio jambo la ajabu kweli kwa tajiri kama wewe kuamua mwanao amuoe mfanyakazi wa ndani?”

Kabla Alibaba hajajibu, mgeni mwengine akaingilia mazungumzo na kusema, “Marjane ni msichana mwerevu, mjanja, mpole na muaminifu. Hivyo Khalid hakuwa na haja ya kutafuta tajiri mwenzake, bali ni mwanamke bora, hivyo Khalid ana bahati ya kumpata Marjane.”

Alibaba alitabasamu kusikia hivyo na akachukua sahani nyingine ya halua na kuendelea kuburudika pamoja na wageni wake, hatimaye Alibaba alikuwa ni mtu mwenye furaha na amani.

56719304.png

Familia iliishi kwa furaha kwa miezi mingi. Khalid aliendelea na kazi yake ya kuuza mazulia na wanawake watatu walibaki nyumbani kwa kazi za nyumbani. Alibaba hakuwa tena mkata kuni kwani bado kulikuwa na dhahabu zaidi nyumbani kwake zilizobaki. Lakini daima alikuwa akifikiria kuhusu wale wezi arobaini na hazina zilizopo mle pangoni. Hazina bado zipo?

Mwaka mmoja baada ya ndoa, Alibaba alikuwa amekaa kwenye kistuli nje ya nyumba yake, ilikuwa ni jioni iliyotulia na alikuwa akitazama watu wakitembea huku na huko.

“Angalia watu wote hawa wanaoishi mjini hapa,” alijisemea moyoni. “huenda kuna wezi wengine kati yao. Najua kwamba wale wezi arobaini walishakufa, lakini hakuna wengine zaidi ya wale kweli? Huenda wakawa bado wapo na wanaendelea na tabia ya kuiba mali na kuzificha katika lile pango. Dhahabu zangu humu ndani zimebaki chache, na nahitaji dhahabu nyingine zaidi.” Aliendelea kufikiria. “Nitakwenda pangoni kuangalia.”

Baadaye wakati wanapata chakula cha jioni, Alibaba akamwambia mkewe kuhusu mpango wake.

“Nitakwenda kesho asubuhi sana,” alisema. “Nitakwenda na punda wangu.”



“Lakini unaweza kuwa hatarini,” alijibu mkewe. “Huenda kuna wezi zaidi ya wale arobaini. Wakawa na mikuki na visu vikali. Watakuua wakikuona!”

“Nitakuwa salama, mpendwa,” alijibu alibaba. “Usihofu kuhusu mimi.”

“Basi nenda na mwanao Khalid,” Mkewe alimshauri.

“Khalid ana kazi nyingi sana za kuuza mazulia dukani kwake,” Alibaba alijibu. “Nitakwenda pangoni mwenyewe kama nilivyoenda mara ya kwanza.”

Asubuhi iliyofuata, Alibaba aliamka mapema sana, akachukua makapu sita na kuyafunga kwa wale punda wake watatu. Kisha akaiaga familia yake na kuelekea msituni.

Alipofika katika jiwe kubwa la lile pango, alisimama na kuangalia maeneo yaliyozungula pango lile. Aliuona mti mrefu ambao alijificha mara ya kwanza alipogundua pango lile. Alisikiliza kwa makini sana – hakukuwa na sauti za kwato za farasi, wala sauti za wanyama wa porini, hakusikia wala kuona chochote ambacho kingemtia hofu.

Akavuta pumzi nyingi ndani na kusogea karibu na jiwe kubwa la lile pango.

Kisha aksema lile neno la siri, “Fungukaaaa sesmiiiii!!!!

Taratibu kabisa, lango likafunguka na Alibaba akaingia ndani. Akaona sehemu ambayo aliuona mwili wa kaka yake. Alibaba aligeuka haraka sana ili asipatazame sana mahali pale kwani kungemtia huzuni zaidi. Akaendelea kwenda ndani zaidi.

Pango bado lilikuwa na hazina nyingi sana, dhahabu, fedha, sarafu, pete, bilauri za rangi ya fedha na hazina nyingi zaidi ya hizo – kitu ambacho hakukiona pale ni vitambaa vya hariri.

Alibaba akafikiri kidogo.

“Khoja Hussein!” alijisemea moyoni. “Kiongozi wa wezi alijifanya mfanya biashara mkubwa wa vitambaa vya hariri na kufanya urafiki na mwanangu! Alijaza duka vitambaa vya hariri – kumbe vilitoka humu pangoni.”

Alibaba akaendelea kuangalia hazina zote.

“Hakuna mtu aliyekuwepo humu kwa muda mrefu sana,” Alijisemea. “Nafikiri wezi wote wameshakufa. Hazina hii yote ni yangu!”

Hivyo basi, akachukua baadhi ya mifuko ya sarafu za dhahabu, na baadhi ya vito pamoja na bilauri nzuri zenye kung’aa.

96280208.png

“Hizi bilauri zitapendeza sana zikiwa mezani kwetu.” Alifikiri. “Mke wangu atazipenda sana.”

Alibaba akazibeba hazina hizo alizokusanya na kuzijaza katika makapu yake sita yaliyobebwa na punda wake.

“Hii inatosha kwa sasa,” alijisemea. “Sitaki kuwa mroho sana.”

Kisha katoka nje ya pango na kusema neno la siri, “Fungaaaaa sesmiii!!

Jiwe kubwa likajifunga na likaonekana kama mawe mengine tu ya pale msituni.

Wakati jua linakaribia kuzama, na mbingu inabadilika rangi na kuwa kama zambarau iliyokoza, Alibaba na punda wake wakaondoka kurudi nyumbani.

Hazina iliyochukuliwa na Alibaba ilidumu kwa mwaka mwingine zaidi. Wakati huu, Marjane na Khalid walipata mtoto wa kiume na Alibaba akaamua kumpa Khalid siri ya lile pango.

27421649.png

“Wewe ni baba sasa, Khalid,” Alibaba alimwambia mwanae. “Kuna kitu nataka kukuonesha – kitu muhimu sana. Unajua kwamba nina dhahabu, na unajua kwamba nilizipata kutoka kwa kundi lile la wezi. Wale waliokuwa wanataka kuniua.”

“Ndio baba,” Khalid alijibu. “Marjane wangu mwerevu aliwaua! Na ninajua kwamba dhahabu zile ndizo zilizokutajirisha.”

“Ndio, haswaa!!” Alibaba alisema. “Lakini sasa, nimezitumia nyingi sana, na sasa nahitaji nyingine zaidi. Nataka nikupeleke kwenye pango ambalo dhahabu hizo zinapatikana, Khalid. Siku moja wewe au mwanao mnaweza kuhitaji kujua mahala zilipo.”

“Ahsante sana, baba,” Khalid alijibu. “Nina furaha kwa kuniambia hivyo. Nilikuwa nashangaa hizi dhahabu mahali zinapotoka.”

Siku iliyofuata, Alibaba na mwanae wakafunga safari ya kuelekea msituni na walienda na punda wao watatu.

Kisha Alibaba akasema neno la siri, “Funguaaaa sesmiiii!!!”

Lango likafunguka, kisha Alibaba na mwanae wakaingia ndani.

Pango bado lilikuwa na hazina nyingi sana. Dhahabu zote pamoja na fedha na vito mbalimbali vilikuwa vinang’aa kutokana na mwanga unaoingia pangoni kupitia vitundu vya juu ya pango hilo. Khalid aliduwaa sana kuona hivyo.

“Siamini macho yangu!” alisema. “Kuna hazina nyingi sana!”

“Hakuna mtu aliyeingia humu kwa mwaka mzima sasa,” alisema Alibaba huku akiangalia maeneo yote ya pangoni mle. “Tutakuwa salama kabisa.”

Wakachukua baadhi ya hazina na kujaza kapu zao na kurudi nyumbani.

“Ahsante kwa kuniambia siri yako, baba,” Alisema Khalid wakati wanarudi nyumbani. “Mwanangu akiwa mkubwa, nitamwambia pia kuhusu hazina zile na nitampeleka huko pangoni.”

Alibaba alicheka kwa furaha. “Ndiyo,” alijibu. “Na yeye pia atamwambia mwanae.”

Familia ya Alibaba iliishi kwa amani na hawakuwa masikini tena.

Mwisho wa Kisa hiki
 
ALIBABA NA WEZI 40
SURA YA KWANZA:
HAZINA KATIKA PANGO


Hapo zamani za kale katika mji wa persia waliishi ndugu wawili mmoja aliitwa Kasim na mwengine aliitwa Alibaba, ndugu hawa wawili walikuwa na baba yao ambae alikuwa na uwezo wa kifedha kidogo ambae alipokufa waligawana mali zake mgao sawa kwa sawa bila kumzidishia yeyote baina yao, na wala hawakuwa na muda wa kupoteza na kuzitumia mali zile zote.

Mkubwa kati ya wale vijana wawili ambaye ni Kasim alioa mwanamke ambae ni mtoto wa mfanya biashara tajiri, hivyo basi, baba mkwe wake alipotangulia mbele ya haki (kufa) alimiliki duka kubwa lililokuwa na bidhaa adimu pamoja na bidhaa zenye thamani kubwa na pia alimiliki bohari kubwa iliyokuwa na vyombo vyenye thamani kubwa ukiachilia mbali dhahabu nyingi sana ambazo zilikuwa zimefukiwa ardhini.

Hivyo basi alijulikana karibuni mji mzima kama mtu aliye thabiti au imara mwenye nguvu lakini mke aliyemuoa Alibaba alikuwa masikini na tegemezi hata hivyo waliishi katika kibanda duni.

Alibaba alijikimu maisha yake kwa kuuza kuni alizokuwa akikusanya kutoka msituni na kupeleka mjini sokoni kwa kutumia punda wake watatu.

Ilitokea siku moja Alibaba alikuwa akikata matawi yaliyokufa na kukausha kuni zilizotosheleza kwa mahitaji yake, na baada ya hapo akaweka mizigo yake juu ya wale wanyama wake (punda).

Mara ghafla akaona kama wingu la vumbi likiwa linapanda juu angani kwa mbali upande wake wa kulia huku likiwa linakuja upande alioko, lilipofika karibu aliona kundi la waendesha farasi wakiwa wanakuja upande alioko na walikuwa karibuni kumfikia.

Kwa muda huo alikuwa kakata tamaa na kuogopa huenda wale wakawa ni majambazi ambao wanaweza kumuua na kuchukua punda wake, kwa uwoga wake akaanza kukimbia. Lakini kwakuwa walikuwa tayari wamefika karibu na hakuweza kutoka nje ya ule msitu, aliwaficha wanyama wake vichakani naye kujificha kwenye mti mkubwa ambapo alikaa kwenye tawi ili aweze kuona kila kinachoendelea pale na wakati huo hakuna yeyote chini aliyeweza kumuona huko juu aliko. mti ule uliota pembeni kidogo ya mwamba ambao ulikuwa mrefu.

Waendesha farasi, vijana, wenyenguvu na mashujaa walikuja karibu na uso wa ule mwamba na wote wakashuka kwenye farasi wao kitendo ambacho kilifanya Alibaba awaone vizuri watu wale na mara akapata hisia kutokana na muonekano na mwenendo wa tabia za wale watu kwa jinsi alivyowaona ni waporaji ambao wamepora na sasa wameleta mali za uporaji kuja kuziweka katika eneo lile kwa nia ya kuzificha, vilevile aligundua kuwa idadi ya wale watu ilikuwa arobaini (40).

Alibaba aliwaona wale majambazi na walipofika chini ya ule mti kila mmoja alimfunga farasi wake pale, halafu kila mmoja alishusha mizigo yake ambayo Alibaba aligundua kuwa kulikuwa na madini ya dhahabu na fedha ndani yake. Mtu mmoja kati yao ambae alionekana kuwa ndiye kiongozi wao aliendelea mbele huku akiwa na mzigo kwenye bega akipita kwenye mibamiba na vichaka mpaka alipofika sehemu moja kwenye alama chini kama doa hivi akasimama pale halafu akatamka maneno fulani akisema “ Funguaaaaa, Sesmiii!!” na mara moja ukafunguka mlango mkubwa kwenye uso wa ule mwamba, baada ya hapo wezi wote wakaingia mle ndani na mwisho akaingia kiongozi wao kisha lile lango likajifunga lenyewe.

Muda mrefu walikaa ndani ya lile pango huku Alibaba akiendelea kukaa juu ya ule mti akihofu kwamba kama akishuka huenda mude uleule na wale wezi wanaweza kutoka na kumuona kisha wakamuua. Lile lango lilipofunguka tu wa kwanza kutoka alikuwa ni kiongozi wao akaenda kwenye lile doa kisha akawahesabu wale wenzake mpaka walipoisha kutoka wote kisha akasema “ Fungaaaaaaa, Sesmiiii!!” na hapo lango likajifunga. Walipomaliza kukutana wote kila mmoja alichukua mizigo yake na kuondoka wote eneo lile wakiongozwa na kiongozi wao wakielekea kule walikotokea. Alibaba aliendelea kukaa juu ya ule mti huku akiangalia safari ya wale wezi wanapoondoka. Akaona asubiri mpaka wapotee kabisa kwa maana asije mmoja akarudi na kumkuta mahali pale.

Walipopotea kabisa mbele ya macho yake Alibaba akashuka kutoka mtini na kwenda mpaka pale kwenye lile doa kisha akajisemea mwenyewe “nitajaribu kutamka maneno yale ya ajabu nione kama kwa kutamka kwangu lile lango litafunguka na kufunga” kisha akasema kwa kelele yale maneno “Funguka, Sesame!!” alipomaliza tu kutamka mara lango likafunguka, kisha akaingia ndani yake.

Akaona pango kubwa lenye kuba likiwa na urefu upatao kadiri ya urefu wa mtu aliekuwa mrefu zaidi duniani, pango lile lilikuwa limezungukwa na mawe na lilikuwa likipitisha mwanga kupitia vitundu vidogovidogo vilivyokuwa katika pango lile na kushangazwa alipoona limejaa kila aina ya bidhaa mle ndani na kumerundikwa kutoka chini mpaka juu rundo la mizigo ya hariri na nguo nzuri zilizotiwa nakshi na matuta juu ya matuta ya makapet na mazulia yenye rangi tofauti na pia aliona sarafu za dhahabu na fedha zikiwa nyingine zimezagaa chini na nyingine zikiwa ndani ya mifuko. Kwa kuona wingi wa mali hizi Alibaba alijifikiria moyoni kuwa sio kwa miaka michache tu, hii itakuwa ni karne na karne wezi wanapora mali za watu na kuja kuzificha humu. Je nini kitaendelea humo pangoni?
Tunakaa kwa kusubiri
 
SEHEMU YA KUMI

07014989.png

Kutoka sehemu ya tisa:

Baada ya mpango wa mwizi wa kwanza kufeli, ikatokea mwizi wa pili kwenda kujaribu kuitafuta nyumba ya Kassim. Kwa utaratibu uleule, mwizi wa pili alimlipa Mustafa dhahabu ili apate msaada wa kupelekwa kwenye hiyo nyumba. Sasa safari hii mwizi wa pili aliweka alama ndogo sana nyekundu ambayo si rahisi kwa mtu kuiona na kwa furaha kabisa akarudi msituni kwenda kutoa taarifa kwa kiongozi wao.

Endelea sehemu ya Kumi.


Jioni ile, Marjane alikuwa akiandaa chakula cha jioni kwa aajili ya familia ya Alibaba na wenzake nyumbani. Aliandaa nyama ya kuku, kachumbari na mchanganyiko wa mbogamboga mbalimbali, alipomaliza kuandaa mchuzi ule wa kuku na mbogamboga akaanza kuandaa upishi wa wali, alichukua sufuria na kuweka maji kiasi, kisha akaweka sufuria hiyo kwenye jiko. Baada ya hapo alienda mpaka stoo kuchukua mchele ili aweze kuchambua na kuusafisha kabla ya kuutosa kwenye maji, kwa bahati mbaya sasa, akakuta mchele hakuna.

35667032.png

“Itabidi tu niende kununua mchele” alijisemea moyoni. Marjane akachukua kapu lake la sokoni na kuelekea mjini sokoni.

Alipokuwa akirudi aliona alama ndogo nyekundu kwenye fremu ya dirisha, macho ya Marjane yalikuwa mazuri sana, hakuwa na matatizo ya macho hata kidogo.

“Hii alama haikuwa hapa kabla” Marjane alijisemea moyoni. “Mara ya kwanza alama nyeupe, na mara hii tena alama nyekundu!! Vizuri sana! Nitafanya kama nilivyofanya mara ya kwanza.”

Aliingia ndani na kwenda kuchukua chaki nyekundu. Kisha akarudi nje na kuweka alama nyekundu katika kila fremu ya dirisha kwenye nyumba zote za mtaa ule.

“Hii lazima imchanganye huyu aliyeweka ile alama nyekundu pale.” Alijisemea huku akicheka. Kisha akarudi nyumbani kuendelea kuandaa chakula cha jioni, lakini hakumwambia yeyote kuhusu alama ile nyekundu.

Yule mwizi aliyeweka ile alama nyekundu alifika msituni, alipowakaribia wezi wenzake akaanza kupiga kelele za furaha, “Nimeiona! Nimeipata nyumba ambayo suti ya marehemu ilishonwa!!”

Kiongozi wao alimfurahia sana. “Umefanya kazi nzuri!” Alisema. “Umefanya kazi muhimu sana! Sasa tunaweza kumpata aliyetuibia dhahabu zetu.”

“Nilienda mpaka kwa fundi nguo, Mustafa.” Mwizi alisema kwa kujisifu. “Alikubali kunisaidia kama ningempa dhahabu. Nikamfunga macho na kitambaa kama alivyofanya awali, na akanipeleka mpaka kwenye hiyo nyumba. Nikaweka alama ndogo sana nyekundu kwenye fremu ya dirisha ili tuweze kuipata hiyo nyumba tena.”

Wezi wakampigapiga mgongoni kama ishara ya kumpongeza huku wakishangilia. Kisha kiongozi wao akasema, “Nipeleke huko sasa hivi.”

Hivyo basi, wawili hao wakaondoka kuelekea mjini. Baada ya kufika tu mwizi mmoja akamuonesha mkuu wake nyumba ambayo kwenye dirisha kuna alama nyekundu kwenye fremu.

“Hii hapa sasa!” mwizi alimwambia mkuu wake. “hii ndiyo nyumba yenyewe! Unaona alama nyekundu kwenye fremu ya dirisha?”

Kiongozi wa wezi alienda mpaka karibu na kuiangalia alama ile.

“Ndiyo, naiona! alijibu mkuu wa wezi. “pia naona kuna alama kama hii katika fremu ya dirisha katika nyumba ile, na ile pia! Na ile na ile! Kwanini alama hiyo ipo kila dirisha katika nyumba za mtaa huu? Nani atakuwa ameziweka hizo?”

“sijui, “ alisema mwizi yule akiwa hana furaha tena. “Mimi niliweka alama kwenye dirisha moja tu”

“wewe ni mjinga wa pili!!” alifoka mkuu wao. “haya haraka sana turudi msituni!!”

Asubuhi iliyofuata, kiongozi wao aliwaita wezi wote katika eneo lao la kukutana.

“Wawili wenu walishindwa kuitafuta nyumba tunayoihitaji” aliwaambia. “Sasa nitakwenda na kuitafuta nyumba mimi mwenyewe. Nisubirini hapa”

Hivyo basi, kiongozi wao akaondoka kuelekea mjini mwenyewe. Akaonana na Mustafa katika kibanda chake, akampa sarafu ya dhahabu. Mustafa akamuongoza kiongozi huyo wa wezi kulekea kwenye ile nyumbaya Kassim.

Kama kawaida alivaa kitambaa kufunika macho, na kwa kutumia msaada wa harufu na sauti mbalimbali, Mustafa alifanikiwa kumfikisha kiongozi wa wale wezi mpaka kwenye ile nyumba.

“Nasikia harufu ya maua mazuri sana, natumaini hapa ndipo mahala penyewe.” Alisema Mustafa.

15265345.png

“Sitaweka alama yoyote ya chaki,” kiongozi yule alijisemea moyoni. “Alama za chaki zote zilizowekwa hazikuweza kufaa kabisa hapo kabla. Nitaitizama nyumba hii kwa umakini kabisa na kukariri kila kitu ili niweze kukumbuka ninachokiona.

Hivyo basi, Kiongozi yule aliangalia madirisha mazuri ya nyumba ile, pia aliangalia milango iliyopakwa rangi ya samawati na mapazia mekundu yaliyoning’inizwa kwenye madirisha. Aliangalia mimea mirefu iliyopandwa ndani ya mitungi mikubwa meupe na paka wa rangi ya machungwa mwenye macho ya njano akiwa kwenye dirisha akimtazama.

Baada ya kuangalia yote hayo, alimchukua mzee Mustafa na kumrudisha kwenye kibanda chake kisha akarudi msituni kuonana na watu wake.

“ninaifahamu nyumba ile sasa,” Alisema alipofika. “Hatuwezi kuamini alama za chaki tena, hivyo nitaamini kumbukumbu yangu. Nimeangalia kwa undani sana ile nyumba, ina madirisha mazuri sana na milango ya nje iliyopakwa rangi ya samawati, pia kuna mapazia mekundu kwenye madirisha. Nje kuna mimea mirefu iliyopandwa katika mitungi mikubwa yenye rangi nyeupe na kuna paka wa rangi ya machungwa mwenye macho ya njano anaishi humo. Itakuwa rahisi sana kuipata hiyo nyumba.”

“Sasa tunaweza kumpata mtu aliyetuibia dhahabu zetu,” kiongozi aliendelea kusema. “Na lazima tumuadhibu! Lakini kwanza, lazima tuingie ndani ya nyumba ile. Nina mpango. Tutaenda huko usiku wa leo. Njooni hapa karibu, vijana wangu, na nisikilizeni kwa makini kabisa.”

Wezi wote wakasogea karibu kusingia mpango wa kiongozi wao.

“Mtajua wenyewe mjipange vipi,” Kiongozi wao alianza kuwaambia. “Nendeni mjini na kiasi cha kutosha cha dhahabu. Jaribuni kupita kila sehemu ambayo kuna wafanyabiashara wakubwa wakubwa ambao wanatumia punda katika kazi zao. Jaribuni kuongea nao wawauzie punda, hakikisheni mnanunua punda ishirini na mniletee hapa msituni.”

Baada ya hapo wezi wakachukua kiasi cha kutosha cha dhahabu na kulekea mjini.
Mkuu Bujibuji please tuletee hadithi ya Adili na nduguze.
 
.
 

Attachments

  • alibabaandthefortythievesarabiannights.pdf
    192.7 KB · Views: 36
Back
Top Bottom